Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 10/8 kur. 16-19
  • Maisha Ni Tofauti Huku Chini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maisha Ni Tofauti Huku Chini
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ulowezi wa Wazungu
  • Watu Pia Ni Tofauti
  • Uendeshaji wa Gari—Tofauti Kubwa
  • Namna Tofauti za Halihewa
  • Tofauti Nyinginezo
  • Nafasi Zilizo Wazi Sana
  • Mahali Ngamia na Farasi Hurandaranda
    Amkeni!—2001
  • Walienda Kutafuta Dhahabu, Wakapata Makao
    Amkeni!—2011
  • Hatari!—Nina Sumu
    Amkeni!—1996
  • Kasuku Washaufu-Shaufu wa Australia
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 10/8 kur. 16-19

Maisha Ni Tofauti Huku Chini

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

“HUKU CHINI” ni usemi unaotokana na usemi wa Kiingereza Down Under ambao umejulikana na wengi katika miaka ya majuzi. Lakini chini ya nini? Usemi huo hurejezea nchi zilizo chini ya ikweta. Katika maana ya kiistilahi, nchi zote za Kizio cha Kusini zingeweza kuitwa “huku chini.” Hata hivyo, ni Australia na New Zealand pekee zinazorejezewa kwa ukawaida kwa njia hiyo. Makala hii itashughulikia hasa Australia, ambayo jina lake hutokana na neno la Kilatini australis, limaanishalo “-a kusini.”

Maisha katika Australia ni tofauti na maisha katika nchi nyingi katika Kizio cha Kaskazini. Na si tu mahali ilipo kijiografia panapoifanya iwe hivyo. Kuna tofauti nyinginezo nyingi ambazo wageni huziona.

Ulowezi wa Wazungu

Katika mwaka wa 1788, ulowezi wa wazungu katika nchi hii kubwa yenye jua kali ulianza. Kikundi cha meli zenye kuabiri ziitwazo First Fleet kiliingia Sydney Cove. Abiria wake walikuwa hasa wafungwa kutoka Uingereza, Ireland, na Scotland, ambao walikuja na lugha ya Kiingereza. Kwa miaka 150 iliyofuata, wahamiaji wengi walikuwa wa asili ya Uingereza.

Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, namna ya uhamiaji ilibadilika. Leo, kuna maelfu ya “Waaustralia wapya” kutoka nchi tofauti-tofauti, idadi kubwa zaidi ikitoka Italia na Ugiriki. Wahamiaji hao wameongezea unamna-namna wa njia ya maisha ya Australia nao wamekuja na lugha zao wenyewe na namna tofauti za utamkaji wa Kiingereza, na vilevile vyakula vyao na tamaduni zao.

Unamna-namna huo ndio hutokeza namna mbalimbali za lafudhi zisikiwazo hapa. Lakini hata wale ambao familia zao zimeishi hapa kwa vizazi vingi wana lafudhi zao za kipekee na namna ya kuzungumza Kiingereza. Utamkaji wa Waaustralia wa irabu za Kiingereza a, e, i, o, u huwa wa sauti iliyovutika isiyotofautika sana mara nyingi, jambo ambalo hufanya ichukue muda kwa msikilizaji kutofautisha kwa usahihi. Waaustralia pia wana misemo ambayo ni wao tu walio nayo. Kwa kielelezo, haidhuru ni wakati gani wa mchana au usiku, badala ya kusema “Habari ya asubuhi” au “Habari ya jioni,” salamu inayokubaliwa ni salamu ya kirafiki “Siku njema, rafiki!” Mara nyingi hiyo hufuatwa na mazungumzo ya heshima kuhusu afya ya mtu, na mgeni aweza kuulizwa, “Unaendeleaje, rafiki, sawa?”

Watu Pia Ni Tofauti

Kusalimika katika nchi hii yenye magumu kulihitaji kubadilikana na kuwa na utu mvumilivu. Huenda hilo ndilo limechangia hali ya kutazamia mazuri ya Waaustralia wengi, likitokeza usemi, “Mambo yatakuwa sawa, rafiki!” Hilo lamaanisha kwamba mtu hapaswi kuwa na wasiwasi sana mambo yaonekanapo kuwa mabaya, kwa kuwa kila jambo lapaswa kuwa sawa hatimaye.

Utangulizi wa kichapo The Australians wataja hivi: “Inatarajiwa kwamba nchi ambayo wahamiaji wake wa kwanza walikuwa wafungwa, na miaka mia mbili baadaye imekuwa mojawapo ya mataifa madogo yenye nguvu na yenye ufanisi zaidi, ni lazima itokeze nyutu zenye kupendeza na zilizo tofauti. . . . Wao hufanyiza . . . The Australians.”

Sifa ya urafiki huonwa na Waaustralia wengi kuwa ilitokana na hali yenye nguvu ya kisilika ya kusalimika kwa kipindi cha karne mbili zilizopita. Wao hupenda kuelekeza uangalifu kwa askari-jeshi Waaustralia katika Vita ya Ulimwengu ya Kwanza. Pamoja na wanajeshi wa New Zealand, wanajeshi hawa wenye ushupavu waliitwa Anzacs, kifupi cha muungano wa Australian and New Zealand Army Corps. Walikuja pia kujulikana sana kuwa “wachimbaji,” lakini haijulikani kama hilo lilirejezea uchimbaji wao wa mahandaki au uchimbaji wa dhahabu katika Australia, ambapo wanaume walimiminika katika miaka ya 1800.

Uendeshaji wa Gari—Tofauti Kubwa

Wageni kutoka nchi ambazo magari hutumia upande wa kulia wa barabara huona kuendesha gari katika Australia kukiwa tofauti sana. Nchini kote, magari huendeshwa upande wa kushoto wa barabara.

Kwa hiyo ukifika Australia kutoka nchi ambapo kawaida ni kuendesha gari upande wa kulia, hatua zako za kwanza za kuvuka barabara yenye magari mengi zaweza kuwa hatari. Kawaida yako ya ‘kuangalia kushoto, kisha kulia, kisha kushoto tena’ unapovuka barabara yaweza kuleta msiba. Sasa ni lazima ukumbuke, ‘kuangalia kulia, kisha kushoto, kisha kulia tena’ kabla ya kuvuka. Vema sana! Unajifunza haraka. Aa! Karibu uingie katika gari kwenye upande usiofaa. Ulisahau kwamba dereva huketi kwenye upande wa kulia katika nchi hii!

Namna Tofauti za Halihewa

Huku chini, kukilinganishwa na Kizio cha Kaskazini, misimu iko kinyume. Pepo zenye joto na zilizo kavu huja kutoka kaskazini na kaskazini-magharibi, ilihali mabadiliko yote ya baridi huja kutoka kusini. Upepo wa kaskazi wenye kuleta baridi haurejezewi kamwe huku, lakini jihadhari na upepo mkali wa kusi wenye baridi sana na labda kuleta theluji na dhoruba kali ya theluji.

Australia ndiyo kontinenti kavu na yenye joto kuliko zote duniani, ambayo halijoto katika maeneo makame ya barani hufika digrii 30 Selsiasi. Halijoto ya juu kabisa kurekodiwa ilikuwa digrii 53.1 Selsiasi. Ya chini kabisa ilikuwa digrii 22 Selsiasi, karibu na Mlima Kosciusko, ambacho ni kilele cha mlima cha juu zaidi katika Australia, katika eneo la Milima ya Snowy.

Kulingana na viwango vya Kizio cha Kaskazini, hapa hapawi baridi sana. Kwa kielelezo, fikiria Melbourne, jiji kuu la jimbo la Viktoria. Ingawa jiji hilo liko kusini kabisa mwa Australia, halijoto ya wastani ya kila siku katika mwezi wa Julai huanzia digrii 6 hadi 13 Selsiasi. Linganisha hiyo na halijoto ya wastani ya kila siku ya Januari katika Beijing, China, digrii -10 hadi +1 Selsiasi au na ile ya New York digrii -4 hadi +3 Selsiasi. Majiji hayo mawili yako umbali sawa na Melbourne kutoka ikweta. Kwa nini kuna joto zaidi huku chini, hasa ikifikiriwa kwamba Australia iko karibu na mahali penye baridi zaidi duniani—Antaktika?

Tofauti ni kwamba sehemu kubwa ya Kizio cha Kaskazini ni bara lakini sehemu kubwa ya Kizio cha Kusini ni bahari. Australia na New Zealand zimezungukwa na maelfu ya kilometa za mraba za bahari, ambayo hufanyiza kinga ya hewa yenye joto zaidi dhidi ya hewa baridi ya Antaktika, hivyo ikifanya tabia-nchi kuwa yenye joto zaidi.

Kwa sababu ya ukubwa wa kontinenti la Australia, kuna tofauti ya wazi ya tabia-nchi katika sehemu mbalimbali. Katika majimbo yaliyo sehemu za kusini zaidi, misimu inatofautiana waziwazi, vipupwe vikiwa na usiku usio na mawingu na wenye baridi au jalidi, kwa kawaida vikifuatiwa na mchana wenye joto la kupendeza. Siku hizo za mchana za kipupwe zenye kupendeza mara nyingi hufanana na halijoto za kiangazi za nchi nyingi katika Kizio cha Kaskazini. Hata hivyo, katika majimbo ya kaskazini ya Australia, mwaka umegawanyika katika misimu miwili tu—msimu mrefu wa ukame na msimu wa mvua ulio na mvua zake za monsuni. Katika Darwin, jiji kuu la Eneo la Kaskazini, halijoto hubaki karibu na digrii 32 Selsiasi.

Tofauti Nyinginezo

Tokeo la halihewa yenye joto hasa katika sehemu kubwa ya kontinenti hiyo, watu wa Australia sanasana hawavai mavazi rasmi. Lakini kuvaa kofia yenye ukingo mpana ni kwa maana. Kuna visa vingi zaidi vya kansa ya ngozi huku kuliko nchi nyinginezo zenye halijoto ya kiasi kwa sababu ya jua.

Kwa kuwa bado kuna nafasi kubwa zilizo wazi katika Australia, maeneo mengi ya mandari huanzishwa yakiwa na mahali pa kuchomea nyama nje. Nyama si ghali mno, kwa hiyo soseji na steki ndizo huchomwa sana. Lakini, je, wale watu wanaosimama kwenye mahali pa kuchomea nyama nje wanapeana ishara za mkono za kisiri? La, wanapunga mikono yao tu isiyo na kitu ili kufukuza nzi! Nzi na mbu hutokeza tatizo sana kwa ulaji wa nje, hasa katika halihewa yenye joto.

Kwa hiyo, kuishi huku chini kwamaanisha kujifunza kuishi na nzi na mbu, na nyumba nyingi zina milango ya wavu mbele na nyuma. Zamani, watu walivaa kofia zikiwa na vizibo kadhaa vikining’inia ukingoni mwa kofia ili kufukuza nzi. Tangu dawa za kuwafukuza wadudu zitengenezwe, kofia hizo hazionekani sana tena.

Tofauti nyingine inahusu maua ya kifahari, yenye rangi nyingi na vichaka na miti yenye kuchanua maua. Hakuna manukato yenye nguvu ambayo kwa kawaida hupatikana katika Kizio cha Kaskazini. Hapa, ni lazima mpenda-bustani anuse maua yenyewe ili apate harufu kamili ya manukato yake. Bila shaka, si maua yote ya Australia yako hivyo. Kwa kielelezo, vichaka aina ya daphne na yasmini, hufurahisha sana pua yako. Lakini kwa ujumla, maua hayana manukato mengi hapa kama katika tabia-nchi baridi zaidi.

Nafasi Zilizo Wazi Sana

Nafasi ni sehemu ya maisha iliyo tofauti sana huku chini. Dhana ya kilicho karibu au kilicho mbali ni tofauti na nchi nyingi za kaskazini. Umbali kati ya miji fulani midogo ni mkubwa sana hivi kwamba mtu aweza kusafiri kwa muda wa saa nyingi kabla ya kuona mji mwingine. Iko hivyo hasa ambako huitwa kwa shauku porini. Hapa nafasi na utulivu ni mwingi sana, na mgeni aweza kujaza mapafu yake hewa safi, isiyochafuliwa. Karibu pana mkalitusi. Mikalitusi na miwati, au mikakaya, imejaa katika sehemu za barani.

Jioni iingiapo, machweo yenye kupendeza hufurahisha macho yako. Lakini giza laja ghafula kwa kushangaza, kwa kuwa kuna utusitusi wa jioni mfupi sana huku chini. Muda si muda, anga la usiku lenye kung’aa lisilo na mawingu la Kusini ladhihirisha nyota zake nyingi mno, kutia ndani mfanyizo ujulikanao sana uitwao Msalaba wa Kusini. Mikalitusi inatokezwa dhidi ya anga huku wanyama wa pori wakianza kupumzika, na wafunikwa na ukimya unaoonekana kukazia nafasi iliyo wazi sana.

Zima kwa uangalifu moto wa kambi kabla ya kuingia katika fuko lako la kulalia. Ni muhimu kufanya hivyo, kwa kuwa moto ukishindwa kuzuilika katika kichaka cha Australia, muda si muda huwa maangamizi makubwa ambayo huharibu kila kitu njiani mwake. Vilele vya mikalitusi hulipuka katika joto jingi, jambo ambalo hufanya moto uenee kwa kasi yenye kutisha. Katika miezi yenye joto na ukavu ya kiangazi, mioto ya vichakani ni ogofyo la daima la wanaoishi karibu na maeneo ya vichaka. Ni lazima marufuku juu ya moto na maagizo kuhusu kuwasha mioto katika mahali wazi yafuatwe kwa ukamili.

Muda si muda kunapambazuka, nawe waamshwa na kicheko chenye kelele cha kikundi cha mkumburu ambao wamelala usiku katika mkalitusi ulio karibu nao waimba wimbo wa furaha. Ukiwa umeshangazwa, watazama nje ya hema lako na waona miti ikiwa imejaa ndege wenye rangi nzuri-nzuri. Kufikia sasa huenda tayari umekutana na wengi wao, na vilevile viumbe wengine kutia ndani, kangaruu, koala, emu, na huenda hata wombati. Wale ambao hutaki kukutana nao ni nyoka na buibui. Ndiyo, kontinenti hili lina baadhi ya nyoka na buibui wenye sumu zaidi ulimwenguni. Lakini wengi wao hawatakuwa tisho kwako kamwe usipowasumbua.

Wakati wa kifungua-kinywa umefika kando ya moto wa kambi—kwa kawaida kikiwa bekoni na mayai na vipande vya mkate uliochomwa vizuri. Hewa safi imekupatia hamu nzuri ya kula. Kisha, unapojaribu kufurahia kifungua-kinywa chako japo nzi wenye kusumbua, waanza kuwazia-wazia uliyojionea huku porini, ambalo limekupa mwono mfupi wa ukubwa wa kontinenti la Australia.

Sasa safari zako katika nchi hii kubwa zimekwisha, nawe warudi nyumbani. Bila shaka utakumbuka daima uliyojionea katika kuwajua Waaustralia wenye urafiki na maisha yao yenye kiasi. Kama ilivyo na wengi walio wageni, huenda wataka kurudi tena siku fulani. Lakini bila shaka kuna mkataa mmoja umeufikia: Maisha ni tofauti huku chini!

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Kasuku mdogo na kasuku kishungi wa rangi ya waridi: Kwa hisani ya Australian International Public Relations; mwanamke: Kwa hisani ya West Australian Tourist Commission

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki