Kurudi kwa Yule Ndege Mkubwa Mweupe
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAPANI
WAKIWA na kijiti mkononi, wanaume hao walienda kuwapiga wale ndege maridadi weupe mmoja baada ya mwingine hadi wakafa. Ndege hao walikuwa albatrosi. Wanaume hao: Hanemon Tamaoki na washiriki wake. Mahali: Torishima, kisiwa kilichoko kilometa 600 kusini ya Tokyo. Ulikuwa mwaka wa 1887.
Tamaoki alikuwa amepanga jambo hili kwa miaka kadhaa. Manyoya mororo kwa ajili ya magodoro yalitakwa sana katika nchi yake na pia nchi za nje, na Torishima kilikuwa kisiwa cha mbali sana ambacho wakazi wake pekee walikuwa maelfu ya albatrosi ambao walikuja huko kwa ukawaida ili kuzaana. Kati yao kulikuwa na albatrosi mwenye mkia mfupi, ambaye hasa alimpendeza Tamaoki. Alikuwa ndege mkubwa zaidi wa baharini wa Kizio cha Kaskazini. Hebu wazia ni manyoya mangapi yaliyoufunika mwili mnono ambao ulikuwa na uzito wa karibu kilogramu nane na wenye upana wa mabawa upatao meta 2.5! Zaidi ya hayo, ndege huyu alikuwa mwelekevu na hakuthubutu kutoroka hata wakati alipohatarishwa.
Tamaoki alileta wafanyakazi wapatao 300 kwenye kisiwa hicho ili wasaidie kuwaua na kuwakwanyua ndege hao. Walijenga kijiji na barabara ndogo ya reli ili kusafirisha ndege waliouawa. Utendaji huo ulikuwa wenye matokeo sana hivi kwamba Tamaoki akawa tajiri sana—kwa kuua karibu ndege milioni tano. Angamizo hilo lilikuwa kubwa sana hivi kwamba wakati volkano ya kisiwa hicho ilipolipuka katika mwaka wa 1902, ikiharibu kijiji hicho na wakazi wake wote, watu fulani waliona jambo hilo kama “laana kwa sababu ya kuwaua albatrosi.” Ijapokuwa hivyo, mwaka uliofuata, watu wengine walirudi tena, kutafuta ndege walioachwa.
Karibu kilometa 1,500 kwenye Bahari ya Mashariki ya China kwenye kikundi cha visiwa vilivyo ukiwa, vyenye miamba kati ya Taiwan na Okinawa, mwanamume aliyeitwa Tatsushiro Koga alikuwa na biashara kama hiyo yenye kuleta pesa nyingi. Kama vile Tamaoki, Koga alipata kwamba ugavi wake wa ndege ulipungua kwa haraka. Mwishowe alikihama kisiwa hicho katika mwaka wa 1900—lakini tayari alikuwa amewaua albatrosi karibu milioni moja.
Tokeo Lenye Kuhuzunisha la Pupa
Uuaji huo wa jumla wa ndege ulikuwa msiba uliokuwa na matokeo ya kuogofya. Kati ya zile spishi kadhaa za albatrosi, spishi tatu huishi katika Kaskazini mwa Pasifiki, zikiwa na sehemu zao za msingi za kuzalisha kwenye visiwa vilivyoporwa na Tamaoki na Koga. Moja yazo, albatrosi mwenye mkia mfupi (Diomedea albatrus), kwa msingi wa uthibitisho uliopo hakuwa na mahali pengine pa kuzalia ulimwenguni palipojulikana.
Wakati mmoja hawa albatrosi walionwa kwa kicho na mabaharia kwenye bahari iliyo mbali na bara. Hekaya na itikadi za kitamaduni za baharini zilimwonyesha kuwa dalili ya pepo, na ukungu. Hata hivyo, si hekaya kwamba mabawa marefu ya ndege huyu mweupe mkubwa yalimsaidia kupaa juu na kuvuka bahari kwa siku chache wakati mwingi akipepea kwenye pepo mabawa yakiwa karibu bila kusonga kabisa. Uwezo wake wa kunyiririka na kubaki baharini kwa vipindi virefu vya wakati ni usioweza kulinganika.
Ingawa albatrosi aweza kupaa kwa madaha hewani, mwendo wake ardhini ni wa polepole na usio na madaha. Mabawa yake marefu na mwili wake ulio mnono kiasi humzuia asiweze kuruka haraka. Hili, pamoja na kutoogopa mwanadamu, kulimfanya ndege huyu kuwa rahisi kuwindwa. Kwa sababu ya hilo watu walimpa majina kama vile ndege mjinga.
Watu wasiowajibika ambao walichochewa na ujuzi wa kwamba albatrosi waliokufa walitokeza pesa waliendelea kuwaangamiza kwa furaha. Ukaguzi fulani ulifunua kwamba kufikia 1933, kulikuwa na ndege waliopungua 600 huko Torishima. Kwa kutamauka, serikali ya Japani ilitangaza kupigwa marufuku kwa wanadamu kuingia katika kisiwa hicho. Lakini watu wasio waadilifu walikimbia katika kisiwa hicho na kuua ndege wengi kadiri walivyoweza kabla sheria hiyo haijaanza kutumika. Kulingana na mtaalamu mmoja, kufikia mwaka wa 1935, ni ndege 50 tu waliobakia. Hatimaye, ikabidi kumtangaza albatrosi mwenye mkia mfupi kuwa ametoweka. Ni matokeo yenye kuhuzunisha kama nini ya pupa ya mwanadamu! Lakini staajabu kubwa ilikuwa akibani.
Kurudi Kwaanza
Jioni moja katika Januari 1951, mwanamume mmoja aliyekuwa akipanda miamba ya Torishima alishtushwa na kishindo cha ghafula. Alijipata akimwangalia albatrosi moja kwa moja! Albatrosi mwenye mkia mfupi aliokoka kwa njia fulani na sasa alikuwa akizaana katika Torishima tena. Hata hivyo, wakati huu, ndege huyu alikuwa akifanya kiota katika ardhi yenye mwinamo iliyokuwa karibu vigumu kufikiwa na mwanadamu. Na walielekea kuwa na hadhari kuelekea mwanadamu. Wapenda-asili walifurahi jinsi gani!
Serikali ya Japani ilichukua hatua upesi. Walipanda nyasi ili kuifanya ardhi kuwa imara zaidi kwa ajili ya viota na wakapiga marufuku wanadamu kutoenda huko Torishima. Albatrosi alitangazwa kuwa hazina ya kitaifa na akawa ndege aliyelindwa kimataifa.
Tangu 1976, Hiroshi Hasegawa, wa Chuo Kikuu cha Toho, Japani amekuwa akiwachunguza ndege hawa na sasa yeye hutembelea kisiwa hicho mara tatu kwa mwaka ili kuwakagua. Aliambia Amkeni! kwamba kufanya alama za mviringo kwenye miguu ya ndege hao kwa rangi tofauti kila mwaka, amegundua kwamba ni mara moja tu kwa miaka mitatu au minne albatrosi wenye mkia mfupi hurudi mahali walipozaliwa ili kuzaana. Kwanza wao huzaa wakiwa na umri wa miaka sita na wao hutaga yai moja kila wakati. Kwa hiyo, hata wakiwa na wastani wa muda wa maisha ya miaka 20, inachukua muda mrefu kuongeza idadi yao. Kati ya yale mayai 176 yaliyotagwa huko Torishima katika majira ya baridi kali ya miaka ya 1996 na 1997, ni mayai 90 tu yaliyoanguliwa.
Albatrosi hufanya nini wakati huo mwingine? Hasegawa asema kwamba ni mambo machache yajulikanayo kuhusu hili. Kwa wazi wao huepuka bara na wanadamu. Je, albatrosi hufuata na kutua juu ya meli? Kulingana na Hasegawa, hiyo ni hekaya tupu isiyo na uthibitisho wa kuitegemeza. Yeye asema kuwa ana hakika kwamba “albatrosi wa Japani hawatui juu ya meli.” Lakini aongeza kwamba kwingineko katika ulimwengu, “ndege fulani waweza kukaa melini kwa muda mfupi ikiwa wanapewa chakula.” Mara nyingi, wao hufanya lile wafanyalo vizuri zaidi—kupaa kwa kupendeza kwenye pepo na kuzurura-zurura hiyo bahari kubwa. Wanapochoka, wao hulala wakiwa wameelea juu ya bahari. Wao hula ngisi, samaki warukao, kaa, na uduvi. Ndege ambao Hasegawa amewaweka alama za mviringo kwa kawaida huonekana katika Bering Sea na Gulf of Alaska. Na katika mwaka wa 1985 kuonekana kwa albatrosi mwenye mkia mfupi kwenye pwani ya California—kwa mara ya kwanza kwa muda wa karibu karne moja—kulisababisha msisimko kati ya watazama-ndege.
Namna Gani Kuhusu Wakati Ujao?
Kwa uzuri, idadi ya albatrosi wenye mkia mfupi inaongezeka kwa usawa. Mwezi wa Mei uliopita, Hasegawa alikadiria kuwa kulikuwa na “zaidi ya 900 kutia ndani vifaranga.” Aliongezea hivi: “Kufikia mwaka wa 2000, kwapasa kuwa na ndege zaidi ya 1,000 kwenye Torishima pekee, kukiwa na zaidi ya vifaranga 100 wanaozaliwa kila mwaka.” Wenye kusisimua pia ni uhakika wa kwamba katika 1988, baada ya miaka 88, walionekana wakizaana tena katika Bahari ya Mashariki ya China. Ndege hao wamechagua mahali penye miamba katika eneo linaloshindaniwa, ambalo laweza kuandaa usalama kutokana na kuingilia kwa mwanadamu kwa muda kidogo.
Makosa ya miaka mia moja iliyopita sasa yanarekebishwa polepole. Au sivyo? Watafiti mara nyingi hupata kwamba mara nyingi wanapowakamata ndege ili kuwatia alama, wao hushtuka na kutapika. Wao hutoa katika matumbo yao vipande vya plastiki vya viwasha-sigareti vitumiwavyo mara moja, na takataka nyingine ambazo watu wanatupa bila kujali kwenye eneo la malisho ya ndege hao, baharini.
Je, upumbavu wa mwanadamu utamwongoza ndege mkubwa mweupe kwenye ukingo mara nyingine tena?
[Picha katika ukurasa wa 16]
Torishima, makao ya albatrosi mwenye mkia mfupi
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Mabawa marefu membamba ya albatrosi humwezesha kuwa stadi wa ulimwengu wa kunyiririka
[Picha katika ukurasa wa 17]
Albatrosi wenye mkia mfupi walianza kurudi tena huko Torishima