Ufugaji wa Nyuki—Hadithi “Tamu”
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Ugiriki
NURU ya alfajiri yajitapanya polepole inapoangaza anga. Katika baridi hiyo ya asubuhi, gari aina ya pickup lasimama polepole kando ya barabara chini ya mlima fulani. Vivuli viwili vya watu vyatokea—vikiwa vimevaa glavu, mabuti, maovaroli ya pamba, na kofia pana zenye kifuniko cha uso. Kwa uangalifu lakini kwa hamu, wao wapakia visanduku vingi vya mbao kwenye gari. Je, wao ni wezi wanaoiba mali kwa urahisi? La, wao ni wafugaji wa nyuki wanaojaribu kutunza nyuki wao wenye thamani—wakiwa tayari kushika njia kwenda mahali pengine ambapo pana mimea yenye maua ya maji matamu.
Wafugaji wa nyuki ni watu wa kipekee, ambao hufurahia uhusiano wa karibu na mdudu wa kipekee. Kwa upande mmoja kuna nyuki, ambao huenda ndio wadudu wenye mafaa zaidi kiuchumi kuliko wadudu wengine wote, na ambao hutokeza asali na nta na kuchavusha mimea ya aina nyingi. Kwa upande mwingine, kuna watu ambao hupata riziki yao kwa kufuga nyuki na ambao pia wanavipenda sana viumbe hivyo vidogo na “kuvielewa,” kama asemavyo mmoja wao.
Mtunzi wa “Miujiza ya Kila Siku”
Kuwa mfugaji wa nyuki kwaweza kuonekana kuwa rahisi: Kutafuta tu mizinga kadhaa iliyojaa jamii za nyuki, uiweke katika sehemu ambayo inatokeza maua yenye maji matamu, kisha urudi baada ya miezi fulani ili kuvuna mazao. Lakini si hivyo. Ili kupata ni nini hasa kinachohusika, tuliongea na John na Maria, ambao ni wafugaji stadi wa nyuki, na ambao walituambia kwa furaha juu ya kazi yao waipendayo.
“Ufugaji wa nyuki ni wonyesho wa miujiza ya kila siku,” John aeleza anapoinama kidogo juu ya mzinga ulio wazi. “Kufikia sasa, hakuna mtu afahamuye kabisa maisha ya hali ya juu ya jumuiya ya nyuki, zile stadi za hali ya juu za kuwasiliana, na tabia nzuri za kikazi za nyuki.”
Akitaja historia ya utaalamu wa ufugaji wa nyuki, John ataja kwamba katika nyakati zilizopita wafugaji wa nyuki walivuna asali kwa kuharibu jumuiya za nyuki, ambazo ziliishi katika mianya iliyo kwenye miti na nafasi nyinginezo. Hata hivyo, katika 1851, Lorenzo Lorraine Langstroth, mfugaji wa nyuki aliye Mmarekani, aligundua kwamba nyuki huacha nafasi za karibu milimeta sita kati ya masega. Kwa hiyo, mizinga iliyotengenezwa kwa mbao yenye nafasi kama zile kati ya fremu za sega yaweza kutumiwa. Sasa kuondoa fremu moja-moja kutoka kwenye mzinga na kuvuna asali na nta bila kuharibu jumuiya hiyo ya nyuki kukawezekana.
“Kwa ufugaji wenye mafanikio,” aendelea kusema John, “ni lazima upende sana jumuiya zako za nyuki. Unakuwa kama baba kwa nyuki wako, na naamini kwamba wao hutambua hilo na kuitikia ifaavyo. Pia unakuwa daktari wao, mtunzi wao, mlishaji wao katika vipindi vigumu vya kipupwe.”
Maria aongezea: “Mfugaji stadi wa nyuki aweza kujua mengi kwa kutazama tu mzinga, ambao mara nyingi una nyuki kati ya elfu 8 na elfu 80. Ikiwa wewe ni mwenye uzoefu, unapofungua mzinga, sauti tu unayosikia itakuambia kama jumuiya hiyo inanawiri, ina matokeo, na ‘imefurahi’; kama ina njaa; kama imekuwa ‘yatima’ kwa sababu malkia amekufa; kama imekasirika kwa sababu ya jambo fulani baya; na mengi zaidi.”
Mambo Muhimu Katika Kufuga Nyuki kwa Mafanikio
“Mahali ambapo mfugaji wa nyuki achagua kwa uangalifu ili kuweka mizinga ni muhimu sana,” aeleza John. “Sisi hujitahidi sana kutafuta sehemu zenye kuchanua maua ambako nyuki waweza kupata chakula.
“Mfugaji wa nyuki aweza kutafuta maua yaliyochanua ya machungwa na basswood ili kuendeleza jumuiya hizo. Katika misimu ya kiangazi na vuli, eneo lililojaa misunobari na mivinje litasaidia kutokeza asali bora yenye rangi ya nyekundu-nyekundu iliyo wazi, ambayo hupendwa sana na wanunuzi. Nyanja zenye kuchanua maua ya thyme zinazomea peke yazo hufanyiza aina bora zaidi ya asali—mkuu wa asali, kama wafugaji wa nyuki waiitavyo. Nyuki hao pia hutafuta chakula kwenye klova nyeupe, klova tamu ya kimanjano, na alfalfa.”
Busara ni muhimu sana. Maria aeleza: “Tunapoweka mizinga katika maeneo ya milima-milima, hufaa kuiweka chini ya mlima. Basi nyuki waweza kuruka wakipanda mlima, wazuru miti iliyojaa maua, na kisha—wakiwa wamejaa maji matamu ya maua—wao huteremka kwa urahisi wakirudi kwenye mizinga yao. Kama mizinga ingekuwa juu sana mlimani, nyuki wangechoka na mazao ya jumuiya hiyo yangeathirika sana.”
“Kila mfugaji wa nyuki huelewa fungu muhimu linalotekelezwa na malkia kwa habari ya hali-njema na uzalishaji wa jumuiya ya nyuki,” asema John anapobeba kwa upole mojawapo fremu za mzinga wenye malkia mchanga katikati. “Katika mizinga ambayo haizai sana wala haitokezi asali nyingi, ni lazima malkia auawe na kubadilishwa. Jumuiya zenye malkia wachanga ndizo hufanyiza asali nyingi zaidi. Pia tunapotaka kufanyiza jumuiya mpya, sisi hutwaa mzinga wenye sehemu mbili na uliojaa nyuki na kutenganisha visanduku vya juu na vya chini. Kisanduku kimoja kina malkia, na hivyo twaweka malkia mchanga aliyejamiiana katika kisanduku kingine. Kufikia wakati maua yachanuapo, huyo malkia mpya atakuwa akitaga mayai, akijaza mzinga kwa nyuki-wafanyakazi walio wachanga.”
Nyuki huishi kwa muda gani? Tunaambiwa kwamba urefu wa maisha ya nyuki-mfanyakazi hutegemea bidii yake ya kazi. Katika kiangazi, wakati ambapo nyuki hutafuta-tafuta maua kwa karibu muda wa saa 15 kwa siku na kuruka kwa mwendo wa karibu kilometa 21 kwa saa, yeye huishi kwa majuma sita tu. Kipindi cha kipupwe hakichoshi sana nyuki, kwa kuwa hao hufanya kazi kwa muda wa saa mbili au tatu tu kwa siku, na hivyo wao waweza kuishi kwa miezi kadhaa.
Bidhaa Mbalimbali
Jambo la kwanza ambalo huja akilini tunaposema juu ya ufugaji wa nyuki bila shaka ni asali. Umajimaji huo mzito na mtamu hutengenezwa na nyuki-mfanyakazi. Kwa wastani, mzinga wa kibiashara waweza kutokeza kilo 29 kwa mwaka. Nta ni bidhaa nyingine ya kipekee inayotengenezwa na utendaji wa nyuki. Sega la asali ni muhimu kwa karibu miaka mitano hadi sita. Kufikia wakati huo rangi yalo imekuwa nyeusi-nyeusi kwa sababu ya vijiumbe na vimelea kadhaa vinavyoishi ndani yalo na ni lazima libadilishwe. Masega yaliyotupwa huchakatwa kwa sababu yana nta. Uzalishaji wa wastani wa kibiashara ni kati ya kilo 9 hadi 18 ya nta kwa kila tani moja ya asali inayovunwa.
Chavuo—ambayo ni chanzo kikuu cha protini, vitamini, madini, na mafuta kwa ukuzi wa malkia, nyuki-mfanyakazi, na dume—pia husifiwa na watu fulani kuwa dawa nzuri ya asili kwa magonjwa fulani. Mzinga waweza kutoa karibu kilo tano kwa mwaka. Gundi ni kitu ambacho nyuki hutumia kulainisha mzinga wao na pia kufungia mdukizi ambaye ni mkubwa mno kuweza kuondolewa.
Kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja, karibu robo ya chakula chote tulacho hutegemea uwezo wa nyuki wa kuchavusha mimea. Matofaa, lozi, matikitimaji, plums, pears, bilimbi, na beri za aina mbalimbali zote hutegemea uchavushaji wa nyuki. Na ndivyo ilivyo na mimea kadhaa ya mbegu, kutia ndani karoti, vitunguu, na hata alizeti. Nyama na bidhaa za maziwa huhusianishwa pia na nyuki kwa sababu hao huchavusha alfalfa ambayo ni lishe ya mifugo.
‘Mwenye Akili Nyingi Sana’
“Nafikiri kwamba wafugaji wengi wa nyuki huamini katika Mungu,” asema Maria, akitukumbusha jinsi hatuwezi kueleza utata wa maisha ya kijamii ya nyuki, ukuzi wao wenye kuvutia katika maisha tata ya kijumuiya, na uwezo wao bora sana wa kutoweza kupotea na kuwasiliana. Watu wengi ambao huchunguza na kutunza nyuki wangekubali mara moja kwa uhakika wa kwamba nyuki ‘wana akili nyingi sana,’ wakiwa wamepewa kwa ukarimu akili hiyo na Muumba wetu Mtukufu, Yehova Mungu.—Linganisha Mithali 30:24.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]
Kutoka Kwenye Ua Hadi Mezani Pako
1 Nyuki wa kutafuta maji matamu ya maua huzuru ua na kuchukua maji matamu
Wazurupo maua, nyuki hukusanya maji matamu ya maua katika kifuko chao cha asali, ambacho ni mwenezo wa umio. Ili kifuko hicho kijae, nyuki huhitaji kuzuru maua moja-moja kati ya 1,000 na 1,500
2 Kwenye mzinga, maji matamu huhifadhiwa katika sega
Aingiapo tu katika mzinga, nyuki wa kutafuta maji matamu hutapika kile kilichomo katika kifuko cha asali ndani ya mdomo wa nyuki-mfanyakazi. Kisha nyuki-mfanyakazi huweka maji matamu katika chumba na kuyageuza maji kuwa asali
3 Mfugaji wa nyuki huvuna asali
Akiwa na kisu kilichopashwa moto, yeye huondoa nta ambayo hufunika vyumba vilivyomo katika kila fremu. Kisha yeye huweka fremu hizo katika kichujio cha asali, ambacho kitaondoa asali kwa kuifinya
4 Asali huwekwa katika chupa au kutenganishwa sehemu-sehemu
Vibandiko katika chupa za asali huonyesha ni maua gani yaliyotumiwa na nyuki. Kama ni chupa inayopenyezwa na nuru, unaweza kuchunguza ubora kwa rangi ya asali
5 Asali ni nzuri kwa afya yako!
Mwili hufyonza asali kwa urahisi nayo hubadilishwa haraka kuwa nishati. Ripoti zaonyesha kwamba inaweza kutumiwa kutibu majeraha ya kuchomeka na aina mbalimbali za vidonda vya ngozi