Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 9/8 kur. 14-17
  • Kilimanjaro—Kilele cha Afrika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kilimanjaro—Kilele cha Afrika
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Kilele” cha Afrika
  • Vilele Vyake Vyenye Kuvutia
  • Ni Ikolojia Bora
  • Kuukwea “Kili”
  • Barafu Juu ya Ikweta
    Amkeni!—2005
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1998
  • Milima Imo Hatarini
    Amkeni!—2005
  • Milima ya Mwezi
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 9/8 kur. 14-17

Kilimanjaro—Kilele cha Afrika

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA

MIAKA 150 tu iliyopita, sehemu kubwa ya ndani ya Afrika ilibaki bila kujulikana. Kwa ulimwengu wa nje, kontinenti hii kubwa haikuwa imefanyiwa uvumbuzi nayo ilikuwa ya kifumbo. Miongoni mwa hadithi nyingi zilizotoka Afrika Mashariki, mojawapo hasa ilionekana kuwa ya ajabu sana kwa Wanaulaya. Ilikuwa ripoti ya wamishonari Wajerumani walioitwa Johannes Rebmann na Johann L. Krapf, ambao walidai kwamba katika 1848 waliona karibu na ikweta mlima uliokuwa mrefu mno hivi kwamba kilele chake kilikuwa cheupe kwa theluji.

Hadithi ya kwamba kulikuwa na mlima wenye kilele cha theluji katika Afrika ya tropiki haikutiliwa shaka tu bali ilidhihakiwa pia. Lakini, masimulizi ya mlima mkubwa mno yaliamsha udadisi na upendezi wa wanajiografia na wavumbuzi, na hatimaye walithibitisha ripoti za wamishonari hao. Kwa kweli kulikuwa na mlima wa volkeno wenye kilele cha theluji katika Afrika Mashariki ulioitwa Kilimanjaro. Watu wengine walielewa kwamba ulimaanisha “Mlima wa Ukubwa.”

“Kilele” cha Afrika

Leo, Kilimanjaro ulio mkubwa ni mashuhuri kwa uzuri wake mwingi na kimo chake chenye kuvutia. Ni mandhari chache zinazovutia na zenye kukumbukwa kama ile ya kundi la tembo walio malishoni wanaovuka nyanda kavu na zenye mavumbi za Afrika huku “Kili” wenye kilele cha theluji na ulio mkubwa mno ukionekana nyuma.

Kilimanjaro ndio mlima mrefu zaidi katika kontinenti ya Afrika na unahesabiwa kuwa miongoni mwa volkeno zimwe zilizo kubwa zaidi ulimwenguni. Uko Tanzania, kusini tu mwa ikweta na kando ya mpaka wa Kenya. Hapa ardhi imetoa zaidi ya meta za kyubiki milioni nne za vitu vya volkeno, ikifanyiza mlima huu wenye vilele mawinguni.

Ukubwa wenye kupita kiasi wa mlima huu hudhihirika zaidi kwa sababu ya upweke wake. Ukiwa umesimama peke yake, huo umeinuka kutoka kwenye bara kame lenye vichaka la Maasai, ambalo liko kwenye kimo cha karibu meta 900 juu ya usawa wa bahari, hadi kimo cha kustaajabisha cha meta 5,895! Si ajabu kwamba nyakati nyingine Kilimanjaro huitwa kilele cha Afrika.

Kilimanjaro pia uliitwa “Mlima wa Misafara,” kwa kuwa zikiwa kama taa nyeupe, theluji zake na barafuto zake zingeweza kuonwa kwa mamia ya kilometa kutoka upande wowote ule. Katika karne zilizopita kilele chake chenye theluji mara nyingi kiliongoza misafara ambayo ilikuwa ikitoka katika pori za ndani za Afrika, ikiwa imejaa mizigo ya pembe za tembo, dhahabu, na watumwa.

Vilele Vyake Vyenye Kuvutia

Kilimanjaro umefanyizwa kwa vilele viwili vya volkeno. Kibo ndicho kilele kikuu cha volkeno; kilele chake kizuri na chenye ulinganifu wa umbo la pia kina barafu na theluji ya daima. Upande wa mashariki kilele cha pili, kiitwacho Mawenzi, huinuka kufikia meta 5,150 nacho ni kilele cha mlima cha tatu kwa urefu zaidi katika Afrika, kikifuatia Kibo na Mlima Kenya. Kwa kutofautisha na pande za Kibo zenye kuteremka kwa uanana, Mawenzi ni kilele chenye mawemawe na ambacho kimechongoka vizuri sana na kikiwa na miinuko mikali ya mawe pande zote. Vilele vya Kibo na Mawenzi vimeunganishwa kwenye kimo cha meta 4,600 na uwanda mpana, wenye mteremko na wenye majabali yaliyotapakaa. Magharibi ya Kibo kuna Shira, ambayo ni mabaki yaliyoporomoka ya volkeno ya kale ambayo zamani ilimomonyolewa na upepo na maji, sasa ikifanyiza uwanda wa juu ulio tambarare na ambao ni wenye kuvutia sana kwenye kimo cha meta 4,000 juu ya usawa wa bahari.

Ni Ikolojia Bora

Mfumikolojia wa Kilimanjaro umefanyizwa kwa kanda tofauti-tofauti ambazo zimegawanywa na altitudo, mvua, na mimea. Miteremko ya chini zaidi imefunikwa kwa misitu ya kitropiki ambayo haijaharibiwa ambamo makundi ya tembo na nyati hutangatanga ndani yake. Spishi kadhaa za tumbili hukaa juu sana kwenye miti ya msitu, na nyakati nyingine mtu mwenye kuzuru aweza kuona punde tu mbawala na mindi wenye haya, ambao huyoyoma kwa urahisi ndani ya vichaka vinene.

Juu ya msitu kuna ukanda wa mbuga. Miti mizee iliyopondeka-pondeka, iliyokunjwa na upepo mkali na umri, imefunikwa kwa ukungu ufananao na videvu virefu vyenye mvi vya wanaume wazee. Hapa upande wa mlima huwa wazi zaidi, na mimeapori mikubwa husitawi. Milima ya nyasi yenye maua ya rangi nyangavu hufanya eneo hilo livutie sana.

Na juu zaidi ya ukanda wa miti, bara tambarare latokea. Mahali pa miti huchukuliwa na mimea yenye maumbo yasiyo ya kawaida iitwayo groundsels mikubwa, ambayo hufikia kimo cha meta minne, na lobelias, ambayo hufanana na kabichi kubwa au rubaruti. Kandokando ya majabali na miamba-miamba hukua maua iitwayo everlasting, inayofanana na nyasi na ni kavu nayo huongeza rangi kwa mandhari ambayo kama si maua hayo, ina rangi ya kijivu cha fedha.

Juu zaidi, bara tambarare hugeuka kuwa ukanda wa alpini. Mandhari ina rangi hafifu na matone ya rangi ya hudhurungi-nyeusi na kijivu. Mimea michache inaweza kukua katika mazingira haya makavu, yenye uhaba wa mimea. Kufikia kimo hiki vilele viwili vikuu, Kibo na Mawenzi, vimeunganishwa na mwinuko mkubwa wa bara ambao ni jangwa la altitudo ya juu, lililo kavu na lenye mawemawe. Halijoto za hapa hupita kiasi, zikifikia digrii 38 za Selsiasi wakati wa mchana na kudidimia chini sana ya kiwango cha kuganda wakati wa usiku.

Hatimaye twafika ukanda wa kilele. Hapa hewa ni baridi na nyangavu. Dhidi ya anga lenye rangi ya buluu ya nyeusi-nyeusi, barafuto kubwa-kubwa na nyanja za barafu huonekana nyeupe na safi, zikitofautiana kwa njia ya kuvutia na mazingira meusi-meusi ya mlima. Hewa ni haba na ina nusu hivi ya oksijeni ipatikanayo kwenye usawa wa bahari. Kwenye kilele bapa cha Kibo kuna kreta ya volkeno, ambayo imekaribia kuwa mviringo kamili na ina kipenyo cha kilometa 2.5. Ndani ya kreta katikati kabisa mwa huu mlima mna shimo kubwa la majivu lenye kipenyo cha meta zaidi ya 300 na kuingia ndani kwa kina cha meta 120 ya volkeno. Mivuke moto ya salfa huinuka polepole katika hewa baridi ikitoka katika vitundu vidogo, jambo linalothibitisha kizaazaa kilichomo ndani sana ya hii volkeno zimwe.

Ukubwa wenyewe wa Kilimanjaro na tungamo lake huuruhusu ujifanyizie tabia yake yenyewe ya nchi. Pepo nyevu, zinazovumishwa kutoka Bahari Kuu ya Hindi zinazovuka nyanda za chini zilizo kavu, hugonga huo mlima na kuelekezwa juu ambako pepo hizo huganda na kutokeza mvua. Hilo hufanya miteremko ya chini iwe na rutuba kwa ajili ya mashamba ya kahawa na mazao ya chakula ambayo hutegemeza watu wale waishio kwenye sehemu za chini za mlima.

Kuukwea “Kili”

Watu waishio karibu na Kilimanjaro waliamini kishirikina kwamba miteremko yake ilikuwa makao ya roho waovu ambao wangedhuru mtu yeyote ajaribuye kufikia kilele chake chenye barafu. Jambo hilo lilizuia wenyeji wasijaribu kufikia kilele chake. Haikuwa mpaka 1889 ndipo wavumbuzi wawili Wajerumani walipopanda huo mlima na kusimama juu ya kilele cha Afrika. Kilele cha pili, Mawenzi, ambacho ni kigumu zaidi kupanda, hakikukwewa mpaka 1912.

Leo kila mtu mwenye afya nzuri aweza kupanda Kilimanjaro nao hupendwa sana na wageni wanaozuru Afrika Mashariki. Wenye mamlaka ya mbuga za Tanzania wana mipango mizuri kwa wale wanaotaka kupanda huo mlima. Mavazi na vifaa vyaweza kukodiwa. Wapo wapagazi na viongozi ambao wamezoezwa, na hoteli kadhaa hutoa malazi ya starehe tangu mwanzo hadi mwisho wa safari ya kupanda mlima. Kwenye milima kuna vibanda vilivyojengwa vizuri katika altitudo tofauti-tofauti, ambazo humwandalia apandaye makao ya kulala na mahali pa kujikinga.

Kujionea mwenyewe Kilimanjaro kwavutia sana na hutokeza hisia ya utafakari. Mtu aweza kukubaliana kwa urahisi na maneno haya kuhusu Mungu: “Anayeweka imara milima kwa nguvu yake.” (Zaburi 65:6, ZSB) Ndiyo, ukiwa mrefu sana na ukiwa peke yake juu ya Afrika, Kilimanjaro umesimama ukiwa wonyesho mkubwa wa nguvu za Muumba Mtukufu.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

AFRIKA

Kenya

KILIMANJARO

Tanzania

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki