Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 4/8 kur. 3-6
  • Ubaguzi Dhidi ya Wanawake

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ubaguzi Dhidi ya Wanawake
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Fungu Dogo
  • Akina Mama na Watoa-Riziki
  • Kwa Nini Tatizo Hilo Linaenea?
    Amkeni!—2003
  • Kuthamini Wanawake na Kazi Yao
    Amkeni!—1998
  • Matatizo Yanayowakabili Wanawake
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Wanawake Je! Wanastahiwa Nyumbani?
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 4/8 kur. 3-6

Ubaguzi Dhidi ya Wanawake

KATIKA Afrika Magharibi mfanya-biashara amnunua mtoto wa miaka tisa. Katika Asia kitoto kilichozaliwa karibuni chazikwa katika mchanga wa jangwa kikiwa hai. Katika nchi moja ya Mashariki mtoto anayeanza kutembea afa njaa katika nyumba ya kutunzia yatima—asiyetakwa na bila kutunzwa. Jambo moja lahusiana katika kuunganisha misiba hii: Wahasiriwa wote walikuwa wasichana. Kwa sababu walikuwa wa kike walionwa kuwa si wa muhimu.

Hivi si visa vya kipekee. Katika Afrika, maelfu ya wasichana na wanawake wachanga huuzwa katika utumwa, wengine kwa kiasi kidogo sana kufikia dola 15. Na yasemekana kuwa kila mwaka mamia ya maelfu ya wasichana wachanga huuzwa au hulazimishwa kuwa makahaba, hasa katika Asia. Vibaya hata zaidi, tarakimu za idadi katika nchi kadhaa zaonyesha kwamba wasichana wengi kufikia milioni 100 “wamepotea.” Kwa wazi hili ni kwa sababu ya utoaji-mimba, uuaji wa watoto wachanga, au kupuuza tu watoto wa kike.

Kwa wakati mrefu—karne kadhaa—wanawake wameonwa kwa njia hii katika nchi nyingi. Na katika sehemu fulani wangali wanaonwa hivyo. Kwa nini? Kwa sababu katika nchi kama hizo, wavulana huonwa kuwa wenye thamani kubwa. Huko, inahisiwa kuwa mvulana anaweza kuendeleza ukoo wa familia, kurithi mali, na kuwatunza wazazi wanapokuwa wazee, kama ilivyo kawaida katika nchi hizi hakuna malipo ya uzeeni kutoka kwa serikali. Msemo wa Kiasia hudai kwamba “kumlea msichana ni kama kumwagia maji mmea katika shamba la jirani yako.” Atakapokuwa mtu mzima, ataondoka na kuolewa au hata kuuzwa kuwa kahaba na kwa hiyo atasaidia kidogo au hatasaidia katika kuwatunza wazazi wake walio wazee.

Fungu Dogo

Katika nchi zilizo maskini, mtazamo huu wamaanisha chakula kidogo zaidi, utunzaji mdogo zaidi wa kiafya, na kisomo kidogo zaidi kwa wasichana katika familia. Watafiti katika nchi moja ya Asia walipata kwamba asilimia 14 ya wasichana hawakulishwa vizuri, kwa kulinganishwa na asilimia 5 tu ya wavulana. Katika nchi fulani wavulana waliowazidi wasichana mara mbili hupelekwa katika vituo vya afya, yaeleza ripoti kutoka kwa Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF). Na zaidi ya asilimia 40 ya wanawake wachanga katika Afrika vilevile katika kusini na magharibi mwa Asia hawajui kusoma wala kuandika. “Kuna ubaguzi mbaya sana wa jinsia unaoendelea katika nchi zinazositawi,” akaomboleza Audrey Hepburn aliyekufa, aliyekuwa balozi wa UNICEF wa zamani.

“Ubaguzi huu wa jinsia” hautoweki wasichana wanapofikia utu mzima. Umaskini, jeuri, na mmenyeko usiopungua ni kawaida ya maisha ya mwanamke, hasa kwa sababu ni mwanamke. Msimamizi wa Benki ya Dunia alieleza hivi: “Wanawake hufanya thuluthi mbili ya kazi za ulimwengu. . . . Lakini wao huchuma tu sehemu moja ya kumi ya mshahara wa ulimwengu na humiliki chini ya asilimia moja ya mali ya ulimwengu. Wako kati ya walio maskini zaidi wa maskini wa ulimwengu.”

Kulingana na ripoti moja ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 70 ya watu bilioni 1.3 wa ulimwengu wanaoishi katika umaskini wa kupita kiasi ni wanawake. “Na hali yazidi kuwa mbaya,” ripoti hiyo yaongezea. “Idadi ya wanawake wa mashambani wanaoishi katika umaskini kabisa iliongezeka kwa karibu asilimia 50 katika miongo miwili iliyopita. Kwa kuongezeka, wanawake ndio hasa wanaoishi katika umaskini.”

Yenye kufadhaisha zaidi kuliko umaskini wenye kugandamiza ni jeuri inayoharibu maisha ya wanawake wengi. Idadi inayokadiriwa kuwa wasichana milioni moja, hasa katika Afrika, wameteseka kutokana na uchinjaji wa viungo vya uzazi. Kubaka ni kutenda vibaya kulikoenea sana ambako kwabaki kukiwa bila ithibati yoyote iliyoandikwa katika maeneo fulani, hata ingawa chunguzi zaonyesha kwamba katika nchi fulani mwanamke 1 kati ya 6 hubakwa wakati wa maisha yake. Vita huathiri wanaume na wanawake sawasawa, lakini wengi wa wakimbizi wanaolazimishwa kutoroka nyumba zao ni wanawake na watoto.

Akina Mama na Watoa-Riziki

Mzigo wenye kulemea wa kuitunza familia mara nyingi humwangukia zaidi mama. Yaelekea yeye hufanya kazi kwa muda wa saa nyingi na aweza pia kuwa ndiye mtoa-riziki pekee. Katika sehemu fulani za mashambani katika Afrika, karibu nusu ya familia zote husimamiwa na wanawake. Katika mahali fulani katika nchi za Magharibi, idadi kubwa ya familia husimamiwa na mwanamke.

Zaidi ya hilo, hasa katika nchi zinazositawi, kwa kawaida wanawake hufanya kazi zilizo ngumu zaidi, kama vile kuteka maji na kutafuta kuni. Ukataji wa misitu na kulisha wanyama kupita kiasi kumezifanya kazi hizi kuwa ngumu hata zaidi. Katika nchi fulani zinazoathiriwa na ukame, wanawake hutumia muda wa saa tatu au zaidi wakitafuta kuni na muda wa saa nne kila siku wakiteka maji. Wanapomaliza kufanya kazi hii ngumu, ndipo tu wawezapo kufanya kazi wanayotarajiwa kufanya nyumbani na shambani.

Kwa hakika, wote wanaume na wanawake huteseka katika nchi ambako umaskini, njaa, au zogo ni maono ya kila siku. Lakini wanawake huteseka zaidi isivyolinganika. Je, hali hii itabadilika wakati wowote? Je, kuna matumaini yoyote kwamba siku moja wanawake kila mahali watatendewa kwa staha na ufikirio? Je, kuna lolote ambalo wanawake wanaweza kufanya sasa ili waboreshe hali yao?

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

Makahaba Wasichana—Ni Nani Anayepasa Kulaumiwa?

Kila mwaka idadi inayokadiriwa kuwa watoto milioni moja—hasa wasichana—huuzwa au kulazimishwa kuwa makahaba. Araya,a ambaye anatoka Kusini-Mashariki mwa Asia, akumbuka kilichotokea kwa baadhi ya wanadarasa wenzake. “Kulvadee alikuwa kahaba alipokuwa na umri wa miaka 13 tu. Alikuwa msichana mzuri, lakini mama yake alikuwa mlevi mara nyingi na alikuwa akicheza karata, kwa hiyo hakuwa na wakati wa kumtunza binti yake. Mama ya Kulvadee alimtia moyo kuchuma pesa kwa kwenda na wanaume, na punde si punde, alikuwa akifanya kazi akiwa kahaba.”

“Sivun, mwanafunzi mwingine katika darasa langu, alitoka katika sehemu ya kaskazini ya nchi. Alikuwa na umri wa miaka 12 tu wazazi wake walipompeleka kwenda mjini kufanya kazi akiwa kahaba. Ilikuwa lazima afanye kazi kwa miaka miwili ili kulipia mkataba uliotiwa sahihi na wazazi wake. Sivun na Kulvadee si wasio wa kawaida—wasichana 5 kati ya 15 katika darasa langu walikuja kuwa makahaba.”

Kuna mamilioni ya vijana kama Sivun na Kulvadee. “Biashara ya ngono ni soko kubwa lenye mwendo wake wenyewe,” aomboleza Wassyla Tamzali, wa UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni). “Kuuza msichana mwenye umri wa miaka 14 limekuwa jambo la kawaida sana, ni jambo la kawaida mno.” Na mara tu wasichana hawa wakishauzwa katika utumwa wa ngono, kulipia bei ya kununuliwa kwao yaelekea kuwa jambo lisilowezekana. Manju, ambaye baba yake alimuuza alipokuwa na umri wa miaka 12, angali na deni la dola 300 (za Marekani) baada ya miaka saba ya ukahaba. “Hakuna lolote ningaliweza kufanya—nilinaswa,” yeye aeleza.

Kuepuka UKIMWI kwaweza kuwa vigumu kwa wasichana hao kama vile kuwaepuka makuwadi wanaowanasa. Ukaguzi uliofanywa Kusini-Mashariki mwa Asia ulionyesha kwamba asilimia 33 ya makahaba hawa watoto walikuwa wameambukizwa na virusi vya UKIMWI. Mradi biashara ya ukahaba ya dola bilioni tano yaendelea kusitawi, inaelekea kwamba wasichana hawa wataendelea kuteseka. Ni nani anayepasa kulaumiwa kwa zoea hili lenye kuogofya? Bila shaka, wale wanaonunua au kuuza wasichana kwa ukahaba wana sehemu kubwa ya lawama. Lakini pia wa kulaumiwa ni wanaume wasiofaa wanaowatumia wasichana hao ili kutosheleza uchu wao wa kingono. Kwani bila wazoea-ukosefu wa adili kama hao, kuwafanya wasichana hawa kuwa makahaba hakungekuwako.

[Maelezo ya Chini]

a Majina yamebadilishwa.

[Picha]

Kila mwaka karibu wasichana milioni moja hulazimishwa kuwa makahaba

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Siku ya Kazi ya Mwanamke Katika Afrika ya Kati

Mwanamke huamka saa 12 na kutayarisha kiamsha-kinywa cha familia na chake, ambacho watakula asubuhi-kati. Baada ya kuteka maji kutoka katika mto ulio karibu, huelekea kwenye shamba lake—laweza kuwa katika umbali wa mwendo wa muda wa saa moja.

Hadi kufikia karibu saa kumi alasiri, analima, kung’oa magugu, au kumwagia shamba hilo maji, akitua kidogo tu ili ale chakula chochote alichobeba. Muda wa saa mbili uliobaki wa mchana atautumia kukata kuni na kukusanya mhogo au mboga nyingine kwa ajili ya familia—zote ambazo atapeleka nyumbani.

Kwa kawaida, yeye hufika nyumbani jua linaposhuka. Sasa kuna kazi ya kufanywa kutayarisha mlo wa jioni, kazi ngumu ambayo yaweza kuchukua muda wa saa mbili au zaidi. Jumapili hutumiwa kufua nguo katika mto wa hapo kisha kuzipiga pasi, mara zinapokauka.

Mume wake huthamini kwa nadra sana kazi hii ngumu wala hasikilizi madokezo yake. Yeye hatakataa kukata miti au kuchoma magugu ili kwamba aweze kutayarisha ardhi kwa kupanda, lakini hafanyi mengi zaidi. Mara kwa mara, yeye huwapeleka watoto mtoni wakaoge, na huenda akawinda na kuvua samaki kidogo. Lakini wakati mwingi wa siku yake hutumika akizungumza na wanaume wenzake wa kijiji.

Ikiwa mume wake aweza kugharimia, baada ya miaka michache, ataleta nyumbani mke mpya, mchanga zaidi, ambaye atapata shauku zake zote. Hata hivyo, mke wake wa kwanza angali atatarajiwa kuendelea na kazi zake kama kawaida, hadi afya yake iharibike ama afe.

Wanawake Waafrika huchukua mzigo mzito wa kazi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki