Maneno Makali, Roho Zilizopondeka
“Wewe goigoi mpumbavu!”a Mwanamke mmoja nchini Japani akumbuka vizuri sana maneno hayo—alirushiwa maneno hayo kwa ukawaida sana alipokuwa mtoto mdogo. Ni nani aliyekuwa akimrushia maneno hayo? Je, watoto wa shule? Ndugu zake? La. Wazazi wake. Yeye akumbuka: “Nilikuwa nikishuka moyo kwa sababu matukano haya yalikuwa yakiniumiza sana.”
Mwanamume mmoja nchini Marekani akumbuka kwamba akiwa mtoto, alikuwa mwenye hofu na wasiwasi wakati wowote babake alipokuja nyumbani. “Hadi leo hii bado naweza kusikia mlio wa magurudumu ya gari linapokuja nyumbani,” yeye akumbuka, “na bado nakumbuka hofu niliyopata. Dada yangu mdogo alikuwa akijificha. Baba yangu alikuwa anataka ukamilifu na kila wakati alikuwa akitudhulumu kwamba hatukufanya vema kazi tulizopaswa kufanya.”
Dadake mtu huyo aongezea hivi: “Sikumbuki mzazi wangu yeyote akitukumbatia, akitubusu, au hata kusema kitu kama ‘nakupenda’ au ‘ninakuonea fahari.’ Na mtoto asiposikia kamwe maneno ‘nakupenda’ hiyo ni kama kusikia ‘nakuchukia’—kila siku maishani mwake.”
HUENDA wengine wakasema kwamba msononeko ambao watu hawa walipata wakiwa watoto ulikuwa kidogo. Kwa hakika ni jambo la kawaida kwa watoto kuambiwa maneno makali, yasiyo ya fadhili na kutendwa vibaya. Hayo si mambo ambayo hukaziwa katika vichwa vya habari vya magazeti vyenye kushtua na katika vioja vidogo vya televisheni. Madhara hayaonekani. Lakini wazazi wakiwatenda hivyo watoto wao kila siku, bado madhara yaweza kuwa mabaya sana — na kudumu maisha yote.
Fikiria ufuatiliaji wa 1990 kwa uchunguzi uliofanywa mwaka wa 1951 ambao ulichunguza utendaji wa wazazi kwa kikundi cha watoto wenye umri wa miaka mitano. Watafiti waliweza kupata wengi wa watoto hao, sasa wakiwa na umri wa makamo, ili kufahamu athari za muda mrefu za jinsi walivyolelewa. Uchunguzi huo mpya ulikata kauli kwamba watoto ambao baadaye walipata magumu zaidi maishani, ambao walikosa hali njema ya kihisia-moyo, na ambao walipata magumu katika ndoa, urafiki, na hata kazini, si kwamba walikuwa watoto wa wazazi maskini wala wa wazazi matajiri wala wa wazazi ambao walikuwa na matatizo. Walikuwa watoto ambao wazazi wao hawakuwajali na ambao hawakuwaonyesha shauku.
Ugunduzi huu ni wonyesho tu wa kweli iliyokuwa imeandikwa karibu miaka 2,000 iliyopita: “Nyinyi akina baba, msiwe mkichochea watoto wenu wakasirike, ili wasishuke moyo.” (Wakolosai 3:21) Hali ya wazazi kuwatenda vibaya watoto wao kwa maneno na kihisia-moyo hakika huwachochea wakasirike na kwa kweli inaweza kuwafanya washuke moyo.
Kulingana na kitabu Growing Up Sad, muda mrefu haujapita tangu madaktari walipofikiri kwamba hakuna kitu kama mshuko-moyo wa utotoni. Lakini wakati na mambo yaliyoonwa yamethibitisha vingine. Leo, watungaji wa vitabu wasisitiza, mshuko-moyo wa utotoni unatambuliwa na ni jambo la kawaida. Miongoni mwa visababishi vyake ni kukataliwa na kutendwa vibaya na wazazi. Watungaji hao waeleza: “Katika visa vingine mzazi amemfokea mtoto sikuzote kwa kumchambua na kumtweza. Katika visa vingine kunakuwa tu na pengo katika uhusiano wa mzazi na mtoto: upendo wa mzazi kwa mtoto hauonyeshwi kamwe. . . . Matokeo ni yenye msiba hasa kwa watoto wa wazazi kama hao kwa sababu kwa mtoto—au kwa mtu mzima—upendo ni muhimu kama jua na maji vilivyo muhimu kwa mmea.”
Kupitia upendo wa mzazi, ukionyeshwa kwa udhahiri na kwa wazi, watoto hujifunza kweli ya maana: Wao wanapendeka; wana thamani. Wengi hudhania vibaya mambo hayo kuwa aina fulani ya kiburi, kama kujipenda kuliko wengine. Lakini hilo si jambo linalomaanishwa katika muktadha huu. Mtungaji mmoja asema hivi katika kitabu chake juu ya habari hii: “Maoni ya mtoto wako kujielekea yana uvutano juu ya marafiki anaowachagua, jinsi anavyoshirikiana na wengine, mtu atakayefunga ndoa naye, na jinsi atakavyokuwa mwenye kutimiza mambo maishani.” Biblia hukubali jinsi ilivyo muhimu kuwa na maoni yaliyosawazika na yasiyo ya kujipenda juu yako mwenyewe inapoorodhesha kuwa amri ya pili kwa ukubwa zaidi ni: “Lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.”—Mathayo 22:38, 39.
Ni vigumu kuwazia mzazi yeyote mwenye akili timamu akitaka kuvunjavunja kitu kilicho muhimu na dhaifu kama vile kujistahi kwa mtoto. Basi, ni kwa nini jambo hilo hutukia mara nyingi? Na linaweza kuzuiwaje?
[Maelezo ya Chini]
a Katika Kijapani, noroma baka!