Vita Huua Vijana Wengi
UTOTO wapaswa kuwa wakati wenye furaha. Wakati wa kutunzwa sana na wa kulindwa. Huo ni wakati ambapo watoto hawajui mambo mengi. Wachanga hutarajiwa kucheza, kujifunza, na kusitawisha sifa ambazo zitawasaidia kuwa watu wazima wenye kuchukua madaraka. Watoto hawapasi kuuawa, nao kwa hakika hawapaswi kuwa wauaji. Hata hivyo, katika nyakati za vita, mambo mengi ambayo hayapaswi kutukia hutukia.
Kwa kusikitisha, vita vimejaa tele tufeni pote, navyo vimeua vijana wengi sana, vikiharibu maisha za watoto na wakati wao wa utoto. Katika mwaka wa 1993, mapambano makubwa yalipamba moto katika nchi 42 huku ujeuri wa kisiasa ukiwaka katika nchi nyinginezo 37. Katika kila mojawapo ya nchi hizo 79 mlikuwa na watoto.
Vijana wengi leo hawajapata kamwe amani maishani. Kufikia mwisho wa 1995, kumekuwa na vita nchini Angola kwa zaidi ya miaka 30, Afghanistan kwa miaka 17, nchini Sri Lanka kwa miaka 11, na nchini Somalia kwa miaka 7. Mahali pengi, wanasiasa walisema kwa uhakika juu ya “mazungumzo ya kutafuta amani,” lakini vita visivyokoma viliendelea kuangamiza uhai wa wanadamu.
Sikuzote vita vimeumiza watoto, lakini vita vya aina mbalimbali katika nyakati za hivi majuzi vimesababisha vifo vyenye kuongezeka zaidi vya raia, kutia ndani watoto. Katika mapambano ya karne za 18 na 19 na sehemu ya mapema ya karne hii, karibu nusu ya wahasiriwa wa vita walikuwa raia. Katika Vita ya Ulimwengu ya Pili, iliyodumu tokea 1939 hadi 1945, vifo vya raia viliongezeka kufikia thuluthi mbili za jumla ya vifo vilivyosababishwa na vita, sababu moja ikiwa ni kulipua sana majiji kwa mabomu.
Kufikia mwisho-mwisho wa miaka ya 1980, raia waliouawa na vita walikuwa wameongezeka kwa karibu asilimia 90! Sababu moja ya hili ni kwamba vita vimekuwa tata zaidi. Majeshi hayapigani tena katika uwanja wa vita tu. Mapambano mengi leo, si kati ya mataifa tu, bali ni ya wenyewe kwa wenyewe. Isitoshe, mapigano hutokea vijijini au majijini, na huko, wakitumia ukatili na shuku, wauaji hawatofautishi kati ya adui na watu wasio na hatia.
Watoto wengi sana wameuawa. Imekadiriwa kwamba katika miaka kumi pekee ambayo imepita, kulingana na Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa vita vimeua watoto milioni mbili na kulemaza wengine milioni nne hadi tano. Vita vimeacha mayatima zaidi ya milioni moja na kuacha watoto milioni 12 bila makao. Kwa sababu ya vita, watoto wapatao milioni kumi wana usumbufu wa kiakili.
Maktaba zimejaa vitabu kuhusu vita. Vitabu hivyo hujadili jinsi vita vilivyopiganwa na visababishi vya vita; vyafafanua silaha na mbinu zilizotumika; vimeweka kumbukumbu za majenerali walioongoza machinjo. Sinema hukazia msisimuko wa vita na kupuuza mateseko yatokanayo na vita. Vitabu kama hivyo na sinema kama hizo hazisemi juu ya wahasiriwa wasio na hatia. Makala zifuatazo zachunguza jinsi ambavyo watoto wametumiwa vibaya wakiwa wapiganaji, jinsi ambavyo wamekuwa wahasiriwa zaidi kati ya wote, na sababu ya sisi kusema kwamba watoto leo kwa kweli waweza kufurahia wakati ujao mzuri.