Amri ya Nantes—Je, Ilikuwa Mkataba wa Uvumiliano?
“JAMBO hili laniumiza sana,” akateta Papa Clement wa Nane, mwaka wa 1598, aliposikia kwamba mfalme wa Ufaransa, Henry wa Nne alitia sahihi Amri ya Nantes. Miaka 400 baadaye, badala ya amri hiyo kuchukiwa na kupingwa, inaadhimishwa kuwa tendo la uvumiliano na mojawapo ya hatua muhimu ya kuhakikisha kwamba wote wana haki za kidini. Amri ya Nantes ilikuwa nini? Je, kweli ilikuwa mkataba wa uvumiliano? Nayo yaweza kutufunza nini leo?
Ulaya Uliokumbwa na Vita
Ulaya wa karne ya 16 ulijaa kutovumiliana na vita vikali vya kidini. “Kabla ya karne ya 16, fundisho la Kristo, ‘Mwe na upendo nyinyi kwa nyinyi,’ halikuwa limepata kudharauliwa kwa kiasi hicho na wafuasi wake,” asema mwanahistoria fulani. Nchi fulani, kama vile Hispania na Uingereza, ziliwawinda kikatili wafuasi wa dini ndogondogo. Nchi nyinginezo, kama Ujerumani, ilifuata kanuni ya “Cuius regio, eius religio,” yaani mtawala wa eneo ndiye aamuaye dini ya eneo hilo. Mtu yeyote ambaye hakukubaliana na chaguo la dini la mtawala alilazimishwa kuhama. Vita viliepushwa kwa kutenga dini, bila jitihada yoyote ya kufanya watu wa dini tofauti wakae pamoja.
Ufaransa ilichukua hatua tofauti. Ufaransa ipo kati ya Ulaya kaskazini, ambayo ilikuwa na Waprotestanti wengi, na Ulaya kusini, ambayo ilikuwa ya Katoliki. Kufikia katikati ya miaka ya 1500, Waprotestanti walikuwa dini ndogo iliyotambulika katika nchi hii ya Katoliki. Vita kadhaa vya kidini vikazidisha tofauti kati ya dini hizo.a Mikataba mingi, au ‘Amri za Kupunguza Matatizo,’ kama ilivyoitwa, ilishindwa kuwafanya watu wa dini tofauti waishi pamoja kwa amani. Kwa nini Ufaransa iliamua kufuatia uvumiliano badala ya kuiga majirani wake wa Ulaya?
Siasa za Amani
Jambo la kwamba amani na mvurugo wa kidini si kwamba hazikuwa zikipatana lilisitawi japo kuenea kwa kutovumiliana. Kwa ujumla, wakati huo suala la imani la kidini halikutofautishwa na utii kwa serikali. Je, iliwezekana mtu awe Mfaransa na asiwe mfuasi wa Kanisa Katoliki? Inaonekana wengine walifikiri hivyo. Mnamo 1562, Michel de l’Hospital, mkuu mmoja wa serikali ya Ufaransa, aliandika: “Hata mtu ambaye ametengwa na ushirika hakomi kuwa mwananchi.” Kikundi cha Katoliki kilichoitwa Les Politiques (Kikundi cha Kisiasa) pia kilisema hivyo.
Mikataba ya amani ambayo haikufaulu na ambayo ilitiwa sahihi nchini Ufaransa ilihifadhi baadhi ya mawazo hayo mapya. Pia iliendeleza wazo la kwamba kusahau yaliyopita ni njia ya kuganga yajayo. Kwa mfano, Amri ya Boulogne, ya mwaka wa 1573, ilisema: “Mambo yote yaliyotendeka . . . na yasahauliwe kabisa kana kwamba hayakutendeka.”
Ufaransa ikawa na mengi ya kusahau. Kabla ya Henry wa Nne kuwa mfalme mwaka wa 1589, mkataba wa amani uliopata kudumu zaidi ulikuwa umekuwapo kwa miaka minane tu. Ufaransa ilikuwa na matatizo ya kiuchumi na kijamii. Nchi hiyo ilihitaji sana kuwa thabiti. Henry wa Nne alifahamu dini na siasa. Yeye alikuwa amehama-hama kati ya Uprotestanti na Ukatoliki. Baada ya kuweka amani na Wahispania mwaka wa 1597 na hatimaye kutuliza maasi yaliyotokea nchini mwaka wa 1598, akawa katika hali ya kuweza kuweka mkataba wa amani baina ya Waprotestanti na Wakatoliki. Mnamo mwaka wa 1598, baada ya Ufaransa kukumbwa na vita vya kidini kwa zaidi ya miaka 30, Mfalme Henry wa Nne alitia sahihi Amri ya Nantes.
“Sheria ya Haki za Kibinadamu ya Kifaransa”
Amri ya Nantes ambayo Henry alitia sahihi ilikuwa na sehemu nne za msingi, kutia ndani sehemu kuu yenye mafungu 92 au 95 na mafungu 56 ya siri yanayotaja haki na wajibu wa Waprotestanti. Mikataba ya amani ya awali ilikuwa msingi wa mapatano hayo, ikichangia thuluthi mbili za mafungu hayo. Lakini, tofauti na mikataba ya awali, ilichukua muda mrefu kutayarisha amri hiyo. Ni ndefu sana kwa sababu ilishughulikia tatizo mojamoja, ikifanana na hati ya kujitekelezea mambo. Amri hiyo ilitaja baadhi ya haki zipi?
Amri hiyo iliwapa Waprotestanti wa Ufaransa uhuru kamili wa dhamiri. Pia walipewa hadhi ya kuwa wafuasi wa dini ndogo walio na haki na mapendeleo. Mojawapo ya mafungu ya siri hata liliwahakikishia kwamba wamelindwa dhidi ya Baraza la Kuhukumu Wazushi wanaposafiri ng’ambo. Na zaidi, Waprotestanti walipewa haki sawa za kiraia na Wakatoliki na wangeweza kuajiriwa na Serikali. Lakini, je, amri hiyo ilikuwa mkataba wa uvumiliano?
Amri Hiyo Ilikuwa Yenye Uvumiliano kwa Kadiri Gani?
Kwa kufikiria jinsi watu wa dini ndogondogo walivyotendwa katika nchi nyinginezo, Amri ya Nantes ikawa “hati yenye hekima ya kisiasa isiyopatikana kwa urahisi,” asema mwanahistoria Elisabeth Labrousse. Henry alikuwa na tamaa kubwa ya kuona Waprotestanti wakirudia Ukatoliki. Wakati uo huo, ilikubaliwa kwamba watu wa dini tofauti waishi pamoja—njia ya pekee ambayo “raia wetu wote waweza kuomba na kuabudu Mungu,” akasema Henry.
Kwa kweli, amri hiyo ilipendelea Ukatoliki, ambao ulitangazwa kuwa dini kuu na ulikuwa ufuatwe katika ufalme wote. Waprotestanti walilazimika kuwalipa zaka Wakatoliki na kuheshimu sikukuu za Kikatoliki na makatazo kuhusu ndoa. Uhuru wa ibada wa Waprotestanti ulitumika katika maeneo fulani tu. Amri hiyo ilishughulikia tu kuishi pamoja kwa Waprotestanti na Wakatoliki. Dini nyingine ndogondogo hazikuhusishwa. Kwa mfano, Waislamu walifukuzwa Ufaransa mwaka wa 1610. Japo maoni yake yasiyo kamili ya uvumiliano, kwa nini amri hiyo inafurahiwa leo?
Matokeo Muhimu
Hati za wakati huo hazikutaja sana amri hiyo. Wanahistoria wanasema amri hiyo “haikuridhisha.” Lakini, sasa inaonwa kuwa hati bora ya kusuluhisha mambo ya kisiasa. Amri hiyo ilisema Uprotestanti ni dini, wala si uzushi. Kutambua dini nyingine mbali na Ukatoliki kulifanya kuwezekane kuwe na dini nyingi. Kulingana na mwanahistoria mmoja, jambo hili “liliondoa uvutano mkubwa wa ushupavu wa Wafaransa ulioonyeshwa na Waprotestanti na vilevile Wakatoliki.” Amri hiyo ilitambua kwamba dini haikuwa jambo kuu linaloamua uaminifu kwa Serikali au kuwa raia wa taifa. Kwa kuongezea, uhalifu, wala si kuwa mfuasi wa dini fulani, ukawa ndilo jambo la kutokeza hatua ya kisheria. Mawazo hayo yakaonyesha hata mabadiliko makubwa zaidi.
Mfalme Henry alitia sahihi amri hiyo kwa sababu alihangaikia hasa umoja wa raia. Ili kuhakikisha jambo hilo, amri hiyo ilitenganisha umoja wa raia kutokana na umoja wa kidini. “Ilianzisha hatua ya kuondoa mambo ya kidini . . . , kutambua kwamba taifa na dini si kitu kimoja tena,” asema mwanahistoria mmoja. Ingawa Kanisa Katoliki liliendelea kuwa na uwezo wa kadiri fulani, Serikali iliongezewa uwezo zaidi. Maliki angekuwa mpatanishi wakati wa mizozo. Kusuluhishwa kisiasa au kisheria kwa matatizo ya kidini kulimaanisha kwamba siasa ilidhibiti dini. Hiyo ndiyo sababu mwanahistoria mmoja alisema kwamba amri hiyo ni “ushindi wa uwezo wa siasa dhidi ya daraka la Kanisa.” Mwingine naye asema kwamba “hiyo ilikuwa hatua muhimu ya kuibuka kwa Taifa la kisasa.”
Jinsi Ihusuvyo Leo
Baadhi ya mambo yaliyotajwa na Amri ya Nantes baadaye yalitumiwa na serikali nyinginezo. Baadaye, nchi nyingi zikafafanua upya uhusiano baina ya dini na siasa, zikiipa Serikali mamlaka zaidi. Nchini Ufaransa jambo ambalo hatimaye liliamuliwa (mwaka wa 1905) ni kutenganisha kabisa Kanisa na Serikali. Kulingana na Jean Baubérot, profesa mashuhuri wa historia na sosholojia, mpango huu ni “ulinzi bora wa dini ndogondogo” katika mazingira yanayozidi kukosa uvumiliano. Ingawa nchi nyinginezo zashikilia dini ya Serikali, zimeamua kuhakikisha katika katiba zao zote kwamba kuna uhuru wa kidini na kwamba dini zote zinatendewa kwa njia sawa.
Lakini, wengi leo wafikiri kwamba bado maendeleo yanaweza kufanywa katika kulinda uhuru wa kidini. “Amri ya Nantes huadhimishwa mara moja katika karne na kukiukwa muda wote mwingine,” akaomboleza mwandishi wa habari Alain Duhamel. Kwa mfano, wafafanuzi fulani wenye ujuzi hutaja ukosefu wa kuvumilia wengine na hali ya kujiamulia kubandika dini zote ndogondogo kuwa “madhehebu.” Kujifunza kuishi pamoja kwa amani na bila chuki kwa kweli kulikuwa funzo muhimu miaka 400 iliyopita. Lakini funzo hilo lingali latumika leo.
Masuala ya Kubishaniwa
Hakuna uhuru wa ibada wakati wenye mamlaka wajiamuliapo wenyewe kupendelea dini nyingine zaidi ya dini nyingine. Nchini Ufaransa, baadhi ya wenye mamlaka hutambua Mashahidi wa Yehova kuwa dini ilhali wengine hawawatambui. Kwa kushangaza, Serikali ambayo haihusiki na dini inafafanua dini ni nini na dini si nini. Utaratibu huo huanza na ubaguzi na kutokeza mnyanyaso. Isitoshe, “unaweza kuweka mfano wa kufuatwa na nchi nyinginezo na mashirika mengineyo ya kidini,” asema Raimo Ilaskivi, ambaye ni mbunge wa Bunge la Ulaya. Hiyo ndiyo sababu mhadhiri wa sheria Jean-Marc Florand amalizia kwa kusema: “Ni pigo baya kwa Ufaransa na kutekelezwa kwa uhuru. Nikiwa Mkatoliki, nahangaishwa na jambo hilo.” Hata hivyo, historia inaweza kuwafunza wale ambao wako tayari kujifunza.
Kwenye mkutano mmoja wa karibuni wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni, msemaji mmoja alibisha kwamba “njia mojawapo ya kusherehekea Amri ya Nantes ni kufikiria hali ya dini katika wakati wetu.” Kwa kweli, Amri ya Nantes inaweza kuadhimishwa kwa njia bora zaidi kwa kuhakikisha kwamba uhuru wa kweli wa ibada kwa wote umelindwa!
[Maelezo ya Chini]
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20, 21]
Uhuru wa Kidini Nchini Ufaransa Leo
Nyakati nyingine mafunzo ya wakati uliopita husahauliwa. Akitetea Amri ya Nantes, Henry wa Nne alitangaza: “Hakupaswi kuwa tena na ubaguzi baina ya Mkatoliki na Mhuguenoti.” Jean-Marc Florand, mhadhiri mkuu wa sheria kwenye Chuo Kikuu cha Paris-XII, aeleza katika gazeti la Ufaransa Le Figaro kwamba nchini Ufaransa, tangu 1905, “sheria inaweka dini zote, itikadi zote, na madhehebu yote katika kiwango kimoja.” Ubaguzi na chuki zapaswa kuwa mambo yaliyopita.
Kwa kushangaza, mwaka wa 1998, mwaka wa kuadhimisha karne ya nne ya Amri ya Nantes, funzo lake—kwamba raia wote wahakikishiwe uhuru wa kidini na usawa—yamkini limesahauliwa. Mashahidi wa Yehova, ambao ni jumuiya ya tatu kwa ukubwa kati ya jumuiya za kidini za Kikristo nchini Ufaransa, wamefuata dini yao kwa karibu miaka mia moja huko. Lakini, ripoti ya bunge la Ufaransa ilikataa ikisema kwamba Mashahidi wa Yehova si dini halali. Matokeo yakawa kwamba baadhi ya mamlaka nchini Ufaransa mara nyingi hubagua Mashahidi wa Yehova katika masuala ya haki zao. Kwa mfano, katika mizozo ya malezi ya watoto, mara nyingi mahakimu nchini Ufaransa hutilia shaka kama wazazi ambao ni Mashahidi wa Yehova wapaswa kupewa haki ya kulea watoto wao. Maswali hayo huzushwa tu eti kwa sababu ya dini ya wazazi. Na vilevile, kwa sababu ya kuwa Mashahidi wa Yehova, wazazi fulani walezi wanazidi kuwa katika hatari ya kupoteza watoto ambao wanatunza.
Hivi karibuni, wenye mamlaka nchini Ufaransa wamekuwa wakitisha kutoza kodi michango ambayo Mashahidi wa Yehova wanatolea makutaniko yao. Kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Haki za Kibinadamu Zisizo na Mipaka, huo ni “mwendo hatari” ambao unakiuka maazimio yaliyopitishwa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Kwa kweli, Muungano wa Ulaya unahakikisha uhuru wa kidini. Mashahidi wa Yehova wametambuliwa mara kwa mara na Mahakama ya Ulaya kuwa “dini inayojulikana,” jambo linalofanya hata iwe vigumu zaidi kuelewa hatua iliyochukuliwa na mamlaka fulani za Ufaransa.
Mashahidi wa Yehova wamekuwa watendaji nchini Ufaransa kwa karibu miaka mia moja
Juu kulia: Familia nyingi nchini Ufaransa zimekuwa Mashahidi wa Yehova kwa vizazi kadhaa
Juu kushoto: Kutaniko la Roubaix, 1913
Chini kushoto: Mashahidi katika kaskazini mwa Ufaransa, 1922
[Picha katika ukurasa wa 19]
Henry wa Nne, mfalme wa Ufaransa
[Hisani]
© Cliché Bibliothèque Nationale de France, Paris