Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 3/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Usomaji wa Biblia Huleta Manufaa
  • Kile Ambacho Watoto Wachanga Husikia
  • Mchwa wa Ajabu
  • Wawili Ni Bora Kuliko Mmoja
  • Utunzaji wa Sauti
  • Kufuatia Halihewa ya Tibet
  • Mahali Palipokuwa na Serikali ya Roma Pafukuliwa Katika Israeli
  • Mchwa Watumika Kuwa Dawa
  • “Ugonjwa wa Ofisini”
  • Wasomaji Wachanga wa Brazili
  • Watu wa Punjab na Vijiwe Katika Figo
  • Tule Muhogo!
    Amkeni!—1993
  • Majani ya Muhogo—Chakula cha Kila Siku cha Mamilioni
    Amkeni!—1996
  • Buibui Anayejifanya Kuwa Chungu
    Amkeni!—2002
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 3/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Usomaji wa Biblia Huleta Manufaa

Wamarekani wanaosoma Biblia angalau mara moja kwa juma huhisi wakiwa na furaha zaidi na uradhi na kupata kusudi zaidi maishani kuliko wale wanaosoma Biblia mara chache zaidi, kulingana na uchunguzi ulioripotiwa na shirika la habari la Associated Press. Katika ukaguzi uliofanywa bila taratibu maalumu wa watu wazima Wamarekani, na Market Facts, Inc., ya Illinois, karibu asilimia 90 ya wanaosoma Biblia mara nyingi walisema kwamba wanahisi amani ya akili wakati wote au karibu wakati wote, wakilinganishwa na asilimia 58 ya wale wanaoisoma Biblia chini ya mara moja kwa mwezi. Zaidi, asilimia 15 ya wasomaji wa Biblia wa kawaida walisema kwamba wana wasiwasi kuhusu kukubaliwa na wengine, wakilinganishwa na asilimia 28 ya wasomaji wasio wa kawaida. Asilimia 12 tu ya wanaoisoma mara nyingi walisema kwamba huwa na wasiwasi kuhusu kifo nyakati nyingine au huwa na wasiwasi sana, wakilinganishwa na asilimia 22 ya wanaoisoma mara chache.

Kile Ambacho Watoto Wachanga Husikia

Utafiti wa juzijuzi unathibitisha kwamba kiasi na namna ya sauti ya maneno ambayo kitoto kichanga husikia huathiri uwezo wacho wa kufikiri kimantiki, kutatua matatizo, na kusababu kinadharia, laripoti gazeti The New York Times. Uchunguzi katika Chuo Kikuu cha Iowa ulipata kwamba watoto wa wazazi ambao ni weledi walisikia wastani wa maneno 2,100 kila saa moja, huku wale wenye wazazi wafanyao kazi walisikia maneno 1,200 na wale wenye wazazi wanaotoa huduma za jamii, walisikia maneno 600 tu. Namna ya sauti ya wazazi—yenye kutia moyo, kukemea, changamfu, au ya kuamuru—ilijulikana pia. Uchunguzi wa miaka miwili na nusu ulionyesha kwamba kiasi cha maneno vilevile namna ya sauti mtoto husikia “kilikuwa na tokeo lenye kina katika uwezo wa kufikiri kiakili wa mtoto alipofikia umri wa miaka 4.” Mmoja wa watafiti, Dakt. Betty Hart, alisema kwamba miaka mitatu ya kwanza ni ya kipekee katika maisha ya wanadamu kwa sababu vitoto vichanga hutegemea kabisa watu wazima kwa ajili ya malezi yao yote na lugha.

Mchwa wa Ajabu

Mhogo ni chakula kikuu kwa watu milioni 200 hivi katika Afrika. Na sasa, kwa msaada wa mchwa mdogo mwindaji anayeitwa Typhlodromalus aripo, kuna mihogo mingi ya kutosheleza mahitaji. Kulingana na gazeti New Scientist, yule mchwa T. aripo aliingizwa kutoka Brazili kupigana na moja ya wadudu waharibifu zaidi wa mihogo ulimwenguni green spider mite, ambaye alihusika katika kuharibu thuluthi moja ya zao fulani la mhogo wa Afrika. Watafiti waligundua kwamba kaskazini-mashariki ya Brazili, ambapo pana mihogo mingi, kuna matatizo machache yanayosababishwa na green spider mite. Ilionekana kwamba mchwa wawindaji, T. aripo, huketi kwenye ncha ya mmea ili green spider mite watokee na kisha kuwala. T. aripo hawaui asilimia 90 tu ya green spider mite, lasema gazeti hilo, bali husaidia wakulima pia waepuke matumizi ya viuawadudu, ambavyo wengi hawawezi kuvigharimia.

Wawili Ni Bora Kuliko Mmoja

Watu hupata mafanikio zaidi wajaribupo kujitwalia mtindo-maisha wenye afya wanapokuwa na mwenzi anayefanya vilevile, kulingana na gazeti la Uingereza New Scientist. Huu ni umalizio ulioletwa na ukaguzi wa wenzi 1,204, ulioripotiwa kwenye Archives of Family Medicine. Asema Stephen Pyke, wa Shule ya London ya Usafi wa Kiafya na Madawa ya Tropiki: “Watu huelekea zaidi kuacha kuvuta sigareti, kupunguza kolesteroli yao na kupunguza uzito ikiwa wenzi wote wawili wanafuata shauri.”

Utunzaji wa Sauti

Yeyote ambaye anatumia sauti yake sana, kama vile mwalimu, yuko katika hatari ya kuikaza na kuipoteza sauti yake, laripoti gazeti la habari The Toronto Star. Hali kadhalika, kupiga makelele daima ili kusikiwa katika mazingira yenye makelele kwaweza kuharibu vitunga milio. Mnong’onezo na zoea la kuondoa makohozi pia huharibu sauti yako, asema mtaalamu wa usemi na lugha, Bonnie Mann. Ashauri kutongojea mpaka tatizo linapokuwa zito kabla ya kuchukua hatua na atia moyo mkao mzuri ili kulegeza mkazo katika shingo na mabega. Aongezea: “Zaidi ya yote, ni jambo la maana, kulowesha koo yako daima.” Ikiwa utahitaji kutumia sauti yako sana, Mann apendekeza kunywa maji kidogo-kidogo siku yote.

Kufuatia Halihewa ya Tibet

Nchi kumi katika eneo la Asia-Pasifiki zimepanga majaribio ya kuchunguza monsuni, laripoti gazeti New Scientist. Kilimo katika maeneo makubwa ya Asia kinategemea mvua zinazoletwa na monsuni, lakini mvua hizi hutofautiana kila mwaka. Wanametorolojia wanaamini kwamba uwanda wa juu wa Tibet ni kisababishi kikuu cha mvua ya monsuni, lakini data kutoka Tibet hazijapatikana kwa ajili ya mchanganuo. Baada ya maafikiano na China, chombo kisicho na rubani kinasimamishwa katika Tibet ili kufuatilia halijoto, unyevuanga, upepo, na vipengele vingine vya halihewa ya Himalaya. Watafiti wanatumaini ya kwamba data itakayopatikana itachangia uelewevu bora wa halihewa ya monsuni za Asia.

Mahali Palipokuwa na Serikali ya Roma Pafukuliwa Katika Israeli

Wanaakiolojia katika Israeli wamefukua jengo lenye sehemu nyingi la serikali ya Roma katika Kaisaria ambalo huenda lilikuwa ikulu ya praetori ambapo mtume Paulo alitiwa gerezani, yasema ripoti ya Reuters. Yosef Porath, mkuu wa Mamlaka ya Mambo ya Kale ya Israeli yenye kutenda katika Kaisaria, alisema kwamba wanaakiolojia katika mahali hapo walikuwa wamefukua usanii wa mozeiki wenye mchoro wa Kilatini ulioonyesha kwamba ofisi moja pale huenda ilitumika kuwa ofisi kwa ajili ya usalama wa ndani. “Mwandiko huu husaidia kutatua tatizo la mahali ambapo kesi ya Mtk. Paulo ilisikizwa mbele ya gavana Mroma anayefafanuliwa katika Agano Jipya,” akasema Porath. Alisema kwamba mahali hapo ndipo palipokuwa kitovu cha mamlaka pekee ya serikali ya Roma ambayo bado imefukuliwa katika Israeli na moja ya chache katika jamii ya Roma ya kale.

Mchwa Watumika Kuwa Dawa

Wakati wa vita katika 1947, daktari-mpasuaji wa kijeshi Mchina Wu Zhicheng alihitaji kuzuia ambukizo kwa wanajeshi waliojeruhiwa, lakini ugavi wake wa madawa ulimalizika kabisa. Alipokaribia kukata tumaini, alitafuta msaada wa daktari wa mahali hapo, ambaye aliagiza dawa ya kidesturi ya Kichina—maji yaliyochemshwa na mchwa ya kusafishia majeraha na dawa iliyotengenezwa kwa aina za pekee za mchwa. Kulingana na China Today, matokeo yalikuwa yenye kutia moyo hivi kwamba Dkt. Wu akaanza kazi-maisha ya muda mrefu ya kufanyia utafiti matumizi ya dawa ya mchwa. Anaamini kwamba madawa ya mchwa husaidia kusawazisha mfumo wa kinga na kusema: “Mchwa ni nyumba ndogo ya kuwekea akiba ya lishe. Ina zaidi ya virutubishi 50 vinavyohitajiwa na mwili wa kibinadamu, amino asidi 28 na madini ya namna mbalimbali na misombo ya kemikali.”

“Ugonjwa wa Ofisini”

Zaidi ya asilimia 80 ya Waitalia hupatwa na matatizo ya mkao kwa sababu ya mtindo-maisha wa kukaa kitako kulingana na uchunguzi uliofanywa na Profesa Maurizio Ricciardi, mkurugenzi wa kitivo cha mkao cha Chuo Kikuu cha Siena. Zaidi ya nusu ya watu hawa wenye kuteseka kutokana na “ugonjwa wa ofisini” pia hulalamika kuwa na maumivu ya mgongo, kuumwa na kichwa, kichefuchefu, kizunguzungu na masumbufu ya usawaziko wa kimwili, kupanda na kushuka kwa mpigo wa damu, kuharisha, hali ya kufunga choo, uvimbe wa utumbo mpana, na uvimbe wa tumbo, laripoti gazeti la habari Il Messaggero. “Baada ya kila saa moja ya kazi, Wajapani na Wachina hufanya mazoezi sahili” ili kupigana na matatizo haya, asema Ricciardi, “huku kwa upande wetu, pumziko pekee huwa ni la kahawa.”

Wasomaji Wachanga wa Brazili

Kujua kusoma na kuandika na idadi ya miaka ambayo wanafunzi wanatumia shuleni inaendelea kuongezeka katika Brazili, lataarifu gazeti Exame. Ijapokuwa kuna mengi ya kufanyiwa maendeleo, kati ya mwaka wa 1991 na 1995, kulikuwa na upungufu wa asilimia 36 ya wasiojua kusoma na kuandika kati ya kikundi cha miaka 7 hadi 14, kulingana na Taasisi ya Jiografia na Takwimu ya Brazili. Wastani wa idadi ya miaka iliyotumiwa shuleni uliongezeka kwa asilimia 10 kati ya 1990 na 1995. Upendezi unaokua wa kusoma miongoni mwa vijana wa Brazili waweza kudhihirishwa na ongezeko la karibu asilimia 40 la wanafunzi ambao walihudhuria maonyesho ya vitabu ya juzijuzi katika Rio de Janeiro. Vitabu vilivyouzwa sana kwenye maonyesho hayo—ikiwa ni asilimia 24 ya mauzo yote—vilikuwa ni vitabu vilivyoandikwa kwa ajili ya vijana, laripoti gazeti la habari O Estado de S. Paulo.

Watu wa Punjab na Vijiwe Katika Figo

Watu kutoka jimbo la Punjab na maeneo yanayozingira ya India wanaelekea zaidi kupata vijiwe katika figo kuliko jumuiya yoyote ulimwenguni, laripoti India Today International. Watu wa Punjab wanajulikana kwa kufanya kazi kwa bidii na kula kwa kufurahia, lakini mara nyingi hawanywi maji ya kutosha wakati wa miezi ya kiangazi chenye kuunguza sana, yasema ripoti hiyo. Kwa sababu hii, eneo lao lilifafanuliwa kuwa “ukanda au eneo la vijiwe vya figo” ulimwenguni kwenye mkutano wa kimataifa wa hivi majuzi uliohusu mfumo wa mkojo. Wastani wa saizi ya kijiwe cha figo huko ni kati ya sentimeta mbili na tatu [karibu inchi moja], ikilinganishwa na sentimeta moja [inayopungua nusu inchi] katika Ulaya na Marekani. Ripoti hiyo inaonelea haya ni matokeo yanayoletwa na zoea la Wahindi la kupuuza maumivu madogo au kuahirisha matibabu. Matabibu wa mfumo wa mkojo wanasema watu wenye afya nzuri wanapaswa kunywa angalau visaga viwili vya maji safi kila siku.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki