Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Vitumbuizo Vifaavyo Ninajifunza niwe mmoja wa Mashahidi wa Yehova, na ningependa kuwashukuru kwa kuchapisha mfululizo “Kutafuta Vitumbuizo Vifaavyo.” (Mei 22, 1997) Kuna vipindi vifaavyo vichache sana vya kutazama katika televisheni, na mlitupatia sote—vijana kwa wazee—shauri zuri sana. Natumaini mtaendelea kutupa habari juu ya masuala kama hili.
D. W., Marekani
Je, Mungu Ataendelea Kuwa Rafiki Yangu? Ninamshukuru sana Muumba wetu mwenye fadhili kwa ajili ya makala bora sana “Vijana Huuliza . . . Je, Mungu Ataendelea Kuwa Rafiki Yangu?” (Mei 22, 1997) Si kitambo sana, nilijaza orodha ya maswali kuhusu ni marafiki wangapi ningeweza kuwa nao, na matokeo ya mwisho yalinihakikishia kwamba sikuzote ningezingirwa na marafiki. Kwa kusikitisha, hakikisho hili limethibitika kuwa si la kweli kabisa. Bado, ninang’amua kwamba Yehova Mungu pekee ndiye Rafiki yetu aliye bora zaidi. Ni kweli kwamba ikiwa sisi si marafiki wa Yehova Mungu, basi kila kitu kingine hukosa kusudi.
A. T. M., Mexico
Asanteni kwa upendezi mnaoonyesha kuelekea vijana. Nilipokea makala “Vijana Huuliza . . . Je, Mungu Ataendelea Kuwa Rafiki Yangu?” wakati tu nilipoihitaji zaidi. Nilikuwa nimetengwa na ushirika na nilirudishwa hivi karibuni. Nyakati nyingine nimehisi kuwa mpweke na kuvumilia mashaka mengi—mojawapo ilikuwa, Je, Mungu Hunisikiliza? Baada ya kuchanganua kielelezo cha Paulo chini ya kichwa kidogo “Mwiba Katika Mwili,” niliamua kutafuta baraka kutoka kwa Yehova kupitia funzo la Biblia la kawaida na sala yenye kueleza mambo wazi. Swali moja, Je, Yehova ataendelea kuwa rafiki yangu? limejibiwa waziwazi.
J. C. A., Argentina
Ufugaji wa Nyuki Ninaandika kuhusu ile makala “Ufugaji wa Nyuki—Hadithi ‘Tamu’” (Mei 22, 1997), ambayo mnatoa habari kwa ufupi iliyo sahihi kuhusu nyuki. Nilipendezwa na michanganyiko iliyofaa ya maelezo, picha, na maoni—bila makosa yoyote. Mara nyingi mfugaji wa nyuki hutambua habari isiyo sahihi kabisa au kwa sehemu katika vyombo vya habari, lakini hana habari ya namna hiyo hata moja katika makala yenu. Mimi ni mfugaji wa nyuki mwenye idili, na mara nyingi huona ‘busara’ katika wadudu hawa kuliko kwa watu wengi. Kwa hiyo ninafikiri inafaa kusema kwamba katika kushughulika na habari hii, mlitukuza uzuri wa uhai, hasa kama unavyokaziwa katika viumbe wa namna hiyo wadogo.
P. G. M., Italia
Utunzaji Asanteni kwa kuchapisha ule mfululizo “Utunzaji—Kukabili Huo Ugumu.” (Februari 8, 1997) Mama yangu ni mgonjwa wa kansa, na kumtunza katika pindi za mwisho za ugonjwa wake kumenimaliza kabisa. Makala hiyo ilifafanua kwa usahihi hisia za mmoja ambaye ni mtunzaji na kuonyesha wengine jinsi wanavyoweza kuonyesha ufikirio kwa wengine wetu walio katika hali hiyo. Ni mara chache mtu hupata makala kama hizo.
F. T., Taiwan
Vijana Huuliza . . . Nina umri wa miaka 12. Ninaenda shule na huonea shangwe sana kusoma makala zenu. Kabla sijaanza kuzisoma, lilikuwa jambo gumu kwangu kushirikiana na wale ambao walikuwa na umri mkubwa kunishinda. Lakini baada ya kusoma makala za Amkeni! kwenye sehemu “Vijana Huuliza . . . ,” limekuwa jambo rahisi zaidi kufanya hivyo. Asanteni!
N. T., Urusi
Kutoka kwa Wasomaji Wetu Nimekuwa msomaji wa kawaida wa Amkeni! kwa miaka 26, na bado mimi huthamini hilo gazeti kwa kadiri ileile kama wakati wowote. Sikosi kamwe kusoma ile sehemu “Kutoka kwa Wasomaji Wetu,” kwa kuwa mara nyingi maelezo hayo hunichochea kusoma makala tena. Asanteni kwa magazeti haya yaliyo bora kabisa.
M. B., Ufaransa