Vita vya Kidini Katika Ufaransa
JUMAPILI, Machi 1, 1562, dyuki wa Guise na ndugu yake Charles, kadinali wa Lorraine—viongozi wawili wa Ukatoliki wa Ufaransa—walikuwa wamepanda farasi pamoja na walinzi wao waliojihami wakielekea Vassy, kijiji kilichokuwa kilometa 200 mashariki ya Paris. Waliamua kusimama kanisani katika Vassy ili kuhudhuria Misa.
Kwa ghafula walisikia mivumo ya nyimbo za dini. Uimbaji huo ulitoka kwa mamia kadhaa ya Waprotestanti waliokuwa wamekusanyika katika ghala ya nafaka ili kuabudu. Wanajeshi waliokuwa wakisindikiza dyuki na ndugu yake waliingia ndani kwa lazima. Katika vurugu lililofuata watu walitukanana na kurushiana mawe. Wanajeshi hao wakafyatua risasi wakiua Waprotestanti 60 na kujeruhi mamia ya wengine.
Ni matukio gani yaliyoongoza kwenye machinjo haya? Itikio la Waprotestanti lilikuwa nini?
Matukio ya Nyuma ya Kihistoria
Katika nusu ya kwanza ya karne ya 16, Ufaransa ilikuwa na ufanisi na vilevile idadi kubwa ya watu. Ufanisi huu wa kiuchumi na wa idadi ya watu uliandamana na jitihada za kuzoea Ukatoliki wa kiroho na wa namna ya kidugu zaidi. Watu walitaka kanisa ambalo halingekuwa tajiri sana lakini lenye sifa nyingi za kimungu. Baadhi ya makasisi na vilevile wahuishaji wa kiusomi wa mvuvumko walidai marekebisho ya kidini yafanywe ili kupambana na matendo mabaya yaliyokuwa yakifanywa na maaskofu wa ngazi za juu na kutostahili kwa makasisi wa chini. Kasisi mmoja ambaye alijitahidia urekebishaji alikuwa askofu Mkatoliki Guillaume Briçonnet.
Katika dayosisi yake ya Meaux, Briçonnet alitia moyo wote wasome Maandiko. Hata aligharimia kutafsiriwa kwa Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo katika Kifaransa. Muda si muda hasira ya Chuo Kikuu cha Theolojia cha Sorbonne katika Paris, ambacho kilikuwa mlinzi wa uothodoksi wa Katoliki, ilielekezwa kwake, hilo likizuia jitihada zake. Lakini askofu huyo alikuwa na ulinzi wa Francis wa 1, mfalme wa Ufaransa kutoka 1515 hadi 1547. Wakati huo, mfalme huyo alipendelea marekebisho.
Hata hivyo, Francis wa 1, alivumilia uchambuzi wa kanisa mradi tu uchambuzi huo haukutisha utengamano wa umma na muungano wa kitaifa. Katika 1534, Waprotestanti wenye siasa kali walibandika makaratasi ambayo yalishutumu Misa ya Kikatoliki kuwa ibada ya sanamu, hata wakabandika karatasi moja kwenye mlango wa chumba cha kulala cha mfalme. Tokeo ni kwamba, Francis wa 1 alibadili maoni yake na kuanzisha kampeni kali ya ukandamizaji.
Ukandamizaji Mkatili
Muda si muda Waprotestanti walikuwa wakichomwa kwenye miti ya mateso. Wahuishaji wa mvuvumko, waliowasikitikia, na wafuasi wa Uprotestanti uliokuwa mpya walitoroka nchi. Mamlaka zikaanza kuchuja yaliyoandikwa katika vitabu na kudhibiti walimu, wachapishaji, na wapigaji chapa.
Wawaldensi walipata mshindo kamili wa upinzani rasmi. Wao walikuwa kikundi cha watu wachache waliokaza fikira kwenye Biblia ambao waliishi katika vijiji maskini kusini-mashariki mwa nchi hiyo. Wengine walichomwa kwenye miti ya mateso, mamia yakachinjwa, na vijiji 20 hivi vikaangamizwa.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 6.
Likijua juu ya uhitaji wa marekebisho ndani ya kanisa, baraza la maaskofu Wakatoliki lilikutana katika Desemba 1545, katika Trent, Italia. Baraza hilo lilipofikia mwisho walo katika 1563, kulingana na The Cambridge Modern History, “athari yalo ya ujumla . . . ilikuwa kuimarisha mikono ya wale walioazimia kung’oa Uprotestanti.”
Matukio ya Kabla ya Vita
Wakiwa wamechoka kungojea marekebisho, washiriki wengi wa harakati ya marekebisho ndani ya Kanisa Katoliki waliunga mkono Uprotestanti. Kufikia 1560 hivi, wakuu wengi Wafaransa na waungaji mkono wao walijiunga na Wahuguenoti, kama Waprotestanti walivyokuja kuitwa. Wahuguenoti hao waliendelea kujieleza kwa uhuru sana. Mikutano yao ya hadharani nyakati fulani ilikuwa chanzo cha uchokozi na upinzani wenye nguvu. Kwa kielelezo, katika 1558, maelfu yao walikusanyika Paris kwa siku nne mfululizo ili kuimba zaburi.
Yote haya yalikasirisha viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki na vilevile watu wa kawaida. Kwa kuchochewa na Kadinali Charles wa Lorraine, Mfalme Henry wa 2, ambaye alikuwa mwandamizi wa baba yake, Francis wa 1, alitangaza Amri ya Écouen, katika Juni 1559. Kusudi layo lililotangazwa waziwazi lilikuwa kuondosha “watu ovyo wenye sifa mbaya wa Dini ya Lutheri.” Hilo liliongoza kwenye kampeni ya ogofyo katika Paris dhidi ya Wahuguenoti.
Henry wa 2 alikufa majuma machache baadaye kutokana na majeraha aliyopata katika mchezo wa vita. Mwana wake, Mfalme Francis wa 2, akichochewa na familia ya Guise, alianzisha upya amri hiyo ambayo iliweka adhabu ya kifo kwa Waprotestanti shupavu. Mwaka uliofuata Francis wa 2 alikufa, na mamaye, Catherine de Médicis, alitawala mahali pa ndugu ya Francis wa 2, Charles wa 9 mwenye umri wa miaka kumi. Sera ya Catherine ya upatanishaji haikupendwa na familia ya Guise, ambayo ilikuwa imeazimia kung’oa Uprotestanti.
Katika 1561, Catherine alipanga semina katika Poissy, karibu na Paris, ambapo wanatheolojia Wakatoliki na Waprotestanti walikutana. Katika amri iliyotolewa katika Januari 1562, Catherine aliwapa Waprotestanti uhuru wa kukusanyika kwa ajili ya ibada nje ya majiji. Wakatoliki walikasirika wee! Hilo liliongoza kwenye jambo lililotukia miezi miwili baadaye—machinjo ya Waprotestanti kwenye ghala ya nafaka katika kijiji cha Vassy, kama ilivyofafanuliwa mapema.
Vita Vitatu vya Kwanza
Machinjo yaliyotokea Vassy yalianzisha kwa kishindo ya kwanza katika mfululizo wa vita vinane vya kidini ambavyo vilitumbukiza Ufaransa katika ogofyo la kuuana kutoka 1562 hadi katikati mwa miaka ya 1590. Ingawa masuala ya kisiasa na kijamii yalihusika pia, umwagikaji huo wa damu ulichochewa hasa na dini.
Baada ya Pigano la Dreux katika Desemba 1562, ambalo katika hilo watu 6,000 walikufa, vita hivyo vya kwanza vya kidini vilikoma. Amani ya Amboise, iliyotiwa sahihi katika Machi 1563, iliwapa wakuu Wahuguenoti uhuru wenye mipaka wa kuabudu katika mahali fulani-fulani.
“Vita vya pili vilitokea ghafula kwa sababu Wahuguenoti walihofu kwamba Wakatoliki walikuwa na njama ya kimataifa,” yasema The New Encyclopædia Britannica. Kwa wakati huo, mahakimu Wakatoliki kwa kawaida walikuwa wakitoa amri za kunyongwa kwa wananchi kwa sababu tu ya kuwa Wahuguenoti. Katika 1567 jaribio la Mhuguenoti mmoja kumkamata Mfalme Charles wa 9 na mama yake, Catherine, lilianzisha vita vya pili.
Baada ya kueleza pigano lenye umwagikaji wa damu kwelikweli katika St.-Denis, nje ya Paris, wanahistoria Will na Ariel Durant waliandika hivi: “Ufaransa tena ikashangaa ni dini gani hii iliyokuwa ikifanya watu wachinje.” Muda mfupi baada ya hapo, katika Machi 1568, Amani ya Longjumeau iliwapa Wahuguenoti uvumilivu wa kiasi ambao walikuwa wamekuwa nao mbeleni chini ya Amani ya Amboise.
Hata hivyo, Wakatoliki walikasirika na kukataa kutekeleza masharti ya amani hiyo. Hivyo, katika Septemba 1568, vita vya tatu vya kidini vikatokea. Mkataba uliofuata wa amani uliwapa Wahuguenoti ukubali mkubwa hata zaidi. Wakapewa miji iliyozingirwa na ngome, kutia ndani bandari ya La Rochelle. Pia, mkuu mwenye kustahiwa Mprotestanti, Admiral de Coligny, akawekwa rasmi kuwa mshauri wa mfalme. Tena Wakatoliki wakakasirika.
Machinjo ya Siku ya “Mtakatifu” Batholomayo
Mwaka mmoja hivi baadaye, Agosti 22, 1572, Coligny alinusurika shambulio la kuuawa katika Paris ambalo lilitokea wakati alipokuwa akitembea kutoka Louvre Palace kuelekea nyumbani kwake. Wakiwa wameghadhibika, Waprotestanti walitisha kuchukua hatua kali ili kujilipiza ikiwa haki haikutekelezwa haraka. Katika mkutano wa faragha, Mfalme kijana Charles wa 9, mama yake Catherine de Médicis, na wakuu kadhaa waliamua kumwua Coligny. Ili kuepuka kisasi, waliamuru pia kifo cha Waprotestanti wote waliokuwa wamekuja Paris ili kuhudhuria arusi ya Henry wa Navarre Mprotestanti na binti ya Catherine Margaret wa Valois.
Kwenye usiku wa Agosti 24, kengele za kanisa la Saint-Germain-l’Auxerrois, lililoelekeana na Louvre, zilitoa ishara ya machinjo kuanza. Dyuki wa Guise na wanaume wake walikimbia kwenye jengo ambamo Coligny alikuwa amelala. Humo Coligny aliuawa na kutupwa kutoka dirishani, na maiti yake kukatwakatwa. Dyuki Mkatoliki akaeneza neno: “Waueni wote. Ni amri ya mfalme.”
Kutoka Agosti 24 hadi 29, mandhari za kuogofya ziliharibu barabara za Paris. Wengine walidai kwamba mto Siene ulitiririka ukiwa mwekundu kwa damu ya maelfu ya Wahuguenoti waliochinjwa. Miji mingine ilijionea umwagikaji wayo yenyewe wa damu. Makadirio ya idadi ya waliokufa hutofautiana kutoka 10,000 hadi 100,000; hata hivyo, wengi hukubali tarakimu ya angalau 30,000.
“Jambo moja hakika, lililo baya sana kama machinjo yenyewe,” akaripoti mwanahistoria mmoja, “lilikuwa kushangilia ambako machinjo hayo yalitokeza.” Baada ya kusikia juu ya machinjo hayo, Papa Gregory wa 13 aliamuru kuwe na sherehe ya kutoa shukrani na kupeleka pongezi zake kwa Catherine de Médicis. Yeye pia aliamuru medali ya kipekee ifanyizwe ili kukumbuka machinjo hayo ya Wahuguenoti na akaamuru kuchorwa kwa picha ya machinjo hayo, ikiwa na maneno: “Papa aunga mkono mauaji ya Coligny.”
Yaripotiwa kwamba baada ya machinjo hayo, Charles wa 9 alipata maono ya wahasiriwa wake na alikuwa akimlilia mtunzi wake: “Nimefuata shauri ovu jinsi gani! Ee Mungu wangu, nisamehe!” Alikufa katika 1574 akiwa na umri wa miaka 23 na ndugu yake Henry wa 3 akawa mwandamizi wake.
Vita vya Kidini Vyaendelezwa
Kwa wakati huohuo, Wakatoliki walichochewa na viongozi wao dhidi ya Wahuguenoti. Katika Toulouse, makasisi Wakatoliki walihimiza sana wafuasi wao: “Waueni wote, waporeni; sisi ni baba zenu. Tutawalinda.” Kwa kutumia ukandamizaji wenye jeuri, mfalme, bunge, magavana, na wakuu waliweka kielelezo, na Wakatoliki wa kawaida wakafuata.
Hata hivyo, Wahuguenoti walilipiza kisasi. Kwa kipindi cha miezi miwili baada ya machinjo ya Siku ya “Mtakatifu” Batholomayo, walianza vita vya kidini vya nne. Mahali ambapo walikuwa wengi kushinda Wakatoliki, waliharibu sanamu, visalaba, na madhabahu katika makanisa ya Katoliki, na hata kuua. “Mungu hataki wala miji wala watu waachwe,” akatangaza John Calvin, kiongozi wa Uprotestanti wa Ufaransa, katika kijitabu chake Declaration to Maintain the True Faith.
Vita vingine vinne vya kidini vilifuata. Vya tano vilikwisha katika 1576 kwa Mfalme Henry wa 3 kutia sahihi mkataba wa amani ambao uliwapa Wahuguenoti uhuru kamili wa ibada kotekote katika Ufaransa. Jiji la Paris lililojaa Wakatoliki liliasi hatimaye na kumwondosha Henry wa 3, aliyefikiriwa kuwa mwenye huruma sana kuelekea Wahuguenoti. Wakatoliki hao walianzisha serikali ya upinzani, Shirikisho Takatifu, la Katoliki lililoongozwa na Henry wa Guise.
Mwishowe, katika vita vya nane, au Vita vya Henry Watatu, Henry wa 3 (Mkatoliki) alifanyiza muungano na mwandamizi wake wa wakati ujao, Henry wa Navarre (Mprotestanti), dhidi ya Henry wa Guise (Mkatoliki). Henry wa 3 akafaulu kufanya Henry wa Guise auawe, lakini katika Agosti 1589, Henry wa 3 mwenyewe aliuawa na mtawa wa kiume Mdominika. Hivyo, Henry wa Navarre, ambaye hakuuawa miaka 17 mapema wakati wa machinjo ya Siku ya “Mtakatifu” Batholomayo, akawa Mfalme Henry wa 4.
Kwa kuwa Henry wa 4 alikuwa Mhuguenoti, Paris lilikataa kujitiisha kwake. Shirikisho Takatifu la Katoliki lilipanga upinzani wenye kutumia silaha kotekote nchini. Henry alishinda mapigano kadhaa, lakini wakati jeshi la Hispania lilipofika ili kuwategemeza Wakatoliki, mwishowe aliamua kuukana Uprotestanti na kukubali imani ya Katoliki. Akivikwa taji Februari 27, 1594, Henry aliingia Paris, ambapo watu, wakiwa wamechoshwa kabisa na vita, walimshangilia kuwa mfalme.
Basi hivyo Vita vya Ufaransa vya Kidini vikakoma baada ya zaidi ya miaka 30 ambayo katika hiyo Wakatoliki na Waprotestanti walichinjana pindi kwa pindi. Aprili 13, 1598, Henry wa 4 alitoa Amri ya maana sana ya Nantes, ambayo iliamuru uhuru wa dhamiri na ibada kwa Waprotestanti. Kulingana na papa, amri hiyo ilikuwa “jambo baya kupita yote yaliyoweza kuwazika kwa sababu ilipatia kila mtu uhuru wa dhamiri, jambo ambalo lilikuwa baya sana ulimwenguni.”
Kotekote Ufaransa Wakatoliki walihisi kwamba amri hiyo ilikuwa usaliti wa ahadi ya Henry ya kuunga mkono dini yao. Kanisa halikutulia hadi, karibu karne moja baadaye, Louis wa 14 alipotangua Amri ya Nantes, akianzisha mnyanyaso mbaya hata zaidi wa Wahuguenoti.
Matokeo ya Vita Hivyo
Kufikia mwishoni mwa karne ya 16, ufanisi wa Ufaransa ulikuwa umetoweka. Nusu ya ufalme huo ilikuwa imezingirwa, kutekwa, kukombolewa, au kuharibiwa. Wanajeshi walifanyia watu madai ya kupita kiasi, jambo ambalo liliongoza kwenye uasi wa wakulima. Waprotestanti, wakiwa wamepunguzwa na adhabu za kifo, machinjo, kufukuzwa kutoka nchini, na ukanaji, waliingia karne ya 17 wakiwa wachache sana.
Kwa wazi, Wakatoliki walikuwa wameshinda Vita vya Kidini vya Ufaransa. Lakini je, Mungu alibariki ushindi wao. Bila shaka sivyo. Wakiwa wamechoshwa na mauaji haya yote yaliyofanywa katika jina la Mungu, Wafaransa wengi wakaja kutoamini dini. Walikuwa watangulizi wa kile ambacho kimeitwa mwelekeo ulio dhidi ya Ukristo wa karne ya 18.
[Blabu katika ukurasa wa 9]
“Mungu hataki wala miji wala watu waachwe.” Akatangaza kiongozi wa Uprotestanti wa Ufaransa
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Wawaldense Walisimama Imara—Kukiwa na Tokeo Gani?
PIERRE VALDES, au Peter Waldo, alikuwa mfanya-biashara tajiri katika Ufaransa ya karne ya 12. Katika wakati huo ambapo Kanisa Katoliki la Kiroma lilizuia kimakusudi watu kujua Biblia, Waldo aligharimia kutafsiriwa kwa Gospeli na vitabu vingine vya Biblia katika lugha za kawaida za watu wa kusini-mashariki mwa Ufaransa. Kisha akaacha biashara yake na kujitoa kuhubiri Gospeli. Muda si muda wengi walijiunga naye, na katika 1184 yeye na washirika wake walitengwa na ushirika na Papa Lucius wa 3.
Baada ya muda, vikundi hivi vya wahubiri wenye kuelekezea Biblia fikira vikaja kuitwa Wawaldense. Wao walitetea kurudia itikadi na mazoea ya Ukristo wa mapema. Walikataa mazoea na itikadi za kidesturi za Kikatoliki, kutia ndani kuondolewa kwa adhabu ya purgatori, sala kwa wafu, purgatori, ibada ya Maria, kusali kwa “watakatifu,” kubatiza vitoto vichanga, kuheshimu kisalaba, na badiliko la kimuujiza. Likiwa tokeo, Wawaldense mara nyingi waliteseka sana mikononi mwa Kanisa Katoliki. Mwanahistoria Will Durant afafanua hali hiyo wakati Mfalme Francis wa 1 alipoanzisha kampeni dhidi ya watu wasio Wakatoliki:
“Kadinali de Tournon, akidai kwamba Wawaldense walikuwa na njama ya kupindua serikali, alimshawishi Mfalme mgonjwa mwenye kusitasita atie sahihi agizo (Januari 1, 1545) kwamba Wawaldense wote waliopatikana na hatia ya kuasi mafundisho ya kidini wauawe. . . . Kwa kipindi cha juma moja (Aprili 12-18) vijiji kadhaa viliteketezwa kabisa; katika kimoja wanaume, wanawake, na watoto 800 walichinjwa; katika miezi miwili 3,000 waliuawa, vijiji 22 kuteketezwa, na wanaume 700 wakapelekwa kwenye merikebu za kwenda vitani. Wanawake 25 waliopigwa na hofu, wakitafuta kimbilio uvunguni mwa ardhi, walisongwa pumzi kwa kukosa oksijeni kwa sababu ya moto uliowashwa kwenye kiingilio.”
Kuhusu matukio kama hayo ya kihistoria, Durant alisema hivi: “Minyanyaso hii ndiyo iliyokuwa kutofaulu kabisa kwa utawala wa akina Francis.” Lakini hilo lilikuwa na matokeo gani kwa wale waliotazama uthabiti wa Wawaldense wakati wa minyanyaso iliyoamriwa na mfalme? Durant aliandika: “Moyo mkuu wa wafia-imani hao ulipatia mwendo wao adhama na fahari; ni lazima maelfu ya watazamaji yalipendezwa na kusumbuliwa, ambayo bila hukumu hizo zenye kutazamisha, huenda hayangeshughulika kamwe kubadili imani yao iliyorithiwa.”
[Picha katika ukurasa wa 5]
Machinjo katika Vassy yalianzisha kwa kishindo vita vya kidini
[Hisani]
Bibliothèque Nationale, Paris
[Picha katika ukurasa wa 7]
Machinjo ya Siku ya “Mtakatifu” Batholomayo, wakati ambapo maelfu ya Waprotestanti walichinjwa na Wakatoliki
[Hisani]
Photo Musée cantonal des Beaux-Arts, Lausanne
[Picha katika ukurasa wa 8]
Waprotestanti waliua Wakatoliki na kuharibu mali za kanisa (juu na chini)
[Hisani]
Bibliothèque Nationale, Paris
Bibliothèque Nationale, Paris