Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 2/15 uku. 29
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Habari Zinazolingana
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Kunywa Chai Kama Wachina
    Amkeni!—2005
  • “Si kwa Chai Yote Katika China!”
    Amkeni!—1990
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 2/15 uku. 29

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

◼ Je! Mkristo aepuke kahawa na chai kwa sababu vina kafeni, ile dawa yenye kuzoeleza?

Biblia haitaji kahawa wala chai. Lakini iyasemayo yaweza kusaidia Mkristo aamue kama atakunywa kahawa au chai.

Kafeni, ile dawa ya kulevya, yaweza kuathiri akili na mwili. Mamilioni ya vikombe vya kahawa na chai hunywewa kila siku, hiyo ikiongoza Dakt. Melvin Konner kusema hivi: “Kwa uhakika [kafeni] huenda ikawa ndiyo dawa ya kulevya yenye kuchochea akili ambayo hutumiwa kwa mapana sana ulimwenguni.” Yaweza kuongeza kukaa chonjo kwa mtu, kuinua kiwango cha adrenalini, na kuharakisha mzunguko wa damu na metaboli. Jambo lenyewe tu la kwamba hiyo ni dawa ya kulevya silo lenye kuamua kama Mkristo apaswa kuepuka vinywaji vyenye kafeni (kahawa, chai, vinywaji vyenye kola, mate) au vyakula (kama chokoleti).

Alkoholi (kileo) pia ni dawa ya kulevya ambayo yaweza kuathiri mwili na akili, na hata hivyo Maandiko yasema nini kukihusu? Biblia yakiri kwamba divai (au vileo vingine vyenye alkoholi) yaweza kufanya “moyo wa mwanadamu mwenye kufa ushangilie” au kubadili tabiamoyo ya nafsi iliyosononeka. (Zaburi 104:15; Mithali 31:6, 7, NW) Ingawa hivyo, Neno la Mungu halionyeshi kwamba ni lazima waabudu wa kweli waepuke vinywaji vyote vyenye alkoholi. Kile ambacho Biblia yalaani vikali ni kutumia alkoholi (kileo) bila kiasi —ulevi.—Kumbukumbu 21:18-21; Mithali 20:1; Hosea4:11; 1 Wakorintho 5:11-13; 1 Petro 4:3.

Hata hivyo, namna gani lile dai la kwamba huenda mtu akawa mzoelevu wa kafeni? Wengi walio na tabia ya kunywa kahawa, chai, au mate husitawisha kadiri fulani ya zoea la kutegemea vinywaji hivyo, ingawa kuna majadiliano juu ya kama huu ni uzoelevu uliothibitishwa kikweli kwa uchunguzi wa kikliniki. Angalau wao huhisi masumbufu ya mwili kutokana na dalili za kuacha utumizi, kama maumivu ya kichwa au kichefuchefu, wasipopata kipimo chao cha kafeni ya kawaida. Hapa tena kumbuka maoni ya Kibiblia kuhusu vinywaji vyenye alkoholi. Ingawa watu wengi wamezoelea alkoholi, haikatazwi kwa Wakristo ikiwa yatumiwa kwa kiasi. Yesu alikunywa divai; hata alifanyiza divai kimwujiza kwenye karamu ya arusi,—Mathayo 26:29; Yohana 2:3-11.

Na bado, Mkristo angeweza kuhisi kwamba angependelea kutojasiria kutegemea kafeni. Ikiwa kukosa unywaji wake wa kawaida wa kafeni kwamfanya audhike-udhike (“wasiwasi-kahawa”), angeweza kufikiria kuepuka kabisa kafeni ili huo uwe wonyesho wa “kujidhibiti.” (Wagalatia 5:22, 23, NW) Kwa kuwa Biblia haitaji mwepuko wa vinywaji vyenye kafeni, ni lazima uamuzi kuhusu kahawa au chai ufanywe na watu mmoja mmoja. Yafaa kuwa na kiasi ikiwa Mkristo hunywa chochote cha vitu hivyo.—Linganisha Tito 2:2.

Kiasi pia ndilo jambo kuu lenye kuhusika katika hatari za afya ambazo zawezekana kutukia. Yadaiwa kwamba kuna hatari nyingi za kunywa kafeni nyingi kwa ukawaida (iwe ni kutokana na kahawa, chai, vinywaji vyenye kola, au vinywaji au vyakula vingine). Hata hivyo, kwa kila uchunguzi wenye kuhusianisha hatari fulani ya kiafya na kafeni, uchunguzi mwingine huelekea kuonyesha kinyume.

Mantiki ya kiasi yakaziwa na yale ambayo Biblia yasema kuhusu asali. Hicho ni kitu cha kiasili, na kitendo cha kuila kuwa chakula kiamsha-nishati mwilini ni cha kiasili (tofauti na kuvuta moshi ndani ya mapafu). (1 Samweli 14:26, 27; Mathayo 3:4) Hata hivyo, waweza kuwa mgonjwa kwa kuila kwa wingi mno. Biblia yaonya hivi: “Je! umeona asali? Kula kadiri ya kukutosha; usije ukashiba na kuitapika.”—Mithali 25:16, 27.

Watu fulani hawawezi kula asali yoyote kamwe. Vivyo hivyo, huenda kwa sababu za kiafya watu fulani wakahitaji kuepuka kileo, kafeni, vitu vilivyofanyizwa kwa maziwa, au vyakula na vinywaji vingine. Huenda wengine, kwa kutotaka kuudhi mtu yeyote, wakaepuka vitu hivyo kwa uchaguzi wa kibinafsi au kwa sababu ya unyeti wenye kuenea mahali, wasitake kuudhi yeyote. Hiyo yatukumbusha elezo la mtume Paulo: “Ikiwa chakula chafanya ndugu yangu akwazike, mimi sitakula mnofu tena kamwe kamwe, ili kwamba nisipate kufanya ndugu yangu akwazike.”—1 Wakorintho 8:13, NW.

Kwa hiyo, acheni kila mtu atende kulingana na azimio lake mwenyewe bila kuhisi kwamba uamuzi wake wahitaji kulazimishwa juu ya wengine. Paulo aliandika hivi: “Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali. Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine?”—Warumi 14:3,4.

■ Je! agano la Sheria lilifikia mwisho wakati Yesu alipokufa juu ya ule mti, na je! ni lini lilipoondolewa na mahali palo pakachukuliwa na lile agano jipya?

Swali hili limetukia kwa wengi, ambao kwa kawaida wamekuwa na matukio matatu akilini: Kufa kwa Yesu juu ya mti wa mateso katika alasiri ya Nisani 14, 33 W.K., kutokeza kwake mbinguni ile thamani ya damu-uhai yake, na kumimina kwake roho takatifu juu ya wanafunzi siku ya Pentekoste 33 W.K.

Yehova alitabiri kwamba baada ya muda yeye angeondoa lile agano la Sheria aweke mahali palo “agano jipya” ambalo lingeruhusu dhambi isamehewe kabisa, jambo ambalo halikuwezekana chini ya ile Sheria. (Yeremia 31:31-34) Jambo hilo lingetukia lini?

Lile agano la zamani zaidi, Sheria, lilihitaji kwanza kuondolewa njiani likiwa lililokwisha kutimiza kusudi lalo. (Wagalatia 3:19, 24, 25) Jambo hilo lilitukia kwenye kifo cha Yesu. “[Mungu] alitusamehe kwa fadhili miruko yetu ya mipaka na akafuta kabisa ile hati iliyoandikwa kwa mkono dhidi yetu, ambayo ilikuwa na maamuzi ya kiamri na ambayo ilikuwa katika upinzani kwetu; na Yeye ameiondoa kwenye njia kwa kuipigilia misumari kwenye mti wa mateso.” (Wakolosai 2:13, 14, NW) Je! hiyo inamaanisha kwamba dakika ile ambayo Kristo alikufa, ile Sheria iliondolewa na mahali payo pakachukuliwa na lile agano jipya?

Sivyo, kwa maana agano jipya lilipasa kuzinduliwa kwa damu ya dhabihu inayofaa. (Waebrania 8:5, 6; 9:15-22; 12:24) Sawa na vile damu ya dhabihu ya Siku ya Upatanisho ilivyopelekwa ndani ya Patakatifu Zaidi Sana, ilimlazimu Yesu apeleke thamani ya damu yake ‘ndani ya mbingu yenyewe, ili akaonekane mbele za utu wa Mungu kwa ajili yetu.’ (Waebrania 9:23, 24, NW) Yeye alifufuliwa siku ya Nisani 16, na siku 40 baadaye alipaa mbinguni. (Matendo 1:3-9) Hakuna maana ya kujaribu kuonyesha dakika barabara ambapo yeye akiwa Mpatanishi alitokeza kwa Mungu ile thamani ya damu-uhai yake. Lakini sisi tunajua kwamba siku ya Pentekoste, siku kumi baada ya kupaa kwake, wanafunzi ‘walipokea ile roho takatifu iliyoahidiwa kutoka kwa Baba.’—Matendo 2:33, NW.

Hivyo, ni wakati gani agano la Sheria lilipoondolewa na mahali palo pakachukuliwa na lile agano jipya? Kwa kutoboa wazi, majibu mbalimbali yanayofaa yangeweza kutolewa, ikitegemea rai ya mtu. Ikiwa mtu angekuwa akifikiria akilini ule mwisho wenyewe wa Sheria, angeweza kusema kwamba jambo hilo lilitukia kwenye kifo cha Yesu. Kupasuka kwa pazia katikati ya patakatifu na patakatifu zaidi sana pa hekalu kulidhihirisha kwamba hekalu liliachiliwa rnbali; hata hivyo hakukuwa na jambo lo lote la kuonyesha kwamba agano jipya lilikuwa limechukua mahali pa lile la zamani,—Mathayo 27:51.

Kutokana na rai nyingine, mtu huenda akasema kwamba wakati Yesu alipotokeza kwa Mungu ile thamani ya dhabihu yake, agano jipya lilichukua mahali pa lile la zamani. Na bado, hakukuwa na ithibati duniani kwamba hilo agano jipya lilikuwa likitenda kazi. Jambo hilo lilikuja kutukia siku ya Pentekoste kwa kumiminwa kwa roho takatifu juu ya wale wa kwanza walioingizwa ndani ya agano jipya. Kwa sababu hiyo, ingekuwa halali kueleza kwamba siku ya Pentekoste 33 W.K. lile agano jipya lilithibitishwa kuwa lenye kufanya kazi.

Badala ya mtu ye yote kung’ang’ania kishupavu wakati fulani barabara, inatupasa sisi tuthamini kwamba elezo au jibu moja lenye kutolewa kuhusiana na jambo hili huenda likawa linashughulikia upande fulani hususa, hali elezo jingine huenda likatolewa kutokana na rai tofauti, kama vile kukazia ile ithibati yenye kuonekana miongoni mwa wanafunzi wa Kristo duniani. Uhakika ni kwamba, kulikuwa na pande kadhaa zenye kuhusika katika hatua-hatua za kuendelea kutimia kwa kusudi la Mungu kukomesha agano la Sheria, kuzindua lile agano jipya, na kutoa ithibati duniani kwamba mpango mpya huu ulikuwa unafanya utendaji.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki