Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 7/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Biashara ya Utumwa Katika Brazili
  • Wavutaji wa Sigareti wa Ulaya
  • Ni Ugonjwa Utokanao na Kelele?
  • Hatari za Dawa za Kuua Visumbufu
  • Matineja Wafafanua Wazazi Wafaao
  • Tiba Isiyohusisha Damu
  • Tokea “Enzi ya Mawe” Hadi Bunduki za Marisau
  • Nyangumi-Buluu Warudi
  • Masomo Juu ya Talaka?
  • Wafungaji-Watu Gerezani Zaidi Ulimwenguni
  • Uregeshaji wa Vitu Wafaa
  • Kelele—Yale Uwezayo Kufanya Kuihusu
    Amkeni!—1997
  • Kelele—Kisumbufu cha Kisasa
    Amkeni!—1997
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2004
  • Nyangumi Wamefika!
    Amkeni!—2015
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 7/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Biashara ya Utumwa Katika Brazili

“Brazili ilipata watumwa wengi mara kumi kuliko Marekani—lakini idadi ya vifo miongoni mwa watumwa waliokuwa wakienda Brazili ilikuwa ya juu sana hivi kwamba mwaka wa 1860 idadi ya weusi katika Brazili ilikuwa nusu tu ya idadi ya wale waliokuwa Marekani,” laripoti ENI Bulletin la Baraza la Makanisa la Ulimwengu (WCC). Imekadiriwa kwamba asilimia 40 ya watumwa Waafrika walikufa melini. Ili kuongeza thamani yao, watumwa Waafrika walibatizwa kwa ujumla kwa kunyunyiziwa maji huku makasisi wakisema “maneno ya ubatizo.” Akizungumza katika maombi ya “ukumbusho, toba na upatano” yaliyofanywa Salvador, Brazili, Aaron Tolen, kiongozi mmoja wa WCC kutoka Kamerun, alisema: “Wale waliotuleta hapa hawakuchangia peke yao msiba huu. Sisi Waafrika tunashiriki lawama hizo. Tumejishusha kwa kuuza ndugu zetu na dada zetu kama bidhaa.”

Wavutaji wa Sigareti wa Ulaya

Kwa kiwango cha kila raia, Ulaya na China zina watumiaji wa tumbaku wengi zaidi ulimwenguni, laripoti Nassauische Neue Presse la Frankfurt, Ujerumani. Katika Muungano wa Ulaya, asilimia 42 kati ya wanaume na asilimia 28 kati ya wanawake huvuta sigareti. Hata hivyo, asilimia hizo ni za juu hata zaidi kwa wenye umri wa kati ya miaka 25 hadi 39. Uvutaji wa sigareti husababisha vifo vya watu 100,000 nchini Ujerumani na wengine 100,000 nchini Uingereza kila mwaka. Hivi majuzi, rais wa Jamhuri ya Cheki, Václav Havel, ambaye ni mvutaji sana kwa miaka mingi, alitibiwa kansa ya mapafu. Gazeti Süddeutsche Zeitung laripoti kwamba rais huyo aliandikia harakati fulani ya Ulaya iitwayo Kuvuta Sigareti au Afya akisema kwamba yeye huvutiwa sana na mtu yeyote awezaye kuacha tabia ya kuvuta sigareti.

Ni Ugonjwa Utokanao na Kelele?

Kuwapo penye kelele, hata kama si kelele kubwa, kwaweza kukufanya uwe mgonjwa, kulingana na uchunguzi ulioripotiwa katika gazeti la Uingereza la New Scientist. Kwa kufikiria matokeo kama hayo, Shirika la Afya Ulimwenguni limepitia upya miongozo yake juu ya kiwango kifaacho cha kelele za usiku. Jambo hasa la kuhangaisha ni uthibitisho uonyeshao kwamba watoto hasa waweza kuwa hatarini zaidi. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba watoto wanaoishi karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Munich walikuwa na msongo wa juu wa damu na vilevile viwango vya juu vya adrenalini. Watafiti hao pia waligundua kwamba watoto hao hupatwa na kasoro za kutoweza kusoma vizuri na za kutoweza kukumbuka mambo yaliyopita. Watu ambao huonekana kukabiliana vizuri na kelele hufanya hivyo “mara nyingi kwa hasara ya mwili wao,” asema mtaalamu wa kelele Arline Bronzaft. “Kelele ni mkazo wa akili na hatimaye mwili hudhuriwa kwa njia fulani.”

Hatari za Dawa za Kuua Visumbufu

Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mchele nchini Filipino, mazao ya mchele yangebaki vilevile hata wakulima wakiacha kutumia dawa zozote za kuua visumbufu. Mwanasayansi mmoja wa taasisi hiyo ya mchele aliuambia Mkutano wa Chakula Ulimwenguni, uliofanywa Filipino, kwamba kunyunyiza sana dawa kwa mimea ni hasara na hakufai. Wakulima hawanyunyizii tu wakati mbaya wa mwaka, laripoti gazeti New Scientist, bali pia wao huua wadudu wasiofaa kuuawa. Isitoshe, wakulima wengi hupuuza mashauri juu ya usalama wanapotumia dawa nao hutumia vinyunyiziaji vyepesi sana, ambavyo hupumuliwa kwa urahisi, au wao huchanganya dawa za kuua magugu pamoja na udongo na kuzieneza kwa mkono. Shirika la Afya Ulimwenguni laripoti kwamba ulimwenguni kote dawa za kuua visumbufu kwa wakati huu zinasababisha vifo 220,000 na watu milioni tatu hudhuriwa sana na sumu kila mwaka.

Matineja Wafafanua Wazazi Wafaao

Matineja waweza kufafanuaje wazazi wafaao? Ili kujua, mshauri mmoja wa shule aliye pia mwanasaikolojia Scott Wooding alifanya uchunguzi kwa matineja zaidi ya 600. Kwa kuwa Wooding alitarajia kwamba vijana hao watasifu uendekevu, majibu yao yalimshangaza. Kwa upatano, matineja walisema kwamba wao wanataka “haki, kujaliwa (‘wanataka kusikia maneno: “Nakupenda”’), ucheshi, [na] kuwekewa vielelezo vyema,” laripoti gazeti la habari The Toronto Star. Wooding pia alipata kwamba matineja wanataka wazazi wao wawasaidie wasitawishe uwajibikaji. Wanapokuwa wamefanya kosa, wanatazamia kutiwa nidhamu. Jambo kuu zaidi, vijana walisema kwamba wao hutamani wazazi wao watumie wakati mwingi zaidi pamoja nao.

Tiba Isiyohusisha Damu

“Hofu za maradhi yatokanayo na damu na uhaba wa daima wa damu inayotolewa kama upaji umetokeza jitihada kubwa za kuacha kutia damu mishipani iwezekanapo,” laripoti gazeti la habari The Globe and Mail. Tiba isiyohusisha damu na upasuaji hutegemea sana kudhibitiwa sana kwa upotezo wa damu, na “mbinu mpya nyingi zilisitawishwa zamani ili kutibu Mashahidi wa Yehova,” lasema Globe. Dakt. James A. Robblee, daktari wa nusukaputi katika Taasisi ya Moyo ya Chuo Kikuu cha Ottawa, ambayo ni mojawapo ya hospitali nyingi zinazofuatia programu za kutibu bila damu, alikiri hivi: “Nafikiri kabisa kwamba wao [Mashahidi wa Yehova] wameinua sana ufahamu wetu juu ya upasuaji bila kutumia damu.”

Tokea “Enzi ya Mawe” Hadi Bunduki za Marisau

Hifadhi kubwa ya msitu iliyo katikati ya Brazili na Venezuela ni makao ya Wahindi Wayanomami. Wayanomami “waligunduliwa” kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1960, nao hatua kwa hatua wamefundishwa uvumbuzi wa kisasa kama vile ndoana, vioo, viberiti, na redio. Lakini, chombo cha kisasa cha kuwafikia karibuni zaidi—bunduki ya marisau—inatisha “kabila la mwisho la Enzi ya Mawe katika Amerika,” laripoti The Daily Journal la Caracas, Venezuela. Kupitia mabadilishano ya vitu na biashara, wachimba-dhahabu, wafanya-biashara katika msitu, na wamishonari wameingiza bunduki za marisau katika utamaduni wa kikale wa Wayanomami. Lakini kuuawa kwa risasi kwa Wayanomami watatu kiaksidenti katika juma moja tu ni kikumbusha chenye kushtua cha jinsi kupatana na ustaarabu wa kisasa kunavyotokeza msiba. Kama asemavyo Claudia Andujar, mkuu wa watetezi wa Tume ya Wayanomami: “Ebu wazia jinsi ongezeko la ghafula la bunduki na baruti liwezavyo kuwa hatari kwa kabila ambalo linajivunia uwezo wake wa kupigana na mishale yenye sumu, mawe na marungu.”

Nyangumi-Buluu Warudi

Kuwinda nyangumi-buluu kumedhibitiwa sana tangu 1946. Kufikia wakati huo, wanyama hawa wakubwa ajabu wenye urefu wa meta 30 na uzani wa tani 150 walikuwa wamewindwa mpaka wakakaribia kutoweka. Lakini sasa, kwa sababu ya Mfumo wa Kufuatisha Sauti wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, imefunuliwa kwamba bahari ya Atlantiki Kaskazini ni makao ya idadi kubwa ya nyangumi, kutia ndani finback na vilevile humpback, minke, na nyangumi-buluu walio nadra kuonekana. “Kuna nyangumi wengi zaidi pwani ya Uingereza kuliko ilivyodhaniwa hapo awali,” lasema The Sunday Telegraph la London. Awali, vinasa-sauti vilivyo chini ya bahari kufikia vina vya meta 3,000 viliwekwa ili kufuatia nyambizi. Lakini, imepatikana kwamba vinafaa pia katika kunasa sauti za chini za nyangumi. Sauti ya nyangumi-buluu yasemekana yaweza kusafiri kilometa 3,000 chini ya maji.

Masomo Juu ya Talaka?

Katika Wilaya ya Pima, Arizona, Marekani, wazazi wanaotaka kuchukua talaka wanahitajika kuhudhuria semina ya muda wa saa nne na nusu ili kuelewa athari itakayowapata watoto wao, laripoti The Dallas Morning News. Masomo hayo yametayarishwa ili kusaidia wazazi kujifunza “jinsi ya kupanga ziara zao” na kufikiria “ni umri upi mtoto awezapo kuwa wa kutosha kukaa na mzazi ambaye hapaswi kumtunza katika kipindi cha kiangazi.” Jambo la maana zaidi, wazazi wanasaidiwa kuelewa talaka kupitia maoni ya mtoto, asema mkurugenzi wa masomo hayo Frank Williams. “Hata hivyo, mimi hushangaa ni kwa nini elimu kama hii inafanywa kuwa ya lazima wenzi wanapochukua talaka,” asema wakili wa mambo ya familia Alyce Pennington. Kwa nini “wasihudhurie masomo hayo hata kabla ya wao kufunga ndoa?”

Wafungaji-Watu Gerezani Zaidi Ulimwenguni

Katika 1995 kulikuwa na watu 615 gerezani kwa kila wakazi 100,000 wa Marekani, yasema Idara ya Sheria ya Marekani. Hiyo ni maradufu ya waliofungwa gerezani mwaka wa 1985, ikifanya hiyo iongoze ulimwenguni, laripoti The Wall Street Journal. Ya pili ni Urusi ikiwa na wafungwa 590 kwa kila watu 100,000, kwa kutegemea habari za majuzi zaidi zipatikanazo (1994).

Uregeshaji wa Vitu Wafaa

Kulingana na gazeti la habari la El Universal la Caracas, Venezuela, uregeshaji wa mikebe ya aluminiamu huokoa asilimia 90 ya nishati inayotumiwa kufanyiza mikebe. Uregeshaji wa karatasi pia hufaa kimazingira. Nusu ya nishati inatumiwa kuregesha karatasi kuliko inayotumiwa kutengeneza karatasi, uchafuzi wa maji unapunguka kwa asilimia 58, na uchafuzi wa hewa unapunguka kwa asilimia 74. Gilasi hufanya hata vizuri zaidi kwa sababu hiyo inaweza kuregeshwa kabisa, tena na tena.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki