Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 6/8 kur. 16-20
  • Sehemu 16: Karne ya 9-16 W.K—Dini Iliyohitaji Sana Marekebisho

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sehemu 16: Karne ya 9-16 W.K—Dini Iliyohitaji Sana Marekebisho
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Wazushi” Watoa Wito Kuwe Marekebisho
  • Lutheri na ‘Mchezo wa Karata wa Karne ya 16’
  • Zwingli na Lutheri Wakosa Kukubaliana
  • Fungu la Calvin Katika Marekebisho Hayo
  • Hatimaye, “Uhakika Wenye Kuhofisha”
  • Yale Mapinduzi Makubwa ya Kidini
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
  • Martin Luther na Mageuzi Aliyoleta
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • Je! Historia ya Kidini Ina Manufaa Yo Yote Kwako Wewe?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • Wessel Gansfort—“Mrekebishaji Aliyetangulia Marekebisho”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 6/8 kur. 16-20

Wakati Ujao wa Dini kwa Kutegemea Wakati Wayo Uliopita

Sehemu 16: Karne ya 9-16 W.K—Dini Iliyohitaji Sana Marekebisho

“Kila upotovu wapasa kurekebishwa.”—Voltaire, mtunga insha na mwanahistoria Mfaransa

WAKRISTO wa mapema hawakufundisha juu ya purgatori (matohara), hawakuabudu sanamu zozote, hawakuadhimisha “watakatifu” wowote, wala hawakutukuza vikumbusho vya watakatifu. Hawakujiingiza katika siasa wala hawakuingilia vita vya kimnofu. Lakini kufikia karne ya 15, hakuna lolote la hayo lililofuatwa na wengi waliodai kuwa waigaji wao.

“Wazushi” Watoa Wito Kuwe Marekebisho

“Vyanzo vya kwanza vya uzushi [dhidi ya Ukatoliki wa Roma] vilitokea katika Ufaransa na Italia ya kaskazini karibu mwaka 1000,” chasema The Collins Atlas of World History. Baadhi ya wanaoitwa wazushi walikuwa ni wazushi machoni pa kanisa tu. Leo ni vigumu kuamua kwa usahihi ni kwa kadiri gani wazushi mmoja mmoja walishikamana na Ukristo wa mapema. Hata hivyo, ni wazi kwamba angalau baadhi yao walikuwa wanajaribu kufanya hivyo.

Mwanzoni mwa karne ya tisa, Kasisi Mkuu Agobard wa Lyons alilaani ibada ya sanamu na kutoa dua kwa “watakatifu.”a Shemasi mkuu wa karne ya 11, Berengar wa Tours, aliondoshwa kwenye ushirika kwa ajili ya kutilia shaka dai la kwamba mkate na divai vinavyotumiwa kwenye Misa ya Katoliki hugeuka kuwa mwili na damu halisi ya Kristo.b Karne moja baadaye Peter de Bruys na Henry wa Lausanne walikataa ubatizo wa watoto wachanga na ibada ya msalaba.* Kwa ajili ya kufanya hivyo, Henry alipoteza uhuru wake; Peter alipoteza uhai wake.

“Kufikia katikati ya karne ya kumi na mbili miji ya Ulaya Magharibi ilijawa na mafarakano ya kiuzushi,” aripoti mwana-historia Will Durant. Wenye kutokeza zaidi kati ya vikundi hivi walikuwa ni wafuasi wa Waldo. Walipata umaarufu mwishoni mwa karne ya 12 chini ya mwanabiashara Pierre Valdè (Peter Waldo). Kati ya mambo mengine, hawakukubaliana na kanisa juu ya ibada ya Mariamu, kuungamia makasisi, Misa kwa ajili ya wafu, kughofiri kwa kipapa, kutofunga ndoa kwa makasisi, na matumizi ya silaha halisi.c Chama hicho kilienea kwa kasi sana Ufaransa wote na Italia ya kaskazini, na pia kufikia Ubelgiji, Ujeremani, Austria, na Bohemia (Chekoslovakia).

Sawia, katika Uingereza, msomi wa Oxford John Wycliffe, ambaye baadaye akaja kujulikana kuwa “nyota ya asubuhi ya Mrekebisho Mpya wa Kiingereza,” alikuwa akilaani ‘utawala wa makasisi wenye kunyakua mamlaka’ wa karne ya 14. Kwa kutafsiri Biblia yote katika Kiingereza, yeye na washiriki wake walifanya ipatikane kwa ujumla kwa raia wa kawaida kwa mara ya kwanza. Wafuasi wa Wycliffe waliitwa Walollard. Walollard walihubiri peupe, wakitawanya trakti na visehemu vya Biblia. Tabia hiyo ya “kizushi” haikupendeza kanisa.

Mawazo yake Wycliffe yalisambaa ng’ambo. Katika Bohemia yalivuta fikira zake Jan Hus (John Huss), mkuu wa Chuo Kikuu cha Prague. Hus alitilia shaka uhalali wa upapa na akakanusha kwamba msingi wa kanisa haukuwa ni Petro.d Kufuatia ubishi juu ya kuuzwa kwa ghofira, Hus alihukumiwa kwa ajili ya uzushi na kuchomwa kwa moto kwenye mti katika 1415. Kulingana na fundisho la Kikatoliki, ghofira ni uandalizi ambao katika huo adhabu kwa ajili ya dhambi yaweza kusamehewa nusu au kabisa, kwa njia hiyo kufupiza au kuondoa kipindi cha wakati ambao mtu anapatwa na adhabu ya muda na kusafishwa katika purgatori kabla ya kuingia mbinguni.

Miito ya kutaka mrekebisho mpya iliendelea. Girolamo Savonarola, mhubiri Mwitaliano katika Dominika, alilalama hivi: ‘Mapapa na makasisi wanalaani kiburi na tamaa ya makubwa, na wao wamejiingiza kabisa katika hayo. Wanahubiri usafi wa adili na wanaweka masuria. Wao wanafikiria tu juu ya ulimwengu na mambo ya kilimwengu; hawazijali nafsi hata.’ Hata makadinali Wakatoliki walitambua tatizo hilo. Katika 1538, katika barua ya kikumbusho aliyoandikiwa Papa Paul wa 3, walielekeza fikira zake kwenye matumizi mabaya ya kiparokia, kifedha, kihukumu, na kiadili. Lakini upapa ulishindwa kufanya marekebisho ambayo kwa wazi yalihitajiwa, na hilo lilichochea ule Mrekebisho wa Uprotestanti. Viongozi wa mapema walikuwa ni kutia ndani Martin Lutheri, Huldrych Zwingli, na John Calvin.

Lutheri na ‘Mchezo wa Karata wa Karne ya 16’

Mnamo Oktoba 31, 1517, Lutheri alichochea ulimwengu wa kidini aliposhambulia kuuzwa kwa ghofira kwa kugongomelea orodha ya mambo 95 yenye kupinga kwenye mlango wa kanisa katika Wittenberg.

Kuuzwa ghofira kulianza wakati wa vile Vita vya Wakristo, waliopewa waumini waliokuwa na nia ya kuhatirisha uhai wao katika vita “takatifu.” Baadaye walipewa watu wenye kutegemeza kanisa kifedha. Muda si muda, ghofira ikawa ni mbinu inayofaa ya kuchangiza pesa za kujenga makanisa, makao ya watawa, au mahospitali. “Majengo ya hisani ya Enzi za Katikati yaligharimiwa kwa njia hiyo,” asema profesa wa historia ya kidini Roland Bainton, ghofira kuwa “mchezo wa karata wa karne ya 16.”

Kwa maneno makali ambayo alikuja kutambulikana kwayo, Lutheri aliuliza: “Ikiwa papa ana uwezo wa kuweka mtu yeyote huru na purgatori [kwa msingi wa ghofira], ni kwa nini upendo haumfanyi afutilie mbali purgatori kwa kumfungua kila mtu.?” Alipoulizwa achangie pesa ujenzi wa jengo la Roma, Lutheri alijibu vikali kwamba papa “angefanya vizuri kuuza la Mtakatifu Petro na pesa hizo awape jamaa maskini ambao walikuwa wananyonywa na wachuuzi wa ghofira.”

Pia Lutheri alishambulia Ukatoliki kwa ajili ya kukinza Wayahudi, akashauri: “Sisi twapaswa kutumia kwa Wayahudi sheria ya Kristo ya upendo wala si ya papa.” Na kuhusu kuabudu vikumbusho vya watakatifu, alidhihaki: “Mtu fulani anadai ana unyoya kutoka bawa la malaika Gabrieli, na Askofu wa Mainz ana mwali wa moto kutoka kichaka chenye moto cha Musa. Na inatukiaje kwamba mitume 18 wamezikwa katika Ujeremani na hali Kristo alikuwa na kumi na wawili tu?”

Itikio la kanisa kwa mashambulizi yake Lutheri lilikuwa ni kumwondosha kwenye ushirika. Maliki wa Roma Takatifu Charles wa 5, akiongozwa na mkazo wa kipapa, alimpiga marufuku Lutheri. Jambo hilo lilitokeza ubishi mkubwa hata kwamba mnamo 1530 Baraza la Augsburg liliitishwa ili kuzungumza jambo hilo. Jitihada za kupatana zilishindwa, kwa hiyo taarifa ya msingi ya imani ya kimafundisho ya Kilutheri ilitolewa. Ikiitwa Ungamo la Augsburg, ikawa ni tangazo la kuzaliwa kwa kanisa la kwanza la Uprotestanti.e

Zwingli na Lutheri Wakosa Kukubaliana

Zwingli alikazia Biblia kuwa mamlaka ya mwisho na ya pekee kwa kanisa. Ingawa alitiwa moyo na kielelezo cha Lutheri, alikataa kuitwa Mlutheri, akisema alikuwa amejifunza fundisho la Kristo kutoka kwa Neno la Mungu, wala si kutoka kwa Lutheri. Kwa kweli, alikosa kukubaliana na Lutheri juu ya mambo fulani ya msingi ya Chakula cha Jioni cha Bwana na pia juu ya uhusiano unaofaa baina ya Mkristo na mamlaka za kiserikali.

Wana-marekebisho hao wawili walikutana safari moja, mnamo 1529, kwenye kile ambacho kitabu The Reformation Crisis huita “Namna fulani ya kongamano kuu la kidini.” Kitabu hicho kinasema hivi: “Wanaume hao wawili hawakuagana wakiwa marafiki, lakini . . . taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa kongamano hilo, ikiwa imetiwa sahihi na washiriki wote, ilificha kwa ustadi ukubwa wa tofauti hiyo.”

Pia Zwingli alikuwa na matatizo na wafuasi wake mwenyewe. Mnamo 1525 kikundi kimoja kilijitenga, kikiwa hakikubaliani naye juu ya suala la mamlaka ya Serikali juu ya Kanisa, jambo ambalo yeye alitetea nao wakakanusa. Wakiitwa Waanabaptisti (“wabatizaji tena”), walikuwa na maoni kwamba ubatizo wa watoto wachanga ni zoea lisilofaa kitu, wakasema kwamba ubatizo ulikuwa kwa ajili ya waumini walio watu wazima peke yao. Pia walipinga matumizi ya silaha halisi, hata katika viitwavyo vita vya haki. Maelfu yao waliuawa kwa ajili ya imani zao.

Fungu la Calvin Katika Marekebisho Hayo

Wasomi wengi humwona Calvin kuwa mkuu zaidi kati ya wana-marekebisho hao. Yeye alisisitiza kwamba kanisa lirudi kwenye kanuni za awali za Ukristo. Hata hivyo mojawapo la mafundisho yake makuu, yaani, yote yanayotokea huwa yameamuliwa kimbele, lakumbusha juu ya mafundisho katika Ugiriki wa kale, ambako Wastoiki walisema kwamba Zeu anaamua mambo yote na kwamba wanadamu wakubali yasiyoweza kuepukika. Fundisho hilo kwa wazi si la Kikristo.

Wakati wa siku yake Calvin Waprotestanti Wafaransa walikuja kujulikana kuwa Wahuguenoti, nao waliteswa vibaya sana. Katika Ufaransa, kuanzia Agosti 24, 1572, katika Mauaji Makubwa ya Siku ya Mtakatifu Bartholomayo, majeshi ya Wakatoliki yalipiga dharuba maelfu yao, kwanza katika Paris halafu kotekote nchini. Lakini Wahuguenoti pia walitwaa upanga nao wakawa na lawama la kuua wengi wakati wa vita vya kidini vyenye umwagaji mwingi wa damu wakati wa sehemu ya mwisho ya karne ya 16. Kwa hiyo wao walichagua kupuuza agizo lililotolewa na Yesu: “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi.”—Mathayo 5:44.

Calvin alikuwa ameweka kielelezo, akitumia mbinu za kuhimiza masadikisho yake ya kidini ambazo kasisi Mprotestanti Fosdick, ambaye ni mfu sasa, alizieleza kuwa zisizo na huruma na zenye kushtua. Chini ya sheria ya kanisa ambayo Calvin alianzisha Geneva, watu 58 waliuawa na 76 wakafungwa uhamishoni katika kipindi cha miaka minne; kufikia mwisho wa karne ya 16, wanaokadiriwa 150 walikuwa wamechomwa kwa moto juu ya mti. Mmoja wa hao alikuwa ni Michael Servetus, tabibu na mwanatheolojia Mhispania, ambaye alikataa fundisho la Utatu, hivyo akawa “mzushi” kwa kila mtu. Mamlaka za Kikatoliki zilichoma kwa moto sanamu yake; Waprotestanti walichukua hatua kubwa zaidi kwa kumchoma-moto kwenye mti.

Hatimaye, “Uhakika Wenye Kuhofisha”

Wajapokubaliana na Lutheri kikanuni, baadhi yao ambao wangelikuwa wana-marekebisho walisita. Mmoja alikuwa msomi Mdachi Desiderius Erasmus. Mnamo 1516 akawa wa kwanza kuchapisha “Agano Jipya” katika Kigiriki cha awali. “Yeye alikuwa mwana-marekebisho,” chasema kichapo Edinburgh Review, “hadi Marekebisho hayo yalipokuja kuwa uhakika wenye kuhofisha.”

Hata hivyo, wengine, walisonga mbele na Marekebisho hayo, na katika Ujeremani na Skandinavia, Ulutheri ukasambaa kwa kasi sana. Mnamo 1534 Uingereza ilijiondoa kwenye uongozi wa kipapa. Uskochi, chini ya kiongozi wa Marekebisho John Knox, upesi ikafuata. Katika Ufaransa na Polandi, Uprotestanti ukatambuliwa kisheria kabla ya mwisho wa karne ya 16.

Ndiyo, kama Voltaire alivyoeleza hilo kwa kufaa, “Kila upotovu wapasa kurekebishwa.” Lakini Voltaire aliongeza maneno haya yenye kuonyesha ukweli wa mambo, “Isipokuwa rekebisho hilo liwe ni hatari zaidi ya upotovu wenyewe.” Ili kuthamini zaidi ukweli wa maneno hayo, hakikisha kusoma “Uprotestanti—Marekebisho Kweli Kweli?” katika toleo letu lifuatalo.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa kizibiti cha kuonyesha kwamba mafundisho na mazoea haya hayakujulikana na Wakristo wa kwanza, ona Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., chini ya habari “Mwandamano wa Kimitume,” “Ubatizo,” “Ungamo,” “Msalaba,” “Ajali,” “Sanamu,” “Mifano ya Kuabudiwa,” “Mariamu,” “Misa,” “Kutokuwamo,” na “Watakatifu.”

b Kwa kizibiti cha kuonyesha kwamba mafundisho na mazoea haya hayakujulikana na Wakristo wa kwanza, ona Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., chini ya habari “Mwandamano wa Kimitume,” “Ubatizo,” “Ungamo,” “Msalaba,” “Ajali,” “Sanamu,” “Mifano ya Kuabudiwa,” “Mariamu,” “Misa,” “Kutokuwamo,” na “Watakatifu.”

c Kwa kizibiti cha kuonyesha kwamba mafundisho na mazoea haya hayakujulikana na Wakristo wa kwanza, ona Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., chini ya habari “Mwandamano wa Kimitume,” “Ubatizo,” “Ungamo,” “Msalaba,” “Ajali,” “Sanamu,” “Mifano ya Kuabudiwa,” “Mariamu,” “Misa,” “Kutokuwamo,” na “Watakatifu.”

d Kwa kizibiti cha kuonyesha kwamba mafundisho na mazoea haya hayakujulikana na Wakristo wa kwanza, ona Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., chini ya habari “Mwandamano wa Kimitume,” “Ubatizo,” “Ungamo,” “Msalaba,” “Ajali,” “Sanamu,” “Mifano ya Kuabudiwa,” “Mariamu,” “Misa,” “Kutokuwamo,” na “Watakatifu.”

e Kwa kuonyesha sana, usemi “Uprotestanti” kwa mara ya kwanza ulitumiwa kwenye Baraza la Speyer la 1529 kuhusu wafuasi wa Lutheri, ambao walipinga amri iliyowapa Wakatoliki uhuru mkubwa wa kidini zaidi yao.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Martin Lutheri, alizaliwa katika Ujeremani mnamo 1483, alitawazwa kwenye ukasisi akiwa na miaka 23, alijifunza theolojia kwenye Chuo Kikuu cha Wittenberg, akawa profesa wa Maandiko Matakatifu katika Wittenberg katika 1512, alikufa akiwa na miaka 62

Huldrych Zwingli, alizaliwa katika Uswisi miezi miwili baada ya Lutheri, alitawazwa kwenye ukasisi katika 1506, alikufa katika pigano na miaka 47 akiwa kasisi-jeshi Mprotestanti.

[Hisani]

Kunstmuseum, Winterthur

John Calvin, alizaliwa miaka 25 baada ya Lutheri na Zwingli, alihamia Uswisi kutoka Ufaransa akiwa mwanamume kijana, alisimamisha serikali ya kanisa katika Geneva, alikufa akiwa na miaka 54

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki