“Mashini Bora Zaidi Angani”
NDEGE anayeitwa albatrosi amefafanuliwa kuwa “mashini bora zaidi angani,” na amefafanuliwa hivyo kwa sababu nzuri. Ndege huyo ambaye ndiye mkubwa zaidi kati ya ndege wa baharini ana mabawa yenye upana wa mita 3 kutoka ncha moja hadi nyingine na anaweza kuruka kwa mwendo wa kilomita 115 hivi kwa saa. Huenda albatrosi akaonekana kuwa hapendezi akiwa ardhini, lakini angani yeye hupendeza.
Inakadiriwa kuwa aina 15 kati ya aina 20 za albatrosi wanaojulikana, wanapatikana katika bahari inayozunguka New Zealand. Eneo pekee ambalo ndege hao hutaga mayai katika Kizio cha Kusini ni Rasi ya Taiaroa, kwenye ncha ya Rasi ya Otago, iliyo kwenye Kisiwa cha Kusini cha New Zealand.
Wakiwa huko, albatrosi aina ya northern royal huanza kutaga mayai wakiwa na umri wa kati ya miaka sita hadi kumi. Wao huendelea kufanya hivyo muda wote wa maisha yao marefu. Inasemekana kwamba baadhi ya ndege hao wameishi zaidi ya miaka 50! Albatrosi hutaga yai moja baada ya kila miaka miwili kwani yeye huishi baharini kwa mwaka mmoja. Kwa kawaida, ndege huyo huishi na mwenzi mmoja tu maisha yake yote.
Albatrosi wa kiume na wa kike hushirikiana kujenga kiota chao kuanzia Septemba (Mwezi wa 9). Kisha, Novemba (Mwezi wa 11) inapofika, albatrosi wa kike hutaga yai lenye uzito wa gramu 500 hivi. Kwa siku 80 hivi, ndege wote wawili husaidiana kulalia yai hilo hadi linapoanguliwa mwanzoni mwa Februari (Mwezi wa 2). Kisha wazazi hao husaidiana kulinda na kumlisha kinda wao. Kinda huyo hula hasa samaki na ngisi waliocheuliwa na wazazi wake. Anapokuwa na umri wa miezi sita, kinda huyo anaweza kuwa na kilogramu 12, uzito unaozidi ule wa albatrosi aliyekomaa!
Baada ya mwaka mmoja hivi, wazazi huondoka kwenye Rasi ya Taiaroa na kuishi kwa mwaka mmoja baharini, kisha wanarudi tena kutaga. Katika kipindi hicho, kinda wao alipunguza uzito, akawa na manyoya mengi, na kujifunza kunyoosha mabawa na kuruka. Anaelekea wapi? Baharini ambapo albatrosi huyo mchanga ataishi kwa miaka kadhaa inayofuata. Anapoanza kubalehe, albatrosi atarudi kwenye Rasi ya Taiaroa. Akiwa huko albatrosi huyo mchanga atatumia wakati wake kujisafisha, kuchezacheza, na kuonyesha ustadi wake wa kuruka, huku wale waliokomaa wakijishughulisha na kujenga viota na madaraka ya uzazi.
[Sanduku katika ukurasa wa 25]
KUWATEMBELEA ALBATROSI WANAOITWA ROYAL
Tangu utotoni, nilifurahia sana hadithi za albatrosi, kwa hiyo, nilisubiri kwa hamu sana kutembelea hifadhi ya albatrosi wanaoitwa royal. Ilikuwa siku yenye upepo mkali, kwa hiyo, mimi na mwenzangu tulipokaribia eneo hilo tulitazama angani ili tuwaone wakiruka. Tulistaajabu kuwaona ndege hao ambao ni stadi wa kupaa angani!
Tulipofika, tuliungana na kikundi cha watalii wengine ili tutembezwe kwa saa moja hivi. Kupitia mifano, picha, na video, tulijifunza kwamba albatrosi anayeitwa northern royal anaweza kuishi baharini na hata kulala juu ya maji! Iwe yuko juu ya maji au juu angani, kwa kweli ndege huyo anastaajabisha na kutupa sababu nyingine ya kumsifu yule ‘aliyeumba vitu vyote,’ Yehova Mungu!—Ufunuo 4:11.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Wazazi wote wawili husaidiana kulinda na kumlisha kinda wao ambaye anapokuwa na umri wa miezi sita anaweza kuwa na uzito wa kilogramu 12
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Rasi ya Taiaroa, ndiyo makao ya albatrosi anayeitwa “northern royal”
[Picha katika ukurasa wa 24]
Albatrosi anayeitwa “northern royal” anaweza kuishi baharini na hata kulala juu ya maji
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Top: © David Wall/Alamy; bottom: © Kim Westerskov/Alamy
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Background: © davidwallphoto.com; page 24, top: Tui De Roy/Roving Tortoise Photos; page 24, bottom: Courtesy Diarmuid Toman; page 25, albatross in flight: © Naturfoto-Online/Wolfgang Bittmann