Kuna Wakati Ujao Gani kwa Albatrosi?
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Uingereza
Kuna wakati ujao gani kwa albatrosi, aliye ndege mkubwa zaidi kati ya ndege wa bahari? “Ni wa kuhofisha sana,” laripoti The Times la London. Makumi ya maelfu ya ndege hawa—watafiti wa Australia wakadiria kama 44,000—huuawa kila mwaka. Kwa hakika, wataalamu fulani wahisi kwamba yule albatrosi mwenye kuruka sana, aliye na upana wa mabawa ufikao meta 3, karibuni atatoweka.
Baada ya albatrosi kuwa tayari kuruka, wao huwa baharini kwa miaka saba mfululizo, wakipaa angani na kunyiririka kwa maelfu ya kilometa na hata kulala usingizi wakiwa hewani. Watu fulani huamini kwamba ndege hao waweza kuzunguka dunia mara kadhaa kabla ya kurudi katika sehemu zao za kutagia mayai.
Albatrosi hulea kinda moja kila mwaka wa pili. Lakini katika miaka 20 ambayo imepita, idadi ya albatrosi wenye kuruka sana katika South Georgia katika eneo la Atlantiki ya Kusini na katika Crozet katika Bahari-Kuu ya Hindi imepungua kwa karibu nusu. Wengine wafikiri sababu yaweza kuwa ni nini? Kuvua samaki kwa kutumia mishipi mirefu.
Ili kuvua samaki aina ya bluefin tuna, wavuvi hutumia mishipi mirefu, kila mmoja ukiwa na mamia ya ndoana. Mishipi hiyo huteremshwa kwenye tezi ya mashua ya uvuvi. Kila ndoana imewekewa ngisi kuwa chambo—ngisi ni chakula kikuu cha albatrosi. Ndege huyo ashukapo kwa kasi kuchukua ngisi, pindi kwa pindi yeye humeza ndoana vilevile. Kisha huyo albatrosi aliyenaswa huzama pamoja na ule mshipi mzito na kufa maji.
Ili kulinda albatrosi, wavuvi fulani wa tuna wametiwa moyo kwa mafanikio kuweka mishipi yao wakati wa usiku, wakati ambapo ndege huyo havui samaki. Pia wavuvi wanatafuta njia za kuweka mishipi kutoka chini ya mashua zao ili albatrosi asiweze kuona chambo. Mbinu nyinginezo ambazo zimetumiwa zatia ndani kuweka mishipi mizito ambayo huzama haraka na aina fulani ya kitu chenye kuwaogofya ndege hao.
Lakini, katika bahari zilizo wazi za Atlantiki ya Kusini, njia za uvuvi hazichunguzwi. Kulingana na mtaalamu wa ndege wa bahari Sandy Bartle, wa Jumba la Kuhifadhi Vitu vya Kale la New Zealand, mashua zilizoko huko “hazijaribu kuzuia albatrosi wasiuawe.” Kwa kweli, kuwezekana kufa kwa ndege hao wenye fahari ni wonyesho wa uzembe na kutojali kwa binadamu.