Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 8/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuona Pafaapo
  • Wachokozi wa Shuleni Australia
  • Kafeni na Mimba
  • Miili Iliyochafuliwa, Mifumo-Mazingira Iliyochafuliwa
  • Kadiri ya Mweneo wa Kasoro za Akili
  • Hatari ya Alkoholi Kuhusiana na Upasuaji
  • Watoto Vitani
  • Jitihada Isiyofua Dafu Dhidi ya Nzige
  • Wataalamu-Anga wa Jadi
  • Lugha ya Wafanyakazi Ofisini
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Tatizo la Hubble—Lilitokeaje?
    Amkeni!—1995
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 8/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kuona Pafaapo

Baada ya kushindwa kwa aibu mara kadhaa, NASA, lile shirika-anga la Marekani, laonekana limefanya ushinde mmoja ukawa ushindi. Darubini iitwayo Hubble Space Telescope, liliyoirusha shirika hilo 1990 kwenda kuzunguka angani, ina kasoro ya kioo kikuu, iliyozuia darubini hiyo kuona pafaapo. Ingawa hivyo, Desemba 1993 wanaanga wanaotembea angani walitumia saa 30 wakiweka vioo vya kurekebisha kasoro hiyo ya darubini isiyoona vizuri na kubadili vifaa vikuukuu. Matokeo? Laripoti gazeti New Scientist: “Katika mambo fulani Hubble inafanya kazi vizuri kuliko ilivyotazamiwa awali.” Kulingana na gazeti Newsweek, “rekebisho la Hubble sasa ni zuri sana hivi kwamba darubini hiyo ingeweza kuona kimulimuli akiwa umbali wa kilometa 14,000.” Baada ya kuona picha za kutoka darubini ambayo sasa imerekebishwa, Duccio Maccheto wa Shirika-Anga la Ulaya asemekana alipaaza sauti hivi: “Sina la kusema ila kushangaa, weee.”

Wachokozi wa Shuleni Australia

Watoto shuleni wanatenda kijeuri katika umri wa mapema Australia, laripoti gazeti The Australian. Katika nchi hiyo asilimia 20 ya watoto husema hawajihisi salama shuleni; mtoto 1 kati ya 7 huchokozwa. Watafiti waeleza kwamba watoto wataka-matata huelekea kutofanikiwa sana masomoni na hawajistahi. Yaliyochunguzwa yadokeza kwamba filamu, vidio, na kuonyesha jeuri katika vyombo vya habari huathiri vijana. Wavulana ndio wakosaji wabaya zaidi, na wasichana na wafanyakazi wa shule ndio hudhulumiwa mara nyingi zaidi. Hata walimu hutaabishwa na wachokozi shuleni, na sasa wengi hawataki kushughulika na wanafunzi matata ili visasi visitokee. Shirika moja la walimu limeomba redio za kupashana habari ziandaliwe walimu wakaguao nyanja za shule saa za chakula cha mchana.

Kafeni na Mimba

Katika 1980 Usimamizi wa Chakula na Dawa Marekani ulipendekeza kwamba wanawake wenye mimba wapunguze kunywa kafeni, kemikali iliyo katika vinywaji vya kahawa, chai, kakao, na kola. Pendekezo hilo lilifanywa kwa kutegemea majaribio yaliyofanyiwa wanyama.[1] Hata hivyo, tangu wakati huo machunguzo yaliyofanyiwa wanawake wenye mimba yameonyesha wazi zaidi uhitaji wa tahadhari ya kutumia kafeni. The Journal of the American Medical Association liliripoti majuzi kwamba asilimia 75 ya wanawake wenye mimba hunywa kafeni, ingawa machunguzo yaliyo mengi zaidi yameonyesha kwamba kunywa zaidi ya miligramu 300 za kafeni kwa siku (karibu vikombe vitatu vya kahawa) kwaweza kudhuru kijusu.[2] Ingawa hivyo, uchunguzi wa karibuni zaidi waonyesha kwamba hata kiasi kidogo zaidi cha kafeni—miligramu 163 kwa siku—kingeweza kuongezea hatari ya mimba kujitoa yenyewe katika wanawake fulani.[3] Waongoza uchunguzi wasema: “Pendekezo lifaalo lingekuwa kupunguza kutumia vinywaji vya kafeni wakati wa mimba.”[4]

Miili Iliyochafuliwa, Mifumo-Mazingira Iliyochafuliwa

Huenda isishangaze sana kwamba watu kama 3,020 Marekani hufa kila mwaka baada ya kutumia kokeni; athari za uchafuzi wa dawa hiyo katika mwili wa kibinadamu yajulikana sana. Lakini National Geographic liliripoti majuzi kwamba kufanyiza dawa ya kulevya hiyo husababisha uchafuzi mzito katika mito na vijito vya misitu-mvua ya Bolivia, Peru, na Kolombia. Gazeti hilo lasema: “Karibu tani 308 za kokeni zilikamatwa ulimwenguni pote na maofisa katika 1992, kulingana na Usimamizi wa Kudhibiti Dawa Marekani. Kutengeneza kokeni ya kiasi hicho—kisehemu tu cha jumla kubwa iliyotengenezwa—kulihitaji lita milioni 106 za mafuta-taa, lita milioni 4.2 za vimumunyishaji, lita milioni 1.1 za asidi sulfuriki, lita 70,000 za asidi hidrokloriki, na lita 14,000 za amonia. Sehemu kubwa ya kiasi cha jumla hutupwa mitoni, ikiharibu viumbe wa majini na kuchafua maji ya unyunyizaji na ya kunywa.”

Kadiri ya Mweneo wa Kasoro za Akili

The New York Times liliripoti mapema katika 1994: “Karibu mmoja kati ya Waamerika wawili—asilimia 48—wamepatwa na kasoro ya akili wakati fulani maishani mwao.” Uchunguzi ulioongozwa na wanasosholojia kwa wanaume na wanawake zaidi ya 8,000, ukitumia mahoji ya kuonana uso kwa uso ili kutafuta visababishi, ulipata kwamba kasoro ya kawaida zaidi ilikuwa mshuko mkuu wa moyo; asilimia 17 walikuwa wamepatwa nao wakati fulani maishani. Asilimia 14 walikuwa wamekuwa wakitegemea kileo wakati fulani. Times liliripoti kwamba mojapo mashangazo ya uchunguzi huo ni kwamba asilimia 12 ya wanawake hao walikuwa wametaabishwa na kasoro ya mkazo wa mawazo baada ya kukabwa sana na mshuko wa moyo, na nusu ya visa hivyo “ilitokana na kunajisiwa au kunyanyaswa kingono.” Kati ya wote wale waliokuwa wametaabishwa na kasoro za kiakili, ni robo tu waliokuwa wametafuta msaada wa wataalamu. Dakt. Ronald C. Kessler, mwanasosholojia aliyeongoza uchunguzi huo, anukuliwa akisema: “Habari mbaya ni kwamba kasoro za kiakili ni nyingi kuliko tulivyokuwa tumefikiri. Habari njema ni kwamba watu wengi zaidi hupona—wengi wakipona wenyewe tu—kuliko vile ungewazia.”

Hatari ya Alkoholi Kuhusiana na Upasuaji

Wagonjwa watumiao vinywaji zaidi ya vitano vya alkoholi kila siku wataelekea kupatwa na matatanishi yafuatayo upasuaji mara tatu kuliko wagonjwa wanywao kidogo zaidi, kulingana na mpasuaji mkuu wa Denmark Dakt. Finn Hardt. Kama vile Jarida la Shirika la Kitiba la Denmark lilivyoripoti majuzi, utumizi mbaya wa alkoholi una athari yenye sumu juu ya karibu mifumo yote ya viungo; husababisha ongezeko la kuelekea kuvuja damu na pia matatizo ya moyo na mapafu. Hali hizo kwa kawaida hufanya madaktari wawalaze hospitalini muda mrefu zaidi na kutiwa damu nyingi zaidi mishipani. Wale wanywao alkoholi nyingi zaidi kila siku huhatarisha kudhoofisha pia mfumo wao wa kinga, hivyo wakisababisha hatari ya ambukizo. Hata hivyo, machunguzo yamethibitisha kwamba baada ya majuma kadhaa ya kujiepusha, mfumo wa kinga huboreshwa sana. Dakt. Hardt apendekeza kwamba kabla ya upasuaji wowote, wagonjwa wajiepushe na kileo kwa kipindi hicho.

Watoto Vitani

Katika miaka kumi iliyopita, karibu watoto milioni 1.5 wameuawa vitani, kulingana na The State of the World’s Children 1994, ripoti ya Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa. Wengine milioni nne wamelemazwa, wakaharibiwa maungo, wakapofushwa, au wakaharibiwa ubongo. Idadi ya watoto ambao wamekuwa wakimbizi yakadiriwa kuwa angalau milioni tano. Watoto hata wameingizwa katika majeshi. Katika nchi nyingi watoto wameteswa na kulazimishwa kutazama au kushiriki katika matendo ya unyama. Katika eneo moja kunajisiwa kwa wasichana kumekuwa “silaha ya vita ya kawaida.” Ripoti hiyo yasema: “Yaonekana sawa kukata shauri kwamba ustaarabu haujapata kukosa matokeo kwa kadiri ulivyo sasa.”

Jitihada Isiyofua Dafu Dhidi ya Nzige

“UM unafanya jitihada isiyofua dafu dhidi ya nzige,” likaripoti gazeti New Scientist mapema 1994. Kulingana na mkutano wa majuzi wa wanasayansi wa kilimo katika Uholanzi, ile jitihada ya kutumia dola milioni 400 ambayo Umoja wa Mataifa ilifanya dhidi ya nzige miaka ya mwishoni ya 1980 ilitimiza machache. Kwa kweli kilichomaliza kumbo hilo la nzige ni upepo usiotarajiwa uliopeperusha wadudu hao baharini. Nzige huzaliana kisha huruka wakiwa mabumba wakati mvua ya vipindi inyunyiziapo jangwa, ikitokeza visehemu vyenye ujani mbichi. Shirika la UM la Chakula na Kilimo hujaribu kuua nzige kabla hawajaruka wakiwa mabumba, likitegemea picha za sateliti zionyeshazo visehemu vilivyo kijani kibichi jangwani. Tatizo ni kwamba sateliti hizo hazipati vingi vya visehemu vidogo zaidi. Ardhini, vita vya mahali na ukosefu wa rasilmali huzuia vikoa vya wanyunyizaji wasifikie hata maeneo yajulikanayo ya uzaliani.

Wataalamu-Anga wa Jadi

Je, wataalamu-anga huishi sana kuliko watu wengine? Gazeti la Ujerumani la sayansi-asili Naturwissenschaftliche Rundschau laripoti juu ya uchunguzi wa urefu wa maisha ya watu waliozaliwa kati ya 1715 na 1825. Katika miaka hii, wanaume 67 waliokuwa wataalamu-anga wakiwa na miaka 25 walifikia mudamaisha wa wastani wa miaka 71.6. Karibu nusu ya wanaume hawa walikuwa Wajerumani, hata hivyo wanaume Wajerumani wa miaka 25 katika kipindi hiki walikuwa na tazamio la wastani la kuishi miaka 60.7 tu. Kwa nini wataalamu-anga waishi zaidi? “Yawezekana kwamba tazamio la maisha la wataalamu-anga lahusiana kwa njia fulani na unyamavu na utulivu uhusuo kazi yao,” laripoti gazeti hilo. Au, gazeti hilo lawaza, “labda kule tu kufanya kazi ihusianayo na maajabu ya ulimwengu wa anga na kuyakazia sana fikira huenda kukawa na matokeo mazuri juu ya afya ya mtu.”

Lugha ya Wafanyakazi Ofisini

Katika Italia lugha ya kikazi na kiofisi ya hati nyingi rasmi ni ngumu sana kueleweka hivi kwamba usimamizi wa umma Italia waamini lazima usahilishwe. Kulingana na Waziri wa Kazi za Umma, Sabino Cassese, “huu ni usimamizi usiowasiliana tena na raia zao, usiosema nao lugha moja.” Kwa hiyo sasa wanaofisi watalazimika kuanza kusema Kiitalia rahisi badala ya “kilugha cha ofisini,” ambacho ni lugha iliyojaa maneno yasiyotumika sana. Badiliko hilo lilitangazwa kwenye utoaji wa “Kanuni za Kufuatwa kwa Mawasiliano ya Maandishi Katika Usimamizi wa Umma.” Kamusi hiyo inayoandaa msamiati wa maneno 7,050 ya msingi yenye kueleweka kwa urahisi ina lengo la kuondoa maneno magumu mengi ya kikale ambayo hufanya sheria, fomu, barua za mweneo mkubwa, na ilani za umma zisieleweke na raia wa wastani.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki