Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 9/22 kur. 18-20
  • Uchongaji wa Vinyago—Sanaa ya Kiafrika ya Kale

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uchongaji wa Vinyago—Sanaa ya Kiafrika ya Kale
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uchongaji wa Vinyago Leo
  • Kujifunza Sanaa ya Mchongaji
  • Kwa Nini Kujenga kwa Mbao?
    Amkeni!—1995
  • Sala Zetu Ni Muhimu kwa Yehova
    Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha Yetu ya Kikristo—2022
  • Ngozi ya Chungu wa Sahara​—Mwavuli Unaomkinga na Joto
    Amkeni!—2017
  • Shingo ya Chungu
    Amkeni!—2016
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 9/22 kur. 18-20

Uchongaji wa Vinyago—Sanaa ya Kiafrika ya Kale

Na mleta-habari za Amkeni! katika Nigeria

WACHONGA-VINYAGO wamekuwa wenye shughuli kwa muda mrefu katika Benin City, jiji lililopo sehemu ambayo sasa ni kusini mwa Nigeria. Miaka mia nne iliyopita, Benin City lilikuwa jiji kuu la ufalme wenye nguvu na wenye kupangwa kitengenezo sana katika eneo la misitu. Wageni kutoka Ulaya walishangaa kuona barabara zilizo pana, zilizonyooka za jiji hilo, nyumba zake zenye mpangilio mzuri, na watu wake wenye heshima na kufuata sheria. Kwa karne kadhaa Benin City limesitawi likiwa moja ya vituo muhimu sana vya kibiashara na kitamaduni katika magharibi ya Afrika.

Ufalme wa Benin ulitawalwa na mfuatano wa wafalme walioitwa oba. Hao oba waliendeleza sana sanaa. Majumba yao ya kifalme katika Benin City yalirembwa kwa vinyago vyenye umbo la vichwa, mapambo ya ukutani yaliyokalibiwa kwa shaba, na pembe za tembo nzuri sana zilizochongwa kwa uangalifu. Ingawa vinyago vya kale havikuokoka uharibifu uliotokana na wakati na mchwa, ni wazi kwamba wachonga-vinyago walikuwa watendaji katika ufalme huo. Martins Akanbiemu, aliyekuwa msimamizi wa Jumba la Makumbusho katika Lagos, aandika: “Ushirika wa wachonga-vinyago . . . waonekana kuwa wa zamani zaidi kuliko mwingine wowote uliofanyia Oba kazi.”

Katika mwaka wa 1897, majeshi ya Uingereza yalipora Benin City na kupeleka Ulaya hazina zake ambazo sasa zina thamani sana—zaidi ya vipande 2,000. Leo, mkusanyo mkubwa wa sanaa za kale za Benin zinaonyeshwa, si nchini Nigeria, bali katika makumbusho huko London na Berlin.

Uchongaji wa Vinyago Leo

Leo, Benin City ni jiji lenye shughuli nyingi kama vile majiji mengine mengi katika Nigeria. Lakini, masalio ya utukufu wake wa kale bado yapo. Jumba la mfalme limejengwa upya, na oba wa sasa aishi hapo. Waweza kuona ushuhuda wa mtaro wenye kina ambao unazunguka hilo jiji la zamani; na ukisikiliza kwa makini, waweza kusikia milio ya tiki tiki tiki ya patasi juu ya mbao.

Mtu fulani aitwaye Johnson amekuwa akichonga vinyago katika Benin City kwa miaka 20. Katika karne zilizopita, vichwa vya mbao na shaba nyeupe vilihifadhi kumbukumbu za wale waliokufa; vilipamba madhabahu za ibada za mababu wa kale. Lakini vichwa ambavyo Johnson avichonga havifanani na vile ambavyo vilitumiwa kwa ajili ya makusudi ya kidini. Vyake ni kwa ajili ya mapambo tu.

Johnson hutumia mpingo, ambao ni mbao ngumu lakini ulio mwepesi kuvunjika unaofaa sana uchongaji. Kwa kawaida hutumia sehemu ya ndani ya mti. Mara nyingi mpingo wa Nigeria ni mweusi tititi, ingawa baadhi ya miti hutokeza sehemu ya ndani ambayo ina michirizi au ina rangi ya kijivu hadi rangi nyeusi. Pia hutia ndani baadhi ya sehemu za nje za mbao katika kuchonga vinyago; hii hufanya rangi nyekundu yenye kupendeza sana, ambayo hukamilisha rangi nyeusi. Mipingo yote miwili ya rangi nyekundu na nyeusi hung’arishwa kutokeza mng’ao mzuri sana.

Mipingo inapatikana kwa wingi katika Nigeria. Mti wa mpingo unapoangushwa, mara nyingi huachwa msituni kwa miezi kadhaa ili ukauke. Hata baada ya gogo la mpingo kuwasili katika karakana yake, Johnson huacha mbao hiyo ikauke kwa miezi kadhaa zaidi kabla hajaitumia. Hili ni muhimu kwani mbao ambayo haijakauka yaweza kubadili umbo na kufanya ufa.

Anapokuwa tayari kuchonga kinyago, Johnson hutumia msumeno wa mkono kukata kipande cha urefu wa sentimeta 37. Baada ya kungoja juma moja zaidi ili kuhakikisha kipande hicho hakitokezi ufa, Johnson aweka alama kwa kutumia chaki ili kuonyesha kichwa anachotaka kukichonga, kisha aanza kazi.

Kwanza hutumia patasi bapa, kisha patasi iliyokunjwa, na kisha patasi kali zaidi. Baada ya hapo, huchonga kwa kutumia tupa. Ndipo kisu cha mchongaji hutumiwa ili kuchonga zaidi. Johnson afanyapo kazi, hukaza fikira sana kwenye mbao. Uzembe waweza kufanya kinyago kuwa na tabasamu ya ajabu au jicho likiangalia upande usiotakiwa .

Kazi ya kuchonga inapokuwa imefanywa, wanafunzi wa Johnson husugua kipande hicho kwa misasa tofauti yenye madaraja tofauti. Hatimaye, hutumia rangi ya fanicha au ya viatu na kisha hung’arisha kwa kutumia burashi ya kiatu ili king’ae. Huchukua siku mbili kuchonga kichwa cha mbao kama hicho katika picha. Huchukua siku nyingine tatu kukisugua na kuking’arisha.

Uchongaji unapokwisha, Johnson hukiweka pembeni kwa miezi kadhaa ili kuhakikisha kwamba nyufa hazitokei. Ikiwa mbao ilikauka kabisa kabla uchongaji haujaanza, hakutakuwa na ufa. Kwa kawaida huwa hivyo. Ikiwa ufa watokea, kinyago hupelekwa tena katika karakana ili kuzibwa, kusuguliwa, na kung’arishwa tena.

Kujifunza Sanaa ya Mchongaji

Johnson ana wanafunzi sita, wenye umri kati ya miaka 10 hadi 18. Wao hujifunza kazi ya sanaa kwa kurudi nyuma, kutoka kazi ya mwisho hadi ya kwanza. Katika utaratibu huu, kitu cha kwanza mwanafunzi anachojifunza ni kung’arisha. Kisha ajifunza kupiga msasa. Baadaye, anaonyeshwa jinsi ya kutumia tupa. Hatimaye, siku yafika ambayo achukua patasi bapa ili kufanya mikato ya kwanza katika kipande kipya cha mbao.

“Si kila mtu aweza kuwa mchongaji,” asema Johnson. “Kwanza, unapaswa kuwa na kipaji pamoja na uwezo wa kukaza fikira. Pia wapaswa kujifunza jinsi ya kuwa mwenye saburi na maendeleo yako na jinsi ya kukabiliana na kushindwa kwako. Wahitaji udumifu pia kwani huchukua angalau miaka mitatu ili kuwa mchongaji mzuri. Lakini huo si mwisho—kujifunza hakuna mwisho. Kwa mazoezi, utazidi kufanya maendeleo.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20]

Mchwa na Mchonga-Kinyago

Baadhi ya watu husema kwamba sanaa ya Kiafrika ina deni kwa mchwa. Mchonga-kinyago achonga kinyago, na mchwa (akisaidiwa kwa kadiri fulani na hali ya hewa ya tropiki) akiharibu, nyakati fulani katika siku chache tu! Kwa karne zilizopita mchwa amemfanya mchonga-kinyago awe mwenye shughuli nyingi. Umekuwa mzunguko usio na mwisho lakini wenye kufaa: Mchwa aharibu, na mchonga-kinyago aanza upya, akiwa na fursa za kuboresha stadi zake na kutokeza mitindo mipya ya ubunifu.

Kitabu African Kingdoms chataarifu hivi: “Kuvu na mchwa wenye bidii ya uendelevu kwa kiasi fulani wameondoa uwezekano wowote wa michongo ya zamani kuigwa au kuwa na uvutano kwa michongo ya vizazi vinavyofuata. Kwa sababu hiyo, pamoja na uhitaji wenye kurudia wa michongo mipya, pia kulikuwa na fursa kubwa za ubadilifu katika muundo; uigaji ukawa kidogo sana, na michongo ikawa inategemea ustadi na ubunifu wa kila mtu.”

Wengine hueleza kwamba uhusiano huu kati ya mchwa na mchonga-kinyago wasaidia kueleza ubora wa kisanaa ambao umefanya sanaa ya Kiafrika kuwa maarufu sana. Katika kitabu chake Nigerian Images, msomi William Fagg asema hivi: “Wacha . . . tumpe mchwa sifa, ambaye, ingawa hapendwi na mwanadamu kwa kazi zake zozote, amejishughulisha katika karne na mileani katika uhusiano wa kufaa na mchonga-kinyago wa tropiki.”

[Hisani]

Kwa niaba ya Dr. Richard Bagine

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kuchonga:

1. kuchagua mbao bora zaidi,

2. kuchora kichwa kitakachochongwa,

3. kutumia patasi, 4. kupiga msasa, 5. kung’arisha

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki