Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 6/22 kur. 3-4
  • Wanadamu Sisi Ni Nani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wanadamu Sisi Ni Nani?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nini Kusudi la Uhai?
  • Tunaloamini Huathiri Maisha Zetu
  • Je, Ni kwa Mfano wa Mungu Au wa Mnyama?
    Amkeni!—1998
  • Kitabu Chashangaza Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • Mageuzi Yajaribiwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Je, Uhai Wote Umetokana na Chanzo Kimoja?
    Maswali Matano Muhimu Kuhusu Chanzo cha Uhai
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 6/22 kur. 3-4

Wanadamu Sisi Ni Nani?

YAONEKANA kwamba wanadamu hawajijui wao ni nani. Mwanamageuzi Richard Leakey aonelea hivi: “Kwa karne kadhaa wanafalsafa wameshughulika na hali za ubinadamu. Lakini, kwa kushangaza hakuna fasili inayokubaliwa kuwa ubinadamu.”

Hata hivyo, Bustani ya Wanyama ya Copenhagen ilitoa maoni yake kwa ujasiri kupitia maonyesho yaliyowekwa katika jumba la kuonyeshea wanyama wa hali ya juu. Kitabu 1997 Britannica Book of the Year chaeleza hivi: “Wenzi fulani kutoka Uholanzi walihamia makao ya muda katika bustani hiyo ya wanyama wakiwa na kusudi la kuwakumbusha wageni juu ya ukoo wao wa karibu pamoja na nyani.”

Vitabu vya marejezo huunga mkono madai hayo ya kuwa kuna ukoo wa karibu kati ya wanyama fulani na wanadamu. Kwa kielelezo, The World Book Encyclopedia, chasema hivi: ‘Binadamu pamoja na nyani, komba, tumbili, ni jumuiya ya mamalia wa hali ya juu.’

Lakini, kwa hakika wanadamu wana tabia nyingi za kipekee ambazo hazifanani na za wanyama. Baadhi ya hizo ni upendo, dhamiri, adili, hali ya kiroho, haki, rehema, ucheshi, ubunifu, ufahamu wa wakati, kujifahamu, uthamini wa umaridadi, hangaiko kuhusu wakati ujao, uwezo wa kuongeza ujuzi katika vizazi vyote, na tumaini la kwamba kifo si mwisho wa kuwapo kwetu.

Katika kujaribu kupatanisha tabia hizi na za wanyama, wengine hutaja saikolojia ya mageuzi, ambayo ni mchanganyiko wa mageuzi, saikolojia, na sayansi ya jamii. Je, saikolojia ya mageuzi imetuelimisha juu ya fumbo la utu wa binadamu?

Ni Nini Kusudi la Uhai?

“Kauli ya saikolojia ya mageuzi ni sahili,” asema mwanamageuzi Robert Wright. “Akili ya binadamu, kama kiungo chochote kile, ilibuniwa kwa kusudi la kupitisha jeni hadi kizazi kifuatacho; hisia na mawazo ambayo akili hufanyiza zaweza kueleweka kwa kutegemea kauli hii.” Yaani, kusudi letu lote maishani, linaloongozwa na jeni zetu na kuonyeshwa katika utendaji wa akili zetu, ni kuzaana.

Kwa kweli, “mwingi wa utu wa kibinadamu,” kulingana na saikolojia ya mageuzi, “kwa ufupi ni ubinafsi unaochangiwa na jeni.” Kitabu The Moral Animal chasema hivi: “Uteuzi asilia ‘wawataka’ wanaume wafanye ngono na wanawake wengi kupindukia.” Kulingana na dhana hii ya mageuzi, chini ya hali fulani ukosefu wa adili kwa upande wa wanawake huonekana pia kuwa jambo la asili. Hata upendo wa wazazi huonekana kuwa mbinu iletwayo na jeni ili kuhakikisha kwamba uzao utasalimika. Hivyo, maoni fulani husisitiza umaana wa urithi wa kijeni katika kuhakikisha kwamba familia ya kibinadamu imeendelezwa.

Vitabu fulani vya mwongozo sasa vimeandikwa kwa kutegemea mawazo mapya ya saikolojia ya mageuzi. Kimojawapo cha vitabu hivyo hufafanua utu wa binadamu kuwa “usio tofauti sana na utu wa sokwe au utu wa nyani.” Pia kinataarifu hivi: “Kuhusu mageuzi, . . . kuzaana ndilo jambo la maana.”

Kwa upande mwingine, Biblia hufundisha kwamba Mungu aliwaumba wanadamu si kwa kusudi la kuzaana tu. Tuliumbwa kwa “mfano” wa Mungu, tukiwa na uwezo wa kudhihirisha sifa zake, hasa upendo, haki, hekima, na nguvu. Ukiongezea zile sifa za kipekee za wanadamu zilizotangulia kutajwa, inakuwa wazi ni kwa nini Biblia hukuza wanadamu juu ya wanyama. Kwa kweli, Biblia hufunua kwamba Mungu aliwaumba wanadamu si wakiwa na tamaa ya kuishi milele tu bali pia wakiwa na uwezo wa kufurahia kutimizwa kwa tamaa hiyo katika ulimwengu mpya wenye uadilifu utakaoletwa na Mungu.—Mwanzo 1:27, 28; Zaburi 37:9-11, 29; Mhubiri 3:11; Yohana 3:16; Ufunuo 21:3, 4.

Tunaloamini Huathiri Maisha Zetu

Kujua sisi ni nani hasa si jambo la kinadharia hata kidogo, kwa kuwa tunaloamini kuhusu asili zetu laweza kuathiri jinsi tunavyoishi. Mwanahistoria H. G. Wells aliandika mikataa ambayo wengi walifikia baada ya kuchapishwa kwa kitabu cha Charles Darwin Origin of Species katika mwaka wa 1859.

“Maadili yakapotoka kabisa. . . . Imani ikazorota kabisa baada ya mwaka wa 1859. . . . Watu wenye uwezo kufikia mwishoni mwa karne ya kumi na tisa waliamini kwamba walipata uwezo kupitia ule Mng’ang’ano wa Kuishi, yaani wenye nguvu na wajanja huwakandamiza walio dhaifu na wenye kuaminika. . . . Waliamua kwamba mwanadamu ni mnyama wa kijumuiya kama mbwa-mwitu wa India wakali. . . . Ilionekana sawa kwao kwamba wenye nguvu kati ya binadamu walipaswa kukandamiza na kutiisha walio dhaifu.”

Kwa wazi, ni muhimu kwamba tupate maoni sahihi kuhusu sisi ni nani hasa. Kwa maana, kama alivyouliza mwanamageuzi mmoja, “ikiwa Nadharia ya Darwin iliyo sahili na ya kikale . . . ilidhoofisha maadili ya ustaarabu wa Magharibi, ni nini litakalotukia wakati [saikolojia mpya ya mageuzi] itakapopata umashuhuri?”

Kwa kuwa jambo tunaloamini kuhusu asili zetu huathiri maoni yetu ya msingi juu ya uhai na kuhusu mema na mabaya, ni muhimu kwamba tuchunguze swali hili kwa makini.

[Blabu katika ukurasa wa 4]

Mwanahistoria H. G. Wells aliandika mikataa ambayo wengi walifikia baada ya kuchapishwa kwa kitabu cha Charles Darwin Origin of Species katika mwaka wa 1859: “Maadili yakapotoka kabisa. . . . Imani ikazorota kabisa baada ya mwaka wa 1859”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki