Sura 13
Yale Mapinduzi Makubwa ya Kidini
1, 2. (a) Kitabu kimoja juu ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini chasimuliaje Kanisa Katoliki la Roma la enzi za katikati? (b) Ni maswali gani yanayotokezwa kuhusu hali ya Kanisa la Roma?
MSIBA halisi wa kanisa la enzi za katikati ni kwamba lilishindwa kusonga kwa kuambatana na nyakati. . . . Tofauti sana na kuwa lenye maendeleo, tofauti sana na kutoa uongozi wa kiroho, lilirudi nyuma na kuzorota, likafisidika katika washiriki walo wote.” Ndivyo kinavyosema kitabu The Story of the Reformation juu ya Kanisa Roma Katoliki lenye nguvu nyingi, ambalo lilikuwa limetawala sehemu kubwa ya Ulaya kuanzia karne ya 5 mpaka karne ya 15 W.K.
2 Kanisa la Roma liliangukaje kutoka cheo chalo cha nguvu zote likawa ‘limezorota na kufisidika’? Upapa ambao ulidai mwandamano wa kimitume, ulishindwaje hata kutoa “uongozi wa kiroho”? Na tokeo la kushindwa huko lilikuwa nini? Ili kupata majibu, twahitaji kuchunguza kifupi lilikuwa limekuwa kanisa la aina gani na ni fungu gani lililotimiza katika jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu wa kweli.
Kanisa Ladidimia
3. (a) Ni nini iliyokuwa hali ya kimwili ya Kanisa la Roma kufikia mwisho wa karne ya 15? (b) Kanisa hilo lilijaribuje kudumisha utukufu walo?
3 Kufikia mwisho wa karne ya 15, Kanisa la Roma, lenye parishi, makao ya watawa wa kiume, na makao ya watawa wa kike katika milki yalo yote, lilikuwa limekuwa kabaila mkubwa zaidi katika Ulaya yote. Iliripotiwa kwamba lilimiliki kufikia nusu ya ardhi katika Ufaransa na Ujerumani na sehemu mbili kwa tano au zaidi katika Sweden na Uingereza. Tokeo likawa nini? “Fahari ya Roma ilikua kwa kadiri kubwa wakati wa miaka ya baadaye ya 1400 na mapema 1500, na umaana wayo wa kisiasa ulisitawi kwa muda,” chasema kitabu A History of Civilization. Hata hivyo, utukufu wote huo uliambatana na bei fulani, na ili kuudumisha, upapa ulipaswa kutafuta vyanzo vipya vya mapato. Akieleza njia mbalimbali zilizotumiwa, mwanahistoria Will Durant aliandika:
“Kila aliyewekwa na kanisa alitakwa apelekee Baraza la kipapa—wakala za usimamizi za kipapa—nusu ya mapato ya ofisi yake kwa mwaka wa kwanza (“malimbuko”), na baada ya hapo kila mwaka sehemu moja ya kumi au zaka. Askofu mkuu mpya alipaswa kulipa papa kiasi kikubwa kwa ajili ya vazi la kikasisi—ukumbuu wa sufu nyeupe uliotumika kuwa uthibitisho na alama ya mamlaka yake. Alipokufa kardinali, askofu mkuu, askofu mdogo, au abati yeyote, mali zake za kibinafsi zilirudia upapa. . . . Kila hukumu au pendeleo lililopatikana kutoka kwa Baraza la kipapa lilitaka shukrani za zawadi, na nyakati nyingine hukumu hiyo iliamuliwa na zawadi hiyo.”
4. Utajiri uliokuwa ukija kwenye kanisa uliathirije upapa?
4 Fedha nyingi zilizomiminika kwenye makasha ya kipapa mwaka baada ya mwaka hatimaye ziliongoza kwenye ufujaji na ufisadi. Imesemekana kwamba ‘hata papa hawezi kugusa lami akose kuchafua vidole vyake,’ na historia ya kanisa ya kipindi hiki ilipatwa na ambacho mwanahistoria mmoja aliita “uandamizi wa mapapa walio wa kilimwengu kweli kweli.” Kati yao alikuwamo Sixtus 4 (papa, 1471-84), ambaye alitumia kiasi kikubwa cha fedha kujenga Sistine Chapel, ambacho kilipewa jina lake, na ili kutajirisha wapwa wake wengi wa kiume na kike; Alexander 6 (papa, 1492-1503), Rodrigo Borgia mwenye sifa mbaya, aliyewakiri na kuwapandisha cheo watoto haramu wake; na Julius 2 (papa, 1503-13), mpwa wa Sixtus 4, aliyejitoa zaidi kwa vita, siasa, na sanaa kuliko kwa wajibu wake wa kikanisa. Ilikuwa kwa haki kabisa kwamba Erasmus msomi Mholanzi wa Katoliki aliandika hivi katika 1518: “Kukosa aibu kwa Baraza la kipapa la Roma kumefikia upeo.”
5. Maandishi ya enzi hizo yalionyesha nini kuhusu mwenendo wa kiadili wa makasisi?
5 Ufisadi na ukosefu wa adili haukuwa wa upapa tu. Usemi wa kawaida wa wakati huo ulikuwa huu: “Ukitaka kumharibu mwana wako, mfanye kasisi.” Hilo laungwa mkono na maandishi ya wakati huo. Kulingana na Durant, katika Uingereza, miongoni mwa “mashtaka ya utovu wa kujizuia [kingono] yaliyofikishwa mahakamani katika 1499, . . . wakosaji wa kikasisi walifikia hesabu ya kama asilimia 23 ya yote, ingawa makasisi yawezekana walipungua asilimia 2 ya idadi ya watu. Baadhi ya wenye kuungamisha watu dhambi waliomba-omba hisani za kingono kwa wenye kutubu walio wa kike. Maelfu ya makuhani walikuwa na masuria; katika Ujerumani ilikuwa karibu wote.” (Linganisha 1 Wakorintho 6:9-11; Waefeso 5:5.) Kuzorota kwa adili kulifikia sehemu nyingine pia. Mhispania mmoja wa wakati huo yasemekana alilalamika hivi: “Mimi naona hatuwezi kupata chochote kutoka kwa wahudumu wa Kristo isipokuwa kwa fedha tu; kwenye ubatizo ni fedha . . . kwenye ndoa ni fedha, kwa ajili ya kitubio ni fedha—la, hakuna sakramenti ya kuwaombea na kuwapaka mafuta walio karibu kufa [sherehe za mwisho] bila ya fedha! Wao hawatapiga kengele bila ya fedha; hakuna maziko katika kanisa bila ya fedha; hivyo yaonekana kwamba Paradiso imefungwa kwa wale wasiokuwa na fedha.”—Linganisha 1 Timotheo 6:10.
6. Machiavelli alisimuliaje juu ya Kanisa la Roma? (Warumi 2:21-24)
6 Ili kujumlisha hali ya Kanisa la Roma mwanzoni mwa karne ya 16, twanukuu maneno ya Machiavelli, mwanafalsafa Mwitalia ajulikanaye sana wa kipindi hicho:
“Kama kanisa la Kikristo lingalihifadhiwa kwa kulingana na amri za Mwanzilishi, hali na dola ya Jumuiya ya Wakristo vingalikuwa na umoja na furaha zaidi sana ya ilivyoko. Wala hakuwezi kuwako uthibitisho mkubwa zaidi wa mzoroto wayo kuliko uhakika wa kwamba kwa kadiri ambavyo watu wako karibu na Kanisa la Roma, kichwa cha dini yao, ndivyo wanavyozidi kuwa wasio wa kidini sana.”
Jitihada za Mapema za Mapinduzi Makubwa ya Kidini
7. Ni jitihada gani hafifu zilizofanywa na kanisa ili kurekebisha baadhi ya ufujaji?
7 Mzozo katika kanisa haukuonwa tu na watu kama Erasmus na Machiavelli bali pia na kanisa lenyewe. Baraza za Kanisa ziliitishwa ili kushughulikia baadhi ya malalamiko na ufujaji, lakini bila ya kuwapo matokeo ya kudumu. Mapapa, wakijifaidi na uwezo na utukufu wa kibinafsi, walivunja moyo jitihada zozote za kweli za kuleta upinduzi wa kidini.
8. Ni nini lililokuwa tokeo la upuuzaji wenye kuendelea wa kanisa?
8 Kama kanisa lingalichukua uzito wa kujisafisha lenyewe, yawezekana hakungalikuwako Mapinduzi Makubwa ya Kidini yoyote. Lakini, kama ilivyokuwa, vilio vya upinduzi wa kidini vilianza kusikiwa ndani na nje ya kanisa. Katika Sura 11 tumekwisha kutaja Wawaldo na Waalbigense. Ingawa walihukumiwa kuwa wazushi na kupondwa kwa ukatili, walikuwa wameamsha katika watu kutoridhika na ufujaji wa makasisi wa Katoliki na walikuwa wamechochea tamaa ya kurejea kwenye Biblia. Hisia hizo zilionyeshwa na idadi fulani ya Wapinduzi wa Kidini wa mapema.
Mateto Kutoka Ndani ya Kanisa
9. John Wycliffe alikuwa nani, naye alihubiri kupinga nini?
9 Mara nyingi akirejezewa kuwa “nyota ya asubuhi ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini,” John Wycliffe (1330?-84) alikuwa kuhani wa Katoliki na profesa wa theolojia kule Oxford, Uingereza. Akitambua sana ufujaji katika kanisa, yeye aliandika na kuhubiri kupinga mambo kama vile ufisadi katika madaraja ya watawa, ushuru wa kipapa, fundisho la kwamba mkate na divai inayotumiwa katika Misa hugeuka kihalisi kuwa mwili na damu ya Yesu Kristo, ungamo, na kujihusisha kwa kanisa katika mambo ya kilimwengu.
10. Wycliffe alionyeshaje ujitoaji wake kwa Biblia?
10 Hasa Wycliffe alitoboa mambo wazi ilipohusu kanisa kupuuza fundisho la Biblia. Pindi moja alijulisha rasmi hivi: “Kama tu Mungu angewezesha kila parishi ya kanisa katika bara hili iwe na Biblia nzuri na mafafanuzi mazuri juu ya gospeli, na kwamba makuhani wangejifunza vizuri hivyo, na kufundisha kikweli gospeli na amri za Mungu kwa watu!” Kwa kusudi hilo, Wycliffe, katika miaka ya mwisho ya maisha yake, alianza kazi ngumu ya kutafsiri Biblia ya Vulgate ya Kilatini katika Kiingereza. Kwa msaada wa washirika wake, hasa Nicholas wa Hereford, alitokeza Biblia kamili ya kwanza katika lugha ya Kiingereza. Bila shaka hiyo ilikuwa mchango mkubwa wa Wycliffe kwa jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu.
11. (a) Wafuasi wa Wycliffe waliweza kutimiza nini? (b) Ni nini kilichowapata Walollard?
11 Maandishi ya Wycliffe na visehemu vya Biblia yaligawanywa katika Uingereza yote na jamii ya wahubiri ambao mara nyingi walirejezewa kuwa “Makuhani Maskini” kwa sababu walizunguka wamevaa mavazi ya hali ya chini, wakiwa miguu mitupu, na bila ya mali za kimwili. Pia kwa kudhihakiwa waliitwa Walollard, kutokana na neno la Kiholanzi la Enzi za Kati Lollaerd, au “mtu anayenong’oneza sala au nyimbo za kidini.” (Brewer’s Dictionary of Phrase and Fable) “Kwa miaka michache, idadi zao ziliongezeka sana,” chasema kitabu The Lollards. “Ilikadiriwa kwamba angalau robo moja ya taifa kwa halisi au kwa jina walikuwa na mwelekeo wa hisia hizo.” Bila shaka, yote hayo hayakuendelea bila kuonwa na kanisa. Kwa sababu ya umaarufu wake miongoni mwa tabaka zenye kutawala na za wasomi, Wycliffe aliruhusiwa afe kwa amani kwenye siku ya mwisho ya 1384. Mambo hayakuwa mazuri hivyo kwa wafuasi wake. Wakati wa utawala wa Henry 4 wa Uingereza, walibandikwa jina wazushi, na wengi wao walifungwa gerezani, wakateswa, au kuteketezwa mpaka kufa.
12. Jan Hus alikuwa nani, naye alihubiri kupinga nini?
12 Mbohemia (Mchekoslovakia) Jan Hus (1369?-1415), pia kuhani Mkatoliki na rekta wa Chuo Kikuu cha Prague, alivutiwa sana na John Wycliffe. Kama Wycliffe, Hus alihubiri juu ya ufisadi wa Kanisa la Roma na kukazia umaana wa kusoma Biblia. Jambo hilo lilitokeza upesi hasira kali ya utawala wa kikasisi juu yake. Katika 1403 mamlaka ilimwagiza akome kuhubiri mawazo ya Wycliffe ya kupinga papa, ambaye vitabu vyake waliteketeza pia hadharani. Hata hivyo, Hus, aliendelea kuandika baadhi ya mashtaka yenye kuchoma zaidi kupinga mazoea ya kanisa, kutia ndani kuuza hati za rehema.a Alihukumiwa na kuondoshwa kwenye ushirika katika 1410.
13. (a) Ni kanisa gani ambalo Hus alifundisha kuwa la kweli? (b) Tokeo la uthabiti wa Hus lilikuwa nini?
13 Hus aliunga mkono Biblia bila kuridhiana. “Kuasi papa mwenye kukosa ni kutii Kristo,” akaandika. Pia yeye alifundisha kwamba kanisa la kweli, tofauti kabisa ya kuwa ni papa na tengenezo la Kiroma, “ni hesabu ya wateule wote na mwili wa kifumbo wa Kristo, ambao kichwa chao ni Kristo; na bibi-arusi wa Kristo, ambaye kwa upendo mkuu wake alimkomboa kwa damu yake mwenyewe.” (Linganisha Waefeso 1:22, 23; 5:25-27.) Kwa sababu ya yote hayo, alijaribiwa kwenye Baraza la Konstansi na kuhukumiwa kuwa mzushi. Akijulisha rasmi kwamba “ni afadhali kufa vizuri kuliko kuishi ukiugua,” yeye alikataa kutangua maneno yake akachomwa mpaka kufa kwenye mti katika 1415. Baraza lilo hilo liliagiza kwamba mifupa ya Wycliffe ifukuliwe na kuchomwa hata ingawa alikuwa amekufa na kuzikwa kwa miaka zaidi ya 30!
14. (a) Girolamo Savonarola alikuwa nani? (b) Savonarola alijaribu kufanya nini, na tokeo likawa nini?
14 Mpinduzi wa Kidini mwingine wa mapema alikuwa ni mtawa wa kiume Mdominika Girolamo Savonarola (1452-98) wa makao ya watawa wa kiume ya San Marcos katika Florence, Italia. Kwa kuchukuliwa na roho ya Mfufuo wa Harakati za Italia, Savonarola alinena juu ya ufisadi katika Kanisa na Serikali pia. Akidai Andiko kuwa msingi wake, na pia njozi na mafunuo mbalimbali ambayo alisema alikuwa amepokea, yeye alijaribu kusimamisha serikali ya Kikristo, au utaratibu wa kitheokrasi. Katika 1497 papa alimwondosha kwenye ushirika. Mwaka uliofuata, yeye alikamatwa, akateswa, na kunyongwa. Maneno yake ya mwisho yalikuwa: “Bwana wangu alikufa kwa ajili ya dhambi zangu; je! mimi nisiutoe kwa furaha uhai wangu huu wa kimaskini kwa ajili yake?” Mwili wake ulichomwa na majivu yakatupwa ndani ya mto Arno. Kwa kufaa, Savonarola alijiita “mtangulizi na dhabihu.” Miaka michache tu baadaye, Mapinduzi Makubwa ya Kidini yalichomoka kwa nguvu kubwa katika Ulaya yote.
Nyumba Iliyogawanyika
15. Jumuiya ya Wakristo katika Ulaya ya Magharibi iligawanywaje na chama cha Mapinduzi Makubwa ya Kidini?
15 Wakati tufani ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini ilipotokea hatimaye, ilivunja-vunja nyumba ya kidini ya Jumuiya ya Wakristo katika Ulaya ya Magharibi. Baada ya kuwa chini ya karibu utawala kamili wa Kanisa Roma Katoliki, sasa ikawa nyumba iliyogawanyika. Ulaya ya Kusini—Italia, Hispania, Austria, na sehemu za Ufaransa—kwa sehemu kubwa zilibaki za Katoliki. Sehemu ile nyingine ikawa migawanyo mitatu mikubwa: Lutheri katika Ujerumani na Scandinavia; Ukalvini (au wa Mapinduzi ya Kidini) katika Switzerland, Uholanzi, Scotland, na sehemu za Ufaransa; na Anglikana katika Uingereza. Vikiwa vimetawanyika miongoni mwa hivyo vilikuwa vikundi vidogo zaidi lakini vyenye kutaka mapinduzi zaidi, kwanza Waanabaptisti na baadaye Wamennoni, Wahuteri, na Wapiuriti, ambao muda si muda walipeleka imani zao kule Amerika ya Kaskazini.
16. Hatimaye, ni nini kilichoipata nyumba ya Jumuiya ya Wakristo? (Marko 3:25)
16 Kwa kadiri miaka ilivyopita, migawanyo hiyo mikubwa ilivunjika-vunjika zaidi kuwa mamia ya madhehebu ya leo—Upresbiteri, Uepiskopo, Umethodisti, Ubaptisti, Ukongrigeshonali, tukitaja michache tu. Jumuiya ya Wakristo ikawa nyumba iliyogawanyika kweli kweli. Migawanyo hiyo ilitokeaje?
Lutheri na Hoja Zake
17. Ni nini kinachoweza kutolewa kuwa chanzo rasmi cha Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya Uprotestanti?
17 Ikiwa chanzo mkataa cha Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya Kiprotestanti chapasa kutolewa, kingekuwa ni Oktoba 31, 1517, wakati Martin Lutheri (1483-1546) mtawa wa kiume Mwagustino alipogongomea hoja zake 95 kwenye mlango wa kanisa la buruji kule Wittenberg katika wilaya ya Kijerumani ya Saksoni. Hata hivyo, ni nini kilichochokora tukio hilo kubwa? Martin Lutheri alikuwa nani? Naye alipinga nini?
18. (a) Martin Lutheri alikuwa nani? (b) Ni nini kilichomsukuma Lutheri atoe hoja zake?
18 Kama vile Wycliffe na Hus waliomtangulia, Martin Lutheri alikuwa msomi mtawa wa kiume. Pia yeye alikuwa mtaalamu wa theolojia na profesa wa mafunzo ya Kibiblia kwenye Chuo Kikuu cha Wittenberg. Lutheri alijifanyia jina kweli kweli kwa mwono-ndani wake wa Biblia. Ingawa alikuwa na maoni yenye nguvu kwa habari ya wokovu, au kuhesabiwa haki, kupitia imani badala ya matendo au kwa toba, yeye hakuwa na wazo la kujitenga na Kanisa la Roma. Kwa kweli, utoaji wa hoja zake ulikuwa ni kupinga kwake kisa fulani wala haukuwa uasi uliopangwa. Yeye alikuwa akipinga kuuzwa kwa hati za rehema.
19. Katika wakati wa Lutheri, hati za rehema zilitumiwaje vibaya?
19 Katika wakati wa Lutheri, hati za rehema za kipapa ziliuzwa hadharani si kwa ajili tu ya walio hai bali pia kwa ajili ya waliokufa. “Mara tu sarafu katika kasha inapolia, nafsi kutoka Purgatori huruka” ulikuwa ni usemi wa kawaida. Kwa makabwela, hati za rehema ikawa karibu ni sera ya bima ya adhabu kwa dhambi yoyote, na toba ikatupiliwa mbali. “Kila mahali,” akaandika Erasmus, “msamaha wa mateso ya purgatori unauzwa; na hauuzwi tu, bali pia wale wanaoukataa hulazimishwa.”
20. (a) Ni kwa nini John Tetzel alienda Jüterbog? (b) Itikio la Lutheri lilikuwa nini kuhusu uuzaji wa hati za rehema wa Tetzel?
20 Katika 1517 John Tetzel, mtawa wa kiume Mdominika, alienda Jüterbog, karibu na Wittenberg, akauze hati za rehema. Fedha zilizopatikana kwa kufanya hivyo zilikuwa za kugharimia kwa sehemu kujengwa upya kwa St. Peter’s Basilica katika Roma. Pia zilikuwa za kusaidia Albert wa Brandenburg arudishe fedha alizokuwa ameazima ili alipe Baraza la kipapa la Roma limpe cheo cha askofu mkuu wa Mainz. Tetzel akatumia ufundi wake wote wa uuzaji, na watu wakamiminika kwake. Lutheri alikasirika sana, naye akatumia njia ya haraka zaidi iliyokuwapo ili kueleza hadharani maoni yake juu ya jambo hilo lililo mfano wa sarakasi—kwa kugongomea mambo 95 ya mjadala juu ya mlango wa kanisa.
21. Ni hoja gani alizotumia Lutheri kupinga uuzaji wa hati za rehema?
21 Lutheri aliziita hoja zake 95 Uteti wa Kutaka Maelezo ya Wazi Kuhusu Nguvu za Hati za Rehema. Kusudi lake halikuwa hasa kupinga mamlaka ya kanisa bali kuonyesha kupita kiasi na ufujaji unaohusu kuuzwa kwa hati za rehema za kipapa. Hilo laweza kuonekana kutokana na hoja zifuatazo:
“5. Papa hana nia wala uwezo wa kutoa adhabu, isipokuwa ile ambayo yeye amelazimisha kwa mamlaka yake mwenyewe. . . .
20. Kwa hiyo papa, anaponena juu ya msamaha kamili wa adhabu zote, hamaanishi zote kikweli, bali zile alizoweka mwenyewe. . . .
36. Kila Mkristo anayehisi lawama la kikweli ana haki ya kupata msamaha kamili kutokana na adhabu na hatia hata bila ya barua za msamaha.”
22. (a) Ni nini kilichositawi kwa kadiri ujumbe wa Lutheri ulivyoenea? (b) Ni nini kilichotukia katika 1520 kuhusiana na Lutheri, na tokeo likawa nini?
22 Kwa kusaidiwa na mashine ya uchapaji iliyokuwa imebuniwa juzijuzi, mawazo hayo moto-moto hayakuchukua muda mrefu kufikia sehemu nyingine za Ujerumani—na Roma. Jambo lililoanza kama mjadala wa kiusomi juu ya kuuzwa kwa hati za rehema upesi likawa ubishi juu ya mambo ya imani na mamlaka ya kipapa. Kwanza, Kanisa la Roma lilifanya mjadala na Lutheri na kumwagiza atangue maneno yake. Lutheri alipokataa, mamlaka za kikanisa na za kisiasa zilitumiwa ili kumkaza. Katika 1520 papa alitoa tangazo, au amri iliyokataza Lutheri kuhubiri na akaagiza vitabu vyake vichomwe. Kwa kukaidi Lutheri alichoma tangazo hilo la kipapa hadharani. Papa alimwondosha kwenye ushirika katika 1521.
23. (a) Baraza la Worms lilikuwa nini? (b) Lutheri alitoaje taarifa ya msimamo wake kule Worms, na tokeo likawa nini?
23 Baadaye mwaka huo, Lutheri aliagizwa aje kwenye baraza, au kusanyiko, kule Worms. Alihukumiwa na Charles 5 maliki wa Milki Takatifu ya Roma, Mkatoliki shupavu, na pia wateule sita wa wilaya za Ujerumani, na viongozi na waadhamu wengine, wa kidini na wa kiserikali. Alipokazwa tena atangue maneno yake, Lutheri alitoa taarifa yake ijulikanayo sana: “Isipokuwa nionyeshwe na Andiko na sababu ya wazi kuwa nina hatia . . . , siwezi wala sitatangua lolote, kwa maana kutenda kinyume cha dhamiri si sawa wala si salama. Mungu nisaidie. Ameni.” Kwa sababu hiyo, maliki akajulisha rasmi kuwa yeye ni haramu. Hata hivyo, Mteule Frederick wa Saksoni, mtawala wa wilaya yake mwenyewe ya Ujerumani, akaja kumsaidia na kumpa makao katika buruji ya Wartburg.
24. Lutheri alitimiza nini alipokuwa katika buruji ya Wartburg?
24 Hata hivyo, hatua hizo zilishindwa kuzuia kuenea kwa mawazo ya Lutheri. Kwa miezi kumi, akiwa katika usalama wa Wartburg, Lutheri alijitoa kuandika na kutafsiri Biblia. Alitafsiri Maandiko ya Kigiriki katika Kijerumani kutokana na maandishi ya Kigiriki ya Erasmus. Maandiko ya Kiebrania yalifuata baadaye. Biblia ya Lutheri ikawa ndicho kitu tu walichohitaji makabwela. Iliripotiwa kwamba “nakala elfu tano ziliuzwa kwa miezi miwili, elfu mia mbili katika miaka kumi na miwili.” Uvutano wayo kwa lugha na utamaduni wa Kijerumani hulinganishwa mara nyingi na ule wa King James Version juu ya Waingereza.
25. (a) Jina Protestanti liliundwaje? (b) Ungamo la Augsburg lilikuwa nini?
25 Katika miaka iliyofuata Baraza la Worms, chama cha Mapinduzi Makubwa ya Kidini kiliungwa mkono na wengi mno hata kwamba katika 1526 maliki alitunuka kila wilaya ya Kijerumani haki ya kuchagua namna yao ya dini, ya Kilutheri au ya Katoliki ya Roma. Hata hivyo, katika 1529, wakati maliki alipotangua uamuzi huo, baadhi ya wakuu Wajerumani walifanya protesti (kuteta); ndivyo lilivyoundwa jina Protestanti kuhusu chama hicho cha Mapinduzi Makubwa ya Kidini. Mwaka uliofuata, 1530, kwenye Baraza la Augsburg, jitihada ilifanywa na maliki ya kumaliza tofauti kati ya vikundi hivyo viwili. Walutheri walieleza imani zao katika hati, Ungamo la Augsburg, iliyotungwa na Philipp Melanchthon lakini ikitegemea mafundisho ya Lutheri. Ingawa hati hiyo ilikuwa yenye lugha ya kutafuta usikizano, Kanisa Katoliki liliikataa, na ufa kati ya Uprotestanti na Ukatoliki ukawa usioweza kuzibika. Wilaya nyingi za Ujerumani zikajiunga na Lutheri, na wilaya za Skandinavia upesi zikafanya vivyo hivyo.
Upinduzi wa kidini au Uasi?
26. Kulingana na Lutheri, mambo ya msingi ya kugawanya Uprotestanti na Ukatoliki yalikuwa nini?
26 Ni nini yaliyokuwa mambo ya msingi yaliyogawanya Waprotestanti na Wakatoliki wa Roma? Kulingana na Lutheri, yalikuwa matatu. Kwanza, Lutheri aliamini kwamba wokovu hutokana na “kuhesabiwa haki kwa imani pekee” (Kilatini, sola fide)b wala si kutokana na msamaha wa kikuhani wala kazi ya toba. Pili, alifundisha kwamba msamaha hutolewa kwa sababu tu ya rehema ya Mungu (sola gratia) wala si kwa mamlaka ya makuhani au mapapa. Mwishowe, Lutheri alishikilia kwamba mambo yote ya kimafundisho lazima yathibitishwe na Maandiko tu (sola scriptura) wala si na mapapa wala baraza za kanisa.
27. (a) Ni mafundisho na mazoea gani ya Kikatoliki yasiyo ya kimaandiko yaliyodumishwa na Waprotestanti? (b) Ni mabadiliko gani waliyodai Waprotestanti?
27 Ijapokuwa hayo, The Catholic Encyclopedia chasema Lutheri “alidumisha nyingi za imani na sherehe za kidini za kale ambazo zingeweza kufanywa zifaane na maoni ya kivyake juu ya dhambi na kuhesabiwa haki.” Ungamo la Augsburg latoa taarifa kuhusu imani ya Kilutheri kwamba “hakuna jambo lolote linalohitilafiana na Maandiko, wala na Kanisa Katoliki, au hata Kanisa la Kiroma, kwa kadiri ambayo Kanisa hili lajulikana na waandikaji.” Kwa kweli, imani ya Kilutheri, kama ilivyoelezwa katika Ungamo la Augsburg, ilitia ndani mafundisho yasiyo ya kimaandiko kama vile Utatu, nafsi isiyoweza kufa, mateso ya milele, na pia mazoea kama ubatizo wa watoto wachanga na sikukuu na karamu za kanisa. Kwa upande ule mwingine, Walutheri walidai mabadiliko kadhaa, kama vile watu waruhusiwe wapokee divai na mkate kwenye Komunyo na kwamba kutofunga ndoa, nadhiri za kitawa, na ungamo la lazima vitanguliwe.c
28. Mapinduzi Makubwa ya Kidini yalifaulu katika jambo gani, nayo yalishindwa katika jambo gani?
28 Kwa ujumla, Mapinduzi Makubwa ya Kidini, kama yalivyotetewa na Lutheri na wafuasi wake, yalifaulu kujiondoa kwenye kongwa la kipapa. Hata hivyo, kama alivyotoa taarifa Yesu kwenye Yohana 4:24, “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” Yaweza kusemwa kwamba kwa habari ya Martin Lutheri, jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu wa kweli ilichukua mgeuko mpya tu; njia nyembamba ya ukweli ilikuwa ingali mbali mno.—Mathayo 7:13, 14; Yohana 8:31, 32.
Upinduzi wa kidini wa Zwingli katika Switzerland
29. (a) Ulrich Zwingli alikuwa nani, naye alihubiri kupinga nini? (b) Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya Zwingli yalikuwaje tofauti na ya Lutheri?
29 Lutheri alipokuwa akishughulika kupambana na wajumbe wa kipapa na mamlaka za kiserikali katika Ujerumani, kuhani Mkatoliki Ulrich Zwingli (1484-1531) alianzisha chama chake cha upinduzi wa kidini katika Zurich, Switzerland. Eneo hilo likiwa lenye kusema Kijerumani, tayari watu walikuwa wameathiriwa na wimbi la upinduzi wa kidini kutoka kaskazini. Karibu 1519, Zwingli alianza kuhubiri kupinga hati za rehema, ibada ya Mariamu, kutofunga ndoa kwa makasisi, na mafundisho mengine ya Kanisa Katoliki. Ingawa Zwingli alidai hana uhusiano na Lutheri, alikubaliana na Lutheri katika mambo mengi na aligawanya trakti za Lutheri katika nchi yote. Hata hivyo, tofauti na Lutheri asiyetaka mabadiliko mengi, Zwingli alitetea kuondolewa kwa mabaki yote ya Kanisa la Kiroma—mifano, misalaba, kanzu za kikasisi, hata muziki wa sherehe za kidini.
30. Suala kuu lililogawanya Zwingli na Lutheri lilikuwa nini?
30 Hata hivyo, ubishi mkubwa zaidi kati ya Wapinduzi wa Kidini hao wawili, ulihusu suala la Ekaristi, au Misa (Komunyo). Lutheri, akisisitiza juu ya ufasiri halisi wa maneno ya Yesu, ‘Huu ni mwili wangu,’ aliamini kwamba mwili na damu ya Kristo vilikuwapo kimwujiza katika mkate na divai iliyoandaliwa kwenye Komunyo. Zwingli, kwa upande ule mwingine, alibisha, katika kitabu chake cha maelezo On the Lord’s Supper, kwamba taarifa ya Yesu “lazima ichukuliwa kitamathali au kimfano; ‘Huu ni mwili wangu,’ humaanisha, ‘Mkate ni ishara ya mwili wangu,’ au ‘ni tamathali ya mwili wangu.’” Kwa sababu ya tofauti hiyo, Wapinduzi wa Kidini hao wawili wakatengana.
31. Ni nini lililokuwa tokeo la kazi ya Zwingli katika Switzerland?
31 Zwingli aliendelea kuhubiri mafundisho yake ya upinduzi wa kidini katika Zurich na akatokeza mabadiliko mengi huko. Upesi majiji mengine yakafuata uongozi wake, lakini watu walio wengi katika maeneo ya mashambani, wakiwa wasiotaka mabadiliko mengi, walishikilia Ukatoliki. Pambano kati ya mafumukano hayo mawili likawa kubwa mno hata vita vya wenyewe kwa wenyewe vikazuka kati ya Waprotestanti wa Switzerland na Wakatoliki wa Roma. Zwingli, akitumika akiwa kuhani wa jeshi, aliuawa katika pigano la Kappel, karibu na Ziwa la Zug, katika 1531. Wakati amani ilipofika hatimaye, kila wilaya ilipewa haki ya kuamua namna yayo ya dini, Protestanti au Katoliki.
Waanabaptisti, Wamennoni, na Wahuteri
32. Waanabaptisti walikuwa nani, nao walipataje jina hilo?
32 Hata hivyo, Waprotestanti fulani walihisi kwamba, Wapinduzi wa Kidini hao hawakuchukua hatua za kutosha katika kukataa kasoro za kanisa la kipapa Katoliki. Waliamini kwamba kanisa la Kikristo lapasa kufanyizwa tu na waumini wenye kutenda waliobatizwa, badala ya watu wote katika jumuiya au taifa. Kwa hiyo, walikataa ubatizo wa watoto wachanga na kusisitiza juu ya mtengano kati ya Kanisa na Serikali. Kisiri-siri wakabatiza tena waumini wenzao na hivyo wakapata jina Waanabaptisti (ana maana yake “tena” katika Kigiriki). Kwa kuwa walikataa kutumia silaha, kula viapo, au kukubali wadhifa wa kiserikali, walionwa kuwa tisho kwa jamii wakanyanyaswa na Wakatoliki na Waprotestanti pia.
33. (a) Ni nini kilichoamsha kitendo chenye jeuri juu ya Waanabaptisti? (b) Uvutano wa Waanabaptisti ulieneaje?
33 Hapo kwanza Waanabaptisti waliishi katika vikundi vidogo-vidogo vilivyotawanyika katika sehemu za Switzerland, Ujerumani, na Uholanzi. Kwa kadiri walivyohubiri mambo waliyoamini kila mahali walikoenda, idadi zao ziliongezeka kwa kasi. Kikundi kimoja cha Waanabaptisti, kwa kusukumwa na msisimuko wacho wa kidini, kiliacha hali yacho ya kutofanya vita kikateka jiji la Münster katika 1534 na kujaribu kulisimamisha liwe Yerusalemu Jipya la shirika, na la ndoa ya wake wengi. Chama hicho kilikomeshwa upesi kwa jeuri kubwa. Hilo liliharibu jina la Waanabaptisti, na kwa ujumla wakamalizwa. Kwa halisi, Waanabaptisti walio wengi walikuwa makabwela wa kidini waliojaribu kuishi maisha ya peke yao na ya utulivu. Miongoni mwa wazao wa Waanabaptisti waliopangwa kitengenezo vizuri walikuwa ni Wamenonni, wafuasi wa Mpinduzi wa Kidini Mholanzi Menno Simons, na Wahuteri, chini ya Tyrolean Jacob Hutter. Ili kuepa mnyanyaso, baadhi yao walihamia Ulaya ya Mashariki—Poland, Hungary, hata Urusi—wengine mpaka Amerika Kaskazini, ambako hatimaye walitokea wakiwa jumuiya za Wahuteri na Waamishi.
Kutokea kwa Ukalvini
34. (a) John Calvin alikuwa nani? (b) Ni kitabu gani cha maana alichoandika?
34 Kazi ya upinduzi wa kidini katika Switzerland ilisonga mbele chini ya uongozi wa Mfaransa aliyeitwa Jean Cauvin, au John Calvin (1509-64), ambaye alipata mafundisho ya Uprotestanti wakati wa siku zake za uanafunzi katika Ufaransa. Katika 1534 Calvin aliondoka Paris kwa sababu ya mnyanyaso wa kidini akakaa katika Basel, Switzerland. Katika kutetea Waprotestanti, yeye alichapisha kichapo Institutes of the Christian Religion, ambamo alifanya muhtasari wa mawazo ya mababa wa kwanza wa kanisa na wanatheolojia wa enzi za kati, na pia yale ya Lutheri na Zwingli. Kitabu hicho kikaja kuonwa kuwa msingi wa kimafundisho kwa makanisa yote ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini yaliyoanzishwa baadaye katika Ulaya na Amerika.
35. (a) Maelezo ya Calvin yalikuwa nini juu ya fundisho lake la kuamuliwa kimbele na Mungu? (b) Ukali wa fundisho hilo ulionyeshwaje katika sehemu nyingine za fundisho la Calvin?
35 Katika Institutes, yeye alitokeza theolojia yake. Kwa Calvin, Mungu ndiye mwenye enzi kuu pekee, ambaye mapenzi yake huamua na kutawala juu ya kila kitu. Kinyume cha hilo, binadamu aliyeasi ni mwenye dhambi na hastahili kabisa. Kwa hiyo, wokovu, hautegemei matendo mema ya binadamu bali Mungu—kwa sababu hiyo, likatokea fundisho la Calvin la kuamuliwa kimbele na Mungu, ambalo juu yalo aliandika:
“Twasisitiza, kwamba kwa ushauri wa milele na usiobadilika, Mungu amekwisha amua kwa umilele wote, wale ambao Yeye atakubali wapate wokovu, na ambao Yeye atalaani kwa uharibifu. Twathibitisha kwamba ushauri huu, kwa kadiri unavyohusu wateule, msingi wao ni rehema Yake ya kupewa bila malipo, ambayo kwa ujumla haina uhusiano na ustahili wa binadamu; lakini kwamba kwa wale ambao Yeye hutolea, lango la uhai limefungwa na hukumu ya haki na isiyo na lawama, lakini isiyoeleweka.”
Ugumu wa fundisho hilo waonyeshwa katika mambo mengine pia. Calvin alisisitiza kwamba Wakristo lazima waishi maisha matakatifu ya wema, wakijiepusha si na dhambi tu bali pia anasa na uzembe. Zaidi ya hayo, yeye alibisha kwamba kanisa, lenye wateule, lazima liwekwe huru na vizuizi vyote vya kiserikali na kwamba jamii ya kimungu kikweli ingeweza kusimamishwa kupitia kwa kanisa tu.
36. (a) Calvin na Farel walijaribu kufanya nini katika Geneva? (b) Ni matakwa gani makali yaliyoanzishwa? (c) Ni nini tokeo moja lenye sifa mbaya la hatua za kupita kiasi za Calvin, naye aliteteaje vitendo vyake?
36 Muda mfupi baada ya kuchapisha Institutes, Calvin alishawishwa na William Farel, Mpinduzi wa Kidini mwingine kutoka Ufaransa, akae katika Geneva. Pamoja wakafanya kazi ya kutekeleza Ukalvini. Lengo lao lilikuwa ni kugeuza Geneva kuwa jiji la Mungu, theokrasi ya utawala wa Mungu wenye kuunganisha kazi za Kanisa na Serikali. Walianzisha matakwa makali, pamoja na vizuizi, vilivyohusu kila jambo tangu mafundisho ya kidini na ibada za kanisa mpaka adili za hadharani na hata mambo kama vile usafi na kuzuia moto. Maandishi fulani ya kihistoria yaripoti kwamba “kwa kielelezo, mtengeneza nywele mmoja, kwa sababu ya kupanga nywele za bibi-arusi katika njia iliyoonwa kuwa haifai, alifungwa gerezani kwa siku mbili; na mama yake, pamoja na marafiki wawili wa kike, waliokuwa wamesaidia katika hilo, walipewa adhabu iyo hiyo. Kucheza dansi na kucheza karata kulitolewa adhabu na hakimu.” Adhabu kali ilitolewa kwa wale waliotofautiana na Calvin juu ya theolojia, kisa chenye sifa mbaya zaidi kikiwa kile cha kuchoma Mhispania Miguel Serveto, au Michael Servetus.—Ona kisanduku, ukurasa 322.
37. Uvutano wa Calvin ulieneaje mbali kupita mipaka ya Switzerland?
37 Calvin aliendelea kutumikisha namna yake ya upinduzi wa kidini katika Geneva mpaka kifo chake katika 1564, na kanisa la Mapinduzi ya Kidini (Reformed) likaimarishwa. Wapinduzi wa Kidini Waprotestanti, wenye kutoroka mateso katika mabara mengine, walimiminika Geneva, wakatwaa mawazo ya Ukalvini, na wakawa vyombo vya kuanzisha vyama vya wapinduzi wa kidini katika mabara ya nyumbani kwao. Upesi Ukalvini ukaenea Ufaransa, ambako Wahugeunoti (kama ambavyo Waprotestanti wa Kikalvini Ufaransa walivyoitwa) walipatwa na mnyanyaso mkali mikononi mwa Wakatoliki. Katika Uholanzi, Wakalvini walisaidia kuanzisha Dutch Reformed Church. Katika Scotland, chini ya uongozi wa bidii wa aliyekuwa kasisi Mkatoliki John Knox, Kanisa Presbiteri la Scotland lilianzishwa kwa kufuatia mawazo ya Ukalvini. Ukalvini pia ulitimiza fungu fulani katika Mapinduzi Makubwa ya Kidini katika Uingereza, na kutoka huko ukaenda na Wapiuriti mpaka Amerika ya Kaskazini. Kwa maana hiyo, ingawa Lutheri alianzisha Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya Uprotestanti, Calvin ndiye aliyekuwa na uvutano mkubwa zaidi katika ukuzi wayo.
Mapinduzi Makubwa ya Kidini Katika Uingereza
38. Roho ya Uprotestanti ilichochewaje na kazi ya John Wycliffe?
38 Tofauti kabisa na vyama vya upinduzi wa kidini katika Ujerumani na Switzerland, mizizi ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya Uingereza yarudi nyuma mpaka siku za John Wycliffe, ambaye kuhubiri kwake kwa kupinga makasisi na mkazo juu ya Biblia kulichochea roho ya Uprotestanti katika Uingereza. Jitihada yake ya kutafsiri Biblia katika Kiingereza ilifuatwa na wengine. William Tyndale, ambaye alilazimika kutoroka Uingereza, alitokeza Agano Jipya lake katika 1526. Baadaye alisalitiwa katika Antwerp na kunyongwa kwenye mti, na mwili wake ukachomwa. Miles Coverdale alikamilisha kazi ya Tyndale ya kutafsiri, na Biblia kamili ikatokea katika 1535. Kuchapishwa kwa Biblia katika lugha ya watu bila shaka kulikuwa sababu moja yenye nguvu zaidi iliyochangia Mapinduzi Makubwa ya Kidini katika Uingereza.
39. Henry 8 alitimiza fungu gani katika Mapinduzi Makubwa ya Kidini kule Uingereza?
39 Kujitenga rasmi na Ukatoliki wa Roma kulitukia wakati Henry 8 (1491-1547), aliyeitwa na papa kuwa Mtetezi wa Imani, alipojulisha rasmi Mamlaka Kuu katika 1534, akijiweka mwenyewe kuwa kichwa cha Kanisa la Uingereza. Henry pia alifunga makao ya watawa na kugawanya mali yao miongoni mwa makabaila. Kuongezea hilo, yeye aliagiza kwamba nakala ya Biblia katika Kiingereza iwekwe katika kila kanisa. Hata hivyo, kitendo cha Henry kilikuwa cha kisiasa zaidi ya kuwa cha kidini. Alichotaka ni kutokuwa chini ya mamlaka ya kipapa, hasa kuhusu mambo yake ya kindoa.d Kidini alibaki Mkatoliki kwa jina.
40. (a) Ni mabadiliko gani yaliyotukia katika Kanisa la Uingereza wakati wa utawala wa Elizabeth 1? (b) Ni vikundi gani vyenye kuasi vilivyositawi hatimaye katika Uingereza, Uholanzi, na Amerika Kaskazini?
40 Ilikuwa wakati wa utawala mrefu (1558-1603) wa Elizabeth 1 ndipo Kanisa la Uingereza likawa la Kiprotestanti katika vitendo ingawa kwa muundo lilibaki la Kikatoliki kwa sehemu kubwa. Lilikomesha utii kamili kwa papa, kutofunga ndoa kwa makasisi, kuungama, na mazoea mengine ya Kikatoliki, hata hivyo lilihifadhi muundo wa kanisa wa namna ya kiepiskopo katika mfumo walo wa makasisi wa kuwa na maaskofu wakuu na maaskofu wadogo na pia madaraja mengine ya watawa wa kiume na wa kike.e Hali ya kutofanya mabadiliko ilisababisha kutoridhika kwingi, na vikundi vingi vyenye kupinga vikatokea. Wapiuriti walidai badiliko kamili zaidi ili kutakasa kanisa mazoea yote ya Katoliki ya Roma; Waseparitisti na Waindipendenti walisisitiza kwamba mambo ya kanisa yapasa kuongozwa na wazee wa mahali (mapresibaita). Wengi walioasi walitorokea Uholanzi au Amerika Kaskazini, ambako walisitawisha zaidi makanisa yao ya Kikongrigeshonali na Kibaptisti. Kukatokea pia katika Uingereza Society of Friends (Wakweka) chini ya George Fox (1624-91) na Wamethodisti chini ya John Wesley (1703-91).—Ona chati chini.
Matokeo Yalikuwa Nini?
41. (a) Kwa maoni ya wasomi fulani, Mapinduzi Makubwa ya Kidini yalikuwa na tokeo gani juu ya historia ya kibinadamu? (b) Ni maswali gani ya kufikiriwa kwa uzito?
41 Tukiwa tumekwisha chunguza matawi matatu makubwa ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini—Ulutheri, Ukalvini, na Uanglikana—ni lazima tutue na kukadiria yale ambayo Mapinduzi Makubwa ya Kidini yalitimiza. Haikanushiki, yalibadili mwendo wa historia ya ulimwengu wa nchi za Magharibi. “Tokeo la Mapinduzi Makubwa ya Kidini lilikuwa ni kukweza watu kwenye kiu ya uhuru na uraia wa juu zaidi na wenye kutakata zaidi. Kokote ambako madhumuni ya Uprotestanti yalienea, yalifanya umati wa watu uwe wenye kujidai zaidi,” akaandika John F. Hurst katika kitabu chake Short History of the Reformation. Wasomi wengi huamini kwamba ustaarabu wa Magharibi kama tuujuavyo leo haungaliwezekana bila ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini. Hata iwe hivyo, ni lazima tuulize: Mapinduzi Makubwa ya Kidini yalitimiza nini kidini? Yalifanya nini kwa ajili ya jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu wa kweli?
42. (a) Bila shaka ni wema gani wa hali ya juu zaidi uliotimizwa na Mapinduzi Makubwa ya Kidini? (b) Ni swali gani kuhusu mambo yaliyotimizwa kikweli na Mapinduzi Makubwa ya Kidini lazima liulizwe?
42 Bila shaka, wema wa hali ya juu zaidi ambao Mapinduzi Makubwa ya Kidini yalitimiza ni kwamba yalifanya Biblia ipatikane kwa makabwela katika lugha yao wenyewe. Kwa mara ya kwanza, watu walikuwa na Neno la Mungu lote mbele yao ili wasome, kusudi walishwe kiroho. Lakini, bila shaka, mengi yahitajiwa zaidi ya kusoma tu Biblia. Je! Mapinduzi Makubwa ya Kidini yalikomboa watu si kwa mamlaka ya kipapa tu bali pia kwa mafundisho na imani zenye kosa ambazo walikuwa wamefundishwa kwa karne nyingi?—Yohana 8:32.
43. (a) Makanisa mengi ya Kiprotestanti leo hufuata kanuni gani za imani, yakidai imani zipi? (b) Roho ya uhuru na utofautiano inayotokana na Mapinduzi Makubwa ya Kidini imefanya nini kwa ajili ya jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu wa kweli?
43 Karibu makanisa yote ya Uprotestanti hufuata imani zilezile—kanuni ya imani ya Nisea, ya Athanasia, na ya Mitume—nayo hufuata baadhi ya mafundisho yale yale ambayo Ukatoliki umekuwa ukifundisha kwa karne nyingi, kama vile Utatu, kutokufa kwa nafsi, na moto wa helo. Mafundisho hayo yasiyo ya kimaandiko huwapa watu wazo lililopotoshwa juu ya Mungu na kusudi lake. Badala ya kuwasaidia katika jitihada ya kutafuta Mungu wa kweli, mafarakano na madhehebu hayo yaliyotokea kwa sababu ya roho ya kutaka kuwa huru ya Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya Uprotestanti yameongoza tu watu katika pande nyingi tofauti-tofauti. Kwa kweli, utofautiano na mvurugo huo umesababisha wengi watilie shaka kuwapo kwenyewe kwa Mungu. Tokeo limekuwa nini? Katika karne ya 19 kulitokea ongezeko kubwa la uatheisti na uagnosti. Hiyo ndiyo itakayokuwa habari ya sura yetu inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Barua za msamaha zinazotolewa na papa kwa ajili ya dhambi.
b Lutheri alisisitiza mno wazo la “kuhesabiwa haki kwa imani pekee” hivi kwamba katika tafsiri yake ya Biblia, aliongeza neno “pekee” kwa Warumi 3:28. Pia yeye alitilia shaka kitabu cha Yakobo kwa ajili ya taarifa ya kwamba “imani isipokuwa na matendo, imekufa.” (Yakobo 2:17, 26) Yeye alishindwa kutambua kwamba katika Warumi, Paulo alikuwa akinena juu ya matendo ya Sheria ya Kiyahudi.—Warumi 3:19, 20, 28.
c Martin Lutheri alimwoa Katharina von Bora katika 1525, ambaye hapo awali alikuwa mtawa aliyetoroka kwenye makao ya kufungiwa ya Cistercia. Walikuwa na watoto sita. Alitoa taarifa kwamba alioa kwa sababu tatu: ili kupendeza baba yake, ili amchokoze papa na Ibilisi, na ili kutia muhuri wa ushahidi wake kabla ya kufia imani.
d Henry 8 alikuwa na wake sita. Kinyume cha matakwa ya papa, ndoa yake ya kwanza ilifutwa, na nyingine ikakomea katika talaka. Aliamuru wake wawili wakatwe kichwa, na wawili walikufa kifo vya asili.
e Neno la Kigiriki e·piʹsko·pos latafsiriwa “askofu” katika Biblia za Kiswahili kama Union Version.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 322]
“Makosa ya Utatu”
Akiwa na miaka 20, Michael Servetus (1511-53), Mhispania aliyezoezwa katika sheria na tiba, alichapisha De Trinitatis erroribus (Makosa ya Utatu), ambamo alieleza kwamba yeye “hatatumia neno Utatu, ambalo halipatikani katika Andiko, na laonekana tu laendeleza kosa la kifalsafa.” Yeye alishutumu Utatu kuwa fundisho “ambalo haliwezi kueleweka, ambalo haliwezekani katika asili ya vitu, na ambalo hata laweza kuonwa kuwa la kukufuru!”
Kwa ajili ya uneni wake wa kutoboa mambo wazi, Servetus alilaaniwa na Kanisa Katoliki. Lakini Wakalvini ndio waliomkamata, wakamhukumu, na kumwua kwa kumchoma polepole. Calvin alitetea vitendo vyake kwa maneno haya: “Mapapa wanapokuwa wakali na wenye jeuri hivyo katika kutetea ushirikina wao hata wanafoka kwa ukatili kumwaga damu isiyo na hatia, je! mahakimu Wakristo hawaaibishwi wakijionyesha hawana bidii katika kutetea ukweli hakika?” Ushupavu wa kidini wa Calvin na chuki ya kibinafsi vilipofusha uamuzi wake na kugandamiza kanuni za Kikristo.—Linganisha Mathayo 5:44.
[Picha]
John Calvin, kushoto, aliagiza Michael Servetus, kulia, achomwe mpaka kifoakiwa mzushi
[Chati katika ukurasa wa 327]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Muhtasari Sahili wa Dini Kubwa-Kubwa za Jumuiya ya Wakristo
Mwanzo wa Uasi-Imani Karne ya 2
Kanisa Roma Katoliki
Karne ya 4 (Konstantino)
Karne ya 5 Coptic
Jacobite
1054 W.K. Orthodoksi ya Mashariki
ya Kirusi
ya Kigiriki
ya Kiromania na nyinginezo
Mapinduzi Makubwa ya Kidini ya Karne ya 16
Kilutheri
Kijerumani
Kisweden
Kiamerika na nyinginezo
Anglikana
Uepiskopo
Umethodisti
Jeshi la Wokovu
Ubaptisti
Upentekosto
Kikongrigeshonali
Ukalvini
Upresbiteri
Makanisa ya Mapinduzi ya Kidini
[Picha katika ukurasa wa 307]
Visehemu hivi vya mbao vya karne ya 16 vyatofautisha kukataa kwa Kristo wabadilisha fedha na uuzaji wa rehema wa papa
[Picha katika ukurasa wa 311]
Jan Hus kwenye mti
John Wycliffe mpinduzi wa kidini na mtafsiri Biblia Mwingereza
[Picha katika ukurasa wa 314]
Martin Lutheri, kulia, aliteta juu ya uuzaji wa hati za rehema na mtawa wa kiume John Tetzel