Kuutazama Ulimwengu
Kadinali Afafanua Maelezo ya Papa
Kwa kuongezea taarifa ya Papa John Paul kwamba nadharia ya mageuzi “haikuwa nadharia tu,” Kadinali O’Connor wa New York amesema kwamba Adamu na Hawa huenda walikuwa “umbo fulani jingine” wala si mwanamume na mwanamke. Kama ilivyoripotiwa katika Daily News la New York, O’Connor alisema: ‘Kanisa Katoliki bado liko tayari kufikiria uchunguzi wa kisayansi, kutia ndani na mageuzi ya kibiolojia.’ Katika mahubiri yaliyotolewa katika St. Patrick’s Cathedral, kadinali huyo alisema: “Je, yawezekana kwamba watu wawili tunaowarejezea kuwa Adamu na Hawa walipoumbwa, walikuwa katika umbo jingine, na Mungu akawapulizia uhai, akawapulizia nafsi ndani yao—hilo ni swali la kisayansi.” Kichwa fulani katika gazeti la habari la Italia lisilopendelea mabadiliko Il Giornale lilisema hivi kwa ufupi: “Papa Asema Huenda Tumetokana na Tumbili.”
Shauri kwa Papa
Mwandishi wa habari wa Katoliki aliye Mwitalia Vittorio Messori aamini kwamba washiriki wa uongozi wa Kanisa Katoliki la kisasa huzungumza kupita kiasi. Yeye apendekeza kwamba wao ‘warahisishe na kukazia akili’ jumbe zao. Katika mahoji yaliyoripotiwa na shirika la habari la Adista la Katoliki, yeye alisema: “Hesabu sahili yaonyesha kwamba katika viwango vyote vya madaraka kanisa limezungumza mambo mengi zaidi katika miaka 20 ambayo imepita kuliko lilivyozungumza katika karne 20 zilizotangulia. Kadiri mtu azungumzavyo zaidi, ndivyo hasikilizwi sana. Nimependekeza pumziko la miaka saba ambalo kanisa lapaswa kunyamaza, tokea naibu wa kasisi wa parokia hadi Papa. . . . Taarifa hizi zote na barua kwa maaskofu . . . Mimi huzisoma, lakini ni wengine wangapi ambao hufanya hivyo? Tunapaswa kujidhabihu na kurudia desturi za papa wa miongo michache iliyopita. Wao hawakuwa wakiandika zaidi ya barua tatu kwa maaskofu.”
Misisimko Inayoua
Kuruka banji, kupanda majabali bila kamba, kuruka angani, kuruka kutoka kwa majengo marefu kwa miavuli—michezo ya kusisimua—imekuja kupendwa sana katika Ufaransa. Gazeti la habari la Paris Le Monde liliuliza wastadi kadhaa sababu inayofanya michezo ya kusisimua ipendwe sana katika Ufaransa. Alain Loret, mkurugenzi wa kituo cha uchunguzi wa michezo mipya, alisema sababu moja ni kwamba michezo ya kawaida, ambayo huhitaji sheria, nidhamu, na mazoezi, haipatani na mapendezi ya vijana wa leo, ambao huona uhuru na raha ni muhimu kuliko uhitaji wa nidhamu. Kulingana na mwanasoshiolojia Mfaransa David Le Breton, “upendezi unaozidi kukua wa michezo hatari ni wonyesho wa tatizo la maadili. Kwa hakika, hata hatujui tunaishi kwa ajili ya nini. Jumuiya yetu haituambii kwamba uhai ni muhimu. Kwa hiyo, kutafuta msisimko . . . kwaweza kueleweka kuwa njia ya kufanya uhai uwe na maana.” Lakini, vijana wengi zaidi na zaidi wanahatarisha uhai wao na kuupoteza.
Aleksandria la Kale Lapatikana
Kwanza, waakiolojia walitangaza kwamba katika bahari iliyo karibu na Aleksandria, Misri, walivumbua ile Pharos, ambao ni mnara wa taa wenye miaka 2,200, na ambao pia ni mmojawapo maajabu saba ya ulimwengu wa kale. Sasa wanasema wamepata “magofu ya makao ya kale ya kifalme ya Aleksandria chini ya maji ya kina cha meta sita hivi sehemu ya mashariki ya bandari ya kale ya Aleksandria,” lasema The Vancouver Sun. Kulingana na mwakiolojia wa maji Mfaransa Franck Goddio, mahali hapo pana magofu ya makao ya Mark Antony na ya hekalu na vilevile magofu ya makao ya Cleopatra, kutia ndani mitungi ya divai, nguzo za mawe magumu, barabara za mawe, na masalio mengine ya jiji hilo la kale. Watafiti hao walipata “bandari nzuri iliyokingwa na gati ndefu ambayo bado ina hali nzuri baada ya miaka 2,000, lakini hiyo iko ndani ya maji,” Goddio akasema. Aleksandria lilipata jina kutokana na Aleksanda Mkubwa, ambaye baada ya kuona bandari hiyo maridadi katika 332 K.W.K. aliazimia kwamba hiyo ingekuwa mahali pa jiji. Ikawa kitovu cha kitamaduni na kibiashara ambacho kililingana na Athene na Roma. Maktaba mashuhuri ya Aleksandria ilikuwa huko. Lakini katika Enzi za Katikati, sehemu kubwa ya jiji hilo la kale haikuwapo tena, kwa sababu iliharibiwa na matetemeko ya dunia na mioto na kuzamishwa na bahari.
Mileani Huanza Lini?
Usiku-kati, Desemba 31, 1999, watu wengi ulimwenguni pote watasherehekea mileani mpya, na mipango ya sherehe zilizo kubwa tayari imefanywa. Lakini ingawa ni “jambo la kawaida kwa mwaka kamili kama huo” kusherehekewa, yasema taarifa kutoka Royal Greenwich Observatory, kule Cambridge, Uingereza, “kusema kwa usahihi, tutakuwa tukisherehekea mwaka wa 2,000, au mwaka wa mwisho wa mileani, wala si mwanzo wa mileani mpya.” Utatanisho watokana na badiliko la kutoka K.W.K. hadi W.K. lililoamuliwa na Bede, ambaye alikuwa mwanahistoria na mwanatheolojia wa karne ya saba, na aliyejaribu kuweka tarehe kulingana na siku ya kuzaliwa kwa Yesu. Hakuna mwaka wa sufuri uliotiwa ndani, kwa hiyo wakati uliokuwa kati ya mwaka wa 1 K.W.K. na siku ya kwanza ya mwaka wa 1 W.K. ulikuwa mwaka mmoja tu. Basi, mileani ya kwanza ilianza kwa siku ya kwanza ya mwaka wa 1 W.K. na kuishia siku ya mwisho ya mwaka wa 1000 W.K. Kisha mileani ya pili ikaanza Januari 1, 1001. “Basi ni wazi kwamba mwanzo wa mileani mpya utakuwa Januari 1, 2001,” watafiti hao wakasema. Kwa vyovyote vile, sherehe hizo zitategemea kalenda ya Gregory pekee bali si kwenye uzaliwa hasa wa Yesu, ambaye sasa imejulikana alikuwa amezaliwa muda fulani mapema zaidi ya hapo.
Rekodi Mbaya
“Marekani ina kiwango cha juu zaidi cha maradhi ya kupitishwa kingono kuliko nchi nyingine yoyote iliyoendelea ulimwenguni na haina mfumo wenye matokeo ya kukabiliana na pigo hilo [chasema] kikoa cha wataalamu wa afya,” kama ilivyoripotiwa katika The New York Times. Kulingana na halmashauri ya Taasisi ya Dawa, ambayo ni tawi la National Academy of Sciences, maradhi mengi yanayopitishwa kingono yanayoambukiza Wamarekani yaweza kuzuilika lakini hayo bado yanaendelea kusababisha matatizo mazito ya afya, kama vile kansa, na maelfu ya vifo kila mwaka. Baada ya uchunguzi wa miezi 18, halmashauri hiyo yenye washiriki 16 ilipata kwamba kwa kila dola 43 zilizotumiwa kwa tiba na gharama nyinginezo, ni dola 1 pekee iliyotumiwa kuzuia maradhi hayo. Ripoti yao yasema kwamba visa vipya vipatavyo milioni 12 kila mwaka huhusisha vijana. Yakiachwa bila kutibiwa, maradhi hayo—ambayo yatia ndani malengelenge ya ngozi, mchochota wa ini aina ya B, klamidia, kisonono, na kaswende—yaweza kusababisha kutoweza kuzaa, kasoro za uzazi, kuharibika kwa mimba, kansa na kifo. Bila kuhesabu gharama ya virusi HIV vinavyopitishwa kingono, ambavyo ndivyo husababisha UKIMWI, maradhi hayo yote hugharimu taifa hilo angalau dola bilioni 10 kwa mwaka.
Kutafuta Antaktika Safi
Japo hali joto za wakati wa kiangazi za digrii 10 Selsiasi chini ya sufuri, idadi ya wageni wanaozuru Antaktika imerudufika katika miaka kumi ambayo imepita. Watu 10,000 walifanya matayarisho ya mapema yaliyogharimu kufikia dola 9,000 ili kuona bara hili lenye ngwini, sili, na maajabu ya bara lililoganda la kilometa milioni 13 za mraba. Lakini wasafiri hao hodari ni wepesi kulalamika kuhusu takataka zilizoachwa na mataifa yaliyofanya kazi huko—vibanda vilivyoachwa, mapipa ya mafuta, takataka, na hata kompyuta za zamani, laripoti The Independent la London. Dakt. Bernard Stonehouse wa Taasisi ya Scott Polar, katika Cambridge, Uingereza, aliyechapisha kitabu cha mwongozo cha kwanza cha usafiri katika eneo hilo, asema hivi juu ya vichafuzi hivyo: “Hawakujali kuondoa takataka katika nyakati zilizopita, lakini sasa wanafanywa wajali. Watalii na wageni wamekuwa wakilalamika kwamba hawakutoa pesa ili waone takataka.”
Bahati Nasibu Zashinda Makanisa
Wamarekani hutumia pesa nyingi zaidi katika bahati nasibu kuliko wanavyochangia makanisa yao, lasema shirika la habari la Associated Baptist Press. Kama ilivyoripotiwa katika Christian Century, ulinganifu wa ripoti ya tarakimu za Ofisi ya Idadi ya Watu ya Marekani na ripoti za Yearbook of American and Canadian Churches waonyesha kwamba katika 1994, Wamarekani walitumia dola bilioni 26.6 katika bahati nasibu za serikali lakini walichanga dola bilioni 19.6 tu kwa makanisa yao.
Havifai kwa Mbu
Vipiga-wadudu, vile vitu ambavyo huning’inizwa nje ambavyo huvutia wadudu usiku na kuwapiga umeme kwa kelele, havifai kwa mbu. “Hivyo vipiga-wadudu havifai kabisa,” asema George B. Craig, Jr., ambaye ni profesa wa elimu ya wadudu. Mbu wengi hawavutiwi na nuru na wanapolenga mlo, wale wa kike—ambao ndio huuma—hutafuta amonia, kaboni dioksidi, joto, na mitoko mingine ya ngozi ambayo haitolewi na vipiga-wadudu. Wasipopata vitu hivyo wao huenda zao. Isitoshe, kujaribu kuua mbu kwa vipiga-wadudu ni kama “kujaribu kuondoa maji baharini kwa kutumia vijiko vya chai,” asema Dakt. Craig. Mbu wa kike aweza kutokeza wazao zaidi ya 60,000 kwa miezi michache tu. Uchunguzi wa miezi mitatu ulionyesha kwamba kwa usiku wa wastani, ni asilimia 3 tu ya wadudu waliouawa walikuwa mbu wa kike. Vipiga-wadudu, asema Craig, “vyapaswa kuuzwa katika sehemu ya duka inayoshughulikia mambo ya nyumbani badala ya sehemu inayohusika na bustani.”