Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Aksidenti au Ubuni? Nimetoka tu kumaliza kusoma ule mfululizo “Tulikujaje Kuwapo? Kwa Aksidenti au kwa Ubuni?” (Mei 8, 1997) Mfululizo huo ulinipendeza kwa sababu kadhaa: (1) Usahili ambao mlilitokeza somo ambalo si rahisi kulielewa, lililo tata, la mageuzi, vilevile ule usadikisho mlioutumia kutetea maoni ya Biblia kuhusu chanzo chetu. (2) Vielezi mlivyotumia ili kupata lengo lenu lenye kusifika. Mimi ni mtafiti na mwanafunzi katika shule kubwa ya uwasiliano. Makala kama hizo huthibitisha kuwa KILA WAKATI nyinyi hufanya utafiti kwa uangalifu sana kabla ya kuzichapisha. Hakuna shaka kwamba hiyo ndiyo sababu waandamani wangu waandishi wa habari, wahariri, na watafiti wote husoma na kufurahia Amkeni! kwa ukawaida.
D. S. T., Kamerun
Kwa Nini Mgonjwa Sana? Mimi hupatwa na hisia-moyo zote zilizoelezwa na Jason katika ile makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Ninalazimika Kuwa Mgonjwa Sana?” (Aprili 22, 1997) Kila wakati ninapoisoma makala hiyo, nahisi kana kwamba nazungumza na mtu fulani anayeelewa, kuthamini, na kujali hali yangu. Asanteni sana kwa kunipunguzia mzigo wangu wenye kulemea. Najua kwamba Yehova anajali na kwa wakati wake, ataondolea mbali maradhi yote.
O. A., Ghana
Majuma mawili kabla ya makala hii kutoka nilidodoswa kuwa na shtuko la moyo. Nilikuwa tu nimefikia umri wa miaka 18, na kuwa mgonjwa kumepunguza sana uhuru wote ambao nilikuwa nimeupata karibuni. Kuna hadhari nyingi za kuchukua na dawa nyingi za kukumbukwa. Pia kumesababisha kuteseka kwingi sana kwa wazazi wangu ambao wamewapoteza watoto wengine wawili katika kifo. Makala hiyo kwa kweli ilinigusa hata nikalia. Iliyaeleza mawazo niliyokuwa nikikandamiza, na kwa jinsi fulani nikajihisi kawaida tena. Niliweza kuona kuwa kunao wengine walio na matatizo na mahangaiko sawa na yangu. Kupitia tengenezo lake, Yehova alichapisha habari ninayohitaji kuwa nayo ili niendelee kuwa mwenye nguvu kiroho.
D. S., Marekani
Nilipoisoma makala hiyo, nilitambua kwamba ugonjwa wangu huwasababishia kuteseka wazazi wangu zaidi ya mtu mwingine yeyote. Wao huniambia kuwa ugonjwa wangu ni wa kurithiwa, na hili huwashusha moyo. Ninapowaona wakiwa wameshuka moyo, mimi huwasikitikia sana.
Y. H., Japani
Nilipokuwa mtoto nilifurahia afya nzuri. Hata hivyo, tangu ubalehe nimekuwa na magonjwa mengi yakifuatana. Nilianza huduma ya wakati wote, na kwa miezi ya kwanza miwili, sikuweza kutimiza miradi yangu kwa sababu ya afya mbaya. Nilishuka moyo sana, nikifikiri (kwa makosa) kuwa nilikuwa nimefanya jambo fulani baya dhidi ya Yehova na nilikuwa nikiadhibiwa kwa ugonjwa. Makala hiyo imenisaidia kujirekebisha ifaavyo kwa hali yangu na kujipa moyo.
C. K., Ghana
Binti yangu mwenye umri wa miaka tisa ana kasoro za kujifunza na pia cerebral palsy. Yeye ni mwerevu sana na anajua kuwa kasoro zake humzuia kuwa na utendaji wa kawaida. Ujapokuwa uchangamfu wake wa kawaida, mwelekeo wake wenye furaha, mara kwa mara hili humshusha moyo kidogo. Makala hii ilikuwa yenye kutia moyo sana kwake, pamoja na mazungumzo ya jioni pamoja na baba yake kuhusu Paradiso ya wakati ujao ambapo atakuwa kama watoto wale wengine.
Y. P., Marekani
Kwa karibu miaka kumi nimekuwa niking’ang’ana na ‘ugonjwa usioonekana,’ unaoathiri mfumo wangu wa umeng’enyaji. Kwa sababu ya huo, nimelazimika kuacha huduma ya wakati wote. Kusoma makala hii, nahisi, kwa mara ya kwanza, kana kwamba mtu fulani anaelewa shindano langu. Ni kitulizo kujua kuwa siko peke yangu. Ni kana kwamba nimeondolewa mzigo mkubwa wenye kulemea. Singeweza kamwe kuwashukuru vya kutosha. Makala hizi zenye kutia moyo na za wakati wake hututia moyo twendelee katika mfumo huu wa zamani.
L. C., Kanada