Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 12/22 kur. 25-26
  • Je, Rave Ni Burudani Zisizo na Madhara?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Rave Ni Burudani Zisizo na Madhara?
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuiangalia Mandhari ya Rave
  • Upande Mbaya wa Rave
  • Je, kwa Kweli Rave Inakufaa?
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1998
  • Mbona Watu Hutumia Dawa za Kulevya?
    Amkeni!—2001
  • Vipi Kwenda Disko?
    Amkeni!—2004
  • Nyimbo na Ngoma Unazochagua Kucheza
    Kupata Faida Zote za Ujana Wako
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 12/22 kur. 25-26

Vijana Huuliza . . .

Je, Rave Ni Burudani Zisizo na Madhara?

“Nichezapo dansi na mikono yangu ikiwa hewani na muziki unasisimua mwili wangu, mimi huhisi nimechangamshwa na wengine wanaocheza dansi. Ni kama kubebwa juu kwa juu na hisia-moyo kali.”— Gena.

HIVYO ndivyo Gena afafanuavyo msisimko wa kuhudhuria rave. Karamu hizi za muziki, ambazo kwa kawaida hudumu usiku kucha, kwanza zilianza kuwa maarufu katika Uingereza wakati wa miaka ya 1980. Kwa sasa zinaonekana katika sehemu zote za dunia, kutia ndani Ubelgiji, Kanada, Ujerumani, India, New Zealand, Afrika Kusini, na Marekani.

Kwa kawaida rave huchezwa katika klabu za kuchezea dansi, maghala yasiyotumika, maeneo yaliyo wazi—mahali popote ambapo watu waweza kukusanyika kwa ajili ya usiku wa kichaa, kucheza dansi kusiko na mwisho. “Hatua kwa hatua rave zinachukua mahali pa klabu za usiku zikiwa chaguo la vijana la tafrija,” akaandika Adam Levin, katika Sunday Times Magazine la Johannesburg, Afrika Kusini. “Ikiwa matineja wako hawajazitaja bado,” aliongeza, “basi una tatizo la uwasiliano.”

Kuiangalia Mandhari ya Rave

Mara nyingine rave hufichwa katika siri, mahali pao hapatangazwi hadi siku ya tukio. Hata hivyo, mara taa zenye madoido zinapowashwa na dansi itokanayo na elektroni inapoanza, idadi yoyote kuanzia dazani kadhaa hadi maelfu ya vijana wakiwa katika mavazi ya kiajabu-ajabu waweza kuwapo. “Ni kama tungamo la watu waliounganishwa wakicheza dansi na kumwaga hasira zao kwenye midundo,” asema Katy, mwanafunzi wa mwaka wa pili chuoni.

Lakini, rave ni zaidi tu ya kukutana pamoja ili kucheza dansi. Pia ni utamaduni, au “mandhari,” kama ambavyo vijana wanaohudhuria rave waiitavyo. Kanuni za msingi za mandhari ya rave zinajulikana kuwa ni amani, upendo, umoja, na staha—bila kujali jamii, uraia, au kama ni mgoni-jinsia-moja au la. “Tumekuwa tukijaribu kuchanganya tamaduni tofauti-tofauti katika karamu hizi,” asema mwenye kumiliki duka lishughulikialo tu muziki wa dansi. “Wazo kuu ni umoja,” aongeza, “na kucheza dansi pamoja ni njia yenye matokeo katika kulifikia lengo hili.”

Kukiwa na maoni hayo yaonekanayo kuwa mazuri sana, waweza kuuliza, ‘Ni nini liwezalo kuwa kosa kuhusu muziki wa rave?’ Lakini kuna upande mwingine wa mandhari ya rave ambao wapaswa kuufikiria kwa uangalifu.

Upande Mbaya wa Rave

Wengine hudai kwamba ni nadra kupata alkoholi katika rave. Hata hivyo, dawa za kulevya zinapatikana kwa kawaida. “Mtu ashangaa ikiwa mandhari za rave zingeweza kukubaliwa na watu ikiwa dawa za kulevya hazikuwa zinatumiwa kwa wingi,” akubali mcheza rave aitwaye Brian. “Bila shaka,” aongeza, “watu wengi zaidi wajiuliza jinsi gani rave zingeweza kudumu bila dawa za kulevya.”

Ingawa bangi na LSD zinapendwa sana katika baadhi ya rave, dawa za kulevya zipendwazo sana miongoni mwa wachezaji wa rave zaonekana kuwa ni MDMA, kwa kawaida hujulikana kuwa Ecstasy. Watumiaji wadai kwamba Ecstasy ni salama kwa kadiri. Wadai kwamba hiyo huwapa tu nishati ili wacheze dansi usiku kucha na kwamba huongeza hisia zao za furaha. Lakini, chini ya kichwa cha habari “Dawa ya Kulevya Ipendwayo Zaidi Yaweza Kuharibu Ubongo,” gazeti la The New York Times lilitaja kwamba Ecstasy “yaweza kuwa na madhara ya muda mrefu, juu ya hamu ya chakula, usingizi, hali ya moyoni, hali ya msukumo na matatizo mengine ya kiakili.” Matatizo si hayo tu. “Kumekuwa na vifo kutokana na Ecstasy,” adai Dakt. Howard McKinney, “na matukio mengine kadhaa ambayo watu ambao walitumia kiasi cha kawaida cha dawa walipatwa na matatizo ya moyo, kushindwa kufanya kazi kwa ini au kuzimia.” Akiwa na sababu nzuri Dakt. Sylvain de Miranda asema: “Wanaoenda kwenye rave na kutumia Ecstasy wanahatarisha maisha yao.”

Hata dawa za kulevya zitokanazo na majani—kama vile Herbal Acid, Acceleration, dawa ya Ecstasy itokanayo na majani, au Rush—zaweza kuwa zenye madhara. Kwa kielelezo, inadaiwa kwamba katika hali fulani, Acceleration itokanayo na dawa za kulevya za majani yaweza kusababisha maradhi ya moyo na hata kifo.

Kwa wale ambao wangali wanasisitiza kwamba dawa za kulevya zitumikazo katika rave hazina madhara, kuna jambo jingine la kufikiria. Polisi mpelelezi Mkanada Ian Briggs adai kwamba asilimia 90 ya dawa za kulevya ziuzwazo kama Ecstasy si Ecstasy hata kidogo. “Nyingi za hizo ni PCP au dawa nyingine za kulevya zilizo hatari,” asema. “Watu wauzao dawa hizi za kulevya si wanyoofu. Hawapo wakati dawa hizo zianzapo kuwa na matokeo.”a

Kwa kukiri wazi, huenda kusiwepo na matumizi ya dawa za kulevya katika baadhi ya rave. Hata hivyo, hata miongoni mwa wachezaji wa rave wakubali kwamba mara nyingi haiwezekani kutabiri ikiwa yeyote, wengi, au walio wengi wa wale ambao wapo katika rave watakuwa chini ya uvutano wa vitu vyenye uraibu kama vile dawa za kulevya au alkoholi.

Je, kwa Kweli Rave Inakufaa?

Kiasili hakuna ubaya wowote katika muziki na kucheza dansi, wala si vibaya kutaka kuwa na wakati wa furaha. Zaidi ya yote, Biblia yasema kwamba “kuna wakati wa shangwe” na “wakati wa kucheza dansi.” (Mhubiri 3:4, Today’s English Version) Pia yashauri: “Uufurahie ujana wako.” (Mhubiri 11:9) Hivyo Muumba ataka uwe na furaha! Hata hivyo, wapaswa kukumbuka kwamba “ulimwengu mzima unakaa katika nguvu ya mwovu,” Shetani Ibilisi. (1 Yohana 5:19) Hivyo, kwa hakika haipasi kushangaza kwamba aina za tafrija ambazo zinatukuzwa na ulimwengu huu mara nyingi zimechafuliwa na mambo yasiyofaa.

Kwa kielelezo, fikiria wale ambao huenda kwenye rave. Je, wanafuata onyo la Biblia la ‘kujisafisha wenyewe kila unajisi wa mwili na wa roho’? (2 Wakorintho 7:1) Kweli, rave zaweza kuunga mkono amani, upendo, na umoja. Lakini “hekima ya kutoka juu” ni zaidi ya “yenye kufanya amani”; pia ni “safi kiadili.” (Yakobo 3:15, 17) Jiulize, ‘Je, maadili ya waendao mara nyingi katika rave zinapatana na viwango vipatikanavyo katika Neno la Mungu, Biblia? Je, ningependa kutumia usiku kucha pamoja na wale ambao ni “wenye kuzipenda raha badala ya kuwa wapenda-Mungu”?’—2 Timotheo 3:4; 1 Wakorintho 6:9, 10; linganisha Isaya 5:11, 12.

Haya ni maswali muhimu kuyafikiria, kwani Paulo aliandika kwamba “mashirika mabaya huharibu mazoea yenye mafaa.” (1 Wakorintho 15:33) Kuendelea kushirikiana na wale ambao wanaonyesha dharau kwa sheria za Mungu hatimaye kutaongoza katika msiba, kwani Biblia yasema hivi: “Atembeaye na mwenye hekima atakuwa na hekima, bali yeye ajishughulishaye na wapumbavu ataumia.”—Mithali 13:20, NW.

Ukweli ni kwamba rave ni mahali pa karamu za dawa za kulevya na wale ambao wanahudhuria waweza kuvuna matokeo mabaya sana. Baadhi ya rave, kwa kielelezo, zinavamiwa na polisi na kufungwa, kwa sababu ama zinaendeshwa kinyume cha sheria ama kwa sababu kuna dawa za kulevya. Je, ungependa ujulikane kuwa umo miongoni mwa watu ambao si wafuata-sheria? (Waroma 13:1, 2) Hata kama hakukuwa na uvunjaji wa sheria, je, ungeweza kuhudhuria karamu kama hiyo na ubaki “bila doa kutokana na ulimwengu”? (Yakobo 1:27) Kwa vile sherehe zenye kelele za ulevi na ulafi, au “karamu za kinyama” (Byington), zinalaaniwa katika Biblia, je, kuwepo kwako katika rave kungekuwezesha kubaki na dhamiri safi mbele ya Mungu na wanadamu?—Wagalatia 5:21; 2 Wakorintho 4:1, 2; 1 Timotheo 1:18, 19.

Kwa wazi, Wakristo wapaswa kujihadhari na hatari za rave. Lakini usikate tamaa. Bado kuna tafrija nyingi uwezazo kufurahia. Kwa kielelezo, familia nyingi miongoni mwa Mashahidi wa Yehova zimeandaa vikusanyiko vyenye kufaa.b Kukiwa na mipango mizuri na usimamizi wenye kufaa, vikusanyiko kama hivi huwaacha wote waliohudhuria wakihisi wameburudishwa kiroho na kimwili. Jambo muhimu zaidi, ushirika unaojenga humfurahisha Yehova, “Mungu mwenye furaha,” ambaye ataka watu wake wafurahi.—1 Timotheo 1:11; Mhubiri 8:15.

[Maelezo ya Chini]

a PCP (phencyclidine) ni nusukaputi ambayo mara nyingine hutumiwa vibaya katika kutokeza maono ya akilini.

b Kwa habari zaidi, ona Mnara wa Mlinzi la Agosti 15, 1992, ukurasa wa 15-20, na Amkeni! la Mei 22, 1997, ukurasa wa 8-10.

[Sanduku katika ukurasa wa26]

Techno Ni Nini?

Kwa kifupi, techno hurejezea muziki wa dansi wa elektroni. Hutia ndani mitindo mbalimbali. Watu wengi wangeufafanua techno kuwa ni wa kimdundo, kwani kwa kawaida huwa kati ya midundo 115 na 160 kwa dakika.

“Kwa wale wasiofahamu techno,” lasema gazeti la The European, “techno husikika kama sauti uzisikiazo kutokana na keekee za daktari wa meno, zikiambatana na kelele uwaziazo kuwa zilikuwapo wakati Sodoma na Gomora zilipoharibiwa.” Lakini, baadhi ya wasikilizaji wananaswa na mdundo wa techno usiobadilika. “Kwa upande wangu,” asema Christine mwenye umri wa miaka 18, “muziki huu hunipa hisia ya uhuru usio na mipaka na hali ya kujitawala.” Sonja ahisi vivyo hivyo. “Kwanza,” akubali, “sikupenda kabisa muziki wa techno. Lakini kadiri uendeleavyo kuusikiliza, ndivyo uendeleavyo kuupenda. Ikiwa utaufungulia kwa sauti ya juu kabisa, hutakosa kupenda mdundo wenye kudunda-dunda. Waamka bila kujijua. Usipokuwa mwangalifu, mdundo huo utaudhibiti mwili wako wote.” Shirley, mwenye umri wa miaka 19, aona jambo fulani zito katika muziki wa techno. “Ni zaidi ya muziki wa kawaida,” asema. “Ni njia yote ya maisha, ikielezwa katika mavazi na lugha.”

Wakristo watamani ‘kufuliza kuhakikisha ni nini lililo lenye kukubalika kwa Bwana.’ (Waefeso 5:10) Kwa hiyo, wapaswa kuwa na hadhari kuelekea muziki wa techno kama ambavyo wangekuwa kwa aina nyingine yoyote ya muziki. Ikiwa wajikuta wavutwa kwa muziki wa techno, jiulize: ‘Mtindo huu wa muziki waniathirije? Je, unanifanya nijihisi mwenye furaha, mtulivu, na mwenye amani? Au hunikasirisha, labda hata ukichochea hasira au mawazo yasiyo ya adili? Je, uvutio wangu kwa aina hii ya mdundo hunivuta karibu zaidi na mtindo-maisha wake? Je, ningeshawishiwa kuhudhuria rave kusikia mtindo huu wa muziki au kuucheza?’

Kwa kweli, jambo la msingi ni hili: Hata upendezi wako wa muziki uwe ni nini, usiuruhusu kamwe ukuzuie kuwa na uhusiano mzuri na Baba yako wa kimbingu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki