Kutoka kwa Wasomaji
Kutiwa Sumu ya Risasi Asanteni sana kwa makala juu ya kutiwa sumu ya risasi. (Novemba 22, 1992, Kiingereza) Kutaja kwenu msongo wa juu wa damu, magonjwa ya figo, maumivu ya tumbo, na kutapika—matatizo ambayo yamenisumbua kwa miaka mingi—kulinifanya niende nikapimwe kwa uwezekano wa kutiwa sumu ya risasi. Matokeo yalionyesha kuwapo kwa risasi nyingi kupita kiasi mwilini. Ninatumaini kwamba utabibu ninaopokea wakati huu utafaulu.
T. W., Ujerumani
Ni dhahiri kwamba mnafanya utafiti sana kwa ajili ya makala zenu. Ninafanya kazi katika taasisi moja ya utafiti katika Idara ya Rangi za Asili. Katika nchi yetu, rangi zenye risasi zilitumiwa kwa miaka mingi kwa sababu ya kustahimili kwazo mmomonyoko. Sasa hazitakikani kabisa kutumiwa, lakini kama mlivyoandika, hatari ya sumu ya risasi ingali iko. Makala hiyo ilinisaidia kuwaonyesha wafanyakazi wenzangu kwamba Amkeni! halijibu tu maswali ya kidini bali pia linasaidia watu kutatua matatizo yao hata kama wao si waamini. Asanteni sana.
A. A., Jamhuri ya Cheki
Pafu la Chuma Ni lazima nieleze uthamini wangu wa kina kirefu kwa ajili ya ono la Laurel Nisbet yenye kichwa “Hata pafu la chuma Halikumzuia Kuhubiri.” (Januari 22, 1993) Ni mfano mzuri kama nini wa ujasiri, imani, uvumilivu, na bidii! Mimi ninaugua ugonjwa wa ngozi, lakini tatizo langu halionekani kuwa kitu ninapofikiria taabu ambayo Dada Nisbet alivumilia kwa muda mrefu.
R. L. H., United States
Kwa sababu nimepooza na siwezi kutembea, nimelalamika kwamba siwezi kwenda nje kuhubiri sana. Sasa ninang’amua kwamba ikiwa mwanamke huyo aliyeishi ndani ya pafu la chuma kwa miaka 37, aliweza kuhubiri na kufanya wanafunzi, basi mimi pia ninaweza kuridhika na yale ninayoweza kufanya.
M. L., Italia
Tunathamini maelezo kama hayo. Bila shaka, mfano wenye uaminifu wa Dada Nisbet haupunguzi kwa njia yoyote ile jitihada ambayo wengi wetu wanayo na matatizo mengine mazito ambayo labda hayaonekani kuwa yanadhoofisha lakini bado ni chanzo cha taabu nyingi.—Mhariri.
Mkate Asanteni sana kwa makala yenu “Mkate Wetu wa Kila Siku.” (Desemba 8, 1992, Kiingereza) Nilijaribu mapishi yenu ya kutengeneza mkate, na nilishangaa kwa jinsi ilivyokuwa rahisi kutengeneza mkate na jinsi mkate huo ulivyokuwa mtamu.
M. M., United States
Nina vitabu kadhaa vya mapishi kwenye rafu, lakini mapishi yote kwenye vitabu hivyo hayana matokeo mazuri kama mapishi yenu. Asanteni sana!
S. H., Ujerumani
Mnyanyaso wa Nazi Nilitiwa moyo sana na makala “Wanazi Hawangeweza Kutuzuia!” iliyoandikwa na Erwin Klose. (Novemba 22, 1992, Kiingereza) Yakiwa tofauti na maono mengine juu ya Wanazi ambayo yamesimuliwa kufikia wakati huu, masimulizi ya Erwin Klose yalielezwa kwa njia ya ucheshi. Nyakati nyingine nilikuwa ninaangua kicheko! Nilitiwa moyo kwa uchangamfu wake na njia yake inayofaa ya kuangalia mambo.
T. K., Japani
Mikusanyiko ya Urusi Ninataka sana kuwashukuru kwa makala “Mkusanyiko wa Kimataifa wa Kwanza wa Mashahidi wa Yehova Katika Urusi.” (Desemba 22, 1992, Kiingereza) Ingawa mimi ni mtumishi wa muda mrefu wa Yehova Mungu, ni lazima nitaje kwamba uthamini wangu kwa maandalizi ya Mungu hauwezi kulinganishwa na wa wale Wakristo katika Urusi! Uso wa dada huyo alipopokea nakala yake binafsi ya kwanza ya Biblia ilinifanya ning’amue jinsi nilivyo na vitu vingi—na kuvipuuza tu. Makala hiyo ilinisaidia nione maeneo ambayo ninahitaji kurekebisha.
B. T. A., United States