Kuutazama Ulimwengu
Papa Ahakikisha Tena Mageuzi
Papa John Paul wa Pili hivi majuzi alitoa taarifa juu ya mageuzi ya binadamu, akitaja “matokeo yaliyokusanywa” ya utafiti wa kujitegemea kuwa “hoja yenye umaana yenye kuunga mkono nadharia hii.” Ingawa hakuwa akikubali kikamili fundisho hilo, John Paul wa Pili alirudia barua ya Papa Pius wa 12 aliyoandikia maaskofu mwaka wa 1950, ambayo “iliona fundisho la ‘mageuzi’ kuwa nadharia ya maana, istahiliyo kuchunguzwa,” kulingana na L’Osservatore Romano. Akijaribu kumhusisha Mungu katika mageuzi ya binadamu, papa aligeukia fundisho la Plato kwamba wanadamu wana nafsi isiyoweza kufa. Tena akinukuu barua ya Pius wa 12 aliyoandikia maaskofu, yeye alisema: “Ikiwa mwili wa mwanadamu uligeuka kutoka mata inayoishi ambayo ilikuwapo hapo awali, nafsi isiyoweza kufa inaumbwa mara moja na Mungu.”
Viwango vya Ndoa Vyashuka
“Twashuhudia kutoweka kwa ndoa ikiwa shirika,” asema Jean Dumas, mkuu wa uchanganuzi wa kisasa wa idadi ya watu kwenye shirika la Statistics Canada. Ndoa zinapungua katika Kanada, hasa katika Quebec, kulingana na The Toronto Star. Kutotaka kujiwajibisha kwa ndoa yenye kudumu, katika visa fulani ni kwa sababu ya mtazamo mbaya ambao watu wanao kuhusu ndoa za wazazi wao, yasema ripoti hiyo. Habari iliyokusanywa kwa zaidi ya kipindi cha miaka 25 hufunua kwamba asilimia 30 ya wenzi wa ndoa waliooana katika 1969 hawakuwa pamoja katika 1993. Takwimu zaonyesha pia kwamba wenzi wa ndoa waliooana hivi karibuni wanatalikiana. Thuluthi moja ya talaka zote katika Kanada katika 1993 huhusisha wenzi waliooana kwa chini ya miaka mitano, ongezeko la robo tangu 1980. Marshall Fine, mkurugenzi wa kitovu cha ndoa na tiba ya familia kwenye Chuo Kikuu cha Guelph, Ontario, aonelea hivi: “Ndoa haionekani kuwa mahali penye usalama sana kwa vijana.”
Matineja Wasiopata Usingizi wa Kutosha
Wataalamu fulani wa usingizi katika Australia na Marekani waamini kwamba huenda kukawa na visababishi vingine vingi zaidi vya matineja kutaka kubaki kitandani asubuhi kwa kuongezea visababishi kama televisheni, uasi, au uvivu, laripoti gazeti Asiaweek. Mtaalamu wa Australia wa usingizi Dakt. Chris Seton asema kwamba mabadiliko ya kihomoni na vipindi vifupi vya ukuzi vyaweza kuwa vyahusiana na mwelekeo wa matineja wengi kulala kupita kiasi. Kuanzia umri wa miaka tisa, uhitaji wa kijana wa usingizi huongezeka. Hata hivyo, katika uchunguzi wa wanafunzi 3,000 wa Marekani wenye umri wa miaka 17 hadi 19, asilimia 85 walikuwa hawapati usingizi wa kutosha. The New York Times laripoti kwamba tokeo ni wanafunzi ambao hujaribu kushindana na kusinzia wakati wote, hasa katika masomo ya mapema asubuhi. “Tuna watoto ambao wamekosa usingizi sana,” asema Profesa wa Chuo Kikuu cha Cornell James B. Maas, “hivi kwamba ni kana kwamba wamepewa dawa za kuwalevya.” Wataalamu waamini kwamba matineja wahitaji angalau saa nane na nusu za usingizi kila usiku.
Ulaji Hupunguza Hatari ya Kansa
Kula matunda na mboga angalau mara tano kwa siku hupunguza hatari ya mtu ya kupatwa na kansa ya pafu, sehemu ya chini ya utumbo mkubwa, tumbo, na aina nyinginezo za kansa, laripoti The Wall Street Journal. “Uthibitisho wenye nguvu” wa hilo watokana na chunguzi zaidi ya 200 zenye kuthibitisha manufaa katika angalau nchi 17. Si lazima ule kiasi kingi. Kulingana na programu ya Taasisi ya Kitaifa ya Kansa ya Marekani, kiasi kifaacho hutia ndani: “Kipande cha kiasi cha tunda, maji ya matunda robo tatu ya kikombe, nusu kikombe cha mboga zilizopikwa, kikombe kimoja cha mboga mbichi zikiwa saladi, au robo nne za kikombe cha matunda yaliyokaushwa.” Taasisi hiyo imeendeleza ulaji huo kwa miaka mitano ambayo imepita, lakini kwa sasa katika Marekani, ni mtu mzima 1 tu kati ya 3 na mtoto 1 kati ya 5 ambaye hufuata mwongozo huo. Kutamani sana vyakula vya kutengenezwa haraka kwaonekana kunazuia mafanikio. Jarida The Wall Street Journal laonelea hivi: “Chipsi zilizoviringwa pamoja na ketchup hazilingani na visehemu viwili vya mboga.”
Idadi Isiyobadilika?
Kulingana na International Institute for Applied Systems Analysis (IIASA), katika Vienna, idadi ya ulimwengu ya sasa haielekei itarudufika. Kadirio lao ni kwamba idadi “itaongezeka kutoka bilioni 5.75 ya sasa hadi bilioni 10 kufikia mwaka 2050, kisha itafikia kilele cha karibu na bilioni 11 kufikia 2075, na kubaki katika kiwango kisichobadilika au kupungua kidogo kuelekea mwaka 2100,” lasema New Scientist. Kulingana na IIASA, kuna uwezekano wa asilimia 64 kwamba idadi yetu ya sasa tufeni pote haitarudufika. Tarakimu zao zaonyesha kwamba yaonekana viwango vya idadi ya watoto wanaozaliwa vilipungua katika kila eneo la dunia katika 1995.
Redio Isiyotumia Betri
Ili kukabiliana na ukosefu wa umeme na kutoweza kupata betri za kutosha katika sehemu kubwa ya mashambani ya Afrika, kiwanda kidogo karibu na Cape Town, Afrika Kusini, kinatengeneza redio zenye kuchukulika zilizo na jenereta ndani ambazo huzungushwa mpini wazo. “Zungusha mpini kwa nguvu mara chache,” laripoti The New York Times, na redio hiyo “itaendelea kucheza kwa saa nzima.” Japo ina ukubwa wa kisanduku cha kuwekea chakula cha mchana na uzani wa kilo tatu, aina hiyo mpya yaelekea itafaulu. Kulingana na Siyanga Maluma, ambaye ndiye mkuu wa shughuli za mauzo za kiwanda hicho, ikiwa redio hiyo yafunguliwa kwa muda wa saa tano hadi kumi kwa siku, itaokoa fedha za betri zipatazo dola 500 hadi 1,000 kwa miaka mitatu. Pamoja na baiskeli na pikipiki, “redio ni moja ya ishara za Kiafrika za kuwa mashuhuri,” asema Maluma. “Waweza kuwa na uhakika,” yeye asisitiza. Kwa kuwa tu na redio, “waweza kujishindia mke.”
Mvua Yenye Kuua
Mvua ya asidi imechangia kwa njia isiyo ya moja kwa moja vifo vya elki wengi wa Skandinavia kulingana na mwanasayansi Msweden Dakt. Adrian Frank. Ili kupambana na athari za mvua ya asidi, chokaa inamwagwa kwenye nyanja na maziwani. Hata hivyo, mimea inayokuwa katika udongo uliotiwa chokaa huonyesha ongezeko la kiwango cha elementi fulani, hasa molybdenum. Elki wanapofyonza molybdenum nyingi kupita kiasi, hiyo husababisha ukosefu wa shaba wenye kufisha ambao huathiri sana mifumo ya kinga ya wanyama hao. Tokeo zaidi la mvua ya asidi ni kwamba katika maziwa zaidi ya 4,000 ya Sweden, samaki hawawezi kuendelea kuishi sasa na idadi ya samaki aina ya tirauti katika Norway imepungua kwa asilimia 50. The Sunday Telegraph la London lataja kwamba ingawa serikali ya Uingereza inapunguza mitoko ya salfa katika vituo vyayo vya umeme ili kudhibiti uchafuzi, matokeo yanayobaki ya mvua ya asidi yanaweza kuendelea kwa miaka mingi.
Kuzoeza Tembo wa Afrika
Tembo wa Asia wametumika kwa karne nyingi kuwa wanyama wa kufanya kazi. Hata hivyo, wenzao wakubwa wa Afrika, wamefikiriwa kuwa wakali sana kuweza kufugwa. Lakini angalau jaribio moja limeelekea kupata mafanikio. Tembo wa Afrika wanatumiwa katika hifadhi ya wanyama wa pori ya Imire ya Zimbabwe kulima mashamba na kubeba walinda misitu hadi mahali ambapo si rahisi kupafikia. Njia ya kuzoeza inayotumiwa inaitwa “upendo na thawabu.” Ripota wa gazeti moja la habari la Afrika alitazama tembo aitwaye Nyasha akilima shamba, akiwa amembeba mgongoni mfanyakazi aitwaye Muchemwa. “Pindi kwa pindi,” ripota huyo alieleza, “tembo huyo alinyoosha mkonga wake nyuma na Muchemwa alimpa kipande cha mlo wa wanyama wenye protini nyingi.” Ripoti hiyo yaendelea hivi: “Nyasha na tembo wengine sita waliozoezwa Imire watatumiwa kutayarisha mashamba kabla ya msimu ufuatao wa mvua kwa ajili ya mazao kama vile mahindi, ambayo yatatumiwa kuwalisha na kulisha wanyama wengineo kwenye shamba hilo.”
Nyongeza Zinazotengenezwa Kutokana na Damu
Prothemol, nyongeza ya protini inayojaribiwa, inatumiwa katika kaskazini-mashariki mwa Brazili kusaidia kutatua tatizo la eneo hilo la ukosefu wa lishe bora. Kulingana na ripoti ya shirika la Associated Press, bidhaa hiyo inatengenezwa hasa kutumia damu ya ng’ombe iliyopatikana vichinjioni, ambayo inasemekana kwamba ina “lishe bora sana hata kuliko nyama.” Majaribio kama hayo yalikuwa yamefanywa katika Guatemala, katika 1990, na bidhaa iliyoitwa “Harina de Sangre” (unga wa damu). Katika Brazili serikali ilipanga ili Prothemol isambazwe kutoka nyumba hadi nyumba, “wakigawanya nyongeza hiyo na kuchunguza watoto walioichukua.” Hapo mbeleni, vichinjio katika eneo la kaskazini-mashariki mwa Brazili vilimwaga damu, kama inavyoelekeza Biblia.—Mambo ya Walawi 17:13, 14.
Majeshi ya Watoto
Robo milioni ya watoto, wengine wakiwa wachanga wenye umri wa miaka saba, wanatumika jeshini ulimwenguni pote, kulingana na utafiti uliofanywa katika nchi 26 na kuripotiwa katika Guardian Weekly la Manchester, Uingereza. Ripoti hiyo, ambayo ni sehemu ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa, ilifunua kwamba watoto walio wanajeshi wapya wenyewe walitendewa kikatili, mara nyingi wakilazimishwa kushuhudia kuteswa na kuuawa kwa watu wa ukoo. Baadaye, walitumiwa wakiwa wafishaji, wauaji, na wapelelezi. Katika nchi moja, “wanajeshi wengi watoto walikuwa wameamriwa kutesa, au kuua watoto au watu wazima waliojaribu kutoroka.” Watoto, mara nyingi wakiwa wamepewa dawa za kulevya au alkoholi kabla ya kupigana, wameonekana wakikimbia kuingia katika mapigano “kana kwamba hawangeweza kuuawa au kuumizwa.”