Kuutazama Ulimwengu
Zoea Ghali la Dawa za Kulevya
Ripoti moja ya serikali ya Marekani inakadiria kwamba Wamarekani walitumia dola bilioni 57.3 kwa dawa haramu za kulevya katika mwaka wa 1995. Kokeini ilichangia thuluthi mbili za mauzo hayo, huku heroini, bangi, na dawa nyingine haramu zikifanyiza kiwango kilichobakia. Mkurugenzi wa Ikulu ya Kitaifa ya Sera ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Barry McCaffrey, alionelea kwamba kiasi cha pesa zilizotumiwa kwa dawa hizo kingeweza kulipia elimu ya miaka minne ya chuo cha elimu kwa watu milioni moja au lita bilioni 83 za maziwa ya kulisha watoto wasiolishwa chakula cha kutosha, shirika la Associated Press laripoti. Isitoshe, tarakimu hii haitii ndani gharama za kijamii, kama vile ongezeko la uhalifu, kuvurugwa kwa maisha ya kibinafsi na ya familia, na kuenea kwa maradhi kama mchochota wa ini na UKIMWI.
Sheria Iliyosahaulika
Ni ngapi kati ya Amri Kumi za Biblia unazoweza kukariri? Uchunguzi katika Rio de Janeiro ulipata kwamba zaidi ya Mbrazili 1 kati ya 4 hakuweza kutaja yoyote kati ya hizo! Kwa wale ambao walijua angalau moja ya amri hizo, asilimia 42 walitaja “Usiue” au “Usiibe.” Wengine walikumbuka “Usimtamani mke wa jirani yako” (asilimia 38), “Waheshimu baba yako na mama” yako (asilimia 22), na ‘Usishuhudie uongo’ (asilimia 14), laripoti Veja. Ni asilimia 13 tu ya waliohojiwa waliokumbuka amri ya tatu: “Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako.”
Majaribio ya Mapema ya Kiwango cha Akili cha Watoto
Wanasayansi wanaochunguza akili ya binadamu sasa wanaamini kwamba akili ya kitoto kichanga hupitia hatua ya maana sana ya ukuzi wake kati ya kuzaliwa na anapokuwa na umri wa miaka mitatu. Pia inafikiriwa kwamba kwa kuitikia kichocheo cha akili, miunganisho ya kudumu huimarishwa katika akili wakati wa awamu hii. Hivyo, wazazi fulani wameanza kuwapa watoto wao majaribio ya kiwango cha akili muda mrefu kabla hawajaingia shule ya watoto wadogo, kuwasaidia wapate maarifa ya ziada laripoti Modern Maturity. Hata hivyo Dakt. Barry Zuckerman, mwenyekiti wa idara ya magonjwa ya watoto katika Shule ya Madawa ya Chuo Kikuu cha Boston, alionyesha hangaiko lake kwa wazazi ambao huhisi “kusongwa ‘kumchochea’ mtoto wao mchanga daima” katika jaribio la kutokeza “mtoto wa kipekee sana.” Profesa wa saikolojia ya watoto, Richard Weinberg, aongezea: “Kuwasukuma watoto waanze kushindana mapema sana mara nyingi hutokeza jambo lililo kinyume. Acha watoto wako wafurahie utoto wao.”
Wanakili Waangalifu
Maandishi yanayofanyiza Maandiko ya Kigiriki ya Biblia yamenakiliwa kwa usahihi na kupokezwa kwa uangalifu asema Dakt. Barbara Aland, msimamizi wa Chuo cha Utafiti wa Agano Jipya, katika Münster, Ujerumani. “Makosa au hata mabadiliko yaliyochochewa na theolojia ni nadra sana,” laripoti Westfälische Nachrichten. Tangu mwaka wa 1959 chuo hicho kimechunguza zaidi ya hati 5,000 zilizoandikwa kwa mkono, ambazo ni za Enzi za Kati na nyaraka za kale zilizo bora. Baadhi ya asilimia 90 ya hati hizo zimerekodiwa katika mikrofilamu. Kwa nini wanakili wa Biblia walikuwa waangalifu sana hivyo wasifanye makosa? Kwa sababu “walijiona wenyewe kuwa ‘wanakili’ wala si waandishi,” gazeti hilo lasema.
Je, kwa Kweli Ni Kahawa Isiyo na Kafeini?
Wale ambao huwa wanyetivu kwa kafeini mara nyingi hugeukia kinywaji kisicho na kafeini kama kibadala. Lakini unaweza kuwa na uwezekano gani wa kupata kahawa halisi isiyo na kafeini unapoitisha upewe? Kulingana na ripoti katika The New York Times, kuna uwezekano wa 1 kati ya 3. Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa za Kulevya la Marekani hufasili kahawa isiyokuwa na kafeini kuwa ina miligramu mbili hadi tano za kafeini. Lakini sampuli 18 kutoka kwa wauza-kahawa katika New York City zilifunua kwamba kiasi cha kafeini katika kikombe chenye aunsi tano kilitofautiana sana, kutoka miligramu 2.3 za kafeini hadi miligramu 114! Kulingana na Shirika la Kitaifa la Kahawa, kikombe cha kahawa cha wastani huwa na miligramu za kafeini kati ya 60 na 180.
Ukataji wa Misitu wa Ulimwenguni Pote
“Thuluthi mbili za misitu ya sayari tayari zimeharibiwa,” laripoti Jornal da Tarde. Kati ya kilometa milioni 80 mraba za maeneo ya dunia yaliyokuwa na misitu hapo awali, ni milioni 30 tu zinazobakia. Hazina ya Ulimwengu ya Wanyama wa Pori (WWF) imepata kwamba Asia ndiyo kontinenti iliyo na ukataji mkubwa sana wa misitu, asilimia 88 ya mimea yake ikiwa imeharibiwa. Katika Ulaya tarakimu hiyo ni asilimia 62, katika Afrika asilimia 45, katika Amerika ya Latini asilimia 41, na katika Amerika Kaskazini asilimia 39. Amazonia, kao la msitu wa mvua wa kitropiki ulio mkubwa zaidi ulimwenguni, ina asilimia 85 ya misitu yake ya awali iliyobakia. Gazeti la habari O Estado de S. Paulo humnukuu mkurugenzi wa WWF Garo Batmanian akisema: “Brazili ina fursa ya kuepuka kurudia makosa yaliyofanywa katika misitu mingine.”
Hazina Zilizoibwa
Habari mpya za hivi majuzi kutoka Kanada zilitangaza kwamba “hazina za Mesopotamia ambazo zimeachwa bila kulindwa kufuatia vita vya Ghuba ya Uajemi vya mwaka wa 1991 zimekuwa shabaha ya magenge ya uhalifu ya kimataifa,” laripoti World Press Review. Katika mwaka wa 1996, wezi walivunja Jumba la Makumbusho la Babiloni mchana na kutwaa micheduara na mabamba yaliyochorwa kwa maandishi ya kikabari. Vitu hivyo vya kale vilivyo nadra sana, vingine vikiwa vya wakati wa milki ya Nebukadreza wa Pili, vilikadiriwa kuwa vyenye thamani inayozidi dola 735,000 kwenye masoko ya kimataifa ya sanaa. Eneo jingine lililokuwa shabaha ya wezi ni jiji la kale la Al-Hadhr. Katika jitihada za kulinda hazina zilizobakia, serikali imefunga kabisa milango yote ya jiji na njia kwa matofali na sementi, lataarifu gazeti hilo.
Kanisa Katoliki Latafuta Msamaha
Kanisa Katoliki ya Kiroma katika Ufaransa limetoa “Tangazo Rasmi la Toba,” likimwomba Mungu na Wayahudi msamaha kwa sababu ya “ubaridi” ambao Kanisa Katoliki lilionyesha kuelekea mnyanyaso wa Wayahudi chini ya serikali ya Vichy ya Ufaransa wakati wa vita. Kutoka mwaka wa 1940 hadi mwaka wa 1944, zaidi ya Wayahudi 75,000 walikamatwa na kuhamishwa kutoka Ufaransa hadi kwenye kambi za kifo za Nazi. Katika taarifa iliyosomwa na Askofu Mkuu Olivier de Berranger, kanisa lilikiri kwamba liliruhusu mapendezi yake “yatie giza amri ya lazima ya kibiblia ya staha kwa kila binadamu aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu,” gazeti la habari la Ufaransa Le Monde laripoti. Ingawa makasisi wachache Wafaransa waliongea wakipendelea Wayahudi, wengi wao waliunga mkono serikali ya Vichy na sera zake. Tangazo hilo rasmi lilisema hivi kwa sehemu: “Lazima kanisa litambue kwamba kwa habari ya kunyanyaswa kwa Wayahudi, na hasa kwa habari ya hatua za mara nyingi dhidi ya Wayahudi zilizoagizwa na mamlaka ya Vichy, kwa kiwango kikubwa ubaridi ulizidi sana ghadhabu. Kimya kilikuwa jambo la kawaida, na kuongea kwa kupendelea wahasiriwa kulikuwa nadra sana. . . . Leo, twakiri kwamba kimya hiki kilikuwa kosa. Pia twatambua kwamba kanisa katika Ufaransa halikufua dafu katika kazi yake likiwa mwelimishaji wa dhamiri za watu.”
Wadudu Waharibifu
Tangu mdudu aitwaye red palm weevil alipofika kwenye Peninsula ya Arabia miaka ipunguayo 20 iliyopita, mdudu huyu mdogo ameingilia maelfu ya miti ya mitende na kusababisha hasara isiyoelezeka. “Hata kuna hofu kwamba tende—‘matunda ya uhai’ ya zaidi ya miaka 5,000 ya Arabia—yaweza kumalizwa,” laripoti gazeti The Economist. Mdudu huyo, akiwa na urefu wa sentimeta tano tu, hutoboa mfuatano wa mashimo ndani ya shina la mtende na kuua mti huo polepole. Dawa za kuua wadudu hazijawa na matokeo sana kwa mdudu huyu, na anaendelea kuongezeka kwa haraka kotekote katika eneo hilo.
Faida za Waajiriwa Wenye Umri Mkubwa Zaidi
Wafanyakazi waliopitisha umri wa miaka 47 huwa chonjo zaidi na hodari zaidi wakati wa asubuhi kuliko wenzao wenye umri mdogo zaidi, laripoti The Times la London. Kwa kuwa taratibu hii huelekea kujirudia yenyewe baadaye mchana, Tom Reilly, wa Chuo Kikuu cha John Moores cha Liverpool, anadokeza kwamba waajiri wawapangie waajiriwa wenye umri mkubwa zaidi zamu za mapema na wale walio wachanga zaidi zamu za mchana na jioni. Wasemaji katika mkutano uliohusiana na kuzeeka wa Shirika la Kitiba la Uingereza pia walifunua kwamba mara nyingi maduka makubwa na yale ya kujihudumia hupendelea kuwaajiri watu wenye umri mkubwa zaidi. Kwa nini? Kwa sababu wao huhangaikia wateja na kudhihirisha ujuzi kuhusu kufanya mambo yasiyokuwa na maagizo yaliyoandikwa. Pia wao hushikamana sana na “viwango vya maadili ambavyo huenda ikawa kampuni imeviacha,” gazeti hilo la habari laripoti.