Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 10/22 kur. 16-19
  • Nguvu Kutokana na Theluji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nguvu Kutokana na Theluji
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Nchi Yenye Ukame
  • Kutoka Kwenye Magofu Hadi Theluji
  • Maisha Katika Milima
  • Ukubwa na Uwezo wa Mpango Huo
  • Mpango wa Snowy Unavyofanya Kazi
  • Je, Ni Nguvu Iliyo Safi?
  • Hasara Zinazosababishwa na Mabwawa
    Amkeni!—2002
  • Sehemu Zenye Shida Zaidi
    Amkeni!—1997
  • Maisha Ni Tofauti Huku Chini
    Amkeni!—1997
  • Mfumo wa Maji wa London—Sura Mpya
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 10/22 kur. 16-19

Nguvu Kutokana na Theluji

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

MILIMA ya Australia ambayo ipo kati ya majimbo ya New South Wales na Victoria mara nyingine huitwa kilele cha Australia. Kati ya milima hii kuna Milima ya Snowy, ambayo ni chanzo cha Mto Snowy. Akivutiwa na mandhari hii ya milimani yenye mawemawe na wapanda-farasi wake wa awali wenye kuvumilia magumu, A. B.  (Banjo) Paterson alitunga shairi, ambalo baadaye lilikuja kufanywa kuwa sinema, “The Man From Snowy River.”

Hata hivyo, kwa wakati huu miteremko hatari ya mpanda-farasi wa hekaya ni mahali palipo na milizamu ya ajabu ya kitekinolojia—Mpango wa Nguvu za Umeme wa Milima Snowy. Katika mwaka 1967 Shirika la Wahandisi wa Marekani liliainisha mfumo huu tata wa mifereji ya maji, mahandaki, mabwawa, na vituo vya nguvu za umeme kuwa “moja ya maajabu saba ya uhandisi ya ulimwengu wa kisasa.” Je, ungependa kuzuru “ajabu” hii ya mlimani? Hata hivyo, kwanza ebu tuone sababu iliyofanya ijengwe na aliyeijenga.

Nchi Yenye Ukame

Kwa kushangaza, wazo la umeme utokanao na maji halikuingia katika akili za walowezi wa awali ambao tamaa yao ya maji yenye kutegemeka ilikuwa ndiyo msingi wa Mpango huo wa nguvu za umeme. Wakisumbuliwa sana na ukame, wale wakulima wa karne ya 19 wa bonde la Murray-Darling, eneo la Australia lenye umuhimu zaidi katika kilimo, walihitaji maji yenye kutegemeka zaidi.

Walijua mahali maji yalipokuwa—katika Mto Snowy. Lakini, Mto Snowy ulielekea upande mwingine wenye rutuba wa milima na kuingia katika Bahari ya Tasman. Ulionekana kuwa ni upotevu kabisa. Ikiwa huko juu mlimani maji haya yaliyo baridi na safi kabisa yangeweza kuelekezwa hadi kwenye vyanzo vya mito Murray na Murrumbidgee isiyotegemeka, wakulima wangelindwa na kinga yenye gharama ya mabilioni ya dola dhidi ya ukame. Lilikuwa wazo lenye kupendeza sana.

Katika mwaka 1908 ndoto hiyo ilikuwa karibu kutimizwa wakati Bunge Kuu liliichagua wilaya ya karibu ya Canberra kuwa mahali pa mji mkuu wa Australia. Je, nguvu za umeme utokanao na maji zingeweza kutosheleza mahitaji ya jiji hili ambalo bado halikuwa limejengwa? Kwa mara nyingine fikira zilielekea Milima ya Snowy.

Mapendekezo mbalimbali—mengine kwa ajili ya nguvu za umeme utokanao na maji na mengine kwa ajili ya umwagiliaji wa maji katika mashamba—yaliwasilishwa na kuachwa. Kisha katika mwaka 1944, mpango wa kwanza wa umwagiliaji wa maji kwa kutumia umeme uliwasilishwa, na mara moja ukakubaliwa. Katika mwaka 1949 serikali iliipa Mamlaka ya Umeme Utokanao na Maji ya Milima Snowy madaraka ya kubuni na kujenga mpango huo wenye sehemu mbili.

Lakini ingewezekanaje kwa taifa changa, ambalo hasa ni la kilimo na ambalo halina wataalamu wala wafanyakazi wa kujenga mradi huo wenye ukubwa na ugumu usio na kifani?

Kutoka Kwenye Magofu Hadi Theluji

Jibu likawa uhamiaji. Ikiwa bado imedhoofishwa na Vita ya Ulimwengu ya Pili, Ulaya ilikuwa magofu yenye kuogofya, haikuwa na kazi, na watu walikosa makao. Hivyo kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, Australia ilikaribisha Wazungu wowote ambao walikuwa na stadi zilizohitajika wapeleke maombi ya kufanya kazi katika Mpango huo.

Kwa itikio, mamia ya maelfu ya wafanyakazi kutoka nchi 33 waliacha magofu ya Ulaya na kuabiri kwenda Australia. Wangefanyiza thuluthi mbili ya wafanyakazi wote wa Mpango huo, na wangebadili kabisa jamii za watu wa Australia kwa umilele. Brad Collis asema hivi katika kitabu chake Snowy: “Nchi iliyoanzishwa na . . . walowezi Waingereza kwa ghafula ikawa moja kati ya nchi kuu zenye mchanganyiko mkubwa wa watu wa mataifa mbalimbali.” Collis aongezea: “[Wanaume] walipelekwa milimani—bila kujali kama walikuwa maadui au marafiki, mkandamizaji na mhasiriwa—kufanya kazi pamoja.” Ingawa hawakupatana kwa usiku mmoja kama timu, lakini walikuja kupatana baadaye.

Maisha Katika Milima

Katika siku za mwanzo za Mpango huo, safari ya kwenda milimani ilikuwa yenye mashaka. Barabara zenye barafu, matope, zenye kuinuka sana, na zenye kupinda-pinda zilifanya safari kuwa za polepole, na zenye kutisha sana. Kwa kweli, katika maeneo mengine ardhi ilikuwa na magenge yenye kutisha kiasi cha kwamba hata kangaruu hawakuwa wakionekana kwa ukawaida! Ndiyo maana haishangazi kwamba Halmashauri ya Snowy, kulingana na Collis, “ina sifa ya kuwa shirika la kwanza ulimwenguni kuanzisha sheria ya lazima ya kufunga mkanda wa usalama kitini katika gari.”

Malazi hayakuwa bora zaidi ya barabara—mahema ya kijeshi bila ya sakafu! Hatimaye, zaidi ya kambi 100 na miji ya mahema iliibuka kama uyoga juu milimani. Moja kati ya hiyo, Cabramurra—ambalo si jiji la mahema tena—lina sifa ya pekee ya kuwa mji ulio juu zaidi katika Australia.

Kama uwezavyo kuwazia, kufanya kazi na kulala katika mazingira haya sahili, katika hali ngumu kulijaribu uvumilivu wa mtu kufikia kikomo. Pepo kali za wakati wa majira ya baridi kali humfikia mtu mifupani, joto lenye kuchosha wakati wa kiangazi lilifanya kila hatua kuhitaji jitihada kubwa, na mawingu ya inzi wasiovumilika walifanya nyuso zenye kutoka jasho kuwa nyeusi. Wazungu waliwachukia nzi kama nini!

Lakini wengi wao waliweza kuvumilia mateso hayo. Wakiwa wamefanywa wagumu na vita, waliazimia kufanikisha maisha yao mapya. Wengi hata walifurahia maisha ya Australia ya porini, yakiwa na wanyama na nyoka wa ajabu na ndege ambao hutoa sauti kama za kukemea-kemea na  vilio vya maumivu badala ya kuimba kama kwa miluzi na kulia kama ndege. Baadaye, nyumba nzuri za mbao zilichukua mahali pa mahema na wake na watoto wakafika.

Lakini nini kinapaswa kufanywa na wingi wa lugha? Jaribu kuwazia wanaume wakiendesha mashine nzito na keekee au wakifanya kazi na vilipukaji ambao hawawezi kuwasiliana vizuri! Ingeweza kuongoza kwenye hatari, hivyo Mamlaka hiyo ilianzisha madarasa ya lugha ya Kiingereza baada ya kazi bila malipo. Kuendelea kuajiriwa kulitegemea uwezo wa wafanyakazi kufahamu ustadi wa msingi wa lugha, hivyo si ajabu kwamba madarasa yalihudhuriwa kwa wingi!

Ingawa kulikuwa na vizuizi vingi sana, baada ya miaka 25—1949 hadi 1974—mradi huo uliisha kwa wakati uliowekwa na kwa kiasi cha fedha kilichopangwa. Gharama ya dola milioni 820, japo ni kidogo kwa viwango vya wakati huu, hakikuwa kiasi kidogo wakati huo, hasa kwa taifa lenye watu milioni nane tu na ambalo lilikuwa linajitahidi kurudia hali yake baada ya vita.

Katika kusherehekea mafanikio hayo, Mamlaka hiyo sasa inapanga sherehe za miaka 50 zitakazofanyika mwaka 1999. Zitatia ndani kuwaunganisha pamoja wale wote waliofanya kazi katika mradi huo—ikiwa waweza kupatikana. “Watu hawa walisaidia kujenga moja kati ya maajabu ya uhandisi katika ulimwengu na walibadilisha mwelekeo wa historia ya Australia,” asema kamishna wa sasa. “Twataka kuwashukuru.”

Ukubwa na Uwezo wa Mpango Huo

Kulingana na broshua The Power of Water, “mpango huo hutenda katika zaidi ya eneo la kilometa za mraba 3 200 na yatia ndani kilometa 80 za mifereji ya maji, kilometa 140 za mahandaki na mabwawa makubwa 16.” Mabwawa haya huhifadhi lita trilioni 7 za maji—mara 13 zaidi ya uwezo wa Bandari ya Sydney, ambayo huhifadhi maji kiasi cha lita bilioni 530—na Ziwa Eucumbene likiwa hifadhi kuu. Vituo saba vya umeme, ambavyo vimetokeza hadi gigawati 6,400 za umeme kwa mwaka, vyaweza kuchangia hadi asilimia 17 ya mahitaji ya umeme ya barani Kusini-Mashariki ya Australia, kutia ndani Sydney, Melbourne, na Canberra.

Mitambo hiyo haifanyi kazi kwa saa 24 kwa siku, isipokuwa kila siku wakati wa uhitaji mkubwa, wakati ambapo vituo vya nguvu za umeme utokanao na joto vihitajipo msaada. Nguvu za umeme utokanao na maji unafaa hasa wakati wa tegemezo la wakati wenye uhitaji mkubwa kwa sababu ya kuitikia kwake haraka uhitaji unapoongezeka—dakika mbili hadi tatu, kwa kulinganisha na saa kadhaa kutokana na mfumo utumiao makaa ya mawe ili kutokeza umeme.

Mpango wa Snowy Unavyofanya Kazi

Mpango huo, yasema Mamlaka ya Snowy, una “sifa ya kuwa tata zaidi, wenye makusudi tofauti-tofauti, wenye uhifadhi wa maji ulio na shughuli nyingi zaidi katika ulimwengu.” Unatia ndani sehemu mbili zenye kufanya kazi kwa pamoja—maendeleo ya Snowy-Murray na maendeleo ya Snowy-Tumut.

Maendeleo ya Snowy-Murray hubadilisha njia ya maji ya Mto Snowy kutoka Bwawa la Island Bend kupitia handaki lenye kuvuka mlima hadi Bwawa la Geehi, ambalo pia hupata maji kutoka Mto Geehi. Kutoka hapo maji huporomoka meta 820 kuelekea vituo viwili vya umeme vya Murray. Wakati huohuo, Kituo cha Nguvu za Umeme cha Guthega huteka maji kutoka chanzo cha maji cha Snowy kilicho karibu na mlima mrefu zaidi katika Australia, Mlima Kosciusko. Kutoka Guthega, maji hayo huingia katika mfumo mkuu wa handaki wa Island Bend. Zikiongezea uwezo wa Mpango huo wa kutumika kwa njia nyingi sana, handaki kadhaa, kutia ndani handaki la Island Bend na Ziwa Eucumbene, huruhusu mtiririko wa maji kwa njia mbili.

Katika maendeleo ya Snowy-Tumut, maji kutoka Ziwa Eucumbene, Bwawa la Tooma, Bwawa la Happy Jack, na Bwawa la Tumut Pond yatiririka kwa kasi kupitia milizamu na mfululizo wa vituo vinne vya umeme kabla ya kuachiliwa kuelekea Mto Tumut, ambao unaingia katika mto Murrumbidgee. Sehemu hii ina kituo kikubwa zaidi cha umeme, kile Tumut 3, chenye milizamu sita ambayo basi la orofa laweza kutoshea katika kila moja!

Wakati usio na shughuli nyingi, Mpango huo pia hupeleka maji mlimani kutoka Ziwa Jindabyne hadi Ziwa Eucumbene, na kutoka chini ya Kituo cha Nguvu za Umeme cha Tumut 3, ambacho pia ni kituo cha kupiga maji pampu, kuelekea Hifadhi ya Talbingo. Lakini kwa nini kupoteza umeme kwa kupiga maji pampu kuelekea mlimani? Kwa kushangaza, kwa ajili ya faida. Waona, pampu huendeshwa kwa gharama nafuu kutokana na umeme ununuliwao kutoka vituo vya umeme. Kisha wakati wa uhitaji mkubwa, maji huachiliwa tena na umeme utokanao na maji huuzwa tena kwa mfumo wa umeme kwa faida. Bila shaka, maji mengi—zaidi ya lita trilioni 2 kwa mwaka—huachiliwa bila ya gharama yoyote yaingie katika mifumo ya mito ya magharibi.

Je, Ni Nguvu Iliyo Safi?

Ndiyo, kwani maji hayachafui wala hayatokezi takataka. Hakuna minara ya moshi na minara yenye kupooza isiyopendeza yenye kuharibu milima. Hivyo, maelfu wachezao michezo ya kuteleza barafuni kwenye milima hii wakati wa majira ya baridi kali au wapandapo vijia vyake wakati wa kiangazi hawajui juu ya mifumo ya maji na vituo vya nguvu za umeme vilivyo chini.

Zaidi ya hayo, ikiwa umeme utengenezwao na Mpango huo ungetokana na vituo vya umeme unaotokana na joto, zaidi ya tani milioni tano za dioksidi ya kaboni ingemwagwa angani kila mwaka.

Hata hivyo, mazingira hayakuepuka kabisa kuathiriwa, hasa Mto Snowy. Mengi ya maji yake yakiwa yameelekezwa sehemu nyingine, umekuwa kijito tu kwa kulinganishwa na siku zake za awali. Kwa kuongezea, mabwawa makubwa ya Mpango huo yamefunika mbuga fulani za nyasi kwa maji, na maji mengi ya mabwawa hayo yamelazimisha miji ya Adaminaby na Jindabyne kuhamishwa kwingine.

Kwa upande mwingine, Mpango wa Snowy umekuwa wenye kutegemeka kwa njia ya ajabu—ushuhuda wa shauri la hekima la kamishna wa kwanza wa Mamlaka hiyo: “Nia njema na staha huja kutokana na mafanikio, si propaganda.”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Picha zote kwenye ukurasa wa 16-19: Snowy Mountains Hydro-electric Authority

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mwonekano wa kutoka juu wa Kituo cha Nguvu za Umeme cha Tumut 3, kilicho kikubwa zaidi katika Mpango wa Snowy

[Picha katika ukurasa wa 18]

Wafanya kazi walilazimika kukabili hali ngumu za maisha

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ili kufanya kazi pamoja kama timu, wafanyakazi walilazimika kujifunza Kiingereza

[Picha katika ukurasa wa 19]

Ujenzi wa Mpango huo ulitia ndani kujenga mahandaki katika milima

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki