Walinzi wa Minara ya Taa—Kazi ya Kitaalamu Inayofifia
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KANADA
“BILA shaka hakuna kazi nyingine yoyote niwezayo kufanya badala ya hiyo,” walinzi wa minara ya taa wamesema hivyo tena na tena. Mtu mmoja aliyeacha wadhifa wake kama meneja katika kiwanda cha kutengenezea plastiki katika Toronto, Kanada, ili awe mlinzi wa mnara wa taa wenye miaka 106 alisema kwamba kazi hiyo ilimfanya ahisi “ametiwa nguvu.”
Daraka la msingi la mlinzi wa mnara wa taa ni kudumisha nuru iliyo wazi kwa ajili ya mabaharia. Pia hutakwa aendeshe na kudumisha parapanda za kutangazia hatari ya ukungu baharini vilevile kutoa habari za halihewa kupitia redio kwa wavuvi na merikebu zipitazo.
Kwa miaka iliyopita, walinzi wa minara ya taa walihitaji kujaza matangi ya mafuta, kuwasha tambi, na kuweka glasi za taa zikiwa bila moshi. Halikuwa jambo lisilo la kawaida kwa walinzi kutumia usiku mzima wakizungusha kwa mkono mwanga mkubwa wa kujulisha hatari ili kuongoza meli kwenye usalama wakati ambapo taa za mnara hazingeweza kurekebishwa haraka au kutumia usiku wakigota kwa nyundo kengele ya kuonya juu ya ukungu wakati parapanda ya kutangazia hatari ya ukungu baharini ilipoacha kufanya kazi!
Kupambana kwa Mafanikio na Dhoruba
Dhoruba kali ni hangaiko lililo kuu. Wakati mmoja, mlinzi wa taa aliona kitu ambacho aliamini kuwa ni “wingu kubwa sana jeupe” lakini likaja kuwa ni wimbi moja lenye kishindo! Wimbi hilo lilipanda jabali lenye futi 50, na likafikia makazi ya mlinzi. Wimbi hili moja lilifanya madhara kwa kadiri ambayo dhoruba nzima ingefanya.
Kwenye pindi nyingine, usiku kucha dhoruba ya upepo yenye kuvuma ilivurumisha mawimbi kwenye mnara wa taa katika Bandari ya Pubnico, Nova Scotia. Kile ambacho mlinzi na familia yake wangeweza kufanya ni kungoja na kutumaini. Kufikia asubuhi dhoruba ilikuwa imetulia. Lakini wakati mlinzi alipotoka nje, alishangaa kuona kwamba ardhi ambayo ilizunguka mnara wa taa haikuwapo. Mnara wa taa na ardhi ambayo mnara huu ulisimama juu yake sasa ilizungukwa na maji!
Upweke na Ukinaifu
Alipoulizwa kuhusu upweke, mlinzi mmoja wa mnara wa taa alijichekea na kusema: “Watu hutuambia, ‘Lo! mwawezaje kuvumilia upweke huu wote?’ Sisi huwatazama na kuuliza, ‘Vema, mnawezaje kuvumilia kuishi katika jiji kukiwa na makelele hayo yote na msukosuko?’”
Katika nyakati zilizopita, mkusanyo mdogo wa vitabu ulifanywa upatikane kwa minara ya taa iliyojitenga zaidi katika Marekani. Hivyo, kufikia mwaka wa 1885, kulikuwa na maktaba 420 zilizokuwa zikitumiwa. Kwa wazi, walinzi wa minara ya taa wakawa wasomaji wazuri.
Kazi ya Kitaalamu Inayofifia
Katika miaka ya juzijuzi mahali pa minara ya taa yenye kutengenezwa na waashi wa kibinadamu pamechukuliwa na minara iliyojengwa na viunzi vya chuma ngumu ikiwa na minara yenye taa zenye kumweka kwa nguvu. Mabaharia hawahitaji tena kuchungulia kwenye giza, wakitafuta mwanga mkubwa wa kujulisha hatari usio dhahiri au mwale wenye ukungu. Leo, taa zenye mwangaza mwingi zilizotengenezwa na filamenti za madini na mlio, unaopenya ishara za ukungu hutahadharisha mabaharia juu ya hatari za bahari.
Merikebu zilizotengenezwa zikiwa na uwezo wa kupokea ishara kutoka kwenye vituo vya nuru sasa hujua eneo ambalo zipo hata iwe ukungu ni mnene jinsi gani. Tekinolojia ya kisasa huruhusu nahodha asafiri baharini kutoka ukingo hadi ukingo, akiwa na uhakika kwamba aweza kuepuka mafungu ya mchanga yaliyo hatari, miamba hatari, na majabali yaliyofichika karibu na pwani.
Kama tokeo la tekinolojia ya kisasa, walinzi wa minara ya taa wanaendelea kufifia kwa kasi kutoka kwenye mandhari ya ulimwengu. Akihisi kuwa sehemu ya maisha yake imetoweka milele, mlinzi mmoja wa mnara wa taa alitafakari kwa huzuni namna alivyoacha kisiwa cha nyumbani kwake cha miaka 25: “Tulikuwa na maisha yenye kuridhisha hapa. Kwa kweli hatukutaka kuondoka.”
Bado, taa zenye kuzunguka, taa za usaidizi, taa za dharura, ishara za milio, na mianga-rada mikubwa ya kujulisha hatari zote huhitaji ukaguzi, na minara ya taa bado huhitaji gharama za utunzaji. Minara ya taa sasa hukaguliwa na mafundisanifu wanaosafiri.
Wale ambao huthamini huduma ya miaka mingi iliyotolewa na walinzi wa minara ya taa hushiriki hisia za moyoni za mwanamume katika Augusta, Maine, aliyeomboleza: “Bila shaka halitakuwa jambo lilelile kutazama kwenye mnara wa taa na kufahamu kwamba taa zinaendeshwa na kompyuta, ukijua kwamba watu hawaishi tena katika minara ya taa.”
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Mnara wa Taa wa Kwanza
Mnara wa taa wa kwanza katika historia ulimalizika wakati wa utawala wa Ptolemy wa Pili wa Misri. Ulijengwa karibu na mwaka wa 300 K.W.K., na ulisimama katika Kisiwa cha Pharos, kando tu ya mwingilio wa bandari ambayo sasa ni Aleksandria. Ulichukua miaka 20 kuujenga kwa gharama ya dola milioni 2.5.
Maandishi ya kihistoria huonyesha kwamba ulikuwa na urefu wa zaidi ya meta 90. Chumba chake cha juu kilikuwa na madirisha yaliyoelekea baharini, ambapo nyuma yake kulikuwa na mioto ya kuni au labda mienge ambayo, kulingana na Yosefo, ingeweza kuonekana kutoka umbali wa zaidi ya kilometa 50 hivi.
Jengo hili kubwa la mawe lilifikiriwa kuwa mojawapo Maajabu Saba ya Ulimwengu. Moto wake wenye kuwaka vikali ulitumika kama taa ya kuonya kwa miaka 1,600, ukaja kuharibiwa tu, yamkini, na tetemeko la dunia.
Karne zilipopita, maelfu ya minara ya taa ya ukubwa na ufafanuzi wa namna mbalimbali ilijengwa kwenye bandari kotekote katika ulimwengu. Minara ya taa iliyo mizee iliyojengwa na waashi imedumu hadi leo kama majumba ya makumbusho na uvutio wa watalii katika mbuga za kitaifa, taifa, mkoa, na jiji na hutazamwa na mamilioni ya watu.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mnara wa taa wa Cape Spear, Newfoundland, Kanada