Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 4/8 kur. 19-22
  • Hatimaye Nilipata Kweli

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Hatimaye Nilipata Kweli
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mazoezi Makubwa ya Kidini
  • Kati ya Mchafuko
  • Ulimwengu Vitani
  • Napata Kweli
  • Pendeleo Lenye Thamani
  • Baraka za Ajabu
  • Walishangaa kwa Yale Waliyoona
    Amkeni!—1992
  • Licha ya Majaribu, Tumaini Langu Halijafifia
    Amkeni!—2002
  • Mashahidi wa Yehova Katika Ulaya Mashariki
    Amkeni!—1992
  • Nilijifunza Kumtegemea Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 4/8 kur. 19-22

Hatimaye Nilipata Kweli

Kuelekea mwisho wa Agosti 1939, nilitua Moscow nikiwa njiani kwenda nyumbani Budapest, Hungaria. Mkataba wa Ujerumani na Sovieti wa Kutoshambuliana ulikuwa umetiwa sahihi siku kadhaa mapema, Agosti 23, na kuta za Kremlin zilikuwa zimepambwa bendera za swastika za Nazi. Kwa nini nilikuwa Urusi, na ni nini kilichoningoja nyumbani?

KWANZA, ebu niwapeleke kwenye mji mdogo wa Veszprém katika Hungaria, ambako nilizaliwa Januari 15, 1918. Nilikuwa kifungua mimba cha watoto wanne, na wazazi wetu walihakikisha kwamba tulihudhuria kanisa kwa ukawaida. Nilipofikia umri wa miaka mitano, nilikuwa nasaidia kwenye Misa katika makao ya Katoliki ya Roma. Nikiwa nyumbani nilikuwa nikijifanya kuwa naendesha Misa kwa ndugu zangu, nikivaa mavazi ya kikasisi niliyokuwa nimetengeneza kwa karatasi kwa ajili ya Misa hiyo.

Nilipokuwa na umri wa miaka minane, baba aliiacha familia yetu, mama akatulea kwa msaada wa mama yake. Mwaka uliofuata, mama akafa kwa kansa. Katika miaka iliyofuata, sisi watoto tulitenganishwa na kuwekwa katika makao tofauti-tofauti ya mayatima na ya wazazi walezi. Makao ya mayatima ya mwisho niliyoishi yalikuwa karibu na Budapest. Ilisimamiwa na Frères Maristes (Ndugu za Maria), ambao walikuwa jumuiya ya walimu wa Katoliki wa Ufaransa. Nilimpenda Mungu sana, kwa hiyo nilipofikia umri wa miaka 13, nilikubali toleo la kusomeshwa na jumuiya hiyo ya kidini.

Mazoezi Makubwa ya Kidini

Mwaka uliofuata nilipelekwa Ugiriki, ambako nilihudhuria shule ya Frères Maristes iliyokuwa ikiongozwa kwa Kifaransa, ambayo ilinizoeza kuwa mwalimu. Miaka minne baadaye, katika 1936, nilihitimu nikiwa na cheti kilichonistahilisha kufundisha shule ya msingi. Baada ya uhitimu nikawa ndugu katika jumuiya hiyo, nikitoa nadhiri yenye sehemu tatu ya umaskini, utii, na usafi wa kiadili. Ingawa sisi ndugu tulivaa mavazi ya kidini na kufundisha katekisimu, hatukujifunza Biblia kamwe.

Kiangazi hicho nilipeleka maombi ya kufundisha nchini China na kukubaliwa. Oktoba 31, 1936, niliondoka katika meli iliyotoka Marseilles, Ufaransa. Desemba 3, 1936, nilifika Shanghai. Toka hapo nilipanda gari-moshi hadi Beijing, jiji kuu, kaskazini mwa China.

Katika eneo lenye milima kilometa 25 hivi kutoka Beijing, ile jumuiya ya kidini ya Frères Maristes ilikuwa na shule kubwa, mabweni, na majengo ya shamba. Mahali hapo palikuwa karibu na makao ya kiangazi ya maliki nayo yalikuwa na bustani zilizotunzwa vizuri sana na miti ya matunda. Huko nilijifunza sana lugha za Kichina na Kiingereza. Lakini hatukujifunza Biblia kamwe.

Kati ya Mchafuko

Mapema katika miaka ya 1930, Japani ilinyakua eneo la Manchuria, ambayo ni sehemu ya China. Katika Julai 1937, majeshi ya Japani na China yalipigana karibu na Beijing. Hao Wajapani wenye ushindi wakaweka serikali mpya kwa kumchagua Mchina waliyempenda awe kibaraka chao. Hilo lilitokeza vita baina ya wapiganaji wa kuvizia wa China na serikali mpya.

Kwa kuwa makao yetu ya watawa yaliyokuwa nje tu ya Beijing yalitambuliwa kuwa eneo la Ufaransa, yaliepushwa mapigano ya moja kwa moja. Lakini, tulipigwa mizinga na risasi zilizokosa shabaha ambazo ziliwajeruhi baadhi ya Wachina zaidi ya 5,000 waliotafuta kimbilio katika makao yetu ya watawa. Kwa wakati uo huo, wapiganaji Wachina wa kuvizia walitawala maeneo ya mashambani.

Katika Septemba 1937 wapiganaji Wachina wa kuvizia wapatao 300 wenye kujihami walishambulia majengo yetu, wakitafuta silaha, pesa, na chakula. Nilikuwa miongoni mwa Wazungu kumi waliochukuliwa mateka. Baada ya kushikwa kwa siku sita, nilikuwa miongoni mwa mateka wa kwanza kufunguliwa. Nilikuwa nimekuwa mgonjwa kwa kula chakula kibaya, kwa hiyo nililazwa hospitali kwa mwezi mmoja.

Baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, nilihamishwa hadi shule nyingine iliyokuwa inaendeshwa na jumuiya ileile, katika eneo salama zaidi la Beijing. Katika Januari 1938, nilipelekwa Shanghai kufundisha lakini nikarudi Beijing Septemba kufundisha huko. Lakini, baada ya mwaka wa masomo, sikutoa upya nadhiri zangu za kidini. Kwa miaka saba nilikuwa nimefuatia maisha na elimu ya kidini lakini sikuwa nimepata uradhi katika kutafuta kweli. Kwa hiyo niliacha jumuiya hiyo ya kidini ili nirudi nyumbani Budapest.

Kufikia wakati huo ishara za Vita ya Ulimwengu 2 zilikuwa zinaonekana. Wakuu wangu Wafaransa walinitia moyo nitumie Reli ya Trans-Siberia, ambayo ilipitia baadhi ya sehemu za Muungano wa Sovieti. Ilikuwa katika safari hiyo nilipofika Moscow Agosti 27, 1939, na kuona kuta za Kremlin zimepambwa kwa bendera za Nazi.

Ulimwengu Vitani

Nilifika Budapest Agosti 31, 1939. Siku iliyofuata Ujerumani ilishambulia Poland, na kuanzisha Vita ya Ulimwengu 2. Baadaye, Ujerumani ilivunja mkataba wao wa kutoshambulia Muungano wa Sovieti, na Juni 22, 1941, majeshi ya Hitler yalivamia Muungano wa Sovieti. Hayo yalipenya ndani hadi viunga vya Moscow lakini yalishindwa kuliteka hilo jiji.

Gavana wa Hungaria alitia sahihi mapatano ya amani na Ujerumani, na majeshi ya Ujerumani yalipewa uhuru wa kupitia Hungaria. Nilifunga ndoa katika 1942, na katika 1943, nilisajiliwa katika Jeshi la Hungaria. Katika Machi 1944, Ujerumani ilishambulia Hungaria kwa sababu Hitler hakuridhika na jinsi Hungaria ilivyomwunga mkono vitani. Mwaka huo mwana wetu alizaliwa. Ili kuepuka mashambulizi mazito ya mabomu dhidi ya Budapest, mke wangu na mwana wangu walihamia sehemu za mashambani ili kuishi na wazazi wake.

Mkondo wa vita ukabadilika, na Jeshi la Sovieti likaja mpaka Budapest, likifika Desemba 24, 1944. Nilikamatwa na Warusi nikawa mfungwa wa vita. Maelfu ya sisi wafungwa tulilazimishwa kutembea kwa karibu kilometa 160 hadi Baja, Hungaria. Huko, tulisongamana katika mabehewa ya kubebea ng’ombe na kuhamishwa hadi Timisoara na kuwekwa katika kambi kubwa ya mateso. Angalau wafungwa 20,000 kati ya wale 45,000 walikufa mapema katika 1945 wakati wa mweneo mkubwa wa homa ya matumbo.

Katika Agosti waokokaji 25,000 walipelekwa hadi Bahari Nyeusi. Kutoka huko karibu 20,000 walihamishwa hadi Muungano wa Sovieti. Hata hivyo, wengine wapatao 5,000 waliokuwa wagonjwa, kutia na mimi, tulirudishwa Hungaria na kuachiliwa huru. Basi, utekwa wa miezi minane yenye kuogofya sana ukaisha. Majuma machache baadaye, niliungana tena na mke wangu na mwana wangu, tukarudi Budapest ili kuishi huko.

Baada ya vita, watu wengi waliendelea kuteseka. Chakula kilikuwa haba sana, na infleshoni ilikuwa mbaya sana. Kile ambacho pengö moja ya Hungaria iliweza kununua katika 1938 ilihitaji zaidi ya pengö nonilioni (1,000,000,000,000,000,000,000,000,000,000) kununua katika 1946! Baada ya muda, maisha yaliboreka kwetu nilipopata kazi ya ofisi katika reli.

Napata Kweli

Katika 1955 mmoja wa Mashahidi wa Yehova walioishi katika jengo moja na sisi katika Budapest alianza kuzungumza na mke wangu, Anna, juu ya Biblia. Upendezi wangu uliamshwa Anna aliponiambia Biblia haifundishi kwamba helo ni mahali pa moto wa mateso. (Mhubiri 9:5, 10; Matendo 2:31) Nikiwa Mkatoliki, sikuwa nimepata kamwe kujifunza Biblia, hata wakati nilipokuwa nikipata mazoezi ya kipekee katika shule za kanisa. Mimi nilikubali tu mafundisho yasiyo ya Kimaandiko ya Kikatoliki, kama moto wa helo. Sasa nikaja kupenda kweli za Biblia, hasa zile zinazohusu Ufalme wa Mungu na jinsi utakavyotimiza kusudi la Mungu ili kufanya dunia iwe paradiso. (Mathayo 6:9, 10; Luka 23:42, 43; Ufunuo 21:3, 4) Nikawa na furaha nyingi sana ambayo sikupata kuwa nayo kamwe maishani.

Kwa wakati huo, Mashahidi wa Yehova katika Hungaria walikuwa wakiwindwa na kufungwa kwa sababu walifundisha kweli za Ufalme wa Mungu kwa moyo mkuu. Nilisoma vichapo vyote vya Mashahidi ambavyo ningeweza kupata katika Kihungaria na tuliweza kupata vichapo vyao vya Kiingereza na Kifaransa ambavyo havikuwa vimetafsiriwa katika Kihungaria. Nilishukuru kama nini kwamba nilikuwa nimejifunza lugha hizo nyingine!

Katika Oktoba 1956, Wahungaria waliasi dhidi ya utawala wa Kikomunisti uliobandikwa na Urusi. Mapigano yakawa makali sana katika Budapest. Wengi waliokuwa gerezani walifunguliwa, kutia ndani Mashahidi wa Yehova. Katika kipindi hiki mimi na mke wangu tulibatizwa katika kuonyesha wakfu wetu kwa Yehova Mungu. Juma moja baadaye, majeshi ya Urusi yalikandamiza maasi hayo. Wale Mashahidi ambao walikuwa wamefunguliwa walirudishwa gerezani.

Pendeleo Lenye Thamani

Kwa kuwa wengi wa Mashahidi waliokuwa na madaraka katika kazi ya kuhubiri walikuwa gerezani, nilifikiwa na Mkristo mwenzangu na kuombwa kama ningeweza kutafsiri baadhi ya fasihi zetu za Biblia. Kwanza nilipewa barua za watu binafsi kutoka Uswisi ambazo zilikuwa na makala za Mnara wa Mlinzi zilizochapwa kwa taipu katika Kifaransa. Nilizitafsiri katika Kihungaria, kisha makala za nakala zilizotafsiriwa zilipelekwa makutanikoni.

Msimamizi wa ofisi ya tawi ya Hungaria, János Konrád, alipofunguliwa gerezani katika 1959 baada ya kufungwa kwa miaka 12 kwa sababu ya kutokuwamo kwa Kikristo, niliwekwa rasmi kuwa mtafsiri. Kisha nikapokea vitu vya Kiingereza vya kutafsiri. Mara nyingi vililetwa na mwanamke fulani ambaye sikumjua. Hivyo, kama ningalishikwa na kuteswa, singaliweza kutaja jina lake.

Baada ya kutafsiri Mnara wa Mlinzi, Ndugu Konrád alikuwa akilichunguza kuhakikisha ni sahihi. Kisha akina dada walikuwa wakichapa kwa taipu makala zilizotafsiriwa katika karatasi nyembamba sana, wakitumia karatasi ya kaboni ili kufanyiza nakala 12. Hivyo, nyakati nyingi kila mtu aliyekuwa amehudhuria Funzo la Mnara wa Mlinzi alikuwa na makala yake mwenyewe iliyochapwa kwa taipu. Baadaye, wao walipitisha nakala zao kwa kikundi kingine cha kujifunza. Hata hivyo, mara nyingi tuliweza kutokeza makala moja tu ya Mnara wa Mlinzi kwa kila kikundi cha kujifunza. Kisha wote waliokuwapo walipaswa kusikiliza kwa makini sana na kuandika mambo ili kunufaika kabisa na mazungumzo ya Biblia.

Tokea wakati nilipoanza kutafsiri katika 1956 hadi 1978, Mnara wa Mlinzi lilikuwa likienezwa katika lugha ya Kihungaria katika njia ya kupigwa chapa kwa taipu tu. Tokea 1978 hadi 1990, nakala zilizorudufishwa kwa stensili za Mnara wa Mlinzi ziliandaliwa. Na ikawa baraka kama nini kwamba tangu Januari 1990 magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! yanapigwa chapa katika lugha ya Kihungaria katika rangi kamili zenye kuvutia!

Chini ya utawala wa Kikomunisti kila mtu alipaswa kuwa na kazi ya kimwili. Hivyo, kwa miaka 22, mpaka kustaafu kwangu kwa kazi yangu ya kimwili katika 1978, nilikuwa natafsiri katika saa ambazo sikuwa nafanya kazi ya kimwili. Mara nyingi hiyo ilikuwa mapema asubuhi na usiku sana. Baada ya kustaafu nikawa mtafsiri wa wakati wote. Wakati huo, kila mtafsiri alifanya kazi nyumbani, na kwa sababu ya marufuku, ilikuwa vigumu kuwasiliana. Katika 1964, polisi walivamia makao mbalimbali ya watafsiri kwa wakati mmoja na kutwaa vifaa. Kwa miaka mingi baadaye, tulikuwa tukitembelewa na polisi mara nyingi.

Baraka za Ajabu

Katika 1969 ombi langu la kutaka pasipoti lilikubaliwa, kwa hiyo mimi na János Konrád tuliweza kusafiri kutoka Hungaria kwenda Paris ili kuhudhuria Kusanyiko la Kimataifa la “Amani Duniani” la Mashahidi wa Yehova huko. Tulibarikiwa kama nini kukutana na Mashahidi wenzetu kutoka nchi nyinginezo na kutumia siku kadhaa katika ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika Bern, Uswisi! Katika miaka ya 1970 Mashahidi wengi kutoka Hungaria waliweza kwenda Austria na Uswisi kwa ajili ya mikusanyiko.

Baada ya miaka mingi ya vikwazo vya serikali, katika 1986 tukawa na mkusanyiko wetu wa kwanza wenye kibali cha Serikali, kwenye Kamaraerdő Youth Park, Budapest. Wale wahudhuriaji zaidi ya 4,000 walijawa na machozi ya shangwe walipokuwa wakisalimiana na ndugu zao na dada zao na kusoma ishara ya ukaribishaji kwa mkutano wetu iliyokuwa imeandikwa juu ya malango ya uwanja huo.

Hatimaye, Juni 27, 1989, serikali ilitambua rasmi Mashahidi wa Yehova. Habari hiyo ilitangazwa katika televisheni na redio za Hungaria na kuzusha shangwe za ndugu na dada zetu. Mwaka huo, tulikuwa na mikusanyiko yetu ya kwanza ya wilaya bila vizuizi tangu kazi yetu ipigwe marufuku karibu miaka 40 mapema. Zaidi ya watu 10,000 walihudhuria mkusanyiko huo katika Budapest, na maelfu mengine walikuwa katika mikusanyiko mingine minne nchini. Nilifurahi kama nini kuona ndugu yangu mchanga zaidi, László, na mkewe wakibatizwa Budapest!

Kisha, katika Julai ya 1991, tulipata baraka ambayo hatukupata kuwazia kamwe—mkusanyiko kwenye Népstadion iliyo kubwa katika Budapest, uliohudhuriwa na zaidi ya wajumbe 40,000. Huko nilikuwa na pendeleo la kutafsiri hotuba za washiriki wa wafanyakazi wa makao makuu ya Brooklyn.

Leo, mimi na Anna, pamoja na ndugu zetu na dada zetu wapendwa zaidi ya 40 tunafanya kazi katika ofisi ya tawi iliyo maridadi ya Mashahidi wa Yehova katika kiunga cha Budapest. Hapa, ninatumikia katika Idara ya Tafsiri, pamoja na kikundi kizuri cha vijana, na Anna hushiriki katika kazi za nyumbani hapo.

Japo jitihada zetu za kumfundisha mwana wetu kweli ya Biblia, alipokuwa mkubwa aliikataa. Lakini, sasa anapendelea kweli, na tunatumaini kwamba baadaye atamtumikia Yehova.

Mimi na mke wangu tunashukuru sana kwamba tumepata kweli kuhusu Mungu wetu mwenye upendo, Yehova, nasi tumeweza kumtumikia kwa zaidi ya miaka 40 sasa.—Kama ilivyosimuliwa na Endre Szanyi.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Nikiwa na mke wangu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki