Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Internet Najifunza ufundi wa kompyuta, na nataka kuwapongeza kwa ule mfululizo “Internet—Je, Yakufaa?” (Julai 22, 1997) Makala hizo zilikuwa fupi, zenye kuarifu, na sahihi kisayansi. Hamkukubali ubaguzi usio na maana na hofu zinazoizunguka Internet. Kwa upande ule mwingine, hamkuficha hatari halisi.
L. E., Italia
Mimi hufunza masomo ya kompyuta, na ili niweze kujua mambo ya karibuni zaidi, kwa kawaida mimi hununua magazeti yanayohusu kompyuta. Hakuna hata moja la magazeti hayo ambalo limeweza kusema kwa uwazi kuhusu manufaa na hatari za Internet.
A. A. S., Brazili
Karibuni nimekuwa nikisikia mengi kuhusu Internet, lakini sikuweza kuielewa kabisa. Mfululizo wenu ulieleza jambo hilo kwa usahili na kwa njia iliyo rahisi kufuata.
A. H., India
Mliandika kwa njia ambayo hata wasomaji wenye ujuzi mdogo au wasio na ujuzi wowote kuhusu Internet wangeweza kuelewa kwa urahisi. Mlitusaidia pia kutua na kufikiria gharama za kutumia huduma hii.
E. K., Ethiopia
Kulaumiwa Nina umri wa miaka 15, na ile makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Sikuzote Ni Kosa Langu?” (Julai 22, 1997) ilifanya machozi yakanitiririka. Mimi ndiye mdogo kabisa katika familia yetu na kila wakati nasumbuliwa. Asanteni kwa kuandika kuhusu hili.
N. H., Marekani
Bonde la Ufa Nilipendezwa hasa kusoma mara nyingi ile makala “Bonde Kuu la Ufa.” (Julai 22, 1997) Ilikuwa kama kwenda safari. Mume wangu alifanya kazi katika Afrika, na niliweza kusafiri hadi sehemu ya kusini mwa Tanzania. Kila wakati niliangalia nje ya dirisha la Landrova yetu. Kila kitu ni dhahiri na chenye kupendeza katika Afrika; ilifanyiza wazo la kudumu akilini mwangu.
B. S., Kanada
Watoto Wanaositawi Nataka kuwashukuru kwa ule mfululizo maridadi “Uwasaidie Watoto Wako Wasitawi.” (Agosti 8, 1997) Niliupata kuwa wa manufaa sana na wenye kutia moyo. Nina mvulana wa miaka mitatu, na makala hii ilinisaidia kuona hoja zake na kuboresha njia niliyotumia kumtia nidhamu. Shukrani zangu nyingi zamwendea Yehova kwa makala hizi.
P. S., Italia
Niliguswa sana na ile makala “Maneno Makali, Roho Zilizopondeka.” Maisha yangu yote nimejihukumu vikali. Ninapendezwa kuona kwamba badala ya kuhukumu vikali, mwajaribu kwa upendo kuwasaidia wale wote ambao wamevumilia kuteseka kwingi. Yehova na aendelee kuwabariki na kuwaongoza kuandika makala ambazo ni zenye manufaa sana na zenye kutuliza.
L. D., Kanada
Natumaini kuwa makala hizo zitafungua macho ya wengine kuelekea kiini kinachosababisha msukosuko mwingi wa kindani ambao wengi wetu wamepata. Asanteni kwa kushughulikia habari hii.
L. B., Marekani
Makala kama hizi hunisaidia kutimiza kazi yangu nikiwa mwalimu wa shule ya watoto wadogo kwa njia bora zaidi. Asanteni sana kwa kuendelea kutufahamisha mambo mapya na kutusaidia kufanya maendeleo.
G. R., Mexico
Makala hizo zilinipa tumaini fulani. Nilitoka katika familia yenye kasoro na mara nyingi naona vigumu kuhisi kuwa nafaa kumtumikia Yehova na kumtunza binti yangu mdogo. Nitafanya niwezavyo kutumia madokezo yaliyo katika makala hiyo. Asanteni kwa kujali.
A. A., Marekani