Mkazo—“Sumu Inayodhuru Polepole”
“Sikuzote sisi husikia watu wakisema, ‘Usishindwe na mkazo usije ukawa mgonjwa.’ Labda hawatambui kwamba kuna ukweli uliothibitishwa kibiolojia juu ya jambo hilo.”—Dakt. David Felten.
JILL, ambaye ni mama aliye mzazi mmoja mwenye mvulana tineja, na ambaye akaunti yake ya benki ilikuwa inapungua, na pia alikuwa na uhusiano mbaya na wazazi wake, tayari alikuwa na sababu nyingi za kuhisi mkazo sana. Kisha, kwa ghafula vipele vyenye kuwasha vikatokea katika mkono wake. Alijaribu dawa za viuavijasumu, dawa za kupaka za cortisone, na dawa za mizio, lakini hizo dawa zote hazikumsaidia. Badala yake, vipele hivyo vikaenea kotekote mwilini mwa Jill, kutia ndani uso wake. Mkazo ulikuwa ukimfadhaisha kwelikweli.
Jill alirejezewa aende kwenye kliniki inayochunguza hali ya kihisia-moyo ya wagonjwa wake. “Tunajaribu kutafuta mambo yanayoendelea katika maisha zao,” asema Dakt. Thomas Gragg, mmojawapo wa waanzilishi wa kliniki hiyo. Mara nyingi yeye hupata kwamba kwa kuongezea kuhitaji utunzaji wa kitiba, watu wenye matatizo yenye kudumu ya ngozi huhitaji msaada wa kukabili mkazo. “Ni rahisi kusema kwamba jinsi unavyohisi au kutenda husababisha maradhi ya ngozi,” akiri Dakt. Gragg. “Lakini twaweza kusema kwamba hali ya mtu ya kihisia-moyo yaweza kuchangia sana kutokea kwa matatizo ya ngozi, na hatupaswi kudumu kuandika tu dawa za kupaka za steroidi bila pia kumsaidia mtu kuondoa mkazo alio nao maishani mwake.”
Jill ahisi kwamba kujifunza kudhibiti mkazo hasa kuliokoa ngozi yake. “Bado mimi hupatwa na matatizo hayo kwa ghafula-ghafula,” yeye asema, “lakini ngozi yangu si mbaya kama ilivyokuwa awali.” Je, hicho ni kisa cha kipekee? La hasha. Madaktari wengi huamini kwamba mara nyingi mkazo huchangia matatizo kadhaa ya ngozi, kutia ndani mabaka ya ngozi, psoriasis, chunusi, na mibambuko. Lakini mkazo waweza kuathiri zaidi ya ngozi yako tu.
Mkazo na Mfumo Wako wa Kinga
Utafiti wa wakati huu waonyesha kwamba mkazo waweza kudhoofisha mfumo wako wa kinga, labda ukisababisha ushikwe na maradhi kadhaa ya kuambukiza. “Mkazo haukufanyi uwe mgonjwa,” asema mtaalamu wa virusi Ronald Glaser. “Lakini unakuongezea hatari ya kushikwa na ugonjwa kwa sababu ya kile mkazo unachofanyia kinga ya mwili wako.” Kuna uthibitisho wa kutosha unaohusianisha mkazo na mafua, homa, na malengelenge. Ingawa nyakati zote sisi huweza kupatwa na virusi kama hivyo, kwa kawaida mfumo wetu wa kinga huendelea kupigana navyo. Lakini wataalamu fulani wasema kwamba mtu anapokuwa na mfadhaiko wa kihisia-moyo, kinga hizo zaweza kushindwa.
Taratibu za kibiolojia zinazohusika bado hazijafahamika vizuri, lakini wengine husema kwamba homoni ambazo hukuchochea unapokuwa na mkazo zaweza kudhibiti utendaji wa kinga yako zinapopitia mkondo wa damu. Mara nyingi, hilo si jambo la kuhangaisha mtu, kwa kuwa homoni hizi ni za muda tu. Hata hivyo, wengine husema kwamba ikiwa mtu ana mkazo ambao unaendelea na ambao ni mkali sana, mfumo wake wa kinga waweza kudhoofika kiasi cha kwamba yeye aweza kushikwa na magonjwa kwa urahisi.
Hilo laweza kusaidia kujua sababu inayofanya madaktari wa Kanada wakadirie kwamba asilimia 50 hadi 70 ya wagonjwa wanaokuja kuona daktari huwa na malalamishi yanayohusiana na mkazo, mara nyingi walikuwa na maumivu ya kichwa, wenye ukosefu wa usingizi, wakiwa wachovu, na wenye matatizo ya tumbo. Nchini Marekani, idadi hiyo inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 75 na 90. Dakt. Jean King ahisi kwamba hatilii chumvi asemapo: “Mkazo wa daima ni kama sumu inayodhuru polepole.”
Si Kisababishi cha Pekee cha Maradhi Wala Si Tiba ya Pekee
Japo mambo ambayo yametajwa, wanasayansi hawana hakika kama mkazo pekee waweza kuathiri mfumo wa kinga kwa kiasi cha kumfanya mtu awe mgonjwa. Kwa hiyo, haiwezi kusisitizwa kwamba kila mtu ambaye ana mkazo, hata ule wa kudumu zaidi, atashikwa na maradhi. Vilevile, haiwezi kusemwa kwamba ukikosa mkazo ni lazima utakuwa na afya bora, wala si jambo la hekima kukataa kutibiwa kwa kuamini wazo lisilo la kweli kwamba ugonjwa utapotea ikiwa wewe una matazamio mazuri na maoni chanya. Dakt. Daniel Goleman atahadharisha hivi: “Tokeo la kuwa na wazo lionekanalo kuwa lenye kuvutia la kwamba mtazamo wa mtu waweza kutibu ugonjwa wowote limesababisha mvurugo na kuchanganyikiwa ambako kumeenea sana kuhusu kadiri ambavyo ugonjwa waweza kuathiri akili, na, labda kwa ubaya zaidi, jinsi nyakati nyingine inavyofanya watu wahisi kuwa na hatia kwa kuwa wana maradhi, kana kwamba kuwa na maradhi ni ishara ya ukosefu fulani wa adili au kutofaa kiroho.”
Kwa hiyo, ni lazima itambulike kwamba kisababishi cha ugonjwa mara nyingi hakiwezi kuonwa kuwa jambo moja tu. Lakini, bado uhusiano uliopo kati ya mkazo na ugonjwa wakazia hekima ya kujifunza jinsi ya kuondoa “sumu inayodhuru polepole” wakati wowote iwezekanapo.
Kabla ya kufikiria jinsi ambavyo hilo laweza kufanywa, ebu tuchunguze kwa makini zaidi hali ya mkazo na jinsi unavyoweza kukunufaisha katika visa fulani.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Magonjwa Fulani Ambayo Yamehusianishwa na Mkazo
• mizio
• yabisi-kavu
• ugonjwa wa pumu
• maumivu ya mgongo, shingo, na mabega
• mafua
• mshuko wa moyo
• kuhara
• homa
• matatizo ya tumbo
• maumivu ya kichwa
• matatizo ya moyo
• ukosefu wa usingizi
• maumivu ya kichwa ya kipandauso
• vidonda vya tumbo
• matatizo katika kufanya ngono
• matatizo ya ngozi
[Picha katika ukurasa wa 6]
Asilimia kubwa ya wagonjwa wanaoona madaktari huwa na mkazo