Wahuguenoti Wakimbilia Uhuru
“Kwa idhini ya Mfalme na Malkia, . . . Sisi Twatangaza, Kwamba Waprotestanti Wote Wafaransa Watakaotafuta Kimbilio, na Kujileta wenyewe katika huu Ufalme Wetu, hawatakuwa tu na Ulinzi Wetu Wa Kifalme . . . Bali pia Tutajitahidi katika Njia zote na Namna zote zifaazo Kuwategemeza na Kuwasaidia . . . ili kuishi na kuwa kwao katika Milki hii kuwe kwenye kustarehesha na rahisi kwao.”
NDIVYO lisemavyo lile tangazo la 1689 la William na Mary, mfalme na malkia wa Uingereza. Lakini kwa nini Waprotestanti Wafaransa, au Wahuguenoti, kama walivyokuja kujulikana, walihitaji kutafuta kimbilio na ulinzi nje ya Ufaransa? Kwa nini kukimbia kwao kutoka Ufaransa miaka 300 hivi iliyopita kutupendeze leo?
Katika karne ya 16 Ulaya ilikumbwa na vita na mabishano yaliyohusu dini. Ufaransa, pamoja na Vita vyake vya Kidini (1562-1598) kati ya Wakatoliki na Waprotestanti, haikuepuka msukosuko huu. Hata hivyo, katika 1598, Mfalme Mfaransa Henry wa 4 alitia sahihi amri ya kuvumilia dini nyingine, Amri ya Nantes, akiwapa Waprotestanti Wahuguenoti uhuru wa kidini. Kutambuliwa huku kwa kisheria kwa dini mbili kulikuwa kwa pekee katika Ulaya. Kwa muda kulikomesha mabadiliko makubwa ya kidini ambayo yalikuwa yamedhuru nchi ya Ufaransa ya karne ya 16 kwa miaka zaidi ya 30.
Ijapokuwa Amri ya Nantes ilikusudiwa kuwa “ya kudumu na isiyobadilika,” katika 1685 ilifutwa na Amri ya Fontainebleau. Mwanafalsafa Mfaransa Voltaire baadaye alifafanua ufutaji huu kuwa “mojawapo ya mambo ya huzuni kubwa zaidi ya Ufaransa.” Baada ya kipindi kifupi, ilichochea kukimbia kwa Wahuguenoti 200,000 katika nchi nyinginezo. Hata hivyo, kufutwa huko kulisababisha matokeo makubwa zaidi. Lakini kwa nini amri hiyo ya mapema ya kupendelea uvumilivu wa kidini ilifutwa?
Yapingwa Tokea Mwanzoni
Hata ingawa Amri ya Nantes ilitumika rasmi kwa miaka karibu 90, mwanahistoria mmoja asema kwamba tayari ilikuwa “inakufa ilipofutwa katika 1685.” Kwa kweli, amri hiyo haikuwa imewekewa msingi imara. Tokea mwanzo, ilichangia ile ambayo imeitwa “vita baridi” kati ya makasisi Wakatoliki na ile waliyoita “R.P.R.” (Iitwayo kwa kawaida Reformed Religion) Kuanzia wakati ilipotolewa katika 1598 hadi karibu 1630, upinzani wa Amri ya Nantes ulihusu mijadala kati ya Waprotestanti na Wakatoliki, na kuchapishwa kwa vitabu vya kidini. Hata hivyo, kutovumilia dini nyingine kulionyeshwa katika njia nyingi.
Baada ya vita dhidi ya Waprotestanti kuanzia 1621 hadi 1629, serikali ya Ufaransa ilijaribu kuwalazimisha wajiunge na dini ya Katoliki kupitia mfululizo wa hatua za ukandamizaji. Kuwasumbua huku kuliongezeka chini ya Louis wa 14, yule “Mfalme wa Jua.” Sera yake ya mnyanyaso iliongoza kwenye kufuta Amri ya Nantes.
Kule Kubanwa
Zikiwa sehemu ya kule kubanwa, haki za raia Waprotestanti ziliondolewa hatua kwa hatua. Kati ya 1657 na 1685, karibu amri 300, mara nyingi zikidokezwa na makasisi, zilitolewa dhidi ya Wahuguenoti. Amri hizo zilishambulia kila sehemu ya maisha zao. Mathalani, Wahuguenoti walinyimwa kazi nyingi za kitaalamu, kama vile kitiba, sheria, na hata ukunga. Kuhusiana na ukunga, mwanahistoria mmoja alisababu hivi: “Iliwezekanaje kuukabidhi uhai kwa mwasi ambaye mradi wake ni kuharibu utaratibu uliopo?”
Ukandamizaji ulizidishwa katika 1677. Mhuguenoti yeyote aliyepatikana akijaribu kumgeuza imani Mkatoliki alipigwa faini ya pauni elfu moja za Ufaransa. Fedha za serikali kuanzia kodi za kupita kiasi zilitumiwa kuchochea Wahuguenoti wageuze imani. Katika 1675 makasisi Wakatoliki walimpa Mfalme Louis wa 14 pauni milioni 4.5 za Ufaransa, wakisema: “Sasa lazima utende kwa kuonyesha shukrani yako kwa kutumia mamlaka yako kumalizia mbali hao waasi.” Mkakati huu wa “kununua” wageuzwa-imani ulitokeza karibu watu 10,000 waliogeuzwa kuwa Wakatoliki kwa miaka mitatu.
Katika 1663 mgeuzo wa imani ya Protestanti ulifanywa kuwa haramu. Pia kulikuwa na vizuizi vya mahali Wahuguenoti wangeishi. Mfano wa hatua hizo kali ni kwamba watoto wenye umri wa miaka saba wangeweza kuwa Wakatoliki dhidi ya matakwa ya wazazi wao. Wazazi Waprotestanti waliwajibika kulipia elimu ambayo watoto wao walipata kutoka kwa Wayesuiti (mwanachama wa chama cha Kikristo cha Katoliki) au wafunzi wengine Wakatoliki.
Kifaa kingine kilichotumiwa kukandamiza Wahuguenoti ni lile shirika la kisiri liitwalo Compagnie du Saint-Sacrement (Kundi la Sakramenti Takatifu). Hili lilikuwa shirika la Katoliki ambalo mwanahistoria Janine Garrisson husema lilifikia kuwa “mfumo wa upelelezi mkubwa mno” ulioenea Ufaransa yote. Likipenyeza kwenye utaratibu wa juu zaidi wa jamii, halikukosa fedha wala habari inayohusu adui. Garrisson aeleza kwamba mbinu zake zilikuwa nyingi: “Kuanzia msongo mpaka upingamizi, kutawalwa kwa hila mpaka kushutumiwa hadharani, kikundi hicho Compagnie kilitumia kila namna kudhoofisha jumuiya ya Waprotestanti.” Ingawa hivyo, Wahuguenoti wengi walibaki Ufaransa wakati wa kipindi hiki chenye mnyanyaso. Mwanahistoria Garrisson ataarifu: “Ni vigumu kuelewa kwa nini Waprotestanti wengi hawakuacha Ufalme huo wakati uhasama kuwaelekea ulipoongezeka pole kwa pole.” Hata hivyo, walilazimika kukimbilia uhuru hatimaye.
Kurudia Mwanzo Tena
Amani ya Nymegen (1678) na Makubaliano ya Kusimamisha Vita ya Ratisbon (1684) yalimweka huru Mfalme Louis wa 14 kutoka vita ya nje. Ng’ambo ya Mlangobahari huko Uingereza, Mkatoliki akawa mfalme katika Februari 1685. Louis wa 14 angeweza kutumia kwa manufaa hali hii mpya. Miaka michache awali, makasisi Wakatoliki katika Ufaransa walikuwa wametoa zile Kanuni Nne za Ufaransa, ambazo zilizuia mamlaka ya kipapa. Kisha Papa Innocent wa 11 “aliona Kanisa la Ufaransa likiwa karibu sawa na farakano la kidini.” Kwa sababu hiyo, kwa kufuta Amri ya Nantes, Louis wa 14 angeweza kuboresha sifa yake iliyoharibiwa na kurudisha mahusiano ya kawaida na papa.
Sera ya mfalme kuelekea Waprotestanti ilionekana dhahiri. Njia ya uanana (ushawishi na utungaji wa sheria) kwa wazi haikuwa na matokeo. Kwa upande mwingine, minyanyaso ya karibuni kwa kutumia wanajeshi-wanyanyasajia ilifanikiwa. Kwa hiyo katika 1685, Louis wa 14 alitia sahihi Amri ya Fontainebleau, akifuta Amri ya Nantes. Mnyanyaso wenye jeuri uliohusiana na kufuta huko uliacha Wahuguenoti katika hali mbaya zaidi kuliko ile ya Amri ya Nantes. Sasa wangefanyaje?
Wangejificha, Wangepigana, au Wangekimbia?
Baadhi ya Wahuguenoti waliamua kuabudu kisiri-siri. Wakati mahali pao pa kukutania palipoharibiwa na ibada yao ya peupe kupigwa marufuku, waligeukia ‘Kanisa la Jangwani,’ au ibada ya kichini-chini. Hilo lilikuwa licha ya kwamba watu waliofanya mikutano kama hiyo walijihatarisha na kuhukumiwa kifo, kulingana na sheria iliyopitishwa Julai 1686. Baadhi ya Wahuguenoti walikana imani yao, wakifikiri kwamba ingewezekana kuirudia tena baadaye. Wageuzwa-imani hao walizoea Ukatoliki wa juujuu tu ambao ulifuatwa baadaye na vizazi vyao.
Serikali ilijaribu kuimarisha mgeuzo wa imani. Ili kupata kazi, iliwabidi wageuzwa-imani wapya wawe na cheti cha Ukatoliki wao kilichotiwa sahihi na kasisi wa parokia, aliyewaona wakihudhuria. Kama watoto hawakubatizwa na kulelewa wakiwa Wakatoliki, wangechukuliwa kutoka kwa wazazi wao. Shule zilipaswa kuendeleza elimu ya Katoliki. Jitihada zilifanywa ili kutokeza vitabu vya kidini vyenye kupendelea Ukatoliki kwa ajili ya “watu wa kile Kitabu [Biblia],” kama vile Waprotestanti walivyoitwa. Serikali ilichapisha vitabu zaidi ya milioni moja na kuvipeleka kwenye maeneo ambamo idadi kubwa za watu walikuwa wamegeuzwa imani. Hatua hizo zilikuwa kali sana hivi kwamba ikiwa mtu aliyekuwa mgonjwa alikataa sherehe za mwisho za Katoliki na baada ya hapo apone, alihukumiwa adhabu ya kutiwa gerezani au kwenye jahazi kwa maisha yake yote. Na alipokufa baadaye, mwili wake ulitupwa tu kana kwamba ulikuwa takataka, na mali zake zilitwaliwa.
Baadhi ya Wahuguenoti waligeukia silaha ili kujikinga. Katika mkoa wa Cévennes, uliojulikana kwa bidii yake ya kidini, wapiganaji Wahuguenoti walioitwa Wakamisadi waliasi katika 1702. Vikosi vya serikali vilichoma vijiji kwa sababu ya uvamizi na mashambulizi ya usiku ya Wakamisadi. Ijapokuwa mashambulizi ya mara mojamoja ya Wahuguenoti yaliendelea kwa muda fulani, kufikia 1710 nguvu za jeshi la Mfalme Louis liligandamiza Wakamisadi.
Hatua nyingine ya Wahuguenoti ilikuwa kutoroka Ufaransa. Ukimbizi huu umeitwa utawanyikaji wa kweli. Wahuguenoti wengi walikuwa mafukara walipoondoka kwa sababu serikali ilikuwa imetwaa mali zao, Kanisa Katoliki likipokea sehemu ya utajiri huo. Kwa hiyo haikuwa rahisi kutoroka. Serikali ya Ufaransa ilichukua hatua haraka kuhusu yaliyokuwa yakitokea, ikilinda njia ya kuondokea na kutafuta meli. Maharamia waliteka nyara meli zilizoondoka Ufaransa, kwa kuwa wangepokea thawabu kubwa kwa kuwanasa wenye kutoroka. Wahuguenoti waliopatikana wakikimbia walipewa adhabu kali sana. Wakifanya hali iwe ngumu zaidi, wapelelezi waliofanya kazi katika jumuiya walijaribu kupata majina ya wale waliokuwa wakipanga kukimbia na njia zao. Barua zilizozuiliwa, ughushi, na kula njama kulikuwa mambo ya kawaida.
Kimbilio Lenye Ukaribishaji
Kukimbia kwa Wahuguenoti kutoka Ufaransa na kukaribishwa kwao katika nchi zilizo wakaribishaji kulijulikana kuwa Kimbilio. Wahuguenoti walikimbilia Uholanzi, Uswisi, Ujerumani, na Uingereza. Baadaye wengine walikwenda Skandinavia, Amerika, Ireland, West Indies, Afrika Kusini, na Urusi.
Idadi fulani ya nchi za Ulaya zilipitisha amri za kutia moyo Wahuguenoti wahamie huko na kukaa. Miongoni mwa vichocheo vilivyotolewa vilikuwa uandikishwaji wa raia bila malipo, kutolipa kodi, na uanachama wa bila malipo katika biashara. Kulingana na mwanahistoria Elisabeth Labrousse, Wahuguenoti walio wengi walikuwa “vijana wa kiume . . . wajasiri, raia wenye nguvu walio na adili bora isiyo na kifani.” Hivyo, Ufaransa ikiwa katika uwezo wake wa juu, ilipoteza wafanyakazi stadi katika biashara mbalimbali. Naam, “mali, fedha nyingi na mbinu” zilienda ng’ambo. Mambo ya kidini na ya kisiasa pia yalitimiza sehemu fulani katika kutoa kimbilio kwa Wahuguenoti. Lakini matokeo ya muda mrefu ya uhamaji huu yalikuwa yapi?
Kufutwa kwa Amri ya Nantes na mnyanyaso uliofuata ulichochea kuonyeshwa kwa hisia kusikopendeza. William wa Orange aliweza kutumia hisia hizo za kupinga Ufaransa ili apate kuwa mtawala wa Uholanzi. Kwa msaada wa maofisa Wahuguenoti, pia alikuja kuwa mfalme wa Uingereza, akichukua mahali pa Mkatoliki James wa Pili. Mwanahistoria Philippe Joutard aeleza kwamba “sera ya Uprotestanti ya Louis wa 14 ilikuwa mojawapo ya sababu kuu za kupinduliwa kwa James wa Pili [na] kuanzishwa kwa shirika la Augsburg. . . . Matukio [haya] yalitia alama wakati wa badiliko la maana katika historia ya Ulaya, yakifanya mahali pa mamlaka ya Ufaransa pachukuliwe na mamlaka ya Uingereza.”
Wahuguenoti walitimiza fungu la maana la kitamaduni katika Ulaya. Walitumia uhuru wao waliotoka kuupata kutokeza fasihi ambazo zingesaidia kuunda falsafa ya Mnurusho na mawazo ya kuvumilia dini nyingine. Kwa mfano, Mprotestanti aliye Mfaransa alitafsiri fasihi za mwanafalsafa Mwingereza John Locke, akieneza wazo la haki za kiasili. Waandikaji wengine Waprotestanti walikazia umaana wa uhuru wa dhamiri. Wazo hilo lilieleza kwamba utii kwa watawala ni wa kadiri na ungeweza kupuuzwa kama wangevunja mapatano waliyofanya kati yao na watu. Hivyo, kama mwanahistoria Charles Read aelezavyo, kufutwa kwa Amri ya Nantes kulikuwa “mojawapo ya mambo yaliyo dhahiri ya Mapinduzi ya Ufaransa.”
Je, Walijifunza Masomo Fulani?
Kwa kuzingatia matokeo ya mnyanyaso yaliyokuwa kinyume cha ilivyotarajiwa, na serikali kupoteza watu wengi wenye thamani, Marquis de Vauban, mwanajeshi mshauri wa Mfalme Louis wa 14, alimsihi mfalme arudishe ile Amri ya Nantes, akisema: “Kugeuzwa kwa mioyo ni kwa Mungu pekee.” Kwa hiyo kwa nini Serikali ya Ufaransa haikujifunza kutokana na somo lake na kubadilisha uamuzi wake? Kwa hakika jambo moja lililochangia lilikuwa kwamba mfalme alihofu kudhoofisha serikali. Zaidi ya hayo, ilifaa kutosheleza tamaa ya kurudisha Ukatoliki wa zamani na hali ya kutovumilia dini nyingine katika Ufaransa ya karne ya 17.
Matukio yanayozunguka kufuta huko yamefanya wengine waulize, “Jamii yawezaje kuruhusu na kuvumilia hali ya kujitawala ya vikundi mbalimbali?” Kwa kweli, kama vile ambavyo wanahistoria wameandika, haiwaka na upotovu wake.” Leo, katika jamii ambazo zina watu wa jamii na dini mbalimbali, kukimbia kwa Wahuguenoti kutafuta uhuru ni kikumbusha chenye kutia uchungu cha yaliyotukia wakati siasa zenye kuchochewa na kanisa zilipotangulizwa badala ya masilahi ya watu.
[Maelezo ya Chini]
a Ona sanduku kwenye ukurasa wa 28.
Sanduku katika ukurasa wa 28
Wanajeshi-Wanyanyasaji
Wageuza Imani kwa Kutisha
Wengine waliwaona askari wapanda-farasi kuwa “wamishonari bora kabisa.” Hata hivyo, miongoni mwa Wahuguenoti, walisababisha hofu, na katika visa vingine watu wa vijiji vizima-vizima wangegeuka kuwa Wakatoliki baada ya kusikia kuwa wamefika. Lakini askari hao wapanda-farasi walikuwa akina nani?
Askari wapanda-farasi walikuwa wanajeshi waliokuwa na silaha waliojipangisha katika nyumba za Wahuguenoti wakiwa na lengo la kuwatisha wakazi. Matumizi ya askari wapanda-farasi katika njia hii yalijulikana kuwa unyanyasaji wa kijeshi. Ili kuongeza mzigo kwa familia hizo, idadi ya wanajeshi waliotumwa kwenye nyumba moja ilikuwa hailingani na uwezo wa familia hiyo. Askari hao wapanda-farasi waliamriwa kuzifanyia familia ukatili, kuwafanya wakose usingizi, na kuharibu mali zao. Kama wakazi wangekana imani ya Protestanti, askari wapanda-farasi wangeondoka.
Hao wanajeshi-wanyanyasaji walitumiwa kugeuza imani ya watu katika 1681 huko Poitou, Ufaransa Magharibi, eneo lililokuwa na Wahuguenoti wengi. Baada ya miezi michache, kuanzia watu 30,000 hadi 35,000 waligeuza imani yao. Njia hiyohiyo ilitumiwa katika 1685 katika maeneo mengine ya Wahuguenoti. Baada ya miezi michache, kuanzia watu wengine 300,000 hadi 400,000 walikana imani. Kulingana na mwanahistoria Jean Quéniart, mafanikio ya hao wanajeshi-wanyanyasaji “yalifanya ufutaji wa [ile Amri ya Nantes] usiepukike, kwa sababu sasa ilionekana kuwa inawezekana.”
[Hisani]
© Cliché Bibliothèque Nationale de France, Paris
[Picha katika ukurasa wa 25]
Tangazo hili la 1689 lilikuwa kimbilio kwa Waprotestanti Wafaransa waliotafuta kitulizo kutokana na ukandamizaji wa kidini
[Hisani]
By permission of The Huguenot Library, Huguenot Society of Great Britain and Ireland, London
[Picha katika ukurasa wa 26]
Ufutaji wa Amri ya Nantes, 1685 (Huu ni ukurasa wa kwanza wa ufutaji huo)
[Hisani]
Documents conservés au Centre Historique des Archives nationales à Paris
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mahekalu mengi ya Waprotestanti yaliharibiwa
[Hisani]
© Cliché Bibliothèque Nationale de France, Paris