Duma—Paka Mwenye Mbio Zaidi
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA
JOTO lilitanda juu ya mbuga yenye kupigwa na jua. Darubini zetu zilielekezwa kwa kundi la swala-tomi, huku mbavu zao zenye milia za kidhahabu zikiangaza katika miale ya mwisho ya machweo. Si mbali sana, akiwa juu ya kichuguu cha mchwa, mtazamaji mwingine alikuwa akikodoa macho kuelekea upande wa swala hao. Alikuwa paka mwenye madoadoa na watoto wake. Macho yake ya rangi ya kaharabu yaliangalia mandhari hiyo kwa makini sana. Kwa ghafula, misuli yake ilivutana, na akainuka kwa utaratibu kuelekea upande lilipo kundi la wanyama hao. Yaonekana watoto wake walielewa kwamba walipaswa kumngoja arudi.
Kwa tahadhari, aliendelea mbele, akijificha nyuma ya vichaka vidogo na vishungi vya majani marefu. Mwendo wake ulikuwa wa madaha na wa uhakika. Alipofikia meta 200 kutoka kwa mawindo yake, kwa ghafula alisimama tuli. Mmoja kati ya hao swala aliangalia na alikuwa amekodolea macho upande wake; kisha akaendelea kula. Kwa mara nyingine tena, duma huyo aliendelea kukaribia. Alikaribia meta 50 kutoka mahali walipokuwapo wanyama hao wasiohisi hatari yoyote kabla ya kuamua kutimua mbio. Kama springi iliyoachiliwa, akapiga mbio kwa kasi katika nuru iliyokuwa ikififia. Hilo kundi la swala lilitawanyika kuelekea sehemu zote, lakini paka huyo hakuacha kumtazama windo lake alilolichagua. Alivuka nyanda hiyo kwa kasi, akimkaribia huyo swala mwepesi.
Mnyama huyo aliyeogopa sana alikimbia akiruka huku na huku ili kumzubaisha mkimbizaji wake, lakini mbinu zake za ujanja hazikuwa kitu mbele ya uwepesi kama umeme wa paka huyo. Kisha, akiwa karibu meta moja amfikie windo lake, alinyoosha mguu wake mmoja wa mbele ili kumtega mhanga wake. Wakati huo, alijikwaa kidogo. Mara, swala huyo akatoroka.
Akihema, huyo duma alipunguza mwendo ili asimame, akaketi na kuangalia upande waliokuwapo watoto wake wenye njaa. Nilimtazama mke wangu kwa mshangao. Tulikuwa tumeshuhudia tu mwendo wa kasi wa duma mwenye kushangaza.
Paka Mwenye Kasi
Kwa kweli duma aweza kukimbia kama upepo. Kwa kushangaza, aweza kukimbia kutoka mahali alipoanza hadi kilometa 65 kwa saa katika muda wa sekunde mbili tu! Aweza kufikia mwendo wa kilometa 110 kwa saa! Yeye ndiye mnyama mwenye kasi zaidi katika nchi kavu. Kwa kulinganisha, farasi wa mashindano waweza kufikia mwendo uzidio kidogo kilometa 72 kwa saa, na mbwa-mwindaji aweza kukimbia kilometa 65 kwa saa. Hata hivyo, duma aweza kudumisha mwendo wake wa kushangaza kwa umbali mfupi tu.
Duma ana umbo jembamba, miguu mirefu myembamba na mgongo mnyumbufu uliopinda chini kidogo. Mkia wake mrefu wenye madoadoa humsaidia kusawazika apindapo na kugeuka kwa mwendo wa kasi. Akimbiapo kwa mwendo wa kasi sana, aweza kuruka kwa kupiga hatua za zaidi ya meta 6. Msaada mmoja wa wepesi huo ni miguu yake ya kipekee; inafanana zaidi na miguu ya mbwa kuliko ya paka. Yeye hutumia kucha zake kukamata ardhi ili kumwongezea nguvu.
Mwenye Madoadoa Avutiaye
Uso wa duma kwa wazi ni wa kipekee na wenye kuvutia. Mistari miwili myororo yatambaa kutoka kwenye macho hadi kona za mdomo, ikimfanya paka huyo kuwa na uso wenye huzuni, usio na uchangamfu. Yakiwa na madoadoa madogo mazito, manyoya yake ni mafupi na mara nyingi yana rangi nyekundu-kahawia mwilini lakini nyeupe-nyeupe katika tumbo. Watoto wa duma ni weusi-weusi zaidi wakati wa kuzaliwa nao huwa na manyoya mazito ya shingoni yenye rangi ya samawati-kijivu ambayo hutambaa kutoka shingoni hadi mikiani mwao.
Duma ana sauti ya kutetemeka au milio mifupi-mifupi kama ya ndege. Sauti hii inasikiwa hadi umbali wa kilometa mbili na inatumiwa kuwasiliana na watoto wake na pia duma wengine.
Duma wana mwelekeo wa upole na wenye amani kwa kulinganisha na paka wengine kama vile simba na chui. Anapokuwa ameridhika, yeye hung’orota kama paka mkubwa wa nyumbani. Hujipatanisha kwa urahisi na kuwepo kwa binadamu na hata amewahi kufugwa. Bila shaka, duma si paka wa nyumbani. Akiwa amekomaa kabisa, huwa na uzito wa kilogramu 45 au zaidi, na meno yake makali na kucha zake kali humfanya kuwa mnyama hatari—ambaye apaswa kutendewa kwa tahadhari.
Duma hakuzaliwa akiwa na uwezo wa kuwinda na lazima azoezwe sana na mama yake ili afanye hivyo. Ikiwa mtoto amelelewa akiwa utekwani, atakosa uwezo wa kunyemelea na kukimbiza windo lake. Mama na watoto walapo pamoja, hufanya hivyo kwa amani, bila kugombana na kupigana ambayo ni tabia ya kawaida miongoni mwa simba wanaokula. Katika maeneo yenye ukame duma hata wamejulikana kula matikiti yenye maji mengi.
Watalii katika mbuga za wanyama katika Afrika wameshangaa sana kwa jinsi paka hawa wenye amani wasivyoogopa. Si jambo la ajabu kumwona duma aliyekomaa akiwa katika kivuli cha gari la kitalii au kupanda sehemu ya mbele ya gari na kupitia kioo cha mbele kuwaangalia abiria waliopigwa butwaa na ambao mara nyingi huwa wameogopa.
Utunzaji wa Kimzazi wa Paka
Duma jike aweza kuzaa watoto wadogo hadi sita. Jike hilo huwalinda watoto hao kwa ujasiri sana naye huwaficha vizuri, akiwahamisha mara nyingi katika miezi yao ya kwanza. Hata hivyo, licha ya jitihada hizo za akina mama duma za kulinda watoto wao, yaonekana kwamba ni karibu thuluthi moja tu ya watoto hao hupata kuwa wakubwa.
Kutunza familia ya duma si kazi rahisi kwa duma aliye mama. Wana nguvu sana na ni wenye kupenda sana kucheza. Watoto hao mara nyingi huunyemelea mkia wa mama yao anayepumzika na kuurukia wakati mama huyo anapozungusha-zungusha mkia katika njia apendayo kufanya paka. Wakishindana mieleka, kuumana na kufukuzana, mara nyingi hawatambui hatari zilizopo sikuzote za wanyama-wawindaji.
Mwindaji Awindwa
Duma ana maadui wengi katika mwitu, kutia ndani simba, chui na fisi. Hata hivyo, adui mkubwa zaidi wa duma ni mwanadamu. Manyoya yake yenye kupendeza yenye madoamadoa yanapendwa sana kwa nguo, mazulia, na kwa umaridadi. Kiumbe hiki chenye uwezo wa kukimbia sana kimenaswa na kufunzwa michezo ya uwindaji. Kwa sababu ya kukataa kwake kuzaa akiwa utekwani, duma amelazimishwa sana atimize takwa hili anapokuwa katika himaya. Kupotea kwa makao pia kumetokeza mkazo kwa duma, hivi kwamba katika Afrika Mashariki sasa apatikana hasa katika hifadhi za wanyama.
Katika mwaka wa 1900 kulikadiriwa kuwa na duma 100,000 katika nchi 44. Leo labda kuna duma 12,000 wanaoishi katika nchi 26, wengi wakiishi katika Afrika. Juhudi zinafanywa kulinda paka huyu mzuri mwenye madoamadoa, lakini idadi yake yaendelea kupungua.
Baadhi ya watu wahisi kwamba duma hawezi kuokolewa asitoweke. Hata hivyo, inatia moyo kujua kwamba wakati unakuja ambapo mwanadamu atakapopokea kwa ukamili daraka lake alilokabidhiwa na Mungu la kutunza, kulinda, na ‘kutawala kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.’ (Mwanzo 1:28) Wakati huo ndipo kutakapokuwa na hakikisho imara kwamba paka wazuri kama vile duma watafurahisha wakazi wa dunia milele.