Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 1/8 kur. 6-9
  • Uhuru wa Kidini—Je, Ni Baraka au Laana?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uhuru wa Kidini—Je, Ni Baraka au Laana?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mwanzo Wenye Maumivu wa Uvumiliano
  • Uhuru wa Kiasi
  • Tisho kwa Uhuru wa Kidini
  • “Raia Wenye Mifano Mizuri”—Washutumiwa Kuwa “Hatari”
  • Umaana wa Kutopendelea
  • Uhuru wa Kidini Wamaanisha Nini Kwako?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Kutovumiliana kwa Kidini Leo
    Amkeni!—1999
  • Watu Huru Lakini Wanaotakwa Watoe Hesabu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Usikose Kusudi la Uhuru wa Kupewa na Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 1/8 kur. 6-9

Uhuru wa Kidini—Je, Ni Baraka au Laana?

Mwanzo wa wazo la uhuru wa kidini uliambatana na uchungu wa uzazi katika Jumuiya ya Wakristo. Ulikuwa ni pambano dhidi ya kulazimisha kauli, ubaguzi, na kutovumiliana. Ulisababisha kupotezwa kwa maisha ya maelfu yasiyohesabika katika mapambano ya kidini yenye umwagikaji mwingi wa damu. Historia hii yenye kuhuzunisha hutufundisha nini?

“MNYANYASO umekuwa jambo linaloendelea la historia ya Kikristo,” aandika Robin Lane Fox katika kitabu Pagans and Christians. Wakristo wa mapema waliitwa farakano na walilaumiwa kuwa walitisha utengamano. (Matendo 16:20, 21; 24:5, 14; 28:22) Tokeo lilikuwa kwamba, wengine walivumilia mateso na kuuawa na hayawani-mwitu katika nyanja za michezo za Roma. Kwa kuona mnyanyaso huo mkali, wengine, kama vile mwanatheolojia Tertullian (ona picha katika ukurasa wa 8), waliomba kuwepo uhuru wa kidini. Mwaka wa 212 W.K., aliandika hivi: “Ni haki ya kibinadamu ya msingi, pendeleo la asili, kwamba kila mtu apaswa kuabudu kulingana na masadikisho yake.”

Mnamo 313 W.K., mnyanyaso dhidi ya Wakristo uliofanywa na mamlaka ya Roma ulifikia kikomo chini ya utawala wa Konstantino, kwa kutolewa kwa Amri ya Milan, ambayo ilitoa uhuru wa kidini kwa Wakristo na wapagani vilevile. Kuhalalishwa kwa “Ukristo” katika Milki ya Roma kulikomesha wimbi la mnyanyaso dhidi ya Wakristo. Hata hivyo, karibu mwaka wa 340 W.K., mwandishi aliyedai kuwa Mkristo alitoa mwito wapagani wanyanyaswe. Hatimaye, mwaka wa 392 W.K., kupitia kwa Amri ya Constantinople, Maliki Theodosius wa Kwanza alipiga marufuku upagani katika milki hiyo, na uhuru wa kidini ukakoma kabla haujasitawi. “Ukristo” wa Kiroma ukiwa dini ya Serikali, Kanisa na Serikali zilianzisha kampeni ya mnyanyaso ambayo iliendelea kwa karne kadhaa, ikifikia upeo wake katika Krusedi zenye umwagikaji wa damu za karne ya 11 hadi ya 13 na katika ukatili wa Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi, yaliyoanza katika karne ya 12. Wale waliothubutu kutilia shaka imani iliyothibitishwa, kuwapo pekee kwa fundisho hilo, waliitwa wazushi na kusakwa katika mazingira ya uonevu ya wakati huo. Ni nini kilichochochea hatua hizi?

Hali ya kutovumiliana kwa kidini ilikubaliwa kwa msingi wa kwamba muungano wa kidini ulitokeza msingi ulio thabiti zaidi kwa Serikali na kwamba mahitilafiano ya kidini yalitisha utengamano. Nchini Uingereza, katika mwaka wa 1602, mmojawapo wa mawaziri wa Malkia Elizabeth alitoa hoja: “Serikali haiwezi kuwa salama kamwe inaporuhusu dini mbili.” Kwa kweli, ilikuwa rahisi zaidi kupiga marufuku wapinzani wa kidini kuliko kutafuta kama kwa kweli wanasababisha tisho kwa Serikali au kwa dini iliyothibitishwa. Kichapo The Catholic Encyclopedia chasema: “Wala mamlaka za kilimwengu wala za kidini hazikupambanua tofauti ndogo sana kati ya wazushi walio hatari na wasiodhuru.” Hata hivyo, badiliko lingetokea karibuni.

Mwanzo Wenye Maumivu wa Uvumiliano

Badiliko katika Ulaya lilichochewa na mageuzi yaliyosababishwa na Uprotestanti, harakati ya kifarakano ambayo haikukoma. Kwa mwendo wenye kushangaza, Marekebisho ya Uprotestanti yaligawanya Ulaya kwa misingi ya kidini, hilo likatokeza wazo la uhuru wa dhamiri. Kwa kielelezo, Mleta Mabadiliko mashuhuri Martin Luther, alitetea maoni yake katika mwaka wa 1521, akasema: “Dhamiri yangu imetiishwa kwa Neno la Mungu.” Migawanyiko pia ilichochea Vita vya Miaka Thelathini (1618-1648), mfululizo wa vita vyenye ukatili vya kidini ambavyo viliharibu kabisa Ulaya.

Ingawa hivyo, katikati ya vita, wengi walikuja kutambua kwamba mapambano hayakuwa namna ya maendeleo. Hivyo, mfululizo wa amri kama vile Amri ya Nantes katika Ufaransa (1598), ilijaribu bila ya mafanikio kurejesha amani katika Ulaya iliyokumbwa na vita. Ni kupitia kwa amri hizi kwamba wazo la kisiku hizi la uvumiliano likatokea hatua kwa hatua. Hapo kwanza, “uvumiliano” ulidokeza mawazo yasiyofaa. “Ikiwa chini ya hali fulani tungevumilia mafarakano . . . , bila shaka lingekuwa jambo ovu—kwa kweli, uovu mbaya sana—lakini si mbaya kama vita,” akaandika mwanafunzi mashuhuri wa elimu ya binadamu Erasmus katika mwaka wa 1530. Kwa sababu ya maoni haya yasiyofaa, watu fulani kama vile Mfaransa Paul de Foix katika mwaka wa 1561, walipendelea kuongea juu ya “uhuru wa kidini” badala ya “uvumiliano.”

Ingawa hivyo, baada ya muda, uvumiliano haukuonwa tena kuwa uovu hata kidogo, wala uovu wa kiwango cha chini, bali kuwa mlinzi wa uhuru. Haukuonwa tena kuwa kuruhusu udhaifu bali kuwa uhakikisho kamili. Itikadi mbalimbali na haki za kufikiri tofauti zilipoanza kukubaliwa kuwa msingi wa jamii ya kisasa, ushabiki ulianza kupungua.

Kufikia mwisho wa karne ya 18, uvumiliano ukahusianishwa na uhuru na usawa. Hilo lilionyeshwa kupitia sheria na maazimio kadhaa, kama vile Azimio mashuhuri la Haki za Kibinadamu na Raia (1789), katika Ufaransa, au Mswada wa Haki (1791), katika Marekani. Kwa kuwa hati hizi ziliathiri kufikiri kwa uhuru kuanzia karne ya 19 na kuendelea, uvumiliano na hivyo uhuru haukuonwa tena kuwa laana bali baraka.

Uhuru wa Kiasi

Ujapokuwa ni wenye thamani sana, uhuru ni wa kiasi tu. Kwa kutumia udhuru wa uhuru zaidi kwa wote, Serikali hupitisha sheria zinazowekea mipaka uhuru fulani wa watu. Yafuatayo ni masuala fulani yanayohusiana na uhuru ambayo kwa sasa yanajadiliwa katika nchi nyingi za Ulaya: Sheria za kiserikali zapasa kuathiri maisha ya kibinafsi ya watu kwa kiwango gani? Ni zenye matokeo jinsi gani? Zinaathirije uhuru?

Mjadala kuhusu uhuru wa umma na wa kibinafsi umekaziwa na vyombo vya habari. Madai ya kutia kasumba, kutoza fedha kwa nguvu, kutenda watoto vibaya, na uhalifu mwingi ulio mbaya sana yameelekezwa dhidi ya vikundi fulani vya kidini, mara nyingi bila ithibati yenye msingi. Vyombo vya habari vimesambaza sana habari zinazohusisha vikundi vidogo vidogo vya kidini. Majina yenye kushushia hadhi kama vile “dhehebu” au “farakano” sasa yanatumiwa kila siku. Zikiwa chini ya mkazo wa maoni ya umma, serikali hata zimetokeza orodha za zile zinazoitwa eti madhehebu hatari.

Ufaransa ni nchi ambayo inajivunia utamaduni wake wa uvumiliano na utengano wa dini na Serikali. Nchi hii inajivunia kuwa bara la “Uhuru, Usawa, Udugu.” Lakini, kulingana na kitabu Freedom of Religion and Belief—A World Report, “kampeni ya elimu shuleni ya kuendelezwa kukataliwa kwa harakati mpya za kidini” imependekezwa katika nchi hiyo. Hata hivyo, watu wengi wanafikiri kwamba hatua hii inatishia uhuru wa kidini. Jinsi gani hivyo?

Tisho kwa Uhuru wa Kidini

Uhuru wa kweli wa kidini hupatikana tu wakati vikundi vyote vya kidini vinavyostahi na kutii sheria vinapotendewa na Serikali kwa njia sawa. Uhuru huu hukoma wakati Serikali inapoamua bila msingi wowote ni kikundi kipi kati ya vikundi vya kidini si dini, na hivyo kuinyima mapendeleo ambayo Serikali huzipa dini. Gazeti la Time katika mwaka wa 1997 lilisema hivi: “Wazo muhimu la uhuru wa kidini hupoteza maana serikali inapojitwalia bila haki, haki ya kuidhinisha dini kana kwamba inatoa leseni za kuendesha gari kwa madereva.” Hivi karibuni mahakama moja ya rufani nchini Ufaransa ilitangaza kwamba kufanya hivyo “huongoza kwa kufahamu au bila kufahamu, kwenye utawala wa kiimla.”

Haki za msingi hutishwa pia kikundi kimoja kinapodhibiti vyombo vya habari. Kwa kusikitisha, mambo yanazidi kuwa hivyo katika nchi nyingi. Kwa kielelezo, katika jitihada za kufasiri kikundi kilicho sawa kidini, mashirika yanayopinga madhehebu yamejiweka yenyewe kuwa mwendesha-mashtaka, hakimu, na baraza la mahakama na kisha yamejaribu kutumia vyombo vya habari kulazimisha umma kukubali maoni yao yenye kupendelea. Hata hivyo, kama vile gazeti la habari la Kifaransa Le Monde lilivyosema, kwa kufanya hivyo, nyakati nyingine mashirika haya yanadhihirisha “ufarakano uleule ambao hudai kuuzuia na kutisha kuanzisha mazingira ya ‘uonevu.’” Hilo gazeti la habari liliuliza hivi: “Je, kushutumiwa kijamii kwa vikundi vidogo vidogo vya kidini . . . hakutishi uhuru wa kimsingi?” Martin Kriele, aliyenukuliwa katika Zeitschrift für Religionspsychologie (Gazeti la Saikolojia ya Dini), alisema: “Msako wa uonevu kwa madhehebu hutokeza hangaiko kubwa zaidi kuliko dini nyingi ziitwazo madhehebu na vikundi vyenye kuvutia hisia. Kwa wazi: Raia wasiokiuka sheria wapaswa kuachwa kwa amani. Dini na itikadi zapaswa kuwa huru na kubaki zikiwa huru, katika Ujerumani pia.” Acheni tufikirie kielelezo kimoja.

“Raia Wenye Mifano Mizuri”—Washutumiwa Kuwa “Hatari”

Ni kikundi kipi cha kidini kilichosemekana kuwa “hatari zaidi ya mafarakano yote” kulingana na maoni ya wenye mamlaka Wakatoliki walionukuliwa katika gazeti mashuhuri la habari la Hispania ABC? Huenda ukashangaa kujua kwamba ABC lilikuwa likiongea kuhusu Mashahidi wa Yehova. Je, mashtaka yaliyofanywa dhidi yao yana lengo lenye msingi usio na ubaguzi? Ona matangazo yafuatayo kutoka vyanzo vinginevyo:

“Mashahidi hufundisha watu walipe kodi kwa uaminifu, wasishiriki kwenye vita wala matayarisho ya vita, wasiibe na, kwa ujumla, wafuate maisha ambayo yakifuatiwa na wengine yanaweza kuboresha hali ya jamii kuishi pamoja.”—Sergio Albesano, Talento, Novemba-Desemba 1996.

“Kinyume cha visingizio ambavyo vimeenezwa kwenye pindi fulani, kwa upande wangu [Mashahidi wa Yehova] hawahatarishi hata kidogo mashirika ya Serikali. Wao ni raia wapendao amani, wenye kudhamiria, na wanaostahi mamlaka.”—Mbunge wa Ubelgiji.

“Mashahidi wa Yehova wanatambuliwa kuwa watu wenye kufuatia haki zaidi katika Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani.”—Gazeti la habari la Ujerumani Sindelfinger Zeitung.

“Unaweza kuwaona [Mashahidi wa Yehova] kuwa raia wenye mifano mizuri. Wanalipa kodi kwa bidii, wanawatunza wagonjwa, wanapigana na kutokujua kusoma na kuandika.”—Gazeti la habari la Marekani San Francisco Examiner.

“Mashahidi wa Yehova hupata mafanikio makubwa zaidi kuliko washiriki wa dini nyingine katika kudumisha vifungo vya ndoa vilivyo imara.”—American Ethnologist.

“Mashahidi wa Yehova ni miongoni mwa raia walio wanyoofu zaidi na wenye bidii wa nchi za Kiafrika.”—Dakt. Bryan Wilson, Chuo Kikuu cha Oxford.

“Washiriki wa imani hiyo wamechangia sehemu kubwa kwa miongo mingi iliyopita kupanua uhuru wa dhamiri.”—Nat Hentoff, Free Speech for Me—But Not for Thee.

“Wamechangia . . . kihususa kuhifadhiwa kwa baadhi ya vitu vilivyo na thamani zaidi katika demokrasia yetu.”—Profesa C. S. Braden, These Also Believe.

Kama ionyeshwavyo na manukuu yaliyo juu, Mashahidi wa Yehova wanatambuliwa ulimwenguni pote kuwa raia walio kielelezo kizuri. Kwa kuongezea, wanajulikana kwa kutoa elimu ya Biblia bila malipo na kwa kuendeleza maadili ya familia. Madarasa yao ya kujifunzia kusoma na kuandika yamesaidia mamia ya maelfu kwa miongo mingi, huku kazi zao za kibinadamu zikiwasaidia maelfu, hasa katika Afrika.

Umaana wa Kutopendelea

Jamii imejaa watu wasio wanyoofu wanaowawinda wasiokuwa na hatia. Kwa sababu hiyo, kuna uhitaji hususa wa kuwa macho kuhusu madai juu ya dini. Lakini kunakuwa na lengo gani na inafaidi uhuru wa kidini jinsi gani wakati ambapo waandishi wa habari fulani, badala ya kuwafikia wataalamu wasiopendelea upande wowote, wanategemea habari kutoka kwa makanisa yanayoona idadi ya washiriki wake ikididimia au kupata habari kutoka kwa mashirika yanayopinga mafarakano ambayo kutopendelea kwao kunatiliwa shaka sana? Mathalani, gazeti la habari lililowaita Mashahidi wa Yehova “farakano lililo hatari kuliko yote” lilikiri kwamba fasiri yake ilitokana na “wataalamu wa Kanisa [Katoliki].” Kwa kuongezea, gazeti moja la Kifaransa lilisema kwamba makala nyingi zinazoshughulikia mafarakano yanayoshukiwa zilitokana na mashirika yanayopinga mafarakano. Je, jambo hili lasikika kuwa njia bora kabisa ya kupata habari isiyopendelea?

Mahakama na mashirika ya kimataifa yanayoshughulika na haki za kibinadamu za msingi, kama vile UM, yanasema kwamba “tofauti iliyopo kati ya dini na farakano ni bandia sana kuweza kukubaliwa.” Basi kwa nini wengine wanaendelea kutumia neno lenye kushushia hadhi “farakano”? Huu ni ushuhuda zaidi kwamba uhuru wa kidini unatishwa. Ni jinsi gani basi, uhuru huu wa msingi unavyoweza kulindwa?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Watetezi wa Uhuru wa Kidini

Maombi yaliyo dhahiri ya kutaka uhuru wa kidini yalitokana na mauaji ya kikatili ya mapambano ya kidini katika Ulaya mnamo karne ya 16. Maombi haya yangali yanahusu mazungumzo ya uhuru wa kidini.

Sébastien Chateillon (1515-1563): “Mzushi ni nani? Sina jingine isipokuwa kwamba tunawaona wazushi kuwa watu wote ambao hawakubaliani na maoni yetu. . . . Ikiwa katika jiji hili unaonwa kuwa mwamini wa kweli, katika jiji jingine utaonwa kuwa mzushi.” Mtafsiri wa Biblia Mfaransa aliye mashuhuri na mtetezi shupavu wa uvumiliano, Chateillon alitaja jambo moja kuu katika mjadala wa uhuru wa kidini: Ni nani anayefasiri mzushi ni mtu gani?

Dirck Volckertszoon Coornhert (1522-1590): “Twasoma kwamba katika nyakati za kale . . . hata Kristo mwenyewe katika Yerusalemu na kisha wafia-imani wengi katika Ulaya . . . walivuruga [jamii] kwa maneno yao ya kweli. . . . Maana ya neno ‘vuruga’ yahitaji kufafanuliwa kwa usahihi na waziwazi.” Coornhert alitoa hoja kwamba tofauti ya kidini haipasi kulinganishwa na kuvuruga utengamano. Aliuliza: Je, watu ambao ni waadilifu sana katika kutii na kustahi sheria kwa kweli ni tisho kwa utengamano?

Pierre de Belloy (1540-1611): Ni “kukosa ujuzi kuamini kwamba dini zikiwa nyingi huleta na kuendeleza msukosuko Nchini.” Mwanasheria Mfaransa Belloy, akiandika wakati wa Vita vya Dini (1562-1598), alitoa hoja kwamba upatano wa Nchi hautegemei usare wa kidini isipokuwa, bila shaka, serikali iwe inajinyenyekeza chini ya misongo ya kidini.

Thomas Helwys (karibu 1550–karibu 1616): “Ikiwa watu wake [wa Mfalme] ni raia watiifu na waaminifu kwa sheria zote za binadamu, hawezi kuwadai mengi zaidi.” Helwys, mmojawapo wa waanzilishi wa Baptisti ya Uingereza, aliandika kwa kuunga mkono mtengano wa Kanisa na Serikali, akimhimiza mfalme atoe uhuru wa kidini kwa makanisa na mafarakano yote na aridhike na mamlaka ya kiraia na mali. Maandishi yake yalikazia swali la hivi karibuni: Serikali yapasa kudhibiti hali ya kiroho ya watu kadiri gani?

Mwandishi Asiyejulikana (1564): “Ili kuanzisha uhuru wa dhamiri, haitoshi kumruhusu mtu aepuke kufuatia dini ambayo haipendelei ikiwa, kwa sababu hiyohiyo, hakuna uhuru wa kufuatia dini anayoipenda.”

[Picha]

Tertullian

Chateillon

De Belloy

[Hisani]

Picha zote: © Cliché Bibliothèque Nationale de France, Parisy

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki