“Si kwa Chai Yote Katika China!”
MWENDO wa historia ulibadilishwa na kitu hicho. Kampuni iliyokuwa na nguvu nyingi zaidi za kibiashara wakati wa kitu hicho ilianzishwa kwa kukitegemea. Mabaharia Waholanzi walisafiri maelfu ya kilometa kukitafuta. Hicho ndicho kinywaji kipendwacho zaidi ulimwenguni, kufuatia maji. Ni nini hicho? Ni chai!
Je! wewe umepata kushangaa ni jinsi gani chai ilipata umaarufu huo? Ilitoka wapi? Kama mavumbuo mengine yasiyohesabika, asili yayo ilikuwa China. Yapata miaka 500 kabla ya Wakati wa Kawaida, Confucius aligusia chai katika moja la mashairi yake. Historia yasimulia mmaliki Mchina ambaye, miaka 300 baadaye, alijaza pesa tena katika makasha matupu kwa kutumia kodi ya chai.
Ingawa kuna hekaya nyingi mno za kuaridhia asili yayo, labda hatutapata kamwe kujua kwa kweli jinsi chai ilivyogunduliwa. Hadithi moja yaihusianisha na Mmaliki Shen Nung, aliyekunywa maji ya kuchemshwa tu alipokuwa anasafiri kuizunguka nchi. Wakati mmoja tawi la kichaka chenye kuteketea lilirushwa likaingia ndani ya maji yaliyokuwa tayari yakichemka. Mmaliki alishangaa sana kuona ladha ya kupendeza sana na harufu nzuri sana katika kinywaji kipya hicho. Ugunduzi wake ulikuwa chai!
Kulingana na hekaya ya pili, mmoja wa wanafunzi wa Buddha, Bodhidharama fulani, aliamini kwamba utakatifu wa kweli ungeweza kupatwa kwa kutafakari daima tu, mchana na usiku. Wakati wa moja la makesha yake marefu, mwishowe alilemewa na usingizi. Ili asishindwe mara ya pili na huo udhaifu ovyo sana wa kibinadamu, alikata kope zake za macho. Zilianguka chini na kwa mwujiza zikaanza kuchipuka. Siku iliyofuata kichaka cha kijanikibichi kilitokea. Aliyaonja majani akayapata kuwa yenye kuburudisha kwa utamu. Bila shaka, huo ulikuwa mchai.
Chai Yashinda Mashariki ya Mbali
Muda si muda chai iliishinda Japani. Ilipelekwa huko na watawa-waume wa Ubuddha wa China, waliowasili muda fulani katika karne ya tisa wakiwa na ‘birika la chai katika mkoba wa mgongoni.’ Upesi, chai ikapendwa sana miongoni mwa Wajapani hivi kwamba miaka 400 baadaye, “desturi rasmi sana” ya kutayarisha na kuandalia chai, yenye kuitwa chanoyu, ikawa kawaida ya kitaifa.
Hata hivyo, Wajapani walipokuwa wakikuza sherehe ya kujali sana unywaji chai, chai katika China haikufurahiwa sana. Hata ingawa washairi Wachina walishangilia chai kuwa “umajimaji bora wa madini ya jedi,” mara nyingi ilikuwa kama mchuzi. Majani mabichi ya chai yaliyochemshwa katika maji ya chumvi na nyakati fulani yakatiwa ladha ya tangawizi na mdalasini au hata vitunguu, na nyakati nyingine yakapikwa pamoja na maziwa na hata mchele, yalikuwa ndiyo mapishi ya kawaida zaidi wakati huo.
Hata hivyo, ni Mchina aliyeandika kitabu cha kwanza kilichowekwa wakfu kwa ufanyizaji chai. Mwaka 780 W.K. hivi, Lu Yu alichapisha Tscha-King (Kitabu cha Chai), nacho kikaja upesi kuwa ndiyo biblia ya maelezo ya chai kwa wapenzi wa chai katika Mashariki ya Mbali. Kwa kuongozwa na mwanamume huyu mwandishi, China ilianza kufanya maendeleo katika mazoea yayo ya chai, ikitayarisha kinywaji hicho kwa njia yenye ufundi mwingi zaidi, hata hivyo iliyo sahili: Maji matupu yenye kiasi kidogo sana cha chumvi—ambacho ndicho kitu cha pekee kilichoruhusiwa kwenye mapishi ya kale yenye kuthaminiwa kwa muda mrefu—yalimiminwa juu ya majani-chai yaliyokaushwa. Lu Yu alionelea kwamba uzuri wa chai hutegemea harufu yayo. Alitambua kwamba ladha na ubora wayo haiamuliwi na mchai wenyewe tu bali na vitu kama udongo na tabia za hewa nchini, kama vile ilivyo kuhusu divai. Hiyo yaeleza kwa nini yeye angeweza kusema kwamba kuna chai “elfu na elfu kumi.”
Upesi Wachina wakaanza kuzichanganya chai, na mamia ya namna tofauti zikapelekwa sokoni. Haishangazi kwamba nchi iliyoupa ulimwengu chai ndiyo pia iliyoipa jina layo la ulimwenguni pote: Limetokana na herufi ya Kichina iliyo katika kilugha Amoy cha China.
Ulaya Yagundua Chai
Ilichukua muda mrefu kwa Wanaulaya kugundua upendezi wa chai. Hata ingawa Marco Polo (1254-1324), mfanya biashara na mjasiri Mvenisi, alizuru China kwa mapana, alitaja chai lakini mara moja katika ripoti zake za usafiri. Alieleza juu ya waziri wa fedha Mchina aliyefutwa kazi kwa sababu alikuwa ameongeza kiamri kodi ya chai. Yapata miaka 200 baadaye, Mvenisi mwingine, Giovanni Battista Ramusio, aliipa Ulaya maelezo marefu ya kwanza kuhusu ufanyizaji na utumizi wa chai. Hivyo, mwanzoni mwa karne ya 17, sampuli za kwanza za kinywaji kipya hiki cha kigeni ziliuzwa katika maduka ya dawa ya Ulaya, hapo kwanza zikachuma bei ya dhahabu. Basi si ajabu kwamba ule usemi wa asili ya Kiaustralia “Si kwa chai yote katika China!” wamaanisha—“Sivyo hata kidogo!”
Kwa wakati huo, Waholanzi walikuwa wameanza kufanya biashara na Mashariki ya Mbali, chai ikiwa ni moja ya bidhaa zao za kigeni zenye kuingizwa nchini. Mfanya biashara mwenye shughuli nyingi, Johan Nieuhof, aripoti juu ya shughuli nyingi sana alizodumu kufanya na wakuu Wachina, ambazo kwa kawaida zilifikia kilele kwa karamu nono ambapo kinywaji fulani kiliandaliwa. Kwa madharau alikiita kinywaji hiki “mchuzi wa maharagwe.” Baada ya kueleza jinsi kinavyotayarishwa na kwamba “hunywewa kikiwa na joto la kadiri ambayo waweza kuvumilia,” aliongeza kwamba “Wachina huhazini kinywaji hiki kama vile waalkemia hufanya na Lapidum Philosophorum yao . . . . yaani, jiwe la mwanafalsafa.” Hata hivyo, alisifu chai pia kuwa yenye matokeo, ingawa ni ghali, kuwa ni dawa ya namna zote za maradhi.
Kikombe Ambacho Huwachangamsha Waingereza
Hata ingawa Waingereza ndio wanywaji wa chai walio wa kupindukia leo, Waholanzi na Wareno pia walisaidia kuwageuza watumie chai. Yaaminiwa kwamba Wayahudi, ambao Oliver Cromwell alikuwa amewaalika warudi Uingereza kutoka uhamisho wao katika Amsterdam, walikuja wakiwa na chai. Septemba 23, 1658 ikathibitika kuwa tarehe yenye kukumbukika kuhusu chai. Ilikuwa ndiyo mara ya kwanza tangazo la chai kutokea katika gazeti la Kiingereza. Mercurius Politicus ilitangaza kwamba kinywaji ambacho Wachina hukiita tchan lakini ambacho watu wengine hukiita chai kingeuzwa katika Sultan’s Head, mkahawa wa Jiji la London. Miaka mitatu baadaye, mfalme Mwingereza Charles 2 alioa bibi mwenye ladha nzuri ya chai, binti-mfalme wa Kireno Catherine wa Braganza, aliyeanzisha muda wa kunywa chai katika maskani ya kifalme ya Uingereza. Huo ukawa ni ushinde thabiti juu ya vinywaji vyenye alkoholi, ambavyo vyaripotiwa kuwa vilikuwa vikinywewa “wakati wa asubuhi, wakati wa adhuhuri, wakati wa jioni,” na mabwana na hata mabibi wakuu. Kwa ghafula, chai ikawa imekuwa kinywaji cha mtindo ufaao.
Ingawa ilifanyizwa maelfu ya kilometa za mbali, chai ililetwa London kwa wingi mkubwa hata zaidi. Baada ya muda Kampuni ya East India ikajipatia haki kamili za biashara ya chai katika China, ikidhibiti biashara pamoja na Mashariki ya Mbali kwa miaka ipatayo 200. Sehemu kubwa ya Ulaya ilianza kunywa chai, ingawa Ufaransa haikugeuzwa iwe ikitumia kinywaji kipya hicho.
Chai, Kodi, na Vita
Chai ilikuwa ufanisi wa ghafula kwa serikali zenye kusongwa sana na matatizo. Kwanza kodi ilitozwa kila siku kwa wingi halisi wa chai iliyonywewa katika mikahawa ya London. Utaratibu huu wenye jitihada ngumu ulifutiliwa mbali katika 1689, wakati ambapo ushuru ulitozwa kwa kila ratili ya majani makavu ya chai. Kodi za kufikia asilimia 90 na uhitaji wenye kuongezeka uliongoza kwenye ulanguzi wenye kuvuvumka kwenye mwambao wa pwani ya kusini ya Uingereza, kwa maana chai ilikuwa ya bei rahisi zaidi katika Kontinenti hiyo. Hata chai za bandia zilifanyizwa. Majani-chai yaliyotumika yalifanyizwa upya kwa kutiwa asali ya miwa na udongo—ikisemekana ni kurudisha rangi ya asili ya chai—halafu yakakaushwa na kuuzwa tena. “Mtohoaji” mmoja alifanyiza kile kilichoitwa “smochi,” mchanganyo wenye harufu mbaya za majani kijivu na wenye kuchovywa katika samadi ya kondoo, ambayo baada ya hapo ilichanganywa na chai halisi kabla ya kuuzwa!
Chai hata ilibadili mwendo wa historia. Kutoza kodi ya peni tatu kwa ratili kulifyatusha Vita ya Kiamerika ya Uhuru. Wabostoni wenye kasirani walishutumu kodi hii “ndogo sana lakini ya kutumia nguvu.” Wakoloni wenye kasirani nyingi, baadhi yao wakisingizia kuwa Waamerika wenyeji (Wahindi), waliingia kwa fujo katika sitaha za Wahindi Wamashariki watatu iliyotiwa nanga katika bandari, wakapasua makasha ya chai, na kutupa shehena nzima baharini. Kutokana na hilo ukaja ule msemo “Karamuchai ya Boston.” Mengine yote ni historia.
Vita nyingine ilifanywa kuhusu chai, ile Vita ya Kasumba. China ilikuwa imelipwa fedha kwa kusafirisha chai nje, kwa maana hakukuwa na dai la bidhaa za Ulaya. Hata hivyo, kasumba ilikuwa bidhaa yenye kutamaniwa sana, ingawa yenye kukatazwa. Kampuni ya East India ilifanya haraka kutimiza dai hilo kwa kubadilishana kasumba kwa chai. Kampuni hiyo isiyoongozwa na dhamiri ililima mikasumba katika mashariki ya India ili wagawie soko kubwa sana la Kichina. Biashara hii isiyo halali iliendelea kwa miaka kumi, ikitosheleza maficho mengi sana ya kushughulikia ya kasumba, mpaka mwishowe ikakatizwa na serikali ya Kichina. Baada ya mizozo kati ya Waingereza na Wachina kuhusu suala hili, vita ilitokea ambayo ilimalizika kwa ushinde wenye kuwashusha Wachina katika 1842. Chai ilisafirishwa tena Uingereza, na China ikalazimishwa kukubali kasumba ziingizwe nchini.
Kwa Nini Usinywe Kikombe cha Chai?
Mapema katika historia ya chai, ilitambuliwa kwamba chai inasisimua, sana-sana kwa sababu ya kuwa na kafeni. Kwanza chai iliuzwa katika maduka ya dawa na ikaonwa kuwa ponyo la maradhi yote yenye kutofautiana sana kama kujazana kwa maji katika maungo ya mwili na ugonjwa wa kutoka damu na ugonjwa wa kutoka damu katika fizi za meno na ngozi. Pia ilichukuliwa kuwa dawa yenye kufaa ukosefu wa hamu ya kula na pia kula kupita kiasi. Leo, chai yajulikana kuwa ina hesabu fulani ya vitamini za “B-complex.” Hata hivyo, huongezea pia kiasi cha kafeni yenye kuingia mwilini. Zaidi ya hilo, katika jamii ya Magharibi yenye kufikiria sana kalori (vipimo-nishati vyenye kuingia mwilini kutokana na chakula), yastahiki kukumbuka kwamba kikombe kimoja cha chai kina kalori nne tu kikinywewa bila maziwa na sukari.
Chai humalizika nguvu kwa urahisi. Haiwezi kurundikwa pamoja kwa zaidi ya miezi michache. Na juu ya yote, ni lazima iwekwe kwa njia ifaayo. Usiiweke kamwe pamoja na vimea vingine vya unywaji au, hata vibaya zaidi, pamoja na vikolezo. Chai hufyonza kwa urahisi ladha ya kitu chochote chenye kuwekwa kando yayo, tena hufanya hivyo sana hivi kwamba wasimamizi Waingereza wa mashamba ya chai wa karne iliyopita walifanya wachuma chai waoge mwili kwa kujinyunyizia maji kila wakati walipoenda kazini!
Isitoshe, chai yenye kutiwa barafu yaweza kuwa tamu pia. Wakati wa Onyesho la Ulimwengu la St. Louis katika 1904, Mwingereza mmoja hakuweza kuwauzia chai moto sana wageni wake waliokuwa tayari wanatoa jasho. Kwa hiyo jambo alilofanya tu ni kuimimina juu ya barafu, na huo ukawa ndio mwanzo wa kinywaji chenye kuburudisha Amerika wakati wa kiangazi.
Waingereza hunywa chai yao na maziwa, Wafrisia katika kaskazini ya Ujeremani huionea shangwe pamoja na kendi iliyotiwa katika barafu na kupakwa krimu juu, Wamoroko huiongezea ladha ya minti, huku Watibeti wakiongeza chumvi na siagi ya fahali-yaki. Hata hivyo, wapenzi wengi wa chai hufuata sana dokezo la zamani la Lu Yu na kutayarisha chai pamoja na maji safi yenye kuchemka kutoka mlimani, kokote ambako huwa yanapatikana.
Baada ya kusoma mengi sana juu ya chai, je! wewe wahisi ukiwa mwenye kiu? Kwa nini usinywe kikombe kizuri cha chai sasa hivi?
[Sanduku katika ukurasa wa 27]
“Shukrani ziendee Mungu kwa chai! Ulimwengu ungefanya nini bila chai?—ilitokeatokeaje? Mimi naterema sikuzaliwa kabla ya chai.”
Sydney Smith (1771-1845), mwandikaji Mwingereza
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 28]
Kutoka Kwenye Shamba Hadi Kwenye Birika ya Chai
Kuna mamia ya michai tofauti leo, yote ikiwa ni michanganyiko ya namna kubwa tatu. Kwa kawaida mashamba ya chai hupatikana katika maeneo ya milima-milima ambako maji ya mvua yaweza kukauka kwa kutiririka mitaroni. Jimbo kubwa zaidi lenye kukuza chai leo ni Assam, katika mkoa wa kaskazini ya India wenye jina ilo hilo. Hata hivyo, chai iliyo “kabambe” yasemwa kuwa hutoka Darjeeling, katika maeneo yaliyo chini ya Milima Himalaya. Hali za mvua-mvua nchini na udongo wenye asidi hushirikiana kutokeza moja ya chai zilizo bora zaidi, hiyo ikifanya Darjeeling iwe “bara la ahadi” la chai.
Katika Darjeeling zao hilo ni la majira, na wachuma chai huwa na shughuli nyingi katika Machi na Aprili wakikusanya maivo ya kwanza, ambayo yataonewa fahari sana, yakiwa na ladha nyepesi-nyepesi. Maivo ya pili, ambayo huchumwa wakati wa kiangazi, ni chai yenye umbo kamili yenye rangi ya manjano-kahawia, hali chai zile za kawaida huvunwa baadaye wakati wa vuli. Kwingineko uchumaji hufanywa muda wote mwakani kwa vipindi-vipindi vya siku chache hadi majuma kadhaa. Kwa kadiri ambavyo vichipukizi ni vichanga na vyororo, ndivyo chai itazidi kuwa bora. Uchumaji hutaka ustadi mwingi na uangalifu. Ingawaje, vichipukizi kama 30,000 huwa ratili 13 tu za chai ya Darjeeling, hiyo ikiwa ndiyo kazi ya siku ya mchumaji stadi. Lakini kilichovunwa huwa si chai bado.
Sasa, utaratibu wa matayarisho ya hatua nne huanza. Kwanza, vichipukizi hivyo vichanga vya kijani huhitaji kunyauka ili vipoteze kama asilimia 30 ya umajimaji wavyo na kuwa vyororo na laini kama ngozi kavu. Ndipo huwa tayari kufingirishwa, hiyo ikiwa ndiyo hatua ifuatayo. Kupitia kufingirishwa, kuta za chembe za majani huvunjwa zikawa wazi, zikitoa utomvu wa kiasili ambao huipa chai ladha yenye kuipambanua. Wakati wa hatua ya tatu, majani-chai hubadilika kutoka kijani-manjano na kuwa na rangi yayo ya kawaida ya shaba-kahawia. Utaratibu huu huitwa uchachishaji. Majani yaliyovunjwa hutandazwa kwenye meza mbalimbali katika halihewa yenye ujotojoto na kuanza kuchacha. Sasa ni lazima majani hayo yakaushwe, au yapashwe moto. Utaratibu huu hugeuza majani yawe meusi, na ni wakati tu utayamwagia maji moto kwamba yatakuwa tena na rangi ya shaba-kahawia.
Mwishowe, majani yaliyokaushwa huchaguliwa na kupakiwa katika makasha ya mbao-plai iliyozungushiwa karatasi ya mchele na fungio lililofanyizwa kwa aluminamu, tayari kusafirishwa kwa wanabiashara sehemu zote za ulimwengu. Halafu, baada ya kuburugwaburugwa na kuchanganywa vizuri, chai iko tayari kupikwa katika birika lako la chai.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Wachina wakipima chai