Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 7/8 kur. 9-11
  • Dunia Nzima Itakapokuwa Hifadhi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Dunia Nzima Itakapokuwa Hifadhi
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Nini Jitihada Zao Zaambulia Patupu?
  • Tumaini Halisi la Kipekee la Hifadhi ya Kidunia
  • Bustani ya Wanyama—Je, Ni Tumaini la Mwisho la Wanyama wa Pori?
    Amkeni!—1997
  • Kuchunguza Bustani za Kisasa za Wanyama
    Amkeni!—2012
  • “Tazama! Mimi Ninafanya Vitu Vyote Kuwa Vipya”
    “Tazama! Mimi Ninafanya Vitu Vyote Kuwa Vipya”
  • Je, Wanadamu Wataiharibu Dunia Kabisa?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 7/8 kur. 9-11

Dunia Nzima Itakapokuwa Hifadhi

JE, UNATAKA kuona kiumbe kilicho hatari zaidi duniani? Basi tazama kioo! Ndiyo, sisi wanadamu ndio waharibifu wabaya zaidi wa dunia! Sisi hata huuana kwa wingi sana.

Ili kufanya dunia iwe salama kwa wanyama wa pori, hata katika bustani ya wanyama—hasa kama hizo zaja kuwa makimbilio ya mwisho—ni lazima vita ambayo huathiri sana mwanadamu iondolewe. Ni wanyama 91 tu kati ya wanyama 12,000 wa Bustani ya Wanyama ya Berlin waliookoka Vita ya Ulimwengu ya Pili. Bustani nyingine nyingi ziliathirika vivyo hivyo. Katika vita ya majuzi katika nchi za Balkani, wafanyakazi wenye moyo mkuu wa bustani ya wanyama walihamisha wanyama wengi wakapata usalama; lakini mamia mengine, kutia ndani dia, jamii ya paka wakubwa, dubu na mbwa-mwitu, waliuawa. Majuzi, katika misitu ya Kambodia, kulingana na maofisa walionukuliwa katika gazeti la habari The Australian, wapiganaji wa Khmer Rouge wamewachinja kimakusudi wanyama wengi walio nadra kupatikana. Kwa nini? Ili kupata silaha kwa kutoa ngozi na viungo vinginevyo vya wanyama hao!

Uporaji wa kimakusudi wa kimazingira, kama ule unaofanywa katika Visiwa vya Peron vilivyojitenga, vilivyoko kusini-magharibi mwa Darwin, Australia, ni uovu mwingine ambao ni lazima ukomeshwe iwapo wanyama watapata usalama—ndani au nje ya bustani ya wanyama. Mara mbili katika miaka mitatu, makazi ya mwari katika visiwa hivyo yamechomwa bila sababu yoyote ila tu kuua maelfu ya makinda kikatili.

Hata hivyo, katika miongo ya majuzi upotezo mkubwa zaidi wa spishi hausababishwi na uovu; bali ni athari ya ongezeko la idadi ya watu wanaohitaji sana mahali pa kuishi na ardhi ya kulima. Kwa sababu ya kuingilia daima makao ya wanyama na uchafuzi ambao hufuata, The World Zoo Conservation Strategy chaonya: “Karne ya 21 haionekani kuwa nzuri kwa habari ya mfumo wote wa asili wa dunia. Hakuna ishara yoyote ionyeshayo kwamba uharibifu unaotukia katika karibu sehemu zote za ulimwengu utakoma.”

Kwa sababu ya hangaiko linalozidi kuongezeka kuhusu wakati ujao wa dunia, wakati ambapo dunia nzima itakapokuwa hifadhi waweza kuonekana kama ndoto tu. Lakini, tumaini hilo lina msingi mzuri, si kwa maoni ya wanadamu wasioweza kuona mbali—ambao hata kwa miaka michache kama 50 iliyopita, kulingana na mwandikaji fulani wa kisayansi, hawakuweza kuona uharibifu mkubwa wa sasa wa kiikolojia—bali kwa yule ambaye aliliona, Yehova Mungu. Zaidi ya miaka 1,900 iliyopita, yeye alitabiri kikweli kwamba katika wakati wetu mwanadamu angepatikana ‘akiharibu dunia.’ (Ufunuo 11:18) Unabii huo ulipotajwa wakati ambapo dunia haikuwa na watu wengi, huenda ulionekana kana kwamba ni ndoto tu kwa wengi walioishi wakati huo, lakini umethibitika kuwa sahihi kama nini!

Kwa kinyume, uharibifu huo unatukia wakati ambapo sayansi na tekinolojia huonekana karibu kuweza kufanya muujiza: transmita ndogo-ndogo na setilaiti hufuatia miendo ya spishi zilizo hatarini mwa kutoweka, uharibifu wa misitu ya mvua waweza kupimwa barabara hadi meta za mraba kutoka anga za nje, na uchafuzi wa hewa kupimwa katika viwango vidogo sana. Lakini, isipokuwa katika visa vilivyo nadra sana, mwanadamu haonekani kama anaweza kurekebisha hali kwa kutegemea habari nyingi alizo nazo. Labda mwanadamu ni kama dereva wa gari-moshi ambalo limeharibika likiwa mwendoni. Yeye ana vifaa vya ajabu vya elektroni na vichunguzi vinavyomwonyesha kile kinachotendeka, lakini yeye hawezi kusimamisha gari-moshi!

Kwa Nini Jitihada Zao Zaambulia Patupu?

Ebu wazia kwamba katika kiwanda kikubwa, meneja mwenye kiburi asiyefuata kanuni atukia kumsikia mwenye kiwanda akisema kwamba huyo meneja hatapandishwa cheo bali atafutwa kazi katika miezi michache ijayo. Akiwa amekasirika na kuwa na uchungu, yeye atumia uwongo, hongo, na mbinu zozote zile zilizo chafu ili wafanyakazi fulani wasababishe mvurugo. Wao wafanya mashine zikwame, mazao yawe chini, na bidhaa kuwa na kasoro—lakini kwa ujanja hivi kwamba waepuka lawama. Kwa wakati uo huo, wafanyakazi wenye kufuatia haki, bila kujua kinachoendelea hasa, wajaribu kufanya marekebisho; lakini kwa kadiri wajitahidivyo, ndivyo na mambo yawavyo mabaya.

“Meneja” mbaya wa ulimwengu huu ametunga hila kama hizo dhidi ya wanadamu na dunia. Lakini sisi hatupaswi kukaa bila “ujuzi kuhusu mbinu zake,” kwa kuwa Biblia yamfunua na kuonyesha kiumbe-roho mwenye uchungu—Shetani Ibilisi—malaika aliyekuja kutaka makuu na kutamani kuabudiwa. (2 Wakorintho 2:11; 4:4) Mungu alimwondosha kutoka kwa familia Yake ya kimbingu na kumhukumia uharibifu.—Mwanzo 3:15; Waroma 16:20.

Kama yule meneja mbaya wa kiwanda, huyu “baba ya uwongo” pia hutumia mbinu nyinginezo mbaya ili kuonyesha hasira yake. Yeye amemchukia Yehova Mungu naye anataka kuharibu uumbaji Wake. (Yohana 8:44) Silaha kali zaidi za Shetani ni propaganda za uwongo, pupa, ufuatiaji wa vitu vya kimwili, na mafundisho ya kidini yenye kudhuru. Akitumia hizo yeye ‘ameiongoza vibaya dunia yote inayokaliwa’ na kugeuza wanadamu—wale waliokusudiwa kuihifadhi—kuwa waharibifu wakubwa zaidi, na hivyo kuwa kama wafuasi wa Nimrodi wa kale, aliyekuwa “mwindaji hodari dhidi ya Yehova.”—Ufunuo 12:9, 12; Mwanzo 1:28; 10:9, NW.

Tumaini Halisi la Kipekee la Hifadhi ya Kidunia

Hata hivyo, ushindi juu ya kani za kibinadamu na zizidizo za kibinadamu ambazo zinasababisha kutoweka kwa wanyama waweza kupatikana. Muumba mweza-yote wa vitu vyote vilivyo hai aweza kutuondoa kwenye hali hii mbaya sana, naye ameahidi kufanya hivyo kupitia serikali yake ya kimbingu. Yeye aahidi kuangamiza waharibifu hao wanaoharibu dunia. Sisi husali hilo litukie tusemapo: “Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.”—Mathayo 6:9, 10, Union Version; Ufunuo 11:18.

Je, uliona kwamba kuja kwa Ufalme huo kunahusika na kufanywa kwa mapenzi ya Mungu duniani? Hiyo ni kwa sababu Ufalme wa Mungu ni serikali ya Mungu ya kutawala juu ya dunia. Na kwa kuwa huo ni ufalme, basi una mfalme—Yesu Kristo, ambaye ni “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.” (Ufunuo 19:16) Pia una raia. Hata Yesu alisema: “Wenye furaha ni wenye tabia-pole, kwa kuwa wao watairithi dunia.” (Mathayo 5:5) Ndiyo, hao wenye tabia-pole ndio raia watakaoishi duniani, na kwa msaada wa Ufalme wa Mungu, wao watatunza kwa upendo urithi wao, wakiugeuza kuwa paradiso iliyojaa viumbe. Kwa kupendeza, Strategy chasema: “Wakati ujao wa wanadamu na asili waweza tu kuhakikishiwa usalama ikiwa wanadamu wote waweza kuishi kwa upatano mpya na asili.”

Historia na asili ya binadamu isiyokamilika zaonyesha kwamba haiwezekani kwa “wanadamu wote” leo kupata kuishi kwa “upatano mpya” na asili, kwa kuwa hao hawajamtia ndani Yehova. Kwa hakika, kuthibitisha ubatili wa wanadamu kujitawala ndiyo sababu moja inayomfanya Mungu aruhusu ulimwengu huu kuendelea kwa muda mrefu hivyo. Lakini karibuni, wale wanaotamani utawala wa Kristo watafurahia amani tele. Isaya 11:9 lathibitisha hilo, nalo pia laonyesha sababu inayofanya wao pekee waweze kuishi kwa “upatano mpya” na asili: “Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.” (Italiki ni zetu.) Ndiyo, elimu ya kimungu ndiyo ufunguo. Na je, hilo si jambo lifaalo, kwa kuwa ni nani ila Muumba wa asili aliye na hekima kama hiyo?

Vipi juu ya wale wanaodumu kumpuuza Yehova? “Bali waovu watatengwa na nchi,” lasema Mithali 2:22. Ndiyo, uchokozi wao au kutojali kwao kutawagharimu uhai katika “dhiki kubwa” inayokaribia upesi—njia ya Mungu ya kuhukumu wale wote wanaodumu kutumia vibaya na kuharibu uumbaji wake.—Ufunuo 7:14; 11:18.

Je, unataka kushiriki katika programu ya kurekebisha dunia? Basi tafadhali jua yale ambayo Mungu ataka ufanye kwa kujifunza Biblia. Ni hiyo pekee iwezayo kukufanya uone maoni ya Muumba. (2 Timotheo 3:16; Waebrania 4:12) Kwa kuongezea, kwa kutumia yale unayojifunza, hutakuwa tu raia mzuri sasa bali pia utathibitisha kwamba kwa kweli wewe ni mtu ambaye ataaminishwa na Yehova “dunia mpya” yake inayokuja kwa kasi.—2 Petro 3:13.

Ikiwa ungependa, wachapishaji wa gazeti hili au kutaniko la Mashahidi wa Yehova lililo karibu zaidi nawe litafurahia kukusaidia kuwa na funzo la Biblia nyumbani bila malipo au kukupa fasihi zaidi zenye kueleza mambo haya.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki