Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 6/22 kur. 5-7
  • Je, Ni kwa Mfano wa Mungu Au wa Mnyama?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Ni kwa Mfano wa Mungu Au wa Mnyama?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mambo Ambayo Hututofautisha na Wanyama
  • Je, Ni Pengo Kubwa Sana Lisiloweza Kuzibwa?
  • Nadharia Isiyotegemeka
  • Matokeo ya Kuhuzunisha
  • Je, Uabudu Uumbaji au Muumba?
  • Mageuzi Yajaribiwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Wanadamu Sisi Ni Nani?
    Amkeni!—1998
  • Je, Wanyama Wanaenda Mbinguni?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Wanyama
    Amkeni!—2015
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 6/22 kur. 5-7

Je, Ni kwa Mfano wa Mungu Au wa Mnyama?

MWANADAMU wa kwanza, Adamu, aliitwa “mwana wa Mungu.” (Luka 3:38) Hakuna mnyama yeyote ambaye amewahi kuitwa hivyo kamwe. Na Biblia huonyesha kwamba wanadamu wana mambo mengi yanayofanana na ya wanyama. Kwa kielelezo, wote wanadamu na wanyama ni nafsi. Mungu alipomwumba Adamu, “mtu akawa nafsi hai,” yasema Mwanzo 2:7. (Italiki ni zetu.) Wakorintho wa Kwanza 15:45 lakubaliana na jambo hili hivi: “Mtu wa kwanza Adamu akawa nafsi hai.” Wanadamu ni nafsi, kwa hiyo nafsi si kitu fulani kisichoonekana ambacho huendelea kuishi baada ya mwili kufa.

Kuhusu wanyama, Mwanzo 1:24 husema hivi: “Nchi na izae kiumbe hai [“nafsi zilizo hai,” “NW”] kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake.” Kwa hiyo ingawa Biblia yawapa adhama wanadamu kwa kufunua kwamba tuliumbwa kwa mfano wa Mungu, hiyo hutukumbusha pia juu ya hali yetu ya chini, pamoja na wanyama. Na bado, kuna kitu fulani ambacho hupatikana kwa wanadamu na wanyama.

Biblia hueleza hivi: “Kwa maana linalowatukia wanadamu linawatukia wanyama; jambo moja lawatukia; anavyokufa huyu ndivyo anavyokufa huyu . . . mwanadamu hana kitu cha kumpita mnyama . . . Wote huendea mahali pamoja; wote hutoka katika mavumbi; na hata mavumbini hurudi tena.” Ndiyo, katika kifo mwanadamu na wanyama hufanana pia. Wote hurudi kwenye “ardhi,” “mavumbini,” mahali walipotoka.—Mhubiri 3:19, 20; Mwanzo 3:19.

Lakini kwa nini wanadamu huhuzunishwa sana na kifo? Kwa nini sisi hutamani kuishi milele? Na kwa nini twapaswa kuwa na kusudi maishani? Kwa hakika, twatofautiana sana na wanyama!

Mambo Ambayo Hututofautisha na Wanyama

Je, ungefurahi kuishi maisha ambayo hayana kusudi isipokuwa kula, kulala, na kuzaana? Wazo hili hata huwasumbua wanamageuzi wenye bidii. “Mwanadamu wa kisasa mwenye elimu na ambaye ni mwagnosti na mwenye kushuku,” aandika mwanamageuzi T. Dobzhansky, “hawezi kujiepusha angalau kisiri kujiuliza yale maswali ya zamani: Je, maisha yangu yana kusudi fulani kwa kuongezea kuendelea kuishi na kuzaana? Je, ulimwengu ninaoishi una kusudi fulani?”

Kwa kweli, kukana kuwepo kwa Muumba hakumalizi kiu ya mwanadamu ya kutaka kujua maana ya maisha. Akimnukuu mwanahistoria Arnold Toynbee, Richard Leakey aandika hivi: “Kipaji hiki cha kiroho cha [mwanadamu] humfanya ang’ang’ane daima kujipatanisha na ulimwengu ambamo amezaliwa.”

Na bado, maswali ya msingi yadumu kuhusu utu wa binadamu, asili zetu, na hali yetu ya kiroho. Bila shaka kuna pengo kubwa kati ya mwanadamu na wanyama. Pengo hilo ni kubwa kadiri gani?

Je, Ni Pengo Kubwa Sana Lisiloweza Kuzibwa?

Tatizo la msingi linalokabili nadharia ya mageuzi ni lile pengo kubwa ambalo huwatenganisha wanadamu na wanyama. Kwa kweli, ni kubwa kadiri gani? Fikiria baadhi ya mambo ambayo wanamageuzi wenyewe wamesema kuhusu pengo hilo.

Mtetezi mashuhuri wa nadharia ya mageuzi katika karne ya 19, Thomas H. Huxley, aliandika hivi: “Hakuna mtu yeyote aliye na usadikisho mwingi kunishinda juu ya ukubwa wa pengo lililoko kati ya . . . mwanadamu na mnyama . . . , kwa kuwa yeye pekee ana kipawa cha kustaajabisha cha akili na usemi wenye kueleweka [na] . . . kwa hiyo kuwa juu kana kwamba juu ya kilele cha mlima, juu ya kiwango cha wanyama wa hali ya chini.”

Mwanamageuzi Michael C. Corballis aonelea kwamba “kuna pengo kubwa kati ya binadamu na nyani . . . ‘Ubongo wetu ni mkubwa mara tatu zaidi kuliko ule ambao tungetarajia kwa nyani atoshanaye na sisi.’” Na mtaalamu wa ubongo Richard M. Restak aeleza hivi: “Ubongo wa [binadamu] ndicho kiungo pekee kijulikanacho ulimwenguni ambacho hujaribu kujielewa chenyewe.”

Leakey akiri hivi: “Utambuzi hutokeza utatanishi kwa wanasayansi, ambao wengine huamini kuwa hauwezi kutatuliwa. Hali ya kujitambua ambayo kila mmoja wetu anayo ni dhahiri sana hivi kwamba hiyo huonekana katika kila kitu tufikiricho na kufanya.” Pia asema hivi: “Kwa kweli lugha hutokeza pengo kati ya [wanadamu] na viumbe vingine vya ulimwengu.”

Akitaja ajabu nyingine ya akili ya binadamu, Peter Russell aandika hivi: “Bila shaka kumbukumbu ndiyo mojawapo ya uwezo wa binadamu ulio wa maana sana. Hatungeweza kujifunza bila hiyo . . . , hakungekuwako utendaji wenye akili, hakungekuwako ukuzi wa lugha, wala sifa zozote . . . ambazo kwa kawaida hushirikishwa na wanadamu.”

Zaidi ya hayo, hakuna mnyama yeyote ambaye huabudu. Hivyo, Edward O. Wilson aonelea hivi: “Mwelekeo wa kuwa na itikadi ya kidini ndilo jambo lenye nguvu zaidi na lililo tata zaidi katika akili ya kibinadamu na ni utu usioondoleka wa binadamu.”

“Tabia ya binadamu hutokeza mafumbo mengine mengi ya Nadharia ya Darwin,” akiri mwanamageuzi Robert Wright. “Ucheshi na kicheko zina kusudi gani? Kwa nini watu hufanya maungamo wanapokufa? . . . Maombolezo yana kusudi gani hasa? . . . Ikiwa tayari mtu amekufa, kuomboleza kunafaaje jeni?”

Mwanamageuzi Elaine Morgan akiri hivi: “Manne kati ya mambo yenye kujitokeza sana na yasiyoeleweka juu ya binadamu ni kama yafuatavyo: (1) kwa nini wao hutembea kwa miguu miwili? (2) kwa nini wamepoteza manyoya yao? (3) kwa nini wamekuza ubongo mkubwa? (4) kwa nini walijifunza kusema?”

Maswali haya hujibiwaje na wanamageuzi? Morgan aeleza hivi: “Majibu ya kawaida kwa maswali haya ni kama yafuatavyo: (1) ‘Bado hatujui’; (2) ‘Bado hatujui’; (3) ‘Bado hatujui’, na (4) ‘Bado hatujui.’”

Nadharia Isiyotegemeka

Mwandishi wa kitabu The Lopsided Ape alisema kwamba lengo lake “lilikuwa kuandaa picha ya ujumla ya kufafanua mageuzi ya binadamu yaliyofanyika polepole. Mikataa mingi imekuwa makisio tu, ikitegemezwa hasa kwa meno, mifupa, na mawe machache ya kale.” Kwa kweli, hata nadharia ya awali ya Darwin haikubaliwi na wengi. Asema Richard Leakey: “Fasili ya Darwin juu ya namna tulivyogeuka ilitawala sayansi ya elimu ya binadamu mpaka miaka michache iliyopita, na kumbe ikawa yenye makosa.”

Wanamageuzi wengi, kulingana na Elaine Morgan, “wamepoteza uhakika katika majibu ambayo walifikiri walijua miaka thelathini iliyopita.” Hivyo, haishangazi kwamba baadhi ya nadharia zilizoaminiwa na wanamageuzi zimeanguka.

Matokeo ya Kuhuzunisha

Uchunguzi fulani umepata kwamba idadi ya wanyama wa kike ambao mnyama wa kiume hujamiiana nao huhusiana na tofauti iliyoko katika ukubwa wa mwili kati ya mnyama wa kiume na wa kike. Basi, wengine wamefikia mkataa kwamba mazoea ya wanadamu ya kufanya ngono yapaswa kufanana na ya sokwe, kwa kuwa sokwe wa kiume, kama wenzao binadamu, ni wakubwa kidogo tu kuliko sokwe wa kike. Kwa hiyo wengi husababu kwamba kama sokwe, wanadamu wanapaswa kuruhusiwa wawe na zaidi ya mwenzi mmoja wa kufanya naye ngono. Na kwa kweli wengi wanao.

Lakini jambo lionekanalo kufaulu kwa sokwe kwa kawaida limekuwa msiba kwa wanadamu. Mambo ya hakika huonyesha kuwa ngono za ovyoovyo huongoza kwenye familia zilizovunjika, utoaji-mimba, maradhi, vurugu la akili na la kihisia-moyo, wivu, ujeuri katika familia, na watoto walioachwa wanaokua bila mwongozo, ambao nao huendelea kupatwa na mambo haya yenye madhara. Ikiwa ni kweli kwamba wanadamu wana utu ulio sawa na wa wanyama, kwa nini mambo haya husababisha uchungu wa kihisia-moyo kwa wanadamu?

Kufikiri kimageuzi hutokeza shaka juu ya utakatifu wa uhai wa kibinadamu. Ni chini ya msingi gani uhai wa kibinadamu ulivyo mtakatifu ikiwa twasema hakuna Mungu na kujiona kuwa sisi ni wanyama tu wa hali ya juu? Je, labda ni akili yetu? Ikiwa ndivyo, basi swali lililozushwa katika kitabu The Human Difference lingefaa sana: “Je, ni haki kuwaona wanadamu kuwa bora kuliko mbwa na paka eti kwa sababu tu tulifanikiwa na [mageuzi]?”

Kadiri fasili mpya ya dhana ya kimageuzi ieneapo, “bila kuepukika itaathiri sana mawazo ya kiadili,” chasema kitabu The Moral Animal. Lakini ni adili mbaya sana ambayo hutegemea kauli ya kwamba tulifanyizwa kwa “uteuzi asilia,” ambao kuupitia, kama aelezavyo H. G. Wells “wenye nguvu na wajanja huwakandamiza walio dhaifu na wenye kuaminika.”

La maana zaidi, nadharia nyingi za wanamageuzi ambazo zimenyofoa maadili kwa miaka iliyopita zimeshindwa na kikundi kipya cha wenye kufikiri. Lakini jambo la kuhuzunisha ni kwamba madhara ambayo nadharia hizo zimesababisha yangali yako.

Je, Uabudu Uumbaji au Muumba?

Mageuzi huelekeza mtu atazame chini kwa uumbaji ili kupata majibu, si juu kwa Muumba. Kwa upande mwingine, Biblia, hutuelekeza juu kwa Mungu wa kweli kwa ajili ya kanuni zetu za kiadili na kusudi letu maishani. Pia hueleza kwa nini twahitaji kung’ang’ana ili kujiepusha na ukosaji na kwa nini ni wanadamu peke yao ambao wametaabishwa sana na kifo. Zaidi ya hayo, ufafanuzi wa Biblia kuhusu kwa nini sisi huelekea kutenda lililo baya huonekana kuwa kweli katika akili na moyo wa binadamu. Twakualika uchunguze ufafanuzi huo wenye kuridhisha.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Pengo kati ya mwanadamu na mnyama ni kubwa kadiri gani?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki