Fahamiana na Ndege Mwenye Kope
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AFRIKA KUSINI
“KUNA uwezekano mkubwa kwamba hujapata kamwe kukutana nasi. Sisi ni ndege, na watu wengi hutuita mumbi.
“Mbali na uvutio wetu, kuna mambo mengine ya kupendeza kutuhusu ambayo tungependa kukujulisha. Kwanza, twatumia wakati wetu mwingi katika ardhi. Karibu tuwe sawa na batamzinga, na kama ilivyo na batamzinga, kwa kweli haturuki sana.
“Tukitagaa-tagaa kwa uzito sana, twazunguka katika maeneo ya kati na kusini-mashariki ya Afrika. Tukipata kukutana, usingekosa kututambua kwa sababu ya mifuko ya shingo zetu yenye rangi nyekundu nyangavu na mapaku ya macho, na bila shaka, kope zetu ndefu zenye kuvutia sana!
“Sisi mumbi ni wazazi wenye haya—kwa wastani, hulea kifaranga kimoja kila miaka sita. Wakati wa majira ya kutaga, wa kiume huandaa ugavi wa kutosha wa majani makavu ili kuweka ndani ya viota vyetu, ambavyo kwa kawaida viko katika miti yenye shimo au mashimo ya miamba. Kisha majike hutunza mayai kwa uangalifu kwa kipindi cha siku 40. Pamoja na washiriki wengine wa kikundi cha familia yetu, sisi huwa na pilikapilika za kwenda huku na huku, tukihakikisha kwamba kuna ugavi wa kutosha wa nyungunyungu, funza, na mapochopocho mengine kwa ‘mama mtarajiwa.’ Sisi sote hufurahi sana wakati, miezi mitatu baada ya kuanguliwa, vifaranga viachapo viota na kujiunga nasi katika familia.
“Sisi huchukua muda mrefu sana kukomaa—huchukua angalau miaka sita kabla hatujafikia ukomavu kamili. Na inaweza kuchukua hata muda mrefu zaidi kwa mmoja kati yetu kufanikiwa kusitawisha familia yake mwenyewe. Bila shaka, ukweli wa kwamba tunaishi muda mrefu (wengi wetu huishi miaka 30) hutupatia wakati wa kutosha kupitisha jeni zetu kwa vizazi vingine.
“Kama uwezavyo kuona, sisi hukazia fikira sana familia, tukiwa katika vikundi visivyozidi ndege wanane tukiishi na kufanya kazi pamoja. Kila familia ina eneo la karibu kilometa 100 za mraba katika nyanda za Afrika, eneo lenye miti, na mbuga. Katika sehemu fulani za kusini mwa Afrika, tumepoteza hadi asilimia 70 ya makazi yetu kwa kilimo na makao ya wanadamu.
“Sisi hulinda sana eneo letu na kwa kawaida hushika doria kwenye mipaka yetu. Hatutaki kushiriki vyakula vyetu—nyoka, funza, kobe, na wadudu—na wengine, hata mumbi wa familia nyingine. Katika ukali wetu kuwafukuza wadukizaji, nyakati nyingine hufanya mambo ya kipumbavu. Jinsi gani? Tujionapo katika dirisha lenye kioo, mara nyingi hukimbilia dirisha, tukifikiri kwa makosa kwamba huyo ni mdukizi. Bila kuzuilika, pigo la mdomo mgumu mrefu huvunjavunja dirisha. Kwa sababu ya madirisha mengi yaliyovunjika, baadhi ya watu wameweka nyaya za wavu katika madirisha yao, na twashukuru sana kwa jambo hilo!
“Kwa kuhuzunisha, kuna vitisho vibaya sana vinavyotuhangaisha. Baadhi ya watu hutusonga na kutuondoa katika makao yetu. Wengine hutupiga risasi kwa bunduki. Kwa kawaida wakulima huweka chambo chenye sumu kwa ajili ya mbweha na wanyama wengine wasiotakiwa. Lakini tunaweza kujuaje kama chambo kina sumu? Ni wazi kwamba kwa ajili ya usalama wetu, mara nyingine wakulima hufukia sumu hizo. Lakini kwa vile kwa kawaida sisi huchimba chini tukitafuta chakula kwa kutumia midomo yetu mirefu, tuchimbuapo sumu iliyofukiwa, ni kana kwamba tunajichimbia makaburi.
“Baadhi ya watu wanajitahidi sana kutulinda dhidi ya hatari hizi. Twatumaini kwamba hatutatoweka kama ndege wenzetu dodo. Hivyo wakati wowote utukiapo kuwa katika eneo letu na kusikia sauti yetu kubwa, du-du-dududu du-du-dududu, uje ututazame. Tutapepesa kope zetu ndefu na kukukaribisha katika milki ya mumbi.”