Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 1/22 kur. 20-23
  • Nuru Iokoayo Uhai

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nuru Iokoayo Uhai
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Minara ya Taa ya Kwanza
  • Kutoka Miali ya Moto Hadi Taa za Neli
  • Minara ya Taa Inayoelea
  • Ukungu na Dhoruba Vifunikapo Taa
  • Mwisho wa Muhula
  • Walinzi wa Minara ya Taa—Kazi ya Kitaalamu Inayofifia
    Amkeni!—1998
  • Elekea Mahali Ilipo Nuru
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2002
  • Msiba Mwingine Tena wa Kimazingira
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 1/22 kur. 20-23

Nuru Iokoayo Uhai

ILIKUWA safari ngumu ya majuma matano ya kuvuka bahari ya Atlantiki katika mwisho-mwisho wa karne ya 19. Abiria walitarajia kuona nchi kavu siku yoyote. Kisha nuru ikaonekana, nyota iliyo ukiwa kwenye upeo wa macho. Lakini haikuwa nyota; ulikuwa mnara wa taa. “Tulipoiona nuru hiyo, tulipiga magoti na kumshukuru Mungu,” abiria mmoja akasema baadaye. Nuru hiyo iliwaongoza salama hadi walikokuwa wakienda. Lakini, si safari zote za baharini zilizoisha vizuri.

Desemba 22, 1839, ilikuwa siku nzuri yenye jua katika pwani ya New England, Amerika Kaskazini. Mlinzi wa mnara wa taa kwenye Kisiwa cha Plum, Massachusetts, alidhani angeweza kuondoka kwenye kisiwa hicho kwa usalama akitumia mashua yake ya kuendeshwa kwa makasia, amchukue mke wake waende kununua vitu, na kisha arudi kabla giza halijaingia. Lakini walipokuwa mbali, upepo ulianza kuvuma. Dhoruba ilikuwa ikija kwa haraka. Punde, anga na bahari zikaungana kutokeza wingu jeusi lenye ngurumo na mvua nyingi, povu, na rasharasha. Mlinzi aling’ang’ana kurudi kisiwani bila mafanikio. Usiku huo mnara wa taa haukuwashwa.

Karibu usiku wa manane, meli Pocahontas, ikijitahidi kutafuta mto na mwingilio wa bandari ambao kwa kawaida hutolewa ishara na mnara wa taa, haikufanikiwa. Badala yake, meli hiyo iligonga fungu la mchanga. Tezi yake ilivunjika, na kuzama pamoja na wote waliokuwemo. Kabla tu hakujapambazuka, meli nyingine Richmond Packer, ikielekea kwenye bandari ile ile, nayo ilivunjika, lakini ni mtu mmoja tu aliyekufa, mke wa nahodha.

Historia ya ubaharia imejawa na misiba ambayo ingeweza kuepukwa kwa kuwa na minara ya taa. “Nyakati za zamani, meli nyingi zilisafiri bahari yote zikiwa salama, lakini zilivunjika zilipojaribu tu kuingia bandarini,” chasema kitabu America’s Maritime Heritage. “Sehemu ya safari ya baharini iliyokuwa hatari zaidi ilikuwa kilometa chache za mwisho, meli ilipokaribia na hatimaye kuiona nchi kavu.”

Kulingana na mwanahistoria wa minara ya taa D. Alan Stevenson, kati ya 1793 na 1833, wastani wa idadi ya meli zilizovunjika kila mwaka kwenye fuo za Uingereza uliongezeka kutoka 550 hadi 800. Minara ya taa zaidi na hata nuru bora ilihitajiwa.

Katika nchi fulani, kutia ndani Uingereza na Marekani, kusafiri kwa mashua kulikuwa hatari hata zaidi kwa sababu ya walaani-mwezi wenye sifa mbaya, walaghai waliofanyiza nuru bandia ili kushawishi meli zikavunjikie kwenye miamba kwa makusudi ya kuzipora huko. Mara nyingi manusura waliuawa; kwa kuwa walaani-mwezi hawakutaka mashahidi. Hata hivyo, hila yao haingefua dafu kukiwapo mbalamwezi. Hivyo wakaja kuitwa walaani-mwezi. Hata hivyo, hatimaye, minara ya taa zaidi na bora ilisaidia kuwakomesha wezi hao.

Minara ya Taa ya Kwanza

Mtajo wa mapema zaidi wa minara ya taa unapatikana katika Iliad (ngano za Wagiriki wa kale). “Jua linapotua, mioto ya minara ya taa huwaka,” hizo husema. Kitabu Keepers of the Lights chasema kwamba “minara ya taa ya awali ilikuwa tu vigogo vya mti, ambavyo nyakati fulani viliwekwa ndani ya nguzo za mawe, na baadaye katika vizimba vya chuma, vilivyowaka kwa vipindi vya mara kwa mara kukiwa na matokeo mabaya sana.”

Kisha, yapata mwaka 300 K.W.K., katika kisiwa cha Pharos, kwenye mwingilio wa bandari ya Aleksandria, Misri, kukatokea mnara wa taa wa kwanza halisi, ulioitwa Pharos ya Aleksandria. Jengo lenye fahari lililojengwa kwa mawe lenye urefu wa meta 100 hadi 120 (karibu orofa 40), ndio mnara wa taa mrefu zaidi uliopata kujengwa. Ukiwa mmoja wa yale Maajabu Saba ya Ulimwengu, ulidumu miaka karibu 1,600 hadi ulipoangushwa pengine na tetemeko la dunia.

Waroma walijenga minara ya taa angalau 30, kuanzia Bahari Nyeusi hadi Atlantiki. Lakini milki hiyo ilipoanguka, biashara ilididimia, nayo minara ya taa ikaharibika na kuchakaa. Ujenzi ulianza tena yapata mwaka wa 1100. Mnara wa taa maarufu wa muhula mpya ulikuwa Lanterna wa Genoa, uliolindwa mwaka wa 1449 na Antonio Columbo, mjomba wa mvumbuzi Christopher Columbus.

Mnara wa taa wa kwanza kusimamishwa baharini, ni ule uliojengwa kwa mbao na Henry Winstanley katika mwaka wa 1699 kule Eddystone Rocks yenye hatari, karibu na Plymouth, Uingereza. Alijivunia mafanikio yake. Akivua samaki kutoka kwenye mnara wa taa wake, yasema sinema ya video Guardians of the Night, Winstanley angesema hivi: “Inuka, ewe bahari. Njoo na ujaribu kazi yangu.” Siku moja katika mwaka wa 1703, bahari ilitii. Winstanley pamoja na mnara wake walitokomea wasionekane tena.

Ikisherehekea urafiki baina ya watu wa Marekani na Ufaransa, ile sanamu ya Statue of Liberty yenye urefu wa futi 302, katika Bandari ya New York, vilevile iliwasaidia mabaharia. Kwa miaka 16 walinzi watatu walifanya zamu ya kudumisha moto wake ukiendelea kuwaka. “Mkono wake ulio mnara wa taa, huangaza ukialika ulimwengu wote,” lasema shairi miguuni pake.

Kutoka Miali ya Moto Hadi Taa za Neli

Makaa ya mawe, mishumaa—hata vinara vya mishumaa—na mafuta hatimaye vilichukua mahali pa kuni kama vimulikaji kwenye minara ya taa. Majaribio yalifanywa kutumia viakisi-nuru ili kuifanya nuru iwe wazi, lakini moshi na masizi kutoka kwenye moto zilivifanya viwe vyeusi. Hata hivyo, katika mwaka wa 1782, mtaalamu Mswisi Aimé Argand alibuni taa ya kutumia mafuta iliyoelekeza hewa juu kupitia sehemu ya kati ya utambi wenye umbo la mcheduara na kutokea kwenye dohani ya kioo. Sasa vikiwa safi, viakisi-nuru vyenye umbo la pia (vilivyoundwa kama vioo vya taa za mbele za gari) vikawa maarufu kwenye minara ya taa. Kiakisi-nuru kizuri kiliongeza nuru mara zipatazo 350.

Hatua nyingine kubwa ilifikiwa 1815 mwanafizikia Mfaransa Augustin-Jean Fresnel alipobuni lenzi ya aina ya Fresnel iliyo bora zaidi iliyopata kutumiwa kwenye minara ya taa. Kabla ya ubuni wa Fresnel, mifumo ya vioo iliyo bora zaidi—ikitumia taa za aina ya Argand, zilizobaki kuwa maarufu kwa zaidi ya miaka 100—ilitokeza nguvu za nuru inayotoshana na ya mishumaa 20,000.a Lenzi za aina ya Fresnel ziliziongeza nuru hii kufikia 80,000—karibu kiwango kinachotoshana na nguvu za taa za mbele za gari la kisasa—zikitimiza hilo kwa kutumia utambi mmoja tu wenye moto! Stovu za kutumia mafuta zenye kudhibiti kanieneo zilibuniwa mwaka wa 1901, na punde baadaye vipimo vya Fresnel vikaanza kutokeza nguvu za nuru inayotoshana na ya mishumaa ipatayo milioni moja. Karibu na wakati huo, gesi ya asetilini ikaanza kutumiwa nayo ikawa na uvutano mkubwa sana juu ya utendaji na ufundi uliohusu minara ya taa, na hiyo ilitokezwa hasa na Nils Gustaf Dalén wa Sweden. Vali ya jua yenye kujitendesha yenyewe ambayo ilitengenezwa na Dalén ilifanya atunukiwe Tuzo la Nobeli la Fizikia mwaka wa 1912. Hiyo vali yake ilikuwa swichi iliyojiwasha na kujizima kulingana na hali ya jua nayo ilidhibiti gesi ya asetilini. Taa za umeme zikaja kupendwa katika miaka ya 1920 na bado zingali zinatumiwa sana leo. Taa hizo zikiunganishwa na lenzi za Fresnel, balbu yenye wati 250 tu yaweza kutokeza nuru inayotoshana na mamia ya maelfu ya nuru za mishumaa. Siku hizi, mnara wa taa wenye nguvu zaidi ulimwenguni ni ule ulioko Ufaransa, uwezao kuangaza anga la usiku kwa mmweko wenye nguvu za nuru unaotoshana na mishumaa milioni 500.

Ubuni wa karibuni ni ule mmweko wa taa yenye umbo la neli inayotumia gesi ya zenoni. Hiyo hutokeza mmweko mwangavu unaodumu muda mfupi sana. Kwa kuwa mpwito wa nuru ni mfupi sana na wenye nguvu, unajitokeza zaidi unapokuwa pamoja na namna nyingine za nuru.

Minara ya Taa Inayoelea

Minara ya taa inayoelea, au meli zenye taa za kuongozea meli nyingine, zilitumiwa mahali minara haingeweza kujengwa. Hata hivyo, sawa na minara, meli zenye taa za kuongozea meli nyingine zina historia ndefu. Ya kwanza ilikuwa jahazi la Kiroma lililotumika katika kipindi cha utawala wa Kaisari Yulio. Kikiwa kimetundikwa juu sana kwenye mlingoti, kinara cha chuma cha makaa yenye moto kiliangaza anga la usiku—kikiwaangushia majivu yenye moto watumwa wenye kutokwa jasho wa kupiga makasia waliofungiwa vituoni mwao vilivyo chini.

Meli ya kwanza iliyofuata yenye taa za kuongozea meli nyingine ilianza kutumiwa mwaka wa 1732 katika mlango wa mto Thames, karibu na London. Baadaye, idadi ya meli zenye taa za kuongozea meli nyingine iliongezeka. Kwa miaka mingi meli zilizoingia na kutoka Bandari ya New York ziliongozwa na meli iliyoitwa Ambrose iliyokuwa na taa. Hata hivyo, miaka ya karibuni, boya za taa za kujiendesha zenyewe na minara ya taa iliyojengwa kwa vyuma ifananayo na visima vya mafuta ufuoni, imechukua mahali pa meli zenye taa za kuongozea meli nyingine.

Ukungu na Dhoruba Vifunikapo Taa

Hata taa zilizo na nguvu sana hutatizwa kunapokuwa na ukungu mzito na mvua—wakati minara ya taa ihitajikapo zaidi ya wakati mwingineo! Hata hivyo, utatuzi ujapokuwa wenye kasoro, ni sauti—sauti kubwa sana na ya kawaida. Kwa sababu hii, minara ya taa nyingi ina vifaa vya kutokeza sauti kubwa kama vile kengele, pembe za kutangaza hatari ya ukungu, ving’ora, na kwa muda fulani, hata mizinga! Kwa hakika, hata katika miaka ya karibuni ya 1970, minara ya taa fulani ilitumia mizinga.

Hata hivyo, mawimbi ya sauti huelekea kuathiriwa sana na hali zisizo za kawaida za angahewa. Tofauti za halijoto na unyevu katika safu za hewa iliyo juu ya maji zaweza kuiathiri sauti, mara nyingine zikiipeleka juu, na mara nyingi chini. Kwa kuongezea, kama tu vile kijiwe cha mviringo kiwezavyo kudundishwa katika kidimbwi, ndivyo mlipuko wa sauti uwezavyo kudunda na kupaa juu ya meli bila hata kusikika! Mbali na matatizo hayo, ishara za vifaa vya kutokeza sauti kwa kawaida vyaweza kusikika umbali wa kilometa kadhaa.

Mwisho wa Muhula

Kadiri mitambo ya kuendesha minara ya taa ilivyozidi kuja, walinzi wa minara ya taa hawakuhitajika tena. Rada, radio, sona, na safari ya baharini ya kutumia setilaiti sasa hata zimechukua mahali pa minara ya taa yenyewe, na nyingi imeacha kutumiwa. Lakini hatuelekei kuisahau. Kwa watu wengi, minara ya taa ni ishara ya nuru na tumaini katika ulimwengu wenye giza, na zingali zawachochea wapiga-picha, wasanii, na washairi vilevile. Katika jitihada za kudumisha majengo haya maridadi ya kizamani, mashirika ya kudumisha minara ya taa yamejitokeza duniani kote.

Minara ya taa fulani sasa ina makao kwa wageni wenye nia ya kujaribu maisha ya kuwa mlinzi wa mnara wa taa, yajapokuwa ni ya kudekezwa tu. Wageni wengine hutaka tu kufurahia hali ya faragha—wasisikie chochote ila vilio pweke vya shakwe na ngurumo za mawimbi. Katika sehemu fulani za ulimwengu, minara ya taa pia huandaa mahali pafaapo pa kuwatazama nyangumi, ndege, na sili. Yaelekea walinzi nyumbani mwa Aleksandria na mjomba wa Christopher Columbus huko Genoa walitumia muda wao usio na shughuli wakifanya mambo yaleyale.

[Maelezo ya Chini]

a Sasa mahali pake pakiwa pamechukuliwa na kipimo cha nuru kinachoitwa candela. Awali, kipimo hiki cha kimataifa, kinachopimwa kwa nguvu za nuru inayotoshana na ya mishumaa, ndicho kilichokuwa mng’ao wa nuru wenye nguvu nyingi kuelekea upande wowote kwa kulinganishwa na kiwango cha nuru ya mshumaa wa kawaida.

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

Wanawake Wawili Wajasiri

Ile hadithi juu ya minara ya taa hutia ndani masimulizi ya ujasiri na ujitoaji usio na kifani, mara nyingi inapohusu wanawake. Grace Darling (1815-1842) alihatarisha maisha yake ili kuokoa manusura tisa wa meli iliyovunjika karibu na mnara wa taa wa baba yake katika Visiwa vya Farne, nje kidogo ya pwani ya kaskazini-mashariki ya Uingereza. Baada ya kisisitiza, yeye na baba yake walipiga makasia kupitia bahari yenye hatari hadi ilipokuwa meli hiyo iliyovunjika, wakawaweka manusura kwenye mashua, wakapiga makasia kurudi kwenye mnara wa taa, na kuwatunza hadi msaada ulipopatikana. Nguzo ya ukumbusho imejengwa kwa ajili ya kumkumbuka.

Abigail Burgess alikuwa binti mwenye miaka 17 wa mlinzi wa mnara wa taa wa Matinicus Rock, nje kidogo ya pwani ya Maine katika Amerika Kaskazini. Siku moja katika Januari 1857, baba yake aliuacha mnara wa taa lakini hakuweza kurudi kwa muda wa majuma manne kwa sababu ya halihewa mbaya. Abbie, kama alivyoitwa, aliutunza huo mnara wa taa. Pia alimtunza mama yake aliyekuwa mgonjwa na kuwaangalia ndugu na dada zake waliokuwa wachanga mno wasiweze kusaidia katika wajibu wa mnara wa taa. Abbie aandika hivi: “Ijapokuwa nyakati fulani nilichoka sana kutokana na kazi zangu za jasho [kabla ya nguvu za umeme kuja, ilikuwa kazi ngumu sana kudumisha nuru], hatukukosa nuru hata mara moja. Kwa utegemezo wa Mungu, niliweza kutimiza wajibu wangu wote niliouzoea kutia na ule wa baba yangu.” Majira ya baridi kali yaliyofuata, Abbie kwa mara nyingine tena alihitaji kusimamia mambo. Wakati huu yeye na familia yake walipewa posho la yai moja na kikombe kimoja tu cha uji wa mahindi. Lakini taa haikuzimika kamwe.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Lenzi ya Fresnel

Lenzi ya Fresnel hasa ni mchanganyiko wa lenzi, au paneli ya lenzi, yenye lenzi ya katikati iliyozungukwa na miche ya kioo iliyojipinda. Paneli za lenzi za Fresnel zaweza kuunganishwa ili kufanyiza mwanzi uzungukao kabisa chanzo cha nuru. Kila paneli hufanyiza nuru kuwa mwali wa mwanga wa mlalo. Paneli zaidi hutokeza miali zaidi ya mwanga, zifananazo na tindi kutoka kwenye kitovu cha gurudumu. Kadiri mwanzi uzungukavyo chanzo cha nuru, ndivyo miali hii ya mwanga iangazavyo kuelekea upeo. Idadi ya miali ya mwanga, tofauti ya wakati kati ya kila mwali wa mwanga, na hata rangi zao ni mambo mengine yaupao kila mnara wa taa utambulishi wa kipekee, au kitabia. Meli hubeba orodha ya vitambulishi vya nuru mbalimbali ili mabaharia waweze kutambulisha kila mnara wa taa wanapokuwa safarini.

[Hisani]

South Street Seaport Museum

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ghuba Ndogo ya Peggy, Nova Scotia, Kanada

[Picha katika ukurasa wa 23]

Statue of Liberty, New York

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mto Weser, Ujerumani

[Picha katika ukurasa wa 23]

Jimbo la Washington, Marekani

[Picha kaitka ukurasa wa 20 zimeandaliwa na]

The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki