Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Nyakati Zenye Kufurahisha Nakubali kwamba kuna njia nyingi zilizo salama kwa vijana wengi kujifurahisha, kama ilivyotajwa katika makala “Vijana Huuliza . . . Naweza Kuwaje na Wakati Wenye Kufurahisha?” (Septemba 22, 1996) Twaweza kuzuru jumba la kuhifadhi vitu vya kale au makao ya wanyama au kwenda mandari au hata kufanya kikusanyiko. Hata baadhi yetu ambao hatuna pesa sana twaweza kujifurahisha kwa kuwaalika vijana wengine nyumbani kwetu ili kucheza au kwa mlo.
V. A., Brazili
Paka Shujaa Ni lazima niwajulishe jinsi nilivyothamini ile makala “Kifungo Kilichopo Kati ya Mama na Watoto Wake,” ambayo ilitokea katika toleo la Septemba 22, 1996. Naishi katika nchi ambako ngono hufanywa kiholela na ambako wasichana wengi wachanga hawasiti kutoa mimba. Naamini kwamba paka huyo mwenye watoto aliyepewa jina Scarlett ni kielelezo kizuri cha mama mwenye kudhamiria.
E. B., Mali
Nilisisimka kusoma masimulizi ya Scarlett, ambaye hakuwa na hofu kabisa katika kuokoa watoto wake kutoka kwenye gereji iliyokuwa ikichomeka. Alinivutia, nikamwona kama paka ambaye wanadamu wengi waweza kujifunza kwake. Nafikiri mnafanya vizuri sana kuchapisha makala kama hizo.
D. W., Ujerumani
Masimulizi yenu yenye kuchangamsha moyo kuhusu Scarlett na watoto wake ni makala yenye nguvu zaidi kuhusu utoaji-mimba ambayo nimepata kusoma.
J. G., Marekani
Nililia niliposoma makala hiyo. Sikuzote nimependa wanyama wa aina zote nami huthamini mambo ambayo Yehova hutufundisha kupitia hao. Mimi huhuzunika sana kujua kwamba wanadamu “wenye akili” hawawaonyeshi watoto wao utunzi na uangalifu kama huo.
C. C., Marekani
Tinnitus Asanteni sana kwa makala “Tinnitus—Je, Ni Kelele ya Kuishi Nayo?” (Septemba 22, 1996) Nimekuwa nikiiugua kwa miaka sita. Niliogopa kwamba nimeshikwa na maradhi yasiyoweza kutibika kwa sababu hakuna daktari aliyeweza kuniambia hasa tatizo langu liliitwaje. Kusoma makala yenu kumenituliza. Sasa najaribu kuivumilia ningojeapo ulimwengu mpya wa Mungu, ambako hakuna mtu atakayekuwa mgonjwa.—Isaya 33:24.
C. F., Italia
Nilianza kupatwa na tatizo hili karibu miaka kumi iliyopita. Iliogofya kuwazia kwamba ningesikia sauti hii daima! Lakini wakati huu, najaribu kuishi na sikio langu lenye kelele. Natazamia wakati ambapo, kwa sababu ya Yehova, nitasikia tena UKIMYA!
J. S., Jamhuri ya Cheki
Nimekuwa nikiugua tinnitus kwa miaka miwili na nusu ambayo imepita na nimefanyiwa uchunguzi mwingi sana wa kitiba, kutia ndani kuchunguzwa ubongo kupitia kompyuta. Hangaiko na mkazo zilikuwa matatizo ya kufadhaisha maishani mwangu. Baada ya kusoma makala yenu, ninajifunza kuishi na ugonjwa huo.
M. G. T. F., Sri Lanka
Mume wangu anaugua tinnitus. Pia ana tatizo kubwa la mshuko-moyo. Habari hii imenisaidia kuwa na hisia mwenzi zaidi kwake. Nyakati nyingine kelele hiyo humsumbua sana, na lazima nikiri kwamba sijakuwa mwenye huruma kwa kadiri ambayo nimepaswa. Nathamini sana njia yenye akili ambayo makala hiyo iliandikwa. Nina hakika kwamba hiyo itasaidia wenzi wengi wa wale ambao wanaugua tinnitus kuwa wenye uelewevu zaidi.
L. F., Marekani