Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutiwa sumu ya risasi Nimetoka tu kumaliza kusoma zile makala “Kutiwa Sumu ya Risasi—Je! Wewe na Watoto Wako Mko Hatarini?” (Novemba 22, 1992, Kiingereza) na ningependa kuwashukuru kwa makala zenu za wakati unaofaa, na zenye usawaziko. Natumaini kwamba siku moja mtaandika makala kama hiyo juu ya uhusiano wa alumini na ugonjwa wa Alzheimer.
D. C., Kanada
Suala hilo tayari lilitajwa kifupi katika makala “Uchafuzi—Nani Huusababisha?” katika toleo la Oktoba 8, 1990.—Mhariri.
Kitinda-Mimba Nina umri wa miaka 13 na mimi ndiye kitinda-mimba kati ya watoto watano. Nilithamini sana ile makala “Vijana Wanauliza . . . Kwa Nini Mimi Niwe Ndiye Kitinda-Mimba?” (Oktoba 8, 1992). Nahisi sawasawa na baadhi ya watoto mlionukuu, na natumaini makala hiyo itanufaisha familia yetu nzima. Asanteni kwa kutusaidia sisi vijana.
C. M., United States
Mimi ni mtoto wa katikati, na ninahisi mambo mengi yaliyotajwa katika makala hiyo yananihusu. Mimi pia ninahisi kuwa nalipia makosa ambayo ndugu yangu alifanya. Kizuizi changu cha wakati wa kurudi nyumbani ni karibu saa tatu kwa sababu yake. Dada yangu na mimi tunashiriki chumba, na sina usiri wowote. Na bado ninafurahi kuwa mtoto wa katikati, nikiwa na ndugu mkubwa wa kunifundisha na dada mdogo ambaye naweza kumfundisha. Kwa kweli huwa siko peke yangu. Kwa hiyo asanteni kwa kuandika makala kama hiyo; mimi si kitinda-mimba lakini nilinufaika nayo.
N. R., United States
Mikono Nilipokuwa nikisoma makala “Mikono Yetu ya Ajabu” (Agosti 8, 1992, Kiingereza), Nisingejizuia kutazama mikono yangu. Sikuwa nimepata kufikiria jinsi vyombo hivi tulivyopewa na Yehova vilivyo ajabu. Wengine wanaweza kuaminije kwamba wanadamu walitokana na mageuzi? Ninaamini wengi watabadili mawazo yao wakisoma makala hiyo.
E. M., Brazil
Pafu la Chuma Ninawaandikia macho yangu yakijaa machozi baada ya kusoma masimulizi ya Laurel Nisbet, “Hata Pafu la Chuma Halikumzuia Kuhubiri.” (Januari 22, 1993) Imani yake ni mfano mzuri kwa sisi sote. Iligusa moyo kusoma jinsi alivyoweza kutumia hali yake kusaidia watu kadhaa kupata kumjua Yehova. Pia alikuwa ameazimia asikiuke utakatifu wa damu na akatumia nguvu zake zote kueleza msimamo wake kwa daktari wake, hata alipokuwa mahututi. Nawashukuru kwa moyo wangu wote kwa kuchapa ono lake.
Y. C., Italia
Wazazi Wanaochambua Makala za “Vijana Wanauliza . . .” za “Kwa Nini Chochote Ninachofanya Si Kizuri Sana?” (Novemba 22, 1992, Kiingereza) na “Naweza Kukabilianaje na Uchambuzi wa Wazazi?” (Desemba 8, 1992, Kiingereza) zilikuja kwa wakati unaofaa kabisa. Nilihisi nimeshuka moyo kwa sababu baba yangu kila wakati alikuwa na jambo la kunung’unikia. Sasa nitajaribu kufanya bidii sana ili nipokee uchambuzi kwa njia ya utulivu zaidi na kutokuwa na moyo mgumu wa kuupokea.
M. Z., Italia
Makala hizo zilinihusu moja kwa moja. Sikuzote nimekuwa nikiamini kwamba wazazi wangu walinichambua kwa sababu nisingeweza kufanya chochote kwa njia inayofaa. Makala yenu ilinisaidia kuona kwamba nidhamu yao ni tokeo la upendo wao na wanatutaka tufaulu. Tangu nisome makala yenu, wazazi wangu hawajapata mambo ya kunung’unikia sana.
S. P. United States
Mama yangu si Mkristo, na hakuna chochote ambacho nimefanya ambacho kimepata kumridhisha. Lakini makala hiyo ilisaidia nimwelewe vizuri zaidi. Tokeo la jitihada yangu limekuwa nini? Sasa yeye husikiliza na amekuja kuamini ninayomwambia kutoka Neno la Mungu!
M. T., Ufilipino