Kutovumiliana kwa Kidini Leo
“Kila mtu ana haki ya uhuru wa kuwaza, wa dhamiri na wa kidini; haki hii yatia ndani uhuru wa kubadili dini au imani yake, na uhuru, wa kudhihirisha dini au imani katika kufundisha, kuabudu na kushika desturi, ama mtu akiwa peke yake ama akiwa katika jumuiya pamoja na wengine na akiwa hadharani au faraghani.” Kifungu Cha 18, Azimio Rasmi Kwa Wote La Haki Za Kibinadamu, 1948.
JE, WEWE hufurahia uhuru wa kidini katika nchi yako? Nchi nyingi ulimwenguni hukubali kijuu-juu tu kanuni hii nzuri, ambayo mara nyingi imetiwa ndani ya maazimio ya kimataifa. Hata hivyo, inakadiriwa kwamba katika nchi nyingi ambapo kutovumiliana na ubaguzi ni matatizo makubwa, mamilioni yasiyohesabika ya watu leo hawana uhuru wa kidini. Kwa upande mwingine, watu wengi wanaishi miongoni mwa jamii nyingi, makabila mengi, au dini nyingi ambapo uhuru hulindwa na sheria na uvumiliano huhifadhiwa na utamaduni wa taifa.
Na bado, katika sehemu hizo, uhuru wa kidini wa watu fulani unatishwa. “Ubaguzi unaotegemea dini au usadikisho uko karibu katika mifumo yote ya kiuchumi, ya kijamii na ya kiitikadi katika sehemu zote ulimwenguni,” akasema Angelo d’Almeida Ribeiro, Katibu wa Pekee wa zamani aliyeteuliwa na Tume ya Haki za Kibinadamu ya UM. Katika kitabu chao Freedom of Religion and Belief—A World Report, kilichochapishwa mwaka wa 1997, wahariri Kevin Boyle na Juliet Sheen wasema hivi: “Kunyanyaswa kidini kwa dini ndogondogo [na] kupigwa marufuku kwa itikadi na ubaguzi wa kikaidi . . . ni mambo yanayotukia kila siku kwenye mwisho wa karne ya ishirini.”
Hata hivyo, ubaguzi wa kidini hauathiri tu dini ndogondogo. Profesa Abdelfattah Amor, Katibu wa Pekee wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya UM Kuhusu Kutovumiliana kwa Kidini, anaona kwamba “hakuna dini isiyoweza kuvunjiwa haki.” Basi, yawezekana kwamba unakoishi, dini fulani zinakabili kwa ukawaida kutovumiliana na ubaguzi.
Namna Mbalimbali za Ubaguzi
Kuna ubaguzi wa kidini wa namna nyingi. Nchi fulani hupiga marufuku dini zote isipokuwa dini moja tu, ambayo hufanywa iwe dini ya Serikali. Katika nchi nyingine, sheria zinazozuia utendaji wa dini fulani hupitishwa. Nchi fulani zimetunga sheria ambazo zimefafanuliwa kwa njia isiyo na msingi maalumu. Fikiria uwezekano wa ukiukwaji wa sheria iliyopendekezwa nchini Israeli ya kukataza uingizaji, uchapishaji, ugawanyaji, au umiliki wa broshua au vitabu “ambavyo vinaweza kumshawishi mtu ageuze dini.” Haishangazi kwamba gazeti la habari la International Herald Tribune liliripoti hivi: “Katika Israeli, Mashahidi wa Yehova wamesumbuliwa na kushambuliwa.” Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova katika jiji la Lod lilivunjwa mara tatu na kuharibiwa mara mbili na mashabiki wa othodoksi wenye kushikilia kauli yao kupita kiasi. Polisi walikataa kuzuia jambo hilo.
Kitabu Freedom of Religion and Belief chataja mifano mingine ya kutovumiliana: “Uzushi na wazushi si dhana ya kale. . . . Kukataliwa, kunyanyaswa na kubaguliwa kwa wale walio na imani tofauti kwabaki kuwa kisababishi kikuu cha kutovumiliana. Mifano ni kama vile kikundi kinachoitwa Ahmadi katika Pakistan na [Wabaha’i] katika Misri, Iran, na Malasia kama ilivyo na Mashahidi wa Yehova katika nchi kadhaa za Ulaya Mashariki, Ugiriki na Singapore.” Kwa wazi, uhuru wa kidini umo hatarini katika sehemu nyingi za ulimwengu.
Kwa kuona mambo haya, Federico Mayor, mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, alitangaza kwamba kizazi kinachoibuka hivi karibuni “hakitokezi shauku kamili. . . . Uhuru mpya ambao watu wamefurahia umetokeza tena kumbukumbu za chuki.” Akithibitisha hofu hii, mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Kibinadamu cha Chuo Kikuu cha Essex, Uingereza, alisema: “Uthibitisho wote waelekeza kwenye mkataa wa kwamba hali ya kutovumiliana kwa kidini . . . haipungui badala yake inaongezeka katika ulimwengu wa kisasa.” Hali hiyo ya kuongezeka kwa kutovumiliana yatisha uhuru wa kidini, labda uhuru wako wa kidini. Lakini, kwa nini uhuru wa kidini ni wa maana?
Ni Nini Kilicho Hatarini?
“Uhuru wa kidini ni takwa la msingi kabla jamii yoyote haijatangazwa kuwa huru. . . . Bila uhuru wa kidini na haki za kusambaza imani ya mtu, haiwezekani kuwa na haki za dhamiri na demokrasia ya kweli,” akasema mwanasosholojia Bryan Wilson katika kitabu chake Human Values in a Changing World. Na, kama mahakama moja ya Ufaransa ilivyotambua hivi majuzi, “uhuru wa itikadi ni mojawapo ya haki za msingi za uhuru wa umma.” Hivyo, uwe mtu wa kidini au sivyo, unapaswa kupendezwa na kulindwa kwa uhuru wa kidini.
Mtazamo wa nchi kuelekea uhuru wa kidini huathiri kwa kiwango kikubwa sifa yake na kuaminika kwake kimataifa. Ripoti moja iliyotolewa katika mwaka wa 1997 kwa mkutano wa mataifa 54 ya Shirika la Usalama na Ushirikiano katika Ulaya ilisema: “Uhuru wa Kidini ni mojawapo ya kanuni za juu zaidi katika mkusanyo wa haki za kibinadamu, yaani kiini hasa cha adhama ya kibinadamu. Hakuna tengenezo lolote linalokiuka, au kuruhusu ukiukaji wa hatua kwa hatua wa, haki hizo liwezalo kudai kihalali kuwa mwanachama wa jumuiya ya nchi zinazofuatia haki na demokrasia ambazo hustahi haki za kibinadamu za msingi.”
Uhuru wa kidini ni kama sehemu ya msingi wa jengo. Uhuru mwingineo—wa kiraia, kisiasa, kitamaduni, na kiuchumi—unautegemea. Msingi ukifukuliwa, jumba lote linaathirika. Profesa Francesco Margiotta-Broglio aeleza hivi kwa ufupi: “Mahali popote uhuru wa kidini unapokiukwa, uhuru mwingine hufuatia kuathiriwa.” Ikiwa uhuru mwingine utalindwa, uhuru wa kidini wapaswa kulindwa kwanza.
Kusudi ufahamu njia bora ya kulinda kitu fulani, ni muhimu kukielewa. Ni nini visababishi vya uhuru wa kidini? Uliimarishwa jinsi gani na kwa gharama gani?
[Picha katika ukurasa wa 4]
Hali ya kutovumiliana kwa kidini ina historia ndefu