Hofu Kuu Katika Ndege Nambari 811
Februari 24, 1989. Siku ilikuwa changa ikiwa imekwenda saa moja tu. Nikiwa pamoja na mke wangu, Linda, nilitumainia kurudi nyumbani kwenye udongo wetu katika Australia katika muda wa saa 12 hivi. Ndege nambari 811 ya kwenda New Zealand, ikiwa ndiyo mkondo wa kwanza wa safari yetu ya kwenda nyumbani, ikawa si safari ya kikawaida tena.
Dakika ishirini zikiisha kupita katika safari yetu, tuligutushwa na kishindo kikubwa upande wa kulia wa ndege. Kisehemu kimoja upande wa ndani wa ndege kilibonyea, mstari mmoja tu kutoka tulipokuwa. Mabomoko na faibaglasi vilitupwa-tupwa katika ukumbi wa ndege. Upepo imara ajabu ukavuma ndani ya ndege. Hatukujua kwamba abiria tisa walikuwa wamepigwa na upepo huo wakarushwa nje ya ndege—mmoja wao akavutwa ndani ya moja ya injini za mkono wa kulia za ndege hiyo!
Makelele ya bumbuazi la abiria yalimezwa kabisa na mivumo ya upepo huo wenye kubisha na kiwiliwili cha ndege kutikisika. Linda na mimi tulikodoleana macho tu. Maneno hayakuhitajiwa. Tulijua tulikuwa karibu kufa!
Kukabiliana na Kifo cha Hakika
Nilitazama nyuma yangu nikaona kwamba vifunika-uso vya kuvutia oksijeni vilikuwa vimeanguka kutoka kwenye dari kwa ajili ya abiria walio wengi lakini si kwa ajili ya Linda na mimi. Mimi nikasimama kwa jaribio la kufungua chumba cha kuwekea vifunika-uso lakini nikaburutwa na mke wangu kwenye kiti changu.
Hata hivyo, tuliweza kuvuta jaketi zetu za kuokolea uhai chini ya viti na kuchukua ule msimamo wa kujiandaa kwa anguko la ndege. Kadiri tulivyojua, tulikuwa karibu kuanguka ndani ya bahari kuu ya Pasifiki!
Tena Linda na mimi tukatazamana. “Nakupenda wewe, Linda,” mimi nikasema. “Mimi pia nakupenda,” yeye akajibu. Kwa kurudia ule msimamo wa kujiandaa kwa anguko la ndege, nikainamisha kichwa, nikaanza kusali kwa Yehova Mungu.
Wewe husikia mara nyingi kwamba watu walio karibu kufa huona tamasha mbalimbali za maisha zao zikipita-pita mbio mbele yao. Sisi wote wawili tuliziona. Pia tulijiliwa na majuto mengi sana ya kusema-sema ‘laiti.’ Sisi wote wawili, mke wangu na mimi, ni Mashahidi wa Yehova. Mimi nilikuwa nimetumainia kwamba siku moja ningestahili kuwa mtumishi wa huduma katika kundi la kwetu. Lakini sasa ilionekana kuwa hakika kwamba singefikia kamwe mradi huo. Linda aliteswa-teswa na majuto ya kwamba hakupata kamwe kuingia kazi ya kuhubiri wakati wote akiwa painia, jambo ambalo alikuwa amekuwa akiongea mara nyingi.
Tena nikamtolea Yehova wito, wakati huu kwa sauti kubwa, huku mkono wangu wa kulia ukimshika Linda kwa imara. Mmoja wa watumishi wa kike ndegeni akasihi-sihi kwa hekaheka nyingi kwamba abiria wote wabaki wakiwa wameketi. Huko nje, ni giza totoro. Ndani, si hofu hiyo.
‘Iweje Linda akifa nami niokoke?’ nikawaza. ‘Wazazi wake wangefikiri nini juu yangu kwa kuchukua binti yao na kushindwa kumrudisha nyumbani?’ Tumaini la ufufuo halikuwa limepata kuwa la maana sana kwetu kama lilivyokuwa wakati huo.
Kwa kufikiria sana uwezekano mdogo sana wa kuokoka anguko hilo, nikaanza kufikiria kujibwaga baharini nipambane nao papa. Nikatazama chini kwenye miguu yangu kutafuta viatu vyangu chini ya kiti kilicho mbele yangu. ‘Papa akijaribu kunitafuna,’ nikawaza, ‘atataabika zaidi kuniuma kupitia kwenye viatu!’ Eti hilo si wazo la kiakili? Ndiyo. Lakini ni nadra kutumia akili nyakati kama hizo.
Kutua!
Kwa ghafula, likaja tangazo: “Zimebaki dakika mbili tutue!”
“Eti zimebaki dakika mbili tutue?” nikashangaa sana. ‘Watu hawatui katika bahari kuu—wao huanguka,’ nikawaza. ‘Je! tungeweza kuwa tukielekea kurudi Honolulu?’ Muda si muda nikapata jibu. Taa zikawaka, nasi tukatua chini kwa ulaini mzuri wee. Acha abiria wapige makofi ya kishindo ndege ilipokuwa ikisimama tuli! Mimi nikabaki nimejibwagaza katika kiti changu. Lakini si kwa muda mrefu. Upesi ukatokea wito wa kuondoka hima katika ndege hiyo. Tukaelekea kwenye milango ya kuondokea na kushuka mbio kwenye viteremkio hadi kwenye usalama wa kipito cha ndege huko chini.
Tukiwa umbali salama kutoka kwenye ndege yetu kiwete, nikachunguza sababu ya nusu-saa yetu ya ogofyo kuu: kisehemu cha meta 9 za kiwiliwili kilikuwa kimeraruka, kikifunua wazi mistari sita ya kisehemu cha wasafiri wa daraja la kibiashara, kisehemu cha kuwekea shehena, na eneo dogo la daraja la kwanza. Nakumbuka kuona kwamba kisehemu kizima cha viti vya daraja la wasafiri wa kibiashara kilibaki madhubuti na nikahisi nikitusha moyo kwamba ni lazima kila mtu awe aliokoka. Nilikosea we! Kumbe mistari kama sita ilikuwa imepigwa dhoruba ya upepo na kurushwa nje ya jeti ile, ikipeleka abiria tisa kwenye kifo chao cha kuogofya sana.
Basi lilipokuwa likiturudisha kwenye kituo kikubwa, abiria wakaanza kuliwazana. Ilikuwa wazi kwamba wengi zaidi na zaidi walikuwa wakilemewa na mshtuko. Tulipowasili kwenye kituo, simu zote zilizopo zikashikwa mara ile ile. Abiria wenye kimako kikubwa walijaribu kuwapasha habari wanafamilia kabla hawajashtuliwa na ripoti za redio na televisheni.
Mimi sitazisahau kamwe saa sita zilizofuata: Abiria wenye kutoka damu na wenye kimako cha hisia-moyo wakiwa wametapakaa kwenye sakafu ya ukumbi wa uwanja wa ndege. Vikoa vya waandishi wa habari na wanasheria vilikusanyika nje. Nao wafanya kazi wa ndege wakijaribu kuzuia tusifikiwe nao. Hesabu za abiria zikifanywa-fanywa wakati wote huku maofisa wakisongamana kupambanua ni nani kwa kweli asiyekuwapo.
Baadaye, kila abiria alihojiwa na mawakili wa U.S. Federal Bureau of Investigation wakiwa macho kuthibitisha upesi iwezekanavyo kama utendaji wa kiharamia ndio uliosababisha msiba huo. Haikuelekea kuwa hivyo, lakini wenye mamlaka ya kusimamia ndege walikuwa wametingwa na wasiwasi. Miezi miwili tu mapema, ulipusha-bomu wa kiharamia ulikuwa umeangusha jeti moja juu ya Lockerbie, Uskochi. Hata hivyo, baadaye tulipata habari kwamba kasoro ya muundo ndiyo yaelekea ilisababisha tanzia hiyo ya ndege nambari 811.
Kufika Nyumbani Hatimaye!
Baada ya kupata pumziko fupi na mlo moto kwenye hoteli moja ya Waikiki, tuliambiwa kwamba safari hiyo ya ndege iliratibiwa upya iwe baadaye usiku huo. Ingawa wachache walichagua kubaki Waikiki ili wapate nafuu, Linda na mimi na wengine wengi tuliamua kwamba tulitaka kuliacha nyuma jinamizi hili upesi iwezekanavyo. Hata hivyo, safari yetu ya ndege kutoka Honolulu ilikuwa tukio lenye kutikisa fahamu. Hata mtikisiko mdogo kabisa wa ndege ulipitisha mtapo katika uti wetu wa mgongo. Mmoja wa wafanya kazi wa ndege aliangusha kikombe cha barafu na mlio wacho ukatugutusha. Safu za abiria, kutia ndani mimi mwenyewe, tuliruka kutoka kwenye viti vyetu.
Hata hivyo, baada ya muda tuliwasili salama salimini katika Australia. Mtu mmoja wa ukoo, asiyeshiriki imani yetu, alionelea kwamba labda imani yetu ilitusaidia kukabiliana na patashika hiyo ya angani. Nasi tuifikiriapo tena ndege hiyo iliyopigwa na hofu kuu, Linda na mimi hatuna shaka zozote kwamba tegemeo letu juu ya Yehova Mungu na imani yetu hakika katika ahadi yake ya ufufuo lilikuwa faraja kubwa kwetu.
Ingawa hatuwezi kudai kwamba kuokoka kwetu kulikuwa kwa kimwujiza kwa njia yoyote, hakika sisi tunashukuru kuwa hai. Kwa kweli, tukio hilo limetusaidia tuthamini zaidi ya wakati mwingine wowote kwamba uhai ni zawadi ya thamani kubwa kutoka kwa Mungu. Na zaidi ya wakati mwingine wowote tumepiga moyo konde tuutumie kwa ukamili kwa sifa yake.—Kama ilivyosimuliwa na Roger White.