Milima ya Mwezi
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA
ULIKUWA ni uvumi uliodumu kwa karne kadhaa: Mahali fulani katika Afrika ya Kati, kulikuwa na milima iliyofunikwa kwa theluji—chanzo halisi cha Mto Nile. Lakini wazo la kuwepo kwa theluji karibu na ikweta katika Afrika lilionekana kuwa lisilowezekana. Na bado, mapema katika karne ya pili W.K. mwanajiografia Mgiriki Ptolemy alikuwa amedokeza kuwepo kwa milima hii, akiiita Lunae Montes—Milima ya Mwezi.a
Kwa karne kadhaa, jitihada za kutambua mahali palipokuwa milima hii zilithibitika kuwa za ubatili. Lakini ndipo, siku moja katika mwisho-mwisho wa miaka ya 1800, mvumbuzi Henry Stanley—mwenye sifa kwa ajili ya kumpata Dakt. David Livingstone—alishuhudia tukio la nasibu. Utando wa mawingu, ambao ulikuwa umeficha milima na kufanya isionekane na wavumbuzi wa hapo awali, ulitawanyika kwa muda mfupi ukiruhusu Stanley apate mwono wa mara moja ulio mzuri mno wa vikundi vya vilele vilivyofunikwa kwa theluji. Alikuwa ameipata Milima ya Mwezi. Lakini aliiita kwa jina lililokuwa likitumiwa na wakazi wenyeji: Ruwenzori, linalomaanisha “Mfanyiza-Mvua.”
Leo, inakubaliwa kwa ujumla kwamba milima Ruwenzori huchangia fungu dogo sana katika kuandaa maji kwa ajili ya Mto Nile. Ijapokuwa hivyo, bado wengi hupenda kuiita Milima ya Mwezi. Na licha ya safari nyingi sana za uchunguzi na uvumbuzi, hii safu ya milima yenye kutia kicho bado inadumisha fumbo linaloashiria mema. Ikiwa kaskazini tu mwa ikweta, safu ya milima Ruwenzori ni mpaka wa asili kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ikinyooka kwa urefu wa kilometa zipatazo 130 na upana wa kilometa 50.
Tofauti na milima mingi ya Afrika Mashariki, iliyo na asili ya volkeno, safu ya Ruwenzori ni kipande kikubwa cha ganda la dunia ambalo lilirushwa juu mileani kadhaa zilizopita na kanieneo kubwa mno za jiolojia. Ijapokuwa milima Ruwenzori huinuka kufikia meta 5,109, huwa haionekani kwa urahisi na watazamaji. Muda ulio mwingi zaidi, hiyo safu hufunikwa na ukungu na mawingu.
Kama jina hilo lidokezavyo, milima Ruwenzori hupata mvua nyingi sana na theluji huku majira ya “ukavu” yakiwa na ukavu kidogo tu kuliko majira ya “unyevu.” Kwa hiyo kutembea kwaweza kuwa kwenye hatari; katika maeneo fulani matope hufika kwenye kiuno! Mvua nzito zimetengeneza maziwa madogo kadhaa yenye kuvutia, ambayo huandaa unyevu kwa mimea mingi isiyo ya kawaida ambayo hufunika miteremko ya milima. Kwa kweli, milima Ruwenzori ni makao ya mimea kadhaa isiyo ya kawaida, mingine yake hukua kufikia saizi kubwa mno.
Kwa kielelezo, ile hairy fingers iliyo mikubwa mno inayoitwa lobelia kwa kawaida hupungua sentimeta 30 katika urefu mahali fulani, lakini katika milima Ruwenzori huenda ikafikia meta sita. Ile senecio, au groundsels iliyo mikubwa mno, huonekana kama kabichi kubwa zilizo juu ya mikonga yenye matawi. Kuna miti ya mbuga yenye kufunikwa na kuvu iliyo na urefu wa meta 12. Maua ya kila rangi na harufu nzuri huongezea uzuri wa hiyo mandhari. Pia kuna ndege wengi warembo na wa namna mbalimbali, wengine wao ni wa kipekee kwa milima Ruwenzori. Kwenye nyanda za chini wanaishi tembo, sokwemtu, kulungu, chui, na kima.
Mandhari ya Ajabu
Wale ambao husafiri wakifuatia vijia vya mlima hupitia msitu-mvua wa kitropiki na kuvuka Mto Bujuku mara kadhaa. Wanapofikia mwinuko wa meta 3,000, wao waweza kutazama nyuma na kuona huko chini kwenye Bonde la Ufa—mandhari nzuri mno!
Juu zaidi ni eneo la chini la Bigo Bog, lenye nyasi zinazomea kilimani na miti ya mbuga. Hapa mara nyingi matope hufikia magoti. Kupanda sehemu ya juu zaidi ya Bigo Bog na Ziwa Bujuku, juu ya Bonde la Bujuku karibu meta 4,000 kwenda juu, huandaa mandhari ya ajabu sana ya Mlima Baker, Mlima Luigi di Savoia, Mlima Stanley, na Mlima Speke, vilele vinavyojulikana zaidi katika safu.
Juu zaidi ni ile Barafuto ya kudumu iitwayo Elena. Hapa lazima mtu avae panga njumu, vyuma vya kupandia, na atumie kamba na mashoka ya barafu kupanda juu ya barafuto. Kisha hufuata matembezi ng’ambo ya uwanda wa juu wa Stanley kwa njia ambayo huelekea kwenye kilele kiitwacho Margherita juu ya Mlima Stanley, kilele cha juu zaidi katika kikundi cha mlima Ruwenzori. Kutazama chini kutoka kwenye kimo hicho kinachotokeza mandhari yote ya vilele, mabonde, misitu, vijito, na maziwa hutia kicho kwa kweli.
Ingawa hivyo, kwa vyovyote, safu hii ya milima haijapata kushindwa. Milima Ruwenzori imeanza tu kutoa siri zake. Bado mengi hayajajulikana kuhusu jiolojia ya safu, aina mbalimbali za wanyama na mimea. Hivyo milima Ruwenzori yabaki ikiwa imefunikwa ndani ya fumbo—siri zinazojulikana kikamili tu na Muumba wa milima hii aliye mwenye hekima na nguvu zote. Ndiyo, kwa kweli yeye ndiye Yule ambaye “vilele vya milima ni vyake.”—Zaburi 95:4.
[Maelezo ya Chini]
a Kulingana na kitabu The Nile, cha Emil Ludwig, wakazi wa kale hawakuweza kueleza juu ya ile theluji kwenye milima. Kwa hiyo waliamini kwamba “milima ilikuwa imevuta chini mbalamwezi.”
[Picha katika ukurasa wa 17]
1. Kwa kawaida utando mzito wa mawingu husitiri Ruwenzori
2. Mvua nzito za “Mfanyiza-Mvua” hufanya miteremko iliyofunikwa na kuvu kuwa yenye unyevu
3. Kandokando ya kijia, kuna maua mengi na harufu nzuri