Chewa-Ulaya Wote Hao Walienda Wapi?
CHEWA-ULAYA walikuwa wengi sana katika maji hivi kwamba “ilikuwa vigumu kwa mashua kupiga makasia katikati yao.” Akasema mvumbuzi John Cabolt katika mwaka wa 1497 alipokuwa akielezea moja ya sehemu bora zaidi za uvuvi duniani—zile Kingo Kubwa za Newfoundland. Kufikia mwishoni mwa miaka ya 1600, uvuvi wa kila mwaka wa chewa-ulaya katika Newfoundland ulikuwa umefikia karibu tani 100,000. Kufikia karne iliyofuata, pato liliongezeka likawa maradufu.
Hata hivyo, leo, hali hiyo imebadilika sana. Idadi ya chewa-ulaya imepungua sana hivi kwamba katika mwaka wa 1992 serikali ya Kanada ilipiga marufuku uvuvi wa chewa-ulaya katika Atlantiki, hilo likiwaacha watu wapatao 35,000 katika nchi hiyo wakitafuta kazi katika sehemu nyingine. Katika mwaka huu wa 1997 kipindi cha marufuku kingali chaendelea. Lakini chewa-ulaya wote hao walienda wapi?
Katika miaka ya 1960, meli za kimataifa za uvuvi zilikutana pamoja katika pwani ya Newfoundland ili kuvua idadi kubwa ya chewa-ulaya. Kufikia 1968, vyombo vya kuvulia samaki kwa wavu chinichini kutoka katika nchi zaidi ya 12 vilikuwa vikichukua zaidi ya tani 800,000 za samaki kwa mwaka kutoka kwenye kingo za Newfoundland. Hii ilikuwa mara tatu zaidi ya wastani wa uvuvi katika karne zilizopita.
Ijapokuwa maji baridi zaidi, kuongezeka sana kwa sili, na kuhama kwa chewa-ulaya kwaweza kuwa kumechangia kupunguka kwa idadi ya chewa-ulaya, sehemu kubwa ya lawama kwa msiba wa chewa-ulaya lazima iwe kwa pupa ya mwanadamu. “Ulikuwa uvuvi wa kupita kiasi—wazi na moja kwa moja,” asema mwanabiolojia mmoja wa majini.
Kuna wakati ujao gani kwa chewa-ulaya wa Atlantiki? Watu fulani hutilia shaka kuwa kuna samaki wachanga wa kutosha ili kukomaa, kuzaana, na kuijaza tena spishi hiyo. Gazeti The Evening Telegram la St. John’s lilieleza: “Kiwanda cha zamani kabisa katika Kanada, uvuvi wa chewa-ulaya katika Atlantiki, kitasitawi tu katika vitabu vya historia.” Hata hivyo, kuna tumaini!
Biblia hutuhakikishia kuwa karibuni, katika ulimwengu mpya ulioahidiwa wa Mungu wenye uadilifu, hakutakuwa nafasi ya pupa. (2 Petro 3:13) Yehova “atawaleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia” na atafanya dunia na bahari zijae uhai kwa kuwabariki wale wanaotaka kumtumikia na kumpendeza.—Ufunuo 11:18.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
©Tom McHugh, The National Audubon Society Collection/PR
Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.