Yale Maji ya Mgeuzo Mkuu wa Kidini Yabubujika
“KWA GHAFULA mimi nilisikia mvumo mwingine, kama kwamba wa ngurumo, ukija mbio kuelekea sisi. Jamaa yetu . . . ilianza kupiga mbio huku na huku kwenda kwenye kilima cha karibu. Maji yale yenye kutoa povu yalitufikia. Tuliogelea kama ambavyo hatujafanya kamwe kabla ya hapo. Ingawa tulimeza-meza kiasi fulani cha maji ya bahari . . . , tulifanikiwa.”
Hivyo ndivyo Mfilipino mmoja alivyosimulia tukio la kuogopesha sana ambalo lilibadili ulimwengu wake. Labda wewe hujapata kamwe kukumbwa na afa la kiasili, la maji au la aina nyingine yo yote. Lakini kuangalia historia kunafunua kwamba mamilioni ya maisha zimegeuzwa na mabadiliko makubwa sana ya namna moja au nyingine.
Dini imeshuhudia pia hesabu fulani ya misukosuko mikubwa ajabu, ikipindua juu chini fungu la maisha ya kila siku ya watu wasiohesabika. Misukosuko hiyo imetia ndani Wahindu, Wabuddha, Waislamu, Wayahudi, na Wakristo. Je! maisha yako yameathiriwa na mchafuko wa namna hiyo? Kwa uhakika ni kama yameathiriwa, ko kote ambako wewe unaweza kuwa ukiishi. Acheni tutoe mfano wa jambo hilo kwa kufunga safari ya wakati turudi nyuma karibu miaka 400 kwenye karne ya 16. Kwanza kabisa tunakaza fikira zetu juu ya Ulaya, ambayo wakati huo ilikuwa ikivurugika sana kwa migawanyiko, kama wa kisulisuli cha bwawa la maji linaloendelea kuongezeka mwendo.
Kivimbe Kinachokua
Kwa karne nyingi, zenye kuongoza mpaka kwenye kile ambacho sisi tunaita Mgeuzo Mkuu wa Kidini, kanisa Katoliki la Roma na watawala wa Ulaya walikuwa wameshindana mmoja na mwingine, kila mmoja akidai kuwa na mamlaka juu ya yule mwingine na juu ya halaiki ya watu. Jamii ya watu katika bara ile waliinua sauti zao kwa kukataa yale ambao wao waliona kuwa desturi mbaya zenye kufanywa na kanisa.
Ni namna gani ya desturi mbaya ambazo wao waliona? Pupa, ukosefu mbaya sana wa adili, na kujiingiza katika siasa. Watu wa kawaida walichukizwa sana kuelekea wanaume na wanawake ambao kwa upande mmoja walidai mapendeleo ya pekee kwa sababu ya nadhiri zao za umaskini na ubikira lakini wakati ule ule wakapuuza sheria kwa kuwa wafisadi na wakosefu wa adili waziwazi. Washarifu katika Uingereza walikasirikia ile hali ngeni kidogo ya kutolea papa ushuru ambaye wakati huo alikuwa anaishi katika Ufaransa na alikuwa ameungana pamoja nayo, ikiwa ni adui ya Uingereza vitani.
Ufisadi ndani ya Kanisa Katoliki ulipenya chini kutoka juu. Mwanahistoria Barbara W. Tuchman anaandika katika kitabu chake The March of Folly, kwamba wale mapapa sita waliokuwa katika cheo kutoka 1471 na kuendelea waliendeleza “wingi unaopita kiasi wa udanganyifu wa kutumia cheo, ukosefu wa adili, pupa, na siasa za mabavu zenye balaa nyingi ajabu.” Barbara Tuchman anasimulia zaidi jinsi Papa Sixtus wa 4 alivyoweka rasmi binamu watano na binamu-mjukuu wawe makadinali, binamu-mjukuu mwingine awe askofu, na akafanya sita kati ya watu wale wengine wa ukoo wake wafunge ndoa ndani ya jamaa zenye kutawala, ili ainue na kutajirisha jamaa yake iliyokuwa maskini kufikia hapo. Aleksanda wa 6, alipopata kuwa papa, ilijulikana kwamba alikuwa amekuwa na mabibi kadha na watoto saba. Katika jitihada yake ya kupiga moyo konde achaguliwe kwenye cheo, yeye alihonga washindani wakubwa wawili wake, mmoja wao akipokea “vipande vya fedha na dhahabu vilivyobebwa na nyumbu wanne,” akaandika Barbara Tuchman. Baadaye yeye alisimamia karamu moja ya Vatikani ambayo ikawa “yenye sifa kubwa katika kumbukumbu za pornografia.” Ndipo kitabu kile kile kinapotoa muhtasari wa jinsi mchonga sanamu mwenye sifa kubwa Michelangelo alivyoagizwa na Papa Julius wa 2 achonge sanamu yake. Wakati alipoulizwa na fundi huyo kama sanamu hiyo yapasa imwonyeshe yeye akiwa ameshika kitabu, papa yule shujaa wa kivita alijibu: “Weka upanga hapo. Mimi sijui lo lote juu ya herufi-herufi.”
Lile Bwawa la Maji Lapata Ufa
Wanaulaya wa kawaida bado walitamani mwongozo wa kiroho. Kwa kuona mamlaka zenye vyeo mbalimbali zikiwa zimejihusisha mno katika kutosheleza tamaa zao wenyewe, watu hao walio dhalili zaidi waligeukia chanzo cha mamlaka tofauti na hizo, ile ambayo wao waliiona kuwa kuu kuliko nyinginezo zote—Biblia. Kulingana na mtungaji vitabu Joel Hurstfield, ule Mgeuzo Mkuu wa Kidini ulikuwa “tatanisho la mamlaka kwa kina kilicho kirefu zaidi.” Kwa kugutushwa na ufisadi katika kanisa, wahubiri na watawa wa kiume katika Italia walianza kusema peupe juu ya uhitaji wa mgeuzo mkuu. Lakini hakuna mahali ambako maji ya kutoridhika yalikuwa yakikusanyika kwa kuogopesha kuliko katika Ujeremani.
Katika nyakati za kipagani, makabila ya Kijeremani yalikuwa na pokeo ambalo kwalo pesa zingeweza kulipwa ili kufikiliza ufungulio wa kutopata adhabu kwa matendo ya uhalifu. Imani ya Kiroma ilipopanuka, desturi hiyo ilipata nafasi ndani ya kanisa kwa namna ya mauzo ya rehema za dhambi. Jambo hilo liliruhusu mtenda dhambi anunue kutoka kwa papa thamani ya matendo ya ustahili wa “watakatifu” waliokufa na kuyatumia hayo dhidi ya adhabu za kidunia kwa dhambi zilizofanywa. Akiwa chini ya mkazo wa kifedha, uliosababishwa na vita dhidi ya Ufaransa na kazi za ujenzi mwingi katika Roma, Papa Leo wa 10 aliamrisha kwamba rehema za dhambi ziuzwe, zikitolea watu ondoleo kamili la adhabu za kidunia kwa dhambi. Martin Luther mwenye kuchukizwa sana alieleza wazi hoja zake 95 ambazo sasa zilikuwa na sifa kubwa juu ya mafundisho yasiyo ya kweli ya kanisa. Ile harakati ya kuelekea mgeuzo mkuu, ambao ulikuwa umeanza kama kitiririko kidogo cha maji vizazi kadha mapema, ikawa bubujiko huku watu zaidi na zaidi wakiunga mkono.
Katika karne ya 16, watu mmoja mmoja kama vile Luther katika Ujeremani, Zwingli na Calvin katika Uswisi, na Knox katika Uskochi wakawa wakikusanyikiwa na watu wengi ambao waliona nafasi ya kutakasa Ukristo na kurudia maadili na viwango vya kwanza vya Biblia. Neno fulani liliundwa katika Ujeremani kusimulia wale ambao walikataa kukubali vizuizi vilivyowekwa juu ya imani na wana-wafalme wa Katoliki ya Roma, na ambao walikiri wazi ushikamano wao kwa Mungu juu ya mtu mwingine ye yote. Neno hilo lilikuja baadaye kutia ndani wote ambao waliunga mkono ile harakati ya Mgeuzo Mkuu wa Kidini. Neno hilo lilikuwa “Mprotestanti.”
Uprotestanti ulienea katika Ulaya kwa mwendo wa kustaajabisha sana, ukifanyiza upya mandhari ya kidini, ukiweka mipaka mipya ya uanachuo wa kidini. Ujeremani na Uswisi ndizo zilizoongoza zikafuatwa upesi na Uskochi, Sweden, Norwei, na Denmark. Kulikuwa na harakati za mgeuzo mkuu katika Austria, Bohemia, Polandi, Transylvania, Uholanzi, na Ufaransa.
Katika Uingereza kutoridhika kulikuwa kumekuwa kukitokeza wazi kwa zaidi ya karne moja, tangu zile siku za John Wycliffe na wafuasi wa Lollard. Lakini wakati mvunjiko kutoka kwenye Kanisa Katoliki ulipokuja mwishowe sababu zilikuwa za kimwili zaidi. Mfalme aliazimia kubadili si dini yake bali mke wake. Katika 1534 Henry wa 8 alijitangaza mwenyewe kichwa cha Kanisa la Uingereza lililokuwa jipya. Makusudio yake yalikuwa tofauti na yale ya watokeza-mgawanyiko wa bara lile, lakini hata hivyo kitendo chake kilifungua malango ya gharika ili yale maji ya badiliko la kidini yatiririke kuingia Uingereza. Katika sehemu zote za Ulaya, maji hayo yaligeuka kwa haraka sana yakawa mekundu kwa damu ya maelfu ambao walipata mateso makali ya kulazimishwa wafuate dini moja tu.
Mahali po pote ambapo tamaa ya mgeuzo mkuu ilitia mizizi, mali na nyanja za kanisa zilikaziwa macho. Katika muda wa miake minne tu, ufalme wa Uingereza ulinyakua makao ya kitawa 560, mengine yayo yakiwa na mapato makubwa sana. Nchi nyingine ziliona wafalme na pia watu wa kawaida tu wakichukua sehemu za ardhi ya kanisa ziwe zao. Wakati Roma yenyewe ilipoporwa kweli kweli, ukatili ulikuwa hauna mipaka. “Uhayawani na kiu ya damu ya washambulizi hao ‘ungaliweza kufanya jiwe liwe na huruma,’ “ndivyo Barbara Tuchman anavyosimulia jambo hilo. “Kelele za vilio na miguno zilijaza kila upande; ule Mto Tiber ulielea miili iliyokufa.” Walio wachache, Wakatoliki na Waprotestanti, waliteswa kinyama pia. Katika Bohemia, Waprotestanti walinyang’anywa umiliki wa nchi yao, na katika Ailandi ilikuwa zamu ya Wakatoliki kutendwa hivyo. Wahuguenoti waliokuwa Wafaransa wa Kiprotestanti waliwindwa-windwa, kama walivyofanyiwa Wapresbiteri Waskochi na Wapuriti Waingereza. Ilionekana kama kwamba zamu-zamu za machinjo ya kijinga zilikuwa zimeanzishwa, na dini ndiyo iliyokuwa kichocheo kikuu. Je! matendo ya kinyama hayo hayangekoma kamwe?
Kanisa halikuchukua hatua ya kutaka amani. Lakini wale watawala, kwa kuchoshwa na mfululizo wenye hasira wa vita ya wenyewe kwa wenyewe, walifikia mapatano ambayo yaliweka rasmi mipaka kati ya imani zinazopingana. Ile Amani ya Augsburg katika 1555 na ile Amani ya Westphalia katika 1648 ilileta mipaka ya kidini na kitaifa katika upatano, ikaruhusu mwana-mfalme wa mahali penye kuhusika aamue ni imani gani ambayo halaiki ya watu wake wangefuata. Hivyo Ulaya ilianza kipindi kipya, ambacho kingeendelea kwa miaka yapata 300. Mwishoni mwa Vita ya Ulimwengu ya Pili ndipo maongozi katika Ulaya yangefanywa upya kabisa na Mataifa Marafiki waliokuwa washindi wakati huo.
Tamaa kubwa ya uhuru wa kidini na mgeuzo mkuu ilikuwa imekuza mkazo nyuma ya lile bwawa la kizuizi cha kanisa. Baada ya karne za kizuizi kisicholegezwa, mwishowe yale maji yalipasua njia yakibubujika, yakaporomoka yakijipinda-pinda kupita katika mabonde ya Ulaya, yakiacha nyuma mandhari iliyoharibiwa. Mfuriko huo wa maji ulipotulia, mwongozo katika mambo ya imani katika nchi za Kiprotestanti ulikuwa umefagiliwa mbali kutoka kwa viongozi wa kidini na watu wa kawaida wakatafuta utulivu kwenye mamlaka za kilimwengu. Ingawa hivyo, Ulaya ilikuwa bado imeingia sana katika matendo ya kutovumilia dini na watoro walikimbia kutoka nchi moja kwenda nyingine. Bara lile halikuweza tena kuzuia maji yale yaliyofunguka. Maji hayo ya mzidio yalianza kumwagika ng’ambo. Karne ya 17 ilitoa njia ya furiko hilo. Lile bara lililovumbuliwa kuwa Ulimwengu Mpya lilikuwa likifanywa kuwa koloni.
Maji ya Mzidio Yaelekezwa Ng’ambo
“Moja ya sababu zile kubwa-kubwa za uhamaji wa kwanza-kwanza wa kwenda Amerika,” anaandika A. P. Stokes katika Church and State in the United States, “ilikuwa tamaa ya uhuru wa kidini.” Watu walikuwa wamechoka kunyanyaswa-nyanyaswa. Wabaptisti, Wakweka, Wakatoliki Waroma, Wahuguenoti, Wapuriti, Wamenoni, na wengine wote walikuwa na nia ya kuchukuliana na magumu makali ya safari ile na kujitupa ndani ya eneo lisilojulikana. Stokes ananakili mmoja kuwa akisema: “Mimi nilitamani sana nchi ambako mimi ningeweza kuwa huru kuabudu Mungu kulingana na yale ambayo Biblia ilinifunza mimi.” Kipimo cha matendo mabaya ya kutovumiliwa ambayo wahamiaji hao waliacha nyuma kinaweza kukadiriwa kwa magumu ambayo wao walikuwa na nia ya kuvumilia. Kulingana na mwanahistoria David Hawke katika The Colonial Experience, inaelekea kwamba mwondoko wenye kuumiza moyo kutoka nchi ya nyumbani ungeelekea kufuatwa na “miezi miwili, mitatu au minne ya kutazamia kila siku kuzamishwa na mawimbi na kupatwa na maharamia wakatili.” Baada ya hapo, msafiri yule mwenye kudhoofishwa sana na hali ya hewa angejikuta “miongoni mwa Wahindi wenye tabia za kishenzi, wenye sifa kubwa ya ukatili mtupu . . . [na angebaki] katika hali ya njaa kwa muda mrefu.”
Watu mmoja mmoja walijitahidi kufikia uhuru, na mamlaka za kikoloni zikajitahidi kufikia utajiri. Bila kujali kusudio lilikuwa nini, walowezi walienda pamoja na dini yao wenyewe. Ujeremani, Uholanzi, na Uingereza zilifanya Amerika ya Kaskazini ikawa ngome ya Kiprotestanti. Hususa serikali ya Uingereza ilitaka “kuzuia Ukatoliki wa Roma . . . usitawale katika Amerika ya Kaskazini.” Kanada ilikuja chini ya maongozi ya zote Ufaransa na Uingereza. Mwongozo wa serikali ya Kifaransa ulikuwa ule wa “kuendeleza New France katika imani ya Katoliki ya Roma,” hata kukataa kuruhusu Wahuguenoti wahame kwenda Quebec. Kusini mwa Afrika na sehemu za Afrika ya magharibi zilikuja chini ya maongozi pia ya Kiprotestanti. Maongozi hayo yaliongezeka kadiri wakati ulivyoendelea kupita huku Australia, New Zealand, na visiwa vingi vya Pasifiki vikiongezwa kwenye zizi la Kiprotestanti.
Tayari Hispania na Ureno zilikuwa zikikatolikisha Amerika ya Kusini na ya Kati. Wafaransa na Wareno waliinua beramu ya Kikatoliki katika Afrika ya Kati. Katika India, Goa ilikuwa chini ya uongozi wa Kireno, kwa hiyo Ukatoliki ukatia mizizi kule.
Sosaiti ya Yesu (Wayesuiti) ilifanyizwa katika karne ya 16 kusongeza mbele kusudi la Kikatoliki. Kufikia katikati ya karne ya 18, kulikuwa na Wayesuiti zaidi ya 22,000 wakifanya kazi katika sehemu zote za tufe hili, na wao hata waliimarisha maongozi ya Kikatoliki katika China na Japani.
Ile Tamasha Mpya
Maji yanayobubujika yana nguvu nyingi ajabu, kama vile shahidi aliyenakiliwa kwenye mwanzo wa makala hii alivyoshuhudia. Yanatandaza mandhari za nchi, yanachonga mabonde na magenge mapya, yanabomoa-bomoa vipingamizi vilivyo katika mahali yanapopita. Bubujiko linalopita kwa kishindo halina wa kulisimamia, haliwezi kuzuiwa au kuelekezwa. Ndivyo hasa ilivyokuwa kuhusu ile gharika ya Mgeuzo Mkuu wa Kidini.
“Jambo lililotukia . . . basi, halikuwa hasa kushinda kwa imani mpya ya waliojitenga,” anasema G. R. Elton katika The Reformation Crisis, “bali ni kukubaliwa kwa ujumla na kwa polepole kwa Jumuiya ya Wakristo iliyogawanyika ambayo hakuna mtu aliyekuwa ameitaka.” Jumuiya ya Wakristo iligawanyika, ikasukwa-sukwa na dhoruba, ikafyonzwa nguvu zayo. Watu walishikamana karibu zaidi na watawala wa kwao na makanisa madogo zaidi ya kitaifa. Ule utawala uliokuwa umethibitishwa kwa muda mrefu kutoka Roma ukawa umedhoofishwa. Utukuzo wa taifa ulitia mizizi katika mandhari ya nchi iliyokolea Uprotestanti. Uingereza na United States, ambazo zilikuwa zimeshikwa kwa imara katika mikono ya viongozi wa kilimwengu Waprotestanti, zilifanyiza zikiwa pamoja ile serikali kubwa ya saba ya ulimwengu katika historia ya Biblia, zikichukua usukani katika karne ya 18.
Hata hivyo, ile harakati ya Mgeuzo Mkuu wa Kidini haikufanya jambo lile lile ambalo lilikuwa limetumainiwa kwamba yangelitimiza. Lilikuwa jambo gani hilo? Wakati ulipoendelea kupita, mafundisho ya msingi ya makanisa ya Kiprotestanti, yawe ni makanisa ya kitaifa au mengineyo, yalipatana kwa sehemu kubwa pamoja na yale ya Roma. Wafanya-mgeuzo wale wa kwanza-kwanza walikuwa wametazamia sana kurudi kwenye viwango vya Biblia, kwenye Ukristo safi. Lile wimbi la kuungwa mkono lilipoendelea kuongezeka ukubwa na mwendo, mvurugiko wa mwelekezo ulizimisha kabisa matazamio hayo.
Yale mawimbi mazito ya maji yenye kuja polepole ya Mgeuzo Mkuu wa Kidini umeacha nyuma mitaro hata katika karne yetu ya 20. Je! wewe unaweza kutambua baadhi ya mitaro hiyo? Jambo la maana hata zaidi, sisi tumesimama katika ukingo wa badiliko kubwa la kidini litakalokuwa la mwisho kabisa kutukia ulimwenguni pote. Tokeo la matendo ya zamani ya dini linaendelea kuifikilia. Basi je! wewe utaendelea kuwa hai utazame sana upeo mpya huo? Maswali hayo yatajibiwa katika toleo moja la Novemba la gazeti hili.