Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 7/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Shimo la Kipekee Lapatikana Katika Tabaka ya Ozoni ya Antaktiki
  • Mwaka wa Ongezeko la Joto la Tufeni Pote
  • Kizibo, Uchumi, na Wanyama wa Mwitu
  • ‘Vita Baridi’ Vipya
  • Maziko Ambayo Huongeza Umaskini
  • Jinsi Majani Chai Yaliyokaushwa kwa Mvuke Yawezavyo Kupigana na Chembe za Kansa
  • Watoto na Kuumwa na Mbwa
  • Je, Ni Marashi ya Mfumo wa Reli za Chini ya Ardhi?
  • Mazoezi ya Kudumisha Usawaziko ili Kuzuia Kuanguka
  • Elimu na Vifo vya Watoto Wachanga
  • “Si kwa Chai Yote Katika China!”
    Amkeni!—1990
  • Kunywa Chai Kama Wachina
    Amkeni!—2005
  • Angahewa Letu Linapoharibiwa
    Amkeni!—1994
  • Je, Watoto Wako Salama Wakiwa na Mbwa Wako?
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 7/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Shimo la Kipekee Lapatikana Katika Tabaka ya Ozoni ya Antaktiki

Katika Septemba 1998, shimo ambalo hutokea kila mwaka katika tabaka ya ozoni juu ya Antaktiki lilifikia rekodi ya juu kabisa, laripoti The UNESCO Courier. Picha za setilaiti zilionyesha kwamba shimo hilo lilikuwa limekua kufikia ukubwa wa bara Ulaya mara mbili na nusu. Tabaka ya ozoni katika angastrato hulinda viumbe hai ulimwenguni na mifumikolojia kutokana na mnururisho wa urujuanimno wa jua. Mnururisho unapoongezeka hufanya watu wakabili hatari kubwa zaidi ya kubabuliwa na jua, kupata kansa ya ngozi, na magonjwa ya macho, yasema ripoti hiyo. Kloroflourokaboni (CFC), ambazo hutumiwa kama vipoza joto na visukuma-kipulizaji, zinasemekana kuwa kisababishi kikuu kinachoharibu tabaka ya ozoni. Mnamo mwaka wa 1987, kwenye mkutano uliofanywa Montreal, nchi 165 ziliapa kuacha kabisa kutumia vitu hivi. Licha ya hilo, The UNESCO Courier lasema kwamba “itachukua angalau muda wa miaka 60 kwa CFC kutoweka kabisa kutoka kwenye angastrato.”

Mwaka wa Ongezeko la Joto la Tufeni Pote

Mwaka jana, 1998, ulikuwa mwaka wenye joto zaidi tangu 1860, laripoti gazeti Science News. Iliripotiwa kwamba wastani wa halijoto ya dunia ulifikia digrii 0.58 Selsiasi zaidi ya wastani wa halijoto kati ya 1961 na 1990. “Kwa wataalamu wa tabia ya nchi, wanaohangaika kuhusu mabadiliko ya digrii moja kwa mia ya tufeni pote, joto la mwaka jana lilikuwa la juu kupita kiasi,” lasema gazeti hilo. Pia ripoti hiyo yasema kwamba miaka saba kati ya miaka iliyokuwa na joto zaidi kupata kurekodiwa imekuwa tangu 1990, na miaka kumi ya kwanza tangu mwaka 1983. Kulingana na Jonathan Overpeck, wa shirika la Marekani la National Oceanic and Atmospheric Adminstration, huenda miongo miwili iliyopita ndiyo iliyokuwa yenye joto zaidi katika miaka 1,200 iliyopita. Shirika la Kimeterolojia Ulimwenguni laripoti kwamba ni sehemu za kaskazini mwa Ulaya na Asia peke yake ambazo hazikuwa na ongezeko. Sehemu za kusini mwa Marekani zilikuwa na joto kali mno la kiangazi, na katika Urusi ya kati halihewa yenye joto katika Juni iliua zaidi ya watu 100 na kusababisha mioto mikubwa.

Kizibo, Uchumi, na Wanyama wa Mwitu

Asilimia themanini ya vizibo ulimwenguni hutoka kwenye ganda la mti aina ya cork-oak unaopatikana kusini mwa Hispania na Ureno. Wakulima huko hubambua ganda la miti yao mikubwa sana kila baada ya miaka tisa. Mti aina ya cork-oak ndio mti pekee ambao ganda lake humea upya katika njia hii. Hivi karibuni, kazi hii ambayo imefanywa kwa karne nyingi imetishwa na ongezeko la matumizi ya vifuniko vya chupa vya plastiki, laripoti Guardian Weekly la Manchester, Uingereza. Ikiwa kiwanda cha vizibo vya asili kitaporomoka, huenda miti hiyo ikakatwa ili kupanda mazao yenye kuleta faida zaidi. Wahifadhi wa mazingira wanahofu kwamba ndege wengi hawatakuwa na misitu wanayoitegemea ili kuendelea kuishi. “Aina 42 za ndege hutegemea miti ya oak,” lasema gazeti hilo la habari, “kutia ndani tai wa Hispania aliye hatarini mwa kutoweka ambaye hujenga viota kwenye miti hiyo na ambaye idadi yake ni jozi 130.”

‘Vita Baridi’ Vipya

“Wenye maduka wanajaribu kujaza friza zao huku watu wa Slovenia wakinunua kwa hamu aiskrimu za aina tofauti-tofauti na za ladha mbalimbali zinazopatikana,” laripoti gazeti la habari la Delo la Ljubljana. Kulingana na gazeti hilo la habari, watu wa Slovenia wanazidi kupendezwa na aiskrimu—watengenezaji wa aiskrimu wa huko, hivi karibuni walipata ongezeko la asilimia 22 la mauzo ya mwaka mzima. Kwa kiwango hiki cha ukuzi, matumizi ya kitaifa ya aiskrimu ya lita 4.3 kwa mtu mmoja, hatimaye yatapita wastani wa Magharibi mwa Ulaya wa lita 5.5. Hata hivyo, kuhusu ni nani wanaotumia aiskrimu zaidi, bado Wasweden wanaongoza kwa mbali. Kulingana na kikundi cha wasomi wa soko Euromonitor, mkazi mmoja wa Sweden hutumia kwa wastani takriban lita 16 za aiskrimu kila mwaka. Wamarekani wanaongoza ulimwenguni pote, wakila zaidi ya lita 20 kila mwaka kwa mapato ya kila mtu katika taifa.

Maziko Ambayo Huongeza Umaskini

“Gharama ya maisha inazidi kuongezeka,” laripoti Times of Zambia, “lakini . . . gharama ya kufa inaongezeka hata zaidi.” Katika sehemu nyingi za Afrika, kutia ndani Zambia, mara nyingi maziko hucheleweshwa ili kuruhusu muda kwa marafiki na watu wa jamaa kutoka mbali waje kujiunga na desturi za maombolezo zinazochukua muda wa juma moja au zaidi. Mara nyingi, wote wanaokuwapo hutazamia kulishwa na kuandaliwa mahali pa kulala. Pia familia iliyofiwa hutazamiwa iandae nauli kwa wenye uhitaji ili kurudi nyumbani kwao. Maziko ya aina hiyo hufanya familia nyingi zilizofiwa ziingie katika umaskini hata zaidi. “Maziko ya kisasa,” yasema ripoti hiyo, “yanaendelea kuwa ya gharama ya juu zaidi kwa sababu ya idadi kubwa ya waombolezaji ambao hawasaidii kwa njia yoyote.” Gazeti hilo la habari lapendekeza kwamba maziko yafanywe punde tu baada ya mtu kufa kusudi wapunguze mzigo kwa waliofiwa.

Jinsi Majani Chai Yaliyokaushwa kwa Mvuke Yawezavyo Kupigana na Chembe za Kansa

Uchunguzi unaonyesha kwamba watu wanaokunywa chai iliyokaushwa kwa mvuke hupatwa na visa vichache vya kansa na kwamba hata wanyama waliopewa chai hiyo hunufaika kwa njia sawa. Hivi karibuni, watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Purdue huko Indiana, Marekani, waligundua kile ambacho kingeweza kuchangia jambo hilo, laripoti Science News. Kitu fulani kinachoitwa epigallocatechin (EGCg) ambacho hupatikana katika majani chai yaliyokaushwa kwa mvuke, huzuia kimengenya fulani ambacho huhitajiwa na chembe za kansa kusudi zigawanyike. Yaelekea EGCg haina matokeo yaleyale katika ugawanyikaji wa chembe za kawaida. Chai iliyovundishwa, ambayo hupendwa na asilimia 80 ya wanywaji chai ulimwenguni, ina kiasi kidogo cha EGCg. Watafiti wanasema kwamba uhakika huo waweza kueleza sababu inayofanya chai iliyovundishwa iwe na matokeo sawa na chai iliyokaushwa kwa mvuke kwa kiwango cha sehemu moja ya kumi hadi sehemu moja ya mia katika kuzuia utendanaji wa kimengenya katika chembe za kansa zinazokuzwa ndani ya chupa.

Watoto na Kuumwa na Mbwa

Watoto wadogo ndio huumwa na mbwa zaidi huko Marekani, charipoti kijarida UC Berkeley Wellness Letter. Hata hivyo, ripoti hiyo yaeleza kwamba, visa vingi vya kuumwa na mbwa vyaweza kuzuiwa. Ili kupunguza hatari hiyo, Wellness Letter chapendekeza kwamba wazazi waanze kwa kuteua kitoto cha mbwa chenye silika nzuri. Kisha, wanapaswa wakihanithishe, halafu kwa fadhili lakini kwa imara wakizoeze kutii na kuwa na urafiki na watu, hasa watoto. Kijarida Wellness Letter chasema: “Usikate kauli kamwe kwamba hata yule mbwa mwanana zaidi atampokea mtoto mpya au atatofautisha kati ya kitoto kichanga. Msimamie.” Watoto wanapaswa kufundishwa kwamba hawapaswi kumkaribia mbwa wakiwa peke yao. Mwache mwenye mbwa amlete. Sema na mbwa, na mpe ngumi iliyokunjwa ili ainuse. Mbwa akibweka au kuinua malaika kwa hasira, baki ukiwa mtulivu na usigeuke na kukimbia. Kijarida Wellness Letter chasema: “Mbwa, sawa na mbwa-mwitu, kwa kuongozwa na silika watamkimbiza na kumshambulia mtu anayekimbia.”

Je, Ni Marashi ya Mfumo wa Reli za Chini ya Ardhi?

Maofisa wa usafiri katika Ufaransa wametokeza marashi mapya ili kuboresha harufu isiyopendeza sana ya mfumo wa reli za chini ya ardhi wa Paris. Mnukio huo, unaoitwa Madeleine ambalo ni jina la mojawapo ya vituo vya reli za chini ya ardhi, unaongezewa katika bidhaa za kusafishia zinazotumiwa na mfumo wa reli, laripoti shirika la habari la Reuters. Mkurugenzi wa mfumo wa reli za chini ya ardhi Jacques Rapoport alieleza kwamba jitihada hiyo ilihitaji miaka mitano ya utafiti na usitawishaji. “Tulihitaji kutafuta harufu ambayo ni yenye kupendeza badala ya harufu kali, ambayo ingedumu kwa muda wa majuma mawili na ambayo ilitokeza picha ya usafi na hali njema,” akasema. Maofisa wa mfumo wa reli za chini ya ardhi walisema kwamba Madeleine inakusudiwa kutokeza mnukio wa “mashambani, miti, maua na matunda.”

Mazoezi ya Kudumisha Usawaziko ili Kuzuia Kuanguka

“Thuluthi moja ya watu walio na umri wa zaidi ya miaka 65 huanguka angalau mara moja kwa mwaka, wengi wao wakiumia kama vile kuvunjika nyonga ambazo huenda zisipone kamwe,” laripoti The New York Times. Kadiri tuzeekavyo, uwezo wa mwili wetu wa kutambua mahali ulipo hupungua, jambo ambalo hufanya iwe vigumu zaidi kudumisha usawaziko. Uchunguzi wa hivi majuzi kwenye Chuo Kikuu cha Connecticut School of Medicine waonyesha kwamba mazoezi ya kawaida ya kudumisha usawaziko, kama vile kusimama kwa mguu mmoja au kutembea juu ya mhimili wa mbao, yaweza kuboresha usawaziko wa watu wenye umri mkubwa zaidi. Hata hivyo, Gina Allchin wa kituo cha mazoezi cha Sullivan & Cromwell, ashauri kuanza polepole, kufanya vipindi vya mazoezi vichukue muda wa dakika kumi, mara mbili au tatu kwa juma. Asema hivi: “Mazoezi ya namna hii huchosha pasipo kujua na yaweza kukuacha ukiwa umeishiwa nguvu kabisa na kuumwa ukifanya kupita kiasi.”

Elimu na Vifo vya Watoto Wachanga

“Ni dola bilioni 7 zaidi zinazohitajika kila mwaka kwa ajili ya mwongo ujao ili [kuandikisha watoto wote kwenye shule] za msingi ulimwenguni pote kufikia mwaka wa 2010,” yasema The State of the World’s Children 1999—Education, ripoti ya Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa. “Jumla hii ni ndogo kuliko kiasi ambacho Wanaulaya hutumia kwa aiskrimu au kiasi ambacho Wamarekani hutumia kwa vipodozi kila mwaka.” Kulingana na The Times of India, ni asilimia 66 peke yake ya wanaume na asilimia 38 ya wanawake katika India wanaojua kusoma na kuandika. Mahali ambapo wanawake zaidi wanaandikishwa katika shule za msingi, vifo vya watoto wachanga hupungua. Tokeo la elimu hiyo ya msingi laweza kuonekana katika jimbo la Kerala, kusini mwa India, ambako asilimia 90 hivi ya watu wanajua kusoma na kuandika na “kiwango cha vifo vya watoto wachanga ni cha chini zaidi katika nchi zote zinazositawi.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki