Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 6/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuondoka Majijini Kuelekea Mashambani
  • Kanisa Lakubali Mhudumu Aliyegeuzwa Jinsia
  • Alama za Vidole za Koala Zinazofanana na za Binadamu
  • Je, Watu Hujifunza Talaka?
  • Radhi Yaombwa Baada ya Miaka 500
  • Jihadhari na Maagizo Bandia ya Dawa
  • Matatizo Zaidi ya Makasisi
  • Pumzi ya Kitunguu-Saumu
  • Kufunga Uzazi kwa Kike Kwaongezeka
  • Kupigania Samaki
  • “Jinsi Tunavyokumbuka . . . Vitunguu Saumu!”
    Amkeni!—2005
  • Toka Ufukara Hadi Utajiri Mkubwa Zaidi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • Kutumika Tukiwa Wavuvi wa Watu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 6/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kuondoka Majijini Kuelekea Mashambani

Wakiwa wamechoshwa na mkazo na hekaheka za mtindo-maisha wa majijini, idadi ndogo lakini inayoongezeka ya Wajapani inaondoka majijini kuelekea mashambani. Ingawa yaweza kuwa kweli kwamba maisha ya mashambani huandaa kawaida sahili katikati ya mazingira ya kiasili, kuacha maisha ya jijini ili kuishi mashambani kuna matatizo pia. “Wakulima wengi wapya wameacha mishahara thabiti, hali isiyo na taabu ya maisha ya jijini na labda hadhi ya kijamii ya kuwa sehemu ya kampuni mashuhuri,” lasema Asiaweek. Isitoshe, “waliogeuka kuwa watu wa mashambani wanakiri kwamba wamelazimika kupunguza matumizi yao, na nyakati fulani wamelazimika kuongezea mapato yao ya mavuno kwa kufanya kazi za ziada zilizo duni.” Lakini kwa wale ambao wameazimia kufanya badiliko, Wizara ya Kilimo imeanzisha Shule ya Matayarisho ya Ukulima ili kusaidia wakazi wa majijini wabadilikane kwa maisha ya mashambani.

Kanisa Lakubali Mhudumu Aliyegeuzwa Jinsia

Katika Marekani, mhudumu mmoja wa Presbiteri amepata ruhusa ya kubaki akiwa mhudumu baada ya kufanyiwa upasuaji wa kubadilishwa jinsia. Uamuzi huo ulikuja wakati Eric Swenson mwenye umri wa miaka 49 alipoomba Baraza la Kanisa la Presbiteri la Mji wa Atlanta (Georgia) kubadili jina lake kuwa Erin baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa viungo vyake vya uzazi. “Anne Sayre, mshiriki wa hilo baraza anayeshughulikia haki na wanawake, alitaja kwamba baraza la Kanisa la Presbiteri lilikuwa na ‘pambano gumu sana’ lakini likaamua halikuwa na ‘misingi yoyote ama ya kitheolojia ama ya kiadili’ ya kutangua uwekwaji rasmi huo,” laripoti The Christian Century. Lakini Don Wade, mhudumu ambaye alipiga kura dhidi ya ombi la Swenson, alisema kwamba “hakukuwa na mazungumzo mazito ya masuala ya kitheolojia.”

Alama za Vidole za Koala Zinazofanana na za Binadamu

Alama za vidole vya mkono na vidole vya mguu za koala zinafanana sana na za binadamu, asema mwanasayansi mmoja wa Australia. Profesa Maciej Henneberg, mwanabiolojia aliye pia mtaalamu wa mambo ya kitiba na matatizo ya kisheria kwenye Chuo Kikuu cha Adelaide, asema: “Hata hadubini kaguzi ya elektroni haiwezi kupata tofauti.” Ufanano huo si wa umbo la jumla la nyayo za koala bali ni wa dermatoglyphics—kiolezo cha vivimbo, miinuko, na mizingo kwenye mafumba ya nyayo zake. Na zaidi, alama za vidole vya mkono na vya mguu za koala mmoja hazifanani na za koala mwingine, kama tu ilivyo na binadamu.

Je, Watu Hujifunza Talaka?

“Waume na wake walio na wazazi waliotalikana wako katika hali ya kuona ndoa zao zikikosa kufanikiwa zaidi kuliko waume na wake ambao wazazi wao bado wameoana,” laripoti The Sydney Morning Herald, la Australia. Profesa Paul Amato, wa Chuo Kikuu cha Nebraska, Marekani, “alifuatia Wamarekani 2,000 hivi waliofunga ndoa kwa zaidi ya miaka 12” na, kulingana na hilo gazeti la habari, akapata kwamba “wazao wa wazazi waliotalikana ‘hurithi’ stadi zisizofaa za mahusiano na mwenendo ambazo huongeza sana hali ya ndoa yao kuishia katika talaka.” Gazeti Herald lilitaja: “Mahali ambapo wenzi wote wa ndoa wana wazazi waliotalikana, hatari ya mvunjiko wa ndoa iko juu kwa asilimia 300 kuliko waume na wake ambao wazazi wao wako pamoja bado.”

Radhi Yaombwa Baada ya Miaka 500

Katika 1496, Mfalme Manuel wa Kwanza wa Ureno alitoa agizo kwa Wayahudi walioishi katika eneo lake: Geukeni muwe Wakatoliki wa Kiroma, au mwondoke. Miaka ipatayo 500 baadaye, katika 1988, Ureno ilitoa ombi rasmi la radhi. Hivi majuzi, katika ukumbusho wa kidini, Ureno ilijitolea kurekebisha kosa hilo. Kulingana na ripoti ya shirika la Associated Press, rais wa Ureno, Jorge Sampaio, alisema katika hotuba mbele ya Bunge kwamba uondoshaji huo ulikuwa “tendo ovu lenye matokeo ya kina yenye msiba.” Waziri wa Sheria José Eduardo Vera Jardim aliuita uondoshaji huo “kipindi kiovu cha historia.” Aliongeza kwamba serikali yawiwa na Wayahudi “radhi” kwa karne nyingi za “unyanyasaji mkatili.” Ingawa idadi ya watu ya Ureno ni milioni 10 hivi, ni Wayahudi 1,000 hivi wanaoishi huko.

Jihadhari na Maagizo Bandia ya Dawa

Ikiwa na mauzo ya kila mwaka ya dola bilioni 16 hivi, biashara ya dawa bandia inanawiri. Kulingana na gazeti la habari la Paris Le Monde, “Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lakadiria kwamba angalau asilimia 7 ya dawa zinazouzwa ulimwenguni pote kila mwaka ni bandia.” Katika Brazili asilimia hiyo yaweza kuwa juu sana kufikia asilimia 30, na katika Afrika, asilimia 60. Dawa bandia zaweza kuwa kuanzia na miigizo hafifu ya bidhaa halisi hadi vitu bure kabisa hata vyenye sumu. Gazeti Le Monde lataja kielelezo cha maradhi ya utando wa ubongo katika Niger, ambapo maelfu ya watu walichanjwa na kilichogunduliwa baadaye kuwa maji tu. Na katika Nigeria, watoto 109 walikufa walipopewa shira ambayo ilikuwa na kishushamgando. “Hospitali zenyewe mara nyingi hununua dawa kutoka biashara zisizo halali kwa sababu hizo huandaa bidhaa kwa bei zenye kumudika,” lataarifu gazeti hilo la habari. Katika nchi nyingi wataalamu wa afya wana ugumu kupata suluhisho kwa tatizo hilo kwa sababu ya utekelezaji sheria usio na matokeo au wenye ufisadi.

Matatizo Zaidi ya Makasisi

Maaskofu 40 hivi wa Episkopali walitia sahihi taarifa katika Novemba 1996 wakidai kanisa “liandae viwango vya waziwazi na vyenye kuwajibisha kuhusiana na mwenendo wa kingono wa makasisi,” laripoti gazeti Christianity Today. Kanisa limekuwa likivurugwa na kashfa zenye kuhusisha makasisi, ambazo Waepiskopali wasiopendelea mabadiliko husema zinatokana na “kukosa kutaja waziwazi fundisho la kanisa kuhusu mwenendo wa kingono.” Kwa kielelezo, mchungaji mkuu wa kanisa moja la Kiepiskopali katika Brooklyn, New York, alijiuzulu baada ya kukiri kuwa alikuwa na mahusiano ya ugoni-jinsia-moja. Todd Wetzel, mkurugenzi mkuu wa Episcopalians United, alisema: “Kanisa halikabiliani na kashfa moja. Linakabiliana na kashfa nyingi, ambazo hii ndiyo yenye kushtua zaidi.” Hapo awali, kanisa lilikuwa limepata utangazaji mwingi lilipomwekea askofu Walter Righter mashtaka ya uzushi kwa sababu ya kumtawaza rasmi shemasi mgoni-jinsia-moja aliye mtendaji kingono. Mashtaka hayo yaliachwa baada ya “mahakama ya Kiepiskopali kuamua kwamba kanisa hilo halikuwa na ‘fundisho la msingi’ lenye kuwekea mipaka ngono iwe katika ndoa tu.”

Pumzi ya Kitunguu-Saumu

Serikali ya Taiwan hivi majuzi ilichukua hatua za uvumbuzi ili kusaidia kupunguza ugavi wa kupita kiasi wa kitunguu-saumu. Wenye mamlaka wametia moyo watu “wale vitunguu-saumu zaidi,” lataarifu South China Morning Post. Ofisa wa Taiwan kwenye Baraza la Kilimo, Bw. Ku Te-yeh, alieleza: “Kwa kweli tulipanda vitunguu-saumu vingi kupita kiasi mwaka huu.” Katika jitihada ya kuongeza utumizi, serikali inachapisha kijitabu chenye maelezo ya upishi ya kitunguu-saumu. Hata hivyo, Bw. Ku alikiri kwamba “watu wasingeweza kutarajiwa kula vitunguu-saumu vyote ili kusuluhisha tatizo hilo,” lasema gazeti hilo la habari.

Kufunga Uzazi kwa Kike Kwaongezeka

Katika miaka ya 1960 familia ya wastani ya Brazili ilikuwa na watoto 6.1 kwa nyumba moja; leo wastani huo ni watoto 2.5. Kwa nini upungufu huo mkubwa? Kulingana na uchunguzi wa Applied Economy Research Institute, sababu moja ni kwamba “asilimia 40 ya wanawake walioolewa [katika Brazili] wamefungwa uzazi,” lataarifu Jornal do Brasil. Isitoshe, mwelekeo wa kawaida ni kwa wanawake kufungwa uzazi wakiwa katika umri wa mapema. Kwa kielelezo, umri wa wastani kwa mwanamke Mbrazili kufungwa uzazi miaka kumi iliyopita ulikuwa 34; leo ni 29. Uchunguzi huo pia ulitaja kwamba “kufunga uzazi kwingi hufanywa wakati wa kuzaa,” hasa kuhusiana na uzaaji wa kupasuliwa. Kinyume cha hilo, ni asilimia 2.6 tu ya wanaume wa Brazili wamekubali kufungwa uzazi.

Kupigania Samaki

Hali ya mashua nyingi mno kufuatia kwa bidii ugavi wenye kupungua wa samaki “imesababisha mizozano motomoto kati ya vikosi vya mashua za uvuvi na wanamaji wenyeji,” laripoti U.S.News & World Report. Katika 1990 vikosi vya uvuvi viliongezeka hadi mashua milioni tatu, karibu maradufu ya idadi ya 1970. Na zaidi, vifaa vya kisasa vya uvuvi, kama vile sona za kutafuta samaki na nyavu kubwa za kuvulia samaki kwa kukokota, vimeongeza sana matokeo ya wavuvi. “Tokeo halisi ni kwamba serikali za mataifa yanayopakana na bahari zinahusika katika mapigano yasiyokoma na vikosi vya uvuvi vya kutoka nchi za kigeni” huku zikijaribu kulinda ugavi wazo unaopungua wa samaki. Katika miaka miwili pekee iliyopita, mapigano madogo-madogo kwenye bahari kuu kati ya vikosi vya uvuvi vilivyo adui yametokeza vifo vya wavuvi wanane.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki