Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 3/22 kur. 23-25
  • Niliokoka Anguko la Ndege Nambari 801

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Niliokoka Anguko la Ndege Nambari 801
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Anguko na Mandhari ya Baadaye
  • Kutiwa Wasiwasi na Miali
  • Hatimaye Twaokolewa!
  • Hatimaye, Namwona Mke Wangu!
  • Kuweka Mambo ya Kutangulizwa Kwanza
  • Hofu Kuu Katika Ndege Nambari 811
    Amkeni!—1990
  • Kutua Ghafula!
    Amkeni!—2004
  • Ndege Ni Salama Kadiri Gani?
    Amkeni!—1999
  • Mawaidha Kutoka kwa Rubani Stadi
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 3/22 kur. 23-25

Niliokoka Anguko la Ndege Nambari 801

NILITAZAMA nje kutoka kwenye dirisha tulipokuwa tukishuka ili tutue katika Guam. ‘Inashangaza,’ nilifikiri. ‘Inaonekana kuna giza jingi.’ Kweli, wakati ulikuwa umepita katikati ya usiku, na mvua nzito ilifanya isiwe rahisi kuona. Lakini nuru za kawaida na barabara zenye kung’aa za ndege kutua zilikuwa wapi? Kile ningeweza kuona ni taa hafifu kwenye sehemu ya mabawa ya ndege yetu.

Mmoja wa wafanyakazi wa ndege yetu alikuwa ametoa yale matangazo ya kawaida wakati wa matayarisho ya kutua, nikasikia vifaa vya kutua vya ndege vikijiweka katika mahali pake. Kwa ghafula, kulikuwa na kelele kubwa ndege yetu ilipokwangua ardhi. Ndege ikaanza kutingika-tingika kwa mshtuko bila kudhibitiwa, na abiria wakashikilia kwa nguvu sehemu za kuegemezea mikono na kupaaza sauti, “Ni nini kinachotendeka?”

Kufumba na kufumbua, ndege yetu aina ya Boeing 747 iligonga upande wa kilima, ikiwa imekosea uwanja wa ndege kwa kilometa tano, kwa wazi kwa sababu ya kosa la rubani wetu. Likiwa tokeo la msiba wa ndege hiyo siku ya Agosti 6, 1997, jumla ya abiria na wafanyakazi wa ndege 228 walikufa. Nilikuwa mmoja wa waokokaji 26 pekee.

Kabla ya kupanda ndege hiyo katika Seoul, Korea, mwakilishi wa shirika la ndege aliniweka katika sehemu ya daraja la kwanza, akinipa kiti kilichobakia katika daraja la kwanza. Nilifurahia sana jambo hilo hivi kwamba nilimpigia simu mke wangu, Soon Duck, ambaye alikuwa anilaki kwenye uwanja wa ndege katika Guam. Badiliko hilo la kiti lilithibitika kuwa lenye mafaa katika njia ambayo singaliweza kuwazia kamwe.

Anguko na Mandhari ya Baadaye

Kwa sababu ya kutoweza kuona vizuri, huenda wafanyakazi wa ndege hawakutambua hatari yoyote iliyokuwa inakaribia. Kila kitu kilitukia upesi sana! Dakika moja, nilikuwa nikijitayarishia hatari hiyo, na punde si punde, nilikuwa chini ardhini nje ya ndege, bado nikiwa nimebanwa katika kiti changu. Sina hakika kama nilikuwa nimepoteza fahamu zangu au la.

‘Je, hii ni ndoto?’ nilijiuliza. Wakati nilipong’amua kwamba haikuwa ndoto, mawazo yaliyonijia kwanza yalikuwa jinsi ambavyo mke wangu angepokea habari juu ya anguko. Baadaye, aliniambia kwamba hakukata tumaini kamwe. Hata alipopata kusikia mtu fulani katika uwanja wa ndege akisema kwamba ni abiria saba tu waliookoka, aliamini kuwa nilikuwa mmoja wa wale saba.

Ndege yetu ilikuwa imepasuka katika vipande vinne, ambavyo vilienea katika mandhari hiyo ya msituni na yenye mawemawe. Miili ilitapakaa kila mahali. Sehemu fulani za ndege zilikuwa zikiteketea, na nilisikia milipuko pamoja na kite na vilio vyenye kuogofya. “Nisaidieni! Nisaidieni!” sauti zilisihi. Kiti changu kilitua kwenye nyasi zenye kimo cha meta 1.8, na nikiwa katika nuru ya mioto yenye kutia hofu, ningeweza kuona kilima kilicho wima kilichokuwa karibu. Ilikuwa karibu saa 8:00 za usiku na mvua ilizidi kunyesha.

Nilipigwa bumbuazi sana hivi kwamba hata sikufikiri ningeweza kuwa nimejeruhiwa, mpaka nilipoona msichana mdogo ambaye ngozi yake ya kichwa na nywele zake zilikuwa zikining’inia kwenye kisogo chake. Mara moja niligusa kichwa changu na kupata kwamba nilikuwa nikitokwa na damu kutokana na jeraha lililokuwa juu ya jicho langu la kushoto. Nilianza kuchunguza sehemu nyingine za mwili wangu na kugundua majeraha mengi madogo-madogo. Lakini, kwa shukrani, hakuna lolote lililoonekana kuwa baya sana. Hata hivyo, nilikuwa na maumivu yenye kulemaza katika miguu yangu, yakifanya nisiweze kujongea. Yote miwili ilikuwa imevunjika.

Baadaye, nilipofika hospitali, madaktari walisema majeraha yangu yalikuwa “madogo.” Na kwa kweli yalikuwa madogo, yakilinganishwa na yale ya waokokaji wengine. Mtu mmoja alivutwa kutoka kwenye mabaki ya ndege hiyo akiwa bila miguu. Wengine walichomeka vibaya, kutia na watu watatu waliookoka anguko hilo ila tu kufa baadaye, baada ya majuma ya maumivu makali sana.

Kutiwa Wasiwasi na Miali

Badala ya kujishughulisha na majeraha yangu, nilihangaika ikiwa waokoaji wangenifikia kwa wakati. Sehemu za kati za ndege hiyo, mahali ambapo kiti changu kingekuwa, zilikuwa karibu zimebomoka kabisa. Sehemu zilizobakia zilikuwa zikiteketea, na abiria walionaswa ndani walipatwa na kifo chenye maumivu makali. Sitasahau kamwe mayowe yao ya kuomba msaada.

Kiti changu kilitua karibu na pua la ndege hiyo. Nilikuwa umbali wa urefu wa mkono kutoka kwenye mabaki ya ndege hiyo. Kwa kupeleka shingo yangu nyuma, ningeweza kuona miali. Nilihofia kuwa baada ya muda mfupi miali hiyo ingenifikia, lakini kwa shukrani haikunifikia kamwe.

Hatimaye Twaokolewa!

Dakika zilisonga polepole. Zaidi ya saa ilipita. Hatimaye, waokoaji wachache walipata sehemu ya anguko karibu saa 9:00 za usiku. Ningeweza kuwasikia wakiongea juu ya kilima, wakishangazwa na kile walichoona. Mmoja wao aliuliza kwa sauti: “Je, kuna mtu yeyote huko?”

“Nipo hapa,” nilijibu kwa sauti kubwa. “Nisaidieni!” Abiria wengine pia waliitikia. Mwokoaji mmoja alimrejezea mwingine kuwa “Ted.” Kwa hiyo nikaanza kupaza sauti, “We! Ted, niko hapa!” na, “Ted, njoo utusaidie!”

“Tunateremka chini! Ngojeni tu,” wakajibu.

Mvua iliyokuwa ikinyesha, ambayo huenda iliokoa wengi kutokana na miali, ilizuia kuja chini kwenye mteremko uliokuwa ukiteleza. Likiwa tokeo, muda mwingine mrefu ulipita kabla ya waokoaji kuwafikia waokokaji. Muda waliochukua kunipata ulionekana kuwa umilele.

“Tumekuja,” waokoaji wawili waliokuwa na tochi walisema. “Usiwe na wasiwasi.” Upesi waokoaji wengine wawili walijiunga nao, na wakiwa pamoja walijaribu kunisongeza. Wawili walinishika mikono, na wale wengine wawili wakashika miguu yangu. Kubebwa namna hiyo kulisababisha maumivu mengi, hasa kwa kuwa walikuwa wakiteleza-teleza katika matope. Baada ya kwenda kwa umbali mfupi, waliniweka chini. Mmoja wao alienda kuleta machela, kisha nikapelekwa mahali ambapo helikopta ya kijeshi ingeweza kunisafirisha kwenye ambulansi juu ya kilima.

Hatimaye, Namwona Mke Wangu!

Nilifika kwenye chumba cha dharura saa 11:30 alfajiri. Kwa sababu majeraha yangu yalikuwa mabaya, madaktari hawangeniruhusu nipige simu. Kwa hiyo mke wangu hakujua kwamba nimeokoka anguko hilo hadi saa 4:30 asubuhi, karibu muda wa saa tisa baada ya kuanguka kwa ndege. Alipashwa habari na rafiki ambaye alikuwa ameona jina langu katika orodha ya waokokaji.

Hatimaye wakati mke wangu aliporuhusiwa kuniona, karibu saa 10:00 alasiri, sikumtambua mara moja. Hisi zangu zilikuwa nzito kwa sababu ya matibabu ya kuondoa maumivu. “Asante kwa kuwa hai,” ndiyo yaliyokuwa maneno yake ya kwanza. Siyakumbuki mazungumzo hayo, lakini baadaye niliambiwa kwamba nilikuwa nimejibu: “Usinishukuru. Shukuru Yehova.”

Kuweka Mambo ya Kutangulizwa Kwanza

Nilipokuwa nikipona hospitalini, maumivu niliyohisi hayakuwa mapya kwangu. Katika mwaka wa 1987, kipindi kinachopungua mwaka mmoja baada ya kuhamia Guam kutoka Korea, nilianguka kutoka kwenye jukwaa lililokuwa kwenye orofa ya nne katika aksidenti ya ujenzi na kuvunjika miguu yote miwili. Hilo lilibadili maisha yangu. Dada yangu mkubwa, ambaye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alikuwa akinisihi nijifunze Biblia. Kipindi cha miezi sita cha kupata nafuu kiliniandalia fursa ya kufanya hivyo. Likiwa tokeo, mwaka huohuo niliweka maisha yangu wakfu kwa Yehova Mungu na kufananisha huo kwa ubatizo wa maji.

Tangu wakati wa anguko la ndege hiyo, nimekuwa nikifikiri juu ya andiko nilipendalo sana, ambalo linasema: “Basi, fulizeni kutafuta kwanza ufalme [wa Mungu] na uadilifu wake, na vitu vingine vyote hivi mtaongezewa.” (Mathayo 6:33) Nilipokuwa nikipata nafuu kutokana na anguko la ndege, nilikuwa na fursa ya kuchunguza upya maisha yangu.

Kwa njia yenye nguvu sana, anguko la Ndege Nambari 801 lilinikazia jinsi uhai ulivyo wenye thamani. Ningeuawa kwa urahisi sana! (Mhubiri 9:11) Ikawa kwamba, nilihitaji kupasuliwa mara kadhaa ili kurekebisha mwili wangu, na nilitumia zaidi ya mwezi mmoja hospitalini nikipata nguvu tena.

Sasa nataka kumwonyesha Muumba wetu Mtukufu kwamba kwa kweli ninathamini zawadi yake ya kustaajabisha ya uhai, kutia ndani uandalizi wake kwa wanadamu kufurahia uhai udumuo milele katika paradiso ya kidunia. (Zaburi 37:9-11, 29; Ufunuo 21:3, 4) Ninang’amua kwamba njia bora zaidi ya kuonyesha uthamini wa namna hiyo ni kwa kuendelea kuweka masilahi ya Ufalme kwanza katika maisha yangu.—Imechangwa.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

US Navy/Sipa Press

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki