Kutafuta Paradiso Isiyo na Taabu
“KILE tu tunachotaka ni kufanyiza mtindo wa maisha ulio salama na labda wa kikale ambamo watu wanajali kila mmoja na mwenzake,” wakaeleza wenzi fulani wa ndoa Waingereza. Waliamua kutafuta paradiso moja ya kisiwa cha kitropiki na kuanzisha huko jumuiya ambayo ingeishi pamoja kwa amani. Bila shaka unaweza kuelewa hisia zao. Ni nani asingekubali mara moja toleo la kuishi katika paradiso isiyo na taabu?
Je, Suluhisho Ni Kujitenga?
Wazo la kuishi kisiwani huvutia watafutaji wengi wa paradiso, kwa kuwa kujitenga huwaandalia usalama wa kadiri fulani. Wengine huchagua visiwa vilivyo karibu na Pwani ya Pasifiki ya Panama au visiwa vilivyo katika Karibea, kama vile vilivyo karibu na Belize. Wengine hugeuzia uangalifu wao sehemu zenye kuvutia za Bahari ya Hindi—kwa kielelezo, Shelisheli.
Ni vigumu sana kuwazia hatua za kufuata ili kufanyiza jumuiya iliyojitenga. Hata kama kuna pesa za kutosha, sheria zilizopo za serikali zaweza kuzuia kununuliwa kwa ardhi upesi. Lakini, tuseme kisiwa kifaacho cha kitropiki kinaweza kupatikana, je ungefurahi kuwa huko? Je, paradiso yako haingekuwa na taabu?
Visiwa vilivyojitenga vilivyo karibu na pwani ya Uingereza sasa vinaongezeka watu. Wakazi wake wapya hasa ni watu ambao wanatafuta faragha na amani. Mtu mmoja aishiye peke yake katika kisiwa cha Eorsa chenye eka 250, karibu na pwani ya magharibi ya Scotland, adai kwamba hahisi upweke kamwe kwa sababu ana kazi nyingi sana za kuwatunza kondoo zake mia moja. Wengine ambao wamejitenga kisiwani upesi huhisi upweke. Yaripotiwa kwamba wengine wamejaribu kujiua na walihitaji kuokolewa.
Watu wengi huamini kwamba kisiwa kidogo cha kitropiki chenye kuvutia kingekuwa paradiso. Kuishi katika hali yenye tabia ya nchi yenye uanana na isiyo yenye kuvuka mipaka sana huwavutia. Lakini hangaiko juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa joto duniani na kufuatiwa na kuinuka kwa kiwango cha bahari limesababisha hofu miongoni mwa wakazi wengi wa visiwa. Wakaaji wa visiwa vya matumbawe visivyo na kimo na ambavyo hufanyiza eneo la Tokelau katika Pasifiki ya Magharibi na vilevile wakaaji wa vile visiwa vya Maldives vilivyotawanyika katika Bahari ya Hindi na ambavyo havijainuka zaidi ya meta 2 juu ya usawa wa bahari wakati wa kujaa kwa maji wanahisi wametishwa vilevile.
Karibu serikali 40 tofauti-tofauti zimejiunga pamoja katika shirikisho la Mataifa Yenye Kuendelea ya Visiwa Vidogo ili kutafuta msaada kwa hali yao. Ingawa kwa ujumla wakaaji wa visiwa vidogo wana tarajio la kuishi muda mrefu nao wana vifo vichache vya watoto, wao huendelea kukabili matatizo mazito ya mazingira. Tabaka za mafuta na bahari zilizotiwa uchafu hudhoofisha uchumi wa visiwa fulani. Visiwa vingine huwa mahali pa kutupia takataka zenye sumu ambazo mataifa makubwa yanataka kutupa.
Hata kutamanika kwenyewe kwa visiwa hivyo kuwa mahali pa watafuta-paradiso hutokeza tisho. Jinsi gani? Watalii ambao humiminikia fuo zenye jua za visiwa hivyo hutokeza msongamano mkubwa sana na kupunguka kwa maliasili iliyo kidogo. Watu hao wenye kuzuru pia huongezea tatizo la uchafuzi. Kwa kielelezo, katika Karibea, ni sehemu moja kwa kumi tu za takataka zitokezwazo na wenye kuzuru milioni 20 kila mwaka ambazo hutiwa dawa kabla ya kuondolewa.
Jambo kama hilo hutukia katika sehemu nyinginezo zenye kuvutia. Fikiria kielelezo cha Goa kwenye pwani ya magharibi ya India. “Utalii mwingi ‘unaharibu paradiso,’” likatangaza gazeti The Independent on Sunday la London. Makadirio rasmi yaonyesha kwamba watalii wameongezeka kutoka 10,000 katika mwaka wa 1972 hadi zaidi ya milioni moja katika miaka ya mapema ya 1990. Kikundi kimoja chaonya kwamba ikolojia dhaifu ya Goa na utamaduni wake wa kipekee inatishwa na pupa ya wenye hoteli wanaotamani kuchuma donge nono kutokana na mmiminiko wa watalii. Ripoti ya serikali ya India inathibitisha kwamba baadhi ya hoteli zimechipuka kwenye ufuo kinyume cha sheria. Mchanga umechimbwa, miti ikakatwa, na chungu za mchanga zimelainishwa. Takataka hutupwa kwenye ufuo au huvuja na kuingia katika mashamba yaliyo karibu ya mpunga, zikieneza uchafuzi.
Je, Sehemu Hizo Hazina Uhalifu?
Ongezeko la uhalifu linaharibu sifa ya hata maeneo yenye amani zaidi. Kutoka kisiwa kidogo cha Karibea kiitwacho Barbuda yaja ripoti yenye kichwa “Machinjo Katika Paradiso.” Ripoti hiyo ilitaja kindani mauaji ya kimakusudi ya watu wanne waliokuwa katika mashua ya anasa ambayo ilikuwa imetia nanga karibu na pwani ya kisiwa hicho. Visa kama hivi huongeza hangaiko juu ya kuenea kwa uhalifu kotekote katika hilo eneo.
“Dawa za Kulevya Zazusha Vita vya Magenge Katika ‘Paradiso’” ikasema katika kichwa kikuu ripoti moja katika gazeti The Sunday Times la London kuhusu nchi moja ya Amerika ya Kati. Mhariri mmoja wa huko alilalamika kwamba amani ilikuwa imetoweka, akieleza: “Sasa ni kawaida kuamka asubuhi na kupata kijana mwenye umri wa miaka 16 akiwa amelala katika damu barabarani.”
Wale wanaotaka kuishi katika paradiso ya jumuiya hutumaini kuvutia watu ambao watakubali kuishi kwa amani. Lakini uhalisi wa mambo ukoje? Kutofautiana kulizuka upesi katika kisa cha wale wenzi Waingereza waliotajwa mwanzoni. Baadhi ya waliopeleka maombi ya kujiunga na mradi wao kwa wazi walitaka kuchuma pesa kutokana na mpango huo. “Sisi hatutaki viongozi,” akatangaza mwendelezaji huyo. “Wazo ni kuchanga mali zetu na kuhakikisha kwamba mambo yetu yanaendelea sawa. Naiita jumuiya ya Utopia.” Huu si mradi wa kwanza kamwe.—Ona sanduku “Majaribio ya Jumuiya za Paradiso.”
Watafuta-paradiso wengine huamini kwamba wao watatimiza mradi wao kwa kushinda mchezo wa bahati-nasibu. Lakini fedha zipatikanazo kwa njia hii mara nyingi hazileti furaha. Mnamo Februari 1995, gazeti The Sunday Times liliripoti kwamba familia ya mshindi wa bahati-nasibu iliyo kubwa zaidi nchini Uingereza kufikia sasa ilikuwa na mapigano makali; kushinda hakukuwaletea lolote ila “uchungu, ugomvi na kukata tamaa.” Hii ni kawaida katika hali hizo.
Katika uchunguzi juu ya utafutaji wa mwanadamu wa Utopia, mwandishi wa magazeti Bernard Levin aeleza juu ya “ndoto ya kupata mali mara moja,” na kusisitiza: “Kama ilivyo na ndoto nyingi, ogofyo halipo mbali sana. Kuna habari nyingi mno zilizothibitishwa za kupata mali mara moja ambazo ziliongoza kwenye misiba mibaya sana (kutia ndani ujiuaji) hivi kwamba haziwezi kuwa sadfa tu.”
Vipi Juu ya Mafarakano ya Hukumu?
Mipango mingine kuhusu paradiso imeonekana kuwa hata mibaya zaidi. Likiripoti juu ya polisi kuzingira ua wa Branch Davidians kule Waco, Texas, huko nyuma katika 1993, gazeti fulani la habari lilisema juu ya “mchanganyiko hatari wa bunduki, mbinu za kudhibiti akili na nabii wa hukumu” aliyetokeza msiba huo. Kwa kusikitisha, hiki si kisa cha kipekee.
Wafuasi wa Bhagwan Shree Rajneesh aliyekufa na ambaye alikuwa kiongozi wa kiroho Mhindi, walianzisha jumuiya katika Oregon lakini baadaye waliudhi maadili ya majirani zao. Utajiri wa kiongozi wao na majaribio ya kingono waliyoyafanya yaliharibu madai yao kwamba wamepata “himaya nzuri.”
Madhehebu mengi yenye kuongozwa na watu wenye matumaini ya paradiso husisitiza kwamba wafuasi wao wafuate desturi fulani za ajabu, ambazo nyakati nyingine hutokeza mapambano yenye jeuri. Mwandikaji wa makala za gazeti la habari Ian Brodie aeleza hivi: “Madhehebu hutoa himaya na jamii iliyopangwa kwa uthabiti kwa wale wanaohisi wanaishi kwa upweke au ambao hawawezi kukabiliana na mikazo ya ulimwengu halisi.” Hata hivyo, maneno yake huthibitisha uhakika wa kwamba watu wengi wangependa kuishi katika paradiso.
Paradiso Isiyo na Taabu
Orodha ya taabu yaonekana kana kamba haina mwisho: uchafuzi, uhalifu, matumizi mabaya ya dawa, msongamano, mapambano ya kikabila, msukosuko wa kisiasa—bila kutaja taabu zilizo kawaida kwa wanadamu wote, maradhi na kifo. Ni lazima tufikie mkataa kwamba hakuna popote katika sayari hii ambapo pana paradiso ambayo haina taabu kabisa. Kama Bernard Levin anavyokiri: “Rekodi ya mwanadamu ni mbaya, na inaonekana imekuwa mbaya kwa muda ambao mwanadamu amekuwapo. Rekodi hiyo mbaya ipo kwa sababu watu hawawezi kuishi kwa furaha wakiwa karibu-karibu na wanadamu wengine wachache sana.”
Hata hivyo, kutakuwa na paradiso ya tufeni pote ambayo kwa kweli haitakuwa na taabu. Kudumu kwa paradiso hiyo kumehakikishwa na nguvu izidiyo ile ya kibinadamu. Hakika, zaidi ya watu milioni tano hata sasa wanajitahidi kufikia lengo hilo, nao tayari wanafurahia miongoni mwao muungano wenye thamani na mazingira yasiyo na taabu kwa kulinganisha. Unaweza kuwapata wapi? Unaweza kushirikije tumaini ilo hilo na manufaa ambazo wanafurahia sasa? Na Paradiso hiyo inayokuja itadumu kwa muda gani?
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Majaribio ya Jumuiya za Paradiso
Mapema katika karne ya 19, msoshalisti wa Ufaransa Étienne Cabet (1788-1856) na washiriki wake 280 walianzisha makazi ya jumuiya katika Nauvoo, Illinois, ili waishi kwa kutegemea mawazo yake. Lakini kwa muda wa miaka minane mgawanyiko mkubwa ulitokea katika jumuiya hiyo hivi kwamba upesi ikavunjika, kama ilivyokuwa kwa vikundi kama hivyo katika Iowa na California.
Mfaransa mwingine, Charles Fourier (1772-1837), alisitawisha mawazo kwa ajili ya jumuiya yenye kushirikiana kwa kilimo huku washiriki wake wote wakibadilishana wajibu. Kila mtu alipaswa kupokea malipo kwa kutegemea mafanikio ya kikundi chote kizima. Lakini jumuiya kama hizo katika Ufaransa na Marekani hazikudumu.
Karibu na wakati huo, mrekebishaji wa mambo ya kijamii wa Wales aliyeitwa Robert Owen (1771-1858) alipendekeza kuwe na vijiji vyenye kushirikiana ambamo mamia ya watu wangeishi pamoja wakiwa na jiko na maeneo ya kula ya jumuiya yote. Kila familia ingeishi katika nyumba yao yenyewe na kuwashughulikia watoto wao mpaka wafikie umri wa miaka mitatu. Baada ya hapo utunzaji wa watoto ungechukuliwa na jumuiya yote. Lakini majaribio ya Owen yalishindwa, naye alipoteza kiasi kikubwa cha mali zake binafsi.
John Noyes (1811-1886) akaja kuwa mwanzilishi wa kile ambacho The New Encyclopædia Britannica chakiita “jumuiya yenye mafanikio zaidi kati ya jumuiya za kisoshalisti za utopia Marekani.” Wafuasi wake walipoacha ndoa za mke mmoja na kuruhusu kufanya ngono miongoni mwa wote maadamu wamekubaliana, Noyes alikamatwa kwa mashtaka ya uzinzi.
Laissez Faire City, ambalo ni aina ya “Utopia ya kibepari” katika Amerika ya Kati, ni jaribio la hivi karibuni la kufanyiza jumuiya ya Utopia, laripoti gazeti The Sunday Times la London. Mradi huo ulitafuta waweka-rasilimali. Wakivutwa na tazamio la kuishi katika “jiji la muujiza la karne ya 21,” watafuta-paradiso walialikwa wapeleke dola 5,000 na kujiunga na mfumo fulani wa uuzaji, wakitafuta watu kama wao ambao nao wataweka rasilimali za pesa zao. Inaripotiwa kwamba jumla hiyo yote ya pesa inatoshea tu kulipia tikiti ya ndege ya kuona mradi huo “iwapo nchi hiyo inaweza kushawishika ikubali mradi huo ujengwe, na hoteli ndogo ijengwe huko,” likaeleza gazeti hilo la habari. Hakuna tumaini halisi la kuanzishwa kwa “paradiso” yoyote huko.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kisiwa huvutia watafuta-paradiso wengi. Lakini leo uhalifu huharibu hata maeneo yenye amani zaidi